|
|
|
KAMBI ya kwanza ya wasichana wanafunzi wa shule za sekondari za mjini Mwanza ilimalizika kwa maazimio kadhaa na maombi kwa viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislamu kupigia kelele haki ambazo wanafunzi Waislamu hawapati kwa usawa na wenzao wasiokuwa Waislamu. Kambi hiyo ambayo ilitayarishwa na shule ya sekondari ya Thaqaafa ilikusudiwa kushirikisha shule saba za mjini Mwanza, lakini zote zilishiriki kasoro shule moja tu ya sekondari ya Nganza, Mwalimu Mku wake Rehema alidai kuwa wako katika matayarisho ya mtihani wa kufunga mwaka hivyo haruhusu wanafunzi kuwa nje ya maeneo ya shule yake. Jumla ya wanafunzi 45 walishiriki kuwakilisha wenzao. Kwa mujibu wa ratiba ya kambi, mada ambazo zilikusudiwa kufikishwa ni nne, ambazo ni kusoma Qur’an (Ustaadha Halima na Ustaadha Mwanaidi), Tawhiid (Ustaadha Khadija Juma), Fiqhi (Ustaadha Fatuma Khamis), Hadith (Ustaadha Fatuma na Zuhura Kombo). Nafasi ya mwanamke katika jamii (Ustaadha Saida Ibrahim), Malezi ya Kiislamu (Bi. Khamisa Khamisi), Sayansi na Qur’an (Geography) (Bi. Mariam) na uchambuzi wa masomo (Bi. Zena Opiyo). Baadhi ya washiriki walikuwa ni kutoka vidato vya kwanza, pili, tatu na tano walionyesha furaha yao na shukrani nyingi kwa waandalizi wa kambi hiyo kwa ujumla, walisema ni mengi ambayo walikuwa hawayafahamu au waliyafahamu kwa "wazo mpachiko" (Programmed mind). Kwa niaba ya wenzao, walisema kuwa wanaomba viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislamu kulizungumzia bila ya woga suala la haki za wanafunzi wa Kiislamu katika taasisi mbalimbali za elimu nchini. Walisema wanapata shida sana kupata ruhusa za kwenda kusali, kuvaa nguo za kujisitiri, fomu za kujiunga mashuleni au vyuoni hazifafanuliwi wazi, wakati wa saumu hakuna utaratibu wa maana wa chakula, sala mbalimbali za kila siku hazitekelezwi kutokana na vipindi kutotoa nafasi ya sala. Vile vile walidai upungufu wa walimu wa maarifa ya Uislamu hawatoshelezi mahitaji yao, vitabu vya rejea hakuna sylabasi haifuatwi ila hufundishwa kwa jumla jumla tu mambo ya Uislamu bila kufuata sylabasi. Akitoa nasaha zake, Alhaj Maruzuku Magongo kwa niaba ya waandaaji wa kambi aliwaomba wanafunzi kuzingatia mafunzo yote yatakayotolewa na kuwaomba kuwafikishia wenzao ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria kambi hiyo, aliwaahidi kuwapatia makabrasha mbalimbali ambayo watayatumia mara warudipo mashuleni mwao. Semina hiyo ilianza Ijumaa Novemba 6 hadi 8, 1998 ilifungwa baada ya sala ya Alasiri katika kituo hicho cha Yatima ya Ilemela kilichopo mjini hapa. Kuandaa makongamano ya aina hiyo ni mojawapo ya madhumuni ya kituo hicho. WAISLAMU nchini wametakiwa kushikamana na kusaidiana katika shida na faraja ili kuleta umoja na upendo miongoni mwao. Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Sheikh Abdallah Salum wakati wa sherehe iliyofanyika Mbagala Jijini. Sheikh Abdallah alisema kuwa ili Uislamu uweze kuimarika na kuwa na nguvu miongoni mwa dini zingine ni lazima kwa Waislamu wenyewe kushikamana na kuonyesha ushirikiano wao kwenye shida na faraja. Alisema kuwa Uislamu kama ulivyo hauna budi kupewa changamoto na waalim wa madrasa mbalimbali, Masheikh na maimamu kwani wao ni viongozi kwa Waislamu wengine na hivyo kuwataka Waislamu katika makazi yao kusaidiana kwa hali na mali ili kujenga misingi imara ya dini yao. Kutokuwepo kwa mshikamano kunatoa mwanya kwa maadui wa Uislamu kufanya vyovyote watakavyo na hivyo kuathiri maendeleo ya Waislamu na Uislamu wenyewe. Alisema anashangaa kuona kuwa Waislamu hawana uchungu na dini yao licha ya kuingiliwa na watu wasioitakia mema dini hiyo. Alisema kuwa kuna mifano mingi inayoonyesha kuchokozwa kwa Waislamu katika dini yao, aliitaja mifano hiyo kuwa ni pamoja na madai yanayotolewa na baadhi vikundi vya Kikristo kuwa Uislamu si dini na mambo mengine mengi ambayo hata hivyo hakuwa tayari kuyataja. Wakati huo huo, Waislamu wametakiwa kufuata nguzo kuu tano za Uislamu ili kujenga jamii yenye nidhamu na utashi miongoni mwa watu wengine. Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Alhaj Ibrahim Nassoro wakati wa sala ya Ijumaa iliyofanyika kwenye Msikiti wa Ijumaa uliopo Temeke Jijini. Alhaj Ibrahim alisema kuwa kumong’onyoka kwa maadili katika jamii ya Watanzania hivi sasa kunatokana na vijana kukosa misingi imara ya dini zao. Aliitaja mitindo ya uvaaji, unyoaji nywele, uvaaji hereni kwa wanaume na wanawake kutembea vichwa wazi kuwa ni miongoni mwa vitendo vinavyoonyesha maadili ya dini yanapuuzwa hivi sasa. Akizitaja haya na sura mbalimbali kutoka katika kitabu kitukufu cha Qur’an, Alhaj Ibrahim alisema kuwa kama jamii ya vijana hao haitajizatiti katika kupigana na vitendo hivyo, basi nchi haitakuwa na vijana wenye nguvu imara ya kidini kuweza kuimarisha dini yao. Alisema licha ya juhudi za Masheikh na watu mbalimbali kukemea vitendo hivyo, vijana hao wameonekana kuzidi kuongezeka hali inayowafanya viongozi wa dini ya Kiislamu kulivalia njuga suala hilo. Alisema dawa pekee ya kupunguza janga la kuanguka kwa maadili ni kuanza kuzitekeleza nguzo tano za Uislamu ambazo ni kutoa shahada mbili, kuswali sala tano kila siku, kutao zaka, kufunga Ramadhani na kuhiji Makkah kwa wenye uwezo. Imedaiwa kuwa Sheikh wa Bakwata Wilaya ya Rufiji na viongozi wa Wakiristo Wilayani humo wamekubaliana kuanzisha umoja baina ya Waislamu na Wakristo utakao julikana kama Uwawaru yaani Umoja wa Waislamu na Wakristo Rufiji. Imefahamika kuwa taarifa hizi zilipofikishwa kwa Waislamu wa Ikwiriri na Kibiti zilipokelewa kwa hisia tofauti. Kwa upande wa Ikwiriri wao hawakuwa na upinzani wowote walikubali kuanzishwa kwake kwa madai kuwa itakuwa rahisi wao kusikilizwa na serikali na hivyo kupatiwa misaada kwa ajili ya maendeleo yao. Ilidaiwa kuwa lengo la kuanzishwa umoja huo ni kuleta maendeleo katika sehemu hiyo. Mambo yalikuwa tofuati pale suala hili lilipofikishwa kwa Waislamu wa Kibiti, waliwatuma baadhi ya wajumbe wao kufuatilia ukweli wa suala hilo. Kuhoji nini hasa makusudi yake, majibu waliyopewa na viongozi wenzao wa Waislamu wa Ikwiriri ni kwamba lengo ni kuleta maendeleo na kwa kuwa Wakristo wao ni rahisi kusikilizwa na serikali na hivyo kupatiwa misaada. Waislamu wa Kibiti walipofikishiwa majibu ya ndugu zao wa Ikwiriri na sababu za kuanzishwa kwa umoja huo walionekana kusita. Nao viongozi wa Waislamu Ikwiriri kwa kushirikiana na tajiri mmoja mwenye asili ya Kiarabu wameanzisha shule ya awali ya watoto ndani ya kanisa. Imedaiwa kuwa watoto hao hupewa chakula cha mchana shuleni hapo lakini kabla ya kula wote kwa pamoja bila kujali tofuati zao za kidini hutakiwa kuomba Kikristo kwanza. Baadhi ya wanafunzi waliohojiwa wamedai kuwa kila siku wanapoingia shuleni kabla ya kuanza masomo hutakiwa waanze kumsifu Yesu. Wakati huo huo, jumla ya misikiti 35 ya Kibiti imeamua kuanzisha umoja wao ili kujiletea maendeleo. Imeelezwa kuwa tatizo linalowakabili hivi sasa ni uhaba wa vifaa vya kufundishia madresa kama vile juzuu na wametoa wito kwa Waislamu wenye uwezo wawasaidie. WAUMINI wa Kiislamu kote nchini wametakiwa kutoridhika na elimu walizo nazo badala yake waongeze bidii kusoma ili waweze kuiokoa jamii inayopotea kimaadili. Hayo ameyasema Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya Thaqafa, Bw. Maruzuku Magongo mjini hapa mwishoni mwa wiki alipokuwa akiwahutubia wanafunzi kutoka shule mbalimbali za sekondari, wazazi na walimu walio hudhuria katika sherehe ya Tamsa Day iliyofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Thaqafa. Amesema kuwa jamii ya Kiislamu bado inahitaji wataaalam wa fani mbali mbali kama walimu na madaktari hivyo kila mmoja wetu anahitajika aongeze bidii ili kuweza kuuinua umma wa Kiislamu. Aidha ustadhi Ilunga Kapungu akitoa mada katika sherehe hiyo aliwafahamisha waliohudhuria kuwa jamii inategemea kuona matunda ya vijana wanaohitimu masomo yao, hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu, kusomea fani mbali mbali ili kuweze kupata wataalam wa kila fani. Aliendelea kusema kuwa tatizo kubwa linaloikabili jamii yetu hivi sasa ni kutokuelimika kwa elimu wanazozipata, hivyo inakuwa ni vigumu kuondoka kwa maovu. Amesema kuwa iwapo jamii itaelimika, itayachukia mambo ya anasa kama uasherati, wizi hata ulevi na kuongeza kuwa ni vema tufanye mambo yetu kwa kutaraji radhi za Allah na siyo kwa kujisifu au kutaka kusifiwa. "Hakuna haja ya kuwa na vyeti vingi huku havina manufaa yoyote, ni heri kuwa na elimu kiasi inayoonekana ina manufaa katika jamii", alisema Ust. Ilunga. Jumla ya wanafunzi 150 walipatiwa vyeti na Tamsa Mwanza kwa kushirikiana pamoja walipokuwa masomoni (vyeti vya utambulisho). Wakati huo huo, Jumuiya ya wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari na vyuo mkoani Mwanza (TAMSA) imepata viongozi wapya watakaowaongoza kwa kipindi kijacho. Katika uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Thaqafa, Salum Khalfani toka Taqwa Sekondari alichaguliwa kuwa mwenyekiti. Nafasi ya Katibu ilichukuliwa na Hussein Moshi, wakati Mweka Hazina ni Subira Mrisho wote toka Mwanza Sekondari. Waliochaguliwa kuwa wajumbe ni Habibu Abdallah na Karsan Hussein (Pamba Sekondari), Hashimu Said (Thagafa) Juma Ibrahimu na zena Kajeje (Mwanza Sekondari). Akitoa nasaha mara baada ya uchaguzi mlezi wa Tamsa mkoani hapa Ust. Ally Kulindwa aliwataka viongozi waliochaguliwa kuandaa programu ya shughuli zao mapema na kuiweka wazi ili waweze kusadiana kiutendaji. SHEIKH Yahya Kiduo amewataka watu wanaojiita Waislamu waachane na shirki kwani hawezi mtukuwa mshirikina bado akawa Muislamu. Sheikh Yahya ambaye ni Imam wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa Makole kata ya Kwafungo amewahimiza Waislamu hasa wa sehemu mbalimbali mkoani Tanga ambapo alisema Shirki imezidi, washikamane na swala na kuzitekeleza nguzo zote za Uislamu. Akiwahutubia mamia ya Waislamu hivi karibuni Sheikh Yahya amesema kwamba haitoshi mtu kudai kwamba yeye ni Muislamu na azikwe Kiislamu. Kuzikwa Kiislamu hakumsaidii mtu endapo hakuwa na amali yoyote. |
YALIYOMO
Maoni Kuwa na mawazo ya kufugwa tunajidharaulisha Sakata la
mabucha ya Nguruwe kuibuka upya
Bakwata yairushia polisi makombora Ngaramtoni MACHO YA
SHUTUMA
Serikali
yatakiwa iwachukulie hatua wauaji
Historia ya Msikiti wa Ngaramtoni Silaha yetu
ni kura ya pamoja
Anuani
ya fikra
Tunahitaji
"UN' ya Waislamu!
Kongamano la wanawake wa Kiislamu Newala lafana Umuhimu
wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo - 2
Kesi mojawapo ya mihadhara yafutwa Wasaidieni watoto wenye vipaji - Prof. Kilonzo Mahafali ya kidato cha nne Thaqafa: Wazazi wakumbushwa wajibu wao Wanafunzi
Mwanza wadai haki za kuabudu mashuleni kwa usawa
Saidianeni katika shida - Sheikh Abdallah Waislamu, Wakristo Rufiji watakiwa kuunda umoja Someni muiokoe jamii kimaadili Kesi
nyingine ya Waislamu Mwembechai yaahirishwa
Kusilimu kwa Wakristo kwaleta kero Mwanza Nzasa waomba msaada wa chakula, madawa Katibu wa Bakwata Moro ang'olewa Msikitini Chakula
na lishe
|