AN-NUUR 
Na.176 Shaaban  1419, Novemba 20 - 26, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Kesi nyingine ya Waislamu Mwembechai yaahirishwa
 
  • Mashahidi wa serikali washindwa kufika mahakamani
  • Watuhumiwa wafutiwa sharti la kuripoti polisi
Na Muhibu Said

KESI nyingine namba 184/98 inayowakabili Waislau kumi na moja walioshitakiwa na serikali kwa tuhuma ya kufanya ghasia maeneo ya Mwembechai, Jijini na kumjeruhi askari Simon Nyakoro imeahirishwa hadi Desemba 14, mwaka huu. 

Kuahirishwa kwa kesi hiyo kulizingatia ombi la Mwendesha Mashitaka wa Serikali afande James la kuiomba mahakama iaharishe kesi hiyo kutokana na mashahidi wa upande wa serikali kutofika mahakamani siku hiyo (ya Novemba 13, 1998) kama ilivyopangwa. 

Kesi hiyo ilifunguliwa na serikali katika mahakama ya Kisutu, Jijini mnamo mwezi Machi, mwaka huu. 

Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa mahakamani hapo mapema Novemba 13, mwaka huu ambapo mashahidi wa upande wa serikali walitarajiwa kutoa ushahidi wao. 

Mapema, akiahirisha kesi hiyo, Hakimu wa mahakama hiyo, Bw. Mwankenja, alifuta sharti la watuhumiwa la kuripoti kila wiki katika kituo cha polisi cha Magomeni, Jijini, sharti walilopewa na serikali hapo awali. 

Bw. Mwankenja alisema mahakama yake imefikia uamuzi huo kwa kuridhika na hoja za msingi zilizotolewa na wakili wa kujitegemea wa watuhumiwa Bw. Twaha Taslima za kuiomba mahakama yake iwaondolee wateja wake sharti hilo. 

Bw. Mwankenja aliongeza kuwa mahakama yake pia imeamua kufuta sharti hilo kutokana na kutoweka "hali ya hofu" iliyokuwepo hapo awali juu ya washitakiwa na kwamba mahakama yake sasa ina imani na kamanda wa polisi wa wilaya ya Kinondoni (OCD) kwamba hawezi akaruhusu eneo husika kutokea ghasia kirahisi kwa mara nyingine tena. 

Aidha, Hakimu Mwankenja alisema kuwa sababu nyingine ya msingi aliyoizingatia hata aamue kuwaondolea sharti hilo, ni kwamba mahakama yake imewaona watuhumiwa kuwa ni watu wastaarabu na wenye nidhamu ambao alisema toka wafunguliwe kesi hiyo hawajaacha kufika wanapoitwa mahakamani. 

Awali, wakili wa kujitegemea anayewatetea washitakiwa Bw. Twaha Taslima aliiomba mahakama hiyo iwafutie wateja wake sharti hilo kwa hoja kwamba wateja wake bado hawajavunja amri yoyote ya mahakama na kwamba sharti hilo nigumu ambalo alisema limekuwa likiwasababishia matatizo wateja wake kwa kuwanyima fursa yenye wasaa mzuri wa kuhangaika kutafuta riziki ndani na nje ya Jiji. 


Kusilimu kwa Wakristo kwaleta kero Mwanza
 

MKUTANO mkubwa wa kiutendaji ulioitishwa na AL-MALLID tawi la Mwanza umeazimia kuwashirikisha Waislamu wote ili kuingia vyema katika karne ijayo.  

Akitoa taarifa ya kazi ambazo zinaendelea, Mwenyekiti wa AL-MALLID tawi la Mwanza alisema kuwa pamoja na matatizo waliyonayo na ambayo wanaendelea kukumbana nayo kumekuwepo na wimbi la wasio Waislamu kuvutiwa na mahubiri ya vitabu vinne kwa pamoja jambo ambalo kila mara wameona ukweli na kusilimu. 

Alisema jambo hili limewazidishia maadui na vikwazo wafanyapo mihadhara au waombapo vibali kwa shughuli hizo. Alisema safari yao ya Geita imeleta changamoto ya ajabu mno kutokana na taarifa walizozipata toka huko, idadi ya wanaosilimu nikubwa, mialiko ni mingi na ndiyo maana wameamua kuwaita Waislamu ili kuwapa taarifa. 

Mwenyekiti alisema kuwa propaganda zinazoenezwa na vyombo vya habari sio maoni ya waumini husika bali ni za viongozi wao wanaoogopa Uislamu kuutoa nje ya Misikiti na kuufikisha mbali zaidi, watu kuona ukweli. Aliwakumbusha Waislamu kuihubiri Qur’an na Uislamu kwa ujumla wake. 

"...Uislamu ni dini ya kweli na haina shaka na watu wanaielewa vema kama wanahubiriwa na kuikubali, Uislamu ndiyo njia bora ya pekee ya maisha hapa duniani na akhera", alimalizia Mwenyekiti huyo. 

Awali mkutano huo ulikuwa umeandaliwa kufanyika katika shule ya sekondari ya Taqwa lakini kutokana na sababu zisizofahamika, uongozi wa shule ulikataa ghafla na ikabidi uhamishiwe katika kituo cha Ansaar Sunna jirani na shule hiyo. Kituo hicho cha Ansaar Sunna kijulikanacho kwa jina la Thaqrib Nursery School kinashughulika na kulea watoto wadogo kuwapa elimu zote, na madrasa ya watu wazima saa za jioni. 

Maazimio yaliyopitishwa ni kufanya safari za nje ya mji (vijijini) kwa mwezi mara moja. 

Mihadhara katika maeneo ya karibu iendelee. Gharama zikabiliwe kwa kuitumia Misikiti na Waislamu wote kwa ujumla wachangie kwa mwezi mara moja. 

Akitoa nasaha zake, Makamu Mwenyekiti wa Bakwata mkoa wa Mwanza Sheikh Omar alisema watasaidiana kwa pamoja na Waislamu ili kufanikisha shughuli hizo. 

Awali, mada moja iliwakilishwa na Ustaadh Ilunga Hassan Kapungu mada hiyo iliyojulikana kwa jina la "hali ya Uislamu vijijini" aliwasisimua Waislamu alipowafahamisha kuwa kuna baadhi ya Misikiti ya Ijumaa vijijini ambapo Khatibu husoma Barazanji mlango wa kwanza hadi wa tatu na kukaa yaani khutuba ya kwanza imekwisha halafu husimama na kusoma mlango wa dua na mwisho Waislamu wanasali Ijumaa. Alisema hii ni kutokana na Masheikh kung’ang’ania mijini tu na kugombea Uimamu hawaendi vijijini. 

Alisema kuwa kuna umuhimu mno kwa sasa hivi makundi kusambaa vijijini na kuwazindua Waislamu na pia kuwafikishia ujumbe wasio Waislamu, alisema hiyo ni amri kuitangaza dini hii sio hiari wala haitaki kibali toka kwa mtu yeyote. Ni haki ya kila mtu kukutana na kubadilishana mawazo maadam hawajavunja sheria. 

Wakati huo huo, Waislamu wengi wameonyesha kukerwa mno na habari zilizotangazwa na vyombo vya habari hapa nchini kuwa "Papa kuomba radhi kwa kukandamiza din zingine". 

Katika habari hizo Waislamu wengi wameonyesha dhahiri kuwa malalamiko yao kwa muda mrefu kuwa wanabaguliwa makusudi kabisa ni kweli wala sio uchochezi kama vyombo vya dola, viongozi mbalimbali wa serikali na vyombo vya habari nchini vinavyodai. 

Katika habari hizo ilidaiwa kuwa kuanzia karne ya 13 (BK) ulianzishwa Baraza la Kanisa Katoliki lililojulikana kwa jina la "Iquisition" shughuli yake kubwa ikiwa kufanya upelelezi wa dini nyingine na kuwaadhibu vibaya mno. 

Kwa miaka yote hii Waislamu wameuawa, wameteswa, wamedhalilishwa, wamebaguliwa na kunyanyaswa maeneo muhimu, habari hizo zinadai kuwa ni kinyume na mafundisho ya Kikatoliki pia sio "upendo" inadaiwa kuwa mwaka 1908 Inquisition (mahakama ya Kikatoliki) hiyo ilibadilishwa jina na kuitwa "Ofisi takatifu" pamoja na kubadilishwa badilishwa majina lakini hufanya kazi kwao kumendelea kuwa kwa "mashaka" na kuleta "madhara" makubwa, gazeti hilo lilimalizia kuwa kuwataka "Wana Kanisa Wakatoliki wageuke mioyo yao na watubu wazi wazi!! 


Nzasa waomba msaada wa chakula, madawa

WANAKIJIJI wa Nzasa waliochomewa nyumba zao karibu miezi miwili iliyopita wamesema kuwa hivi sasa wanakabiliwa na tishio la njaa na magonjwa ya kuambukiza. 

Wakiongea na mwandishi wa habari hizi aliyefika katika makazi yao ya muda Alhamisi ya Novemba 12, mwaka huu baadhi ya wakazi hao wamesema kuwa eneo waliko hivi sasa ni katika bonde ambalo linatuama maji nyakati za mvua, hivyo wanahofia kupatwa na maradhi ya kuambukizwa. 

Vile vile wamesema kuwa tatizo jingine kubwa linalowakabili hivi sasa ni ukosefu wa chakula baada ya mashamba yao ya mihogo kufyekwa na kuzuiliwa kuchimba kwa ajili ya matumizi yao ya chakula. 

Wamewaomba watu binafsi na mashirika mbalimbali kuwapatia misaada ya chakula na madawa kipindi hiki ambacho serikali imewafanya wawe ombaomba katika nchi yao. 

Naye Mzee Rashid bin Hemed akiongea kwa masikitiko makubwa alimfahamisha mwandishi wa habari hizi kuwa siku nyumba zao zilipochomwa moto yeye hakuwepo nyumbani kwake na familia yake iliweza kuokoa vitu vichache tu na vingine kuteketea na moto zikiwemo fedha taslimu shilingi 332,000 ambazo familia yake haikuziona. 

Nao wanafunzi Furaha Ramadhani na Estropia Feruzi wanao soma katika shule ya msingi kijijini hapo wakiongea kwa niaba ya wenzao wamedai kuwa mahudhurio ya wanafunzi katika shule yao yamepungua kutokana na wanafunzi walio wengi kuwa wamechomewa sare zao katika operesheni iliyofanywa na serikali kijijini hapo. 

Wameitaka serikali kutoa fidia katika familia hizo ili kuwawezesha wenzao waweze kuhudhuria masomo kama kawaida. 


Katibu wa Bakwata Moro ang’olewa Msikitini
 
  • Adaiwa kuhujumu maendeleo ya Waislamu na Uislamu
Na Mussa Ally, Morogoro

KAIMU Katibu Mkuu wa Bakwata wilaya ya Morogoro, Bw. Mkambala ameng’olewa wadhifa wa Ukatibu wa Msikiti wa barabara ya Boma mjini hapa na waumini mwishoni mwa wiki. 

Katika uchaguzi uliofanyika kwenye Msikiti huo mkubwa mkoani Morogoro, Bw. Mkambala na kamati yake walibanwa na waumini hao hususan katika masuala ya uchumi, elimu na huduma za jamii za Kiislamu. 

Waumini hao waliulaumu uongozi wake kwa kuhujumu maendeleo ya Uislamu na Waislamu ikiwa ni pamoja na kuigeuza shule ya watoto wadogo Msikitini hapo kuwa nyumba ya kupangisha watu kwa maslahi binafsi. 

"Bwana Mkambala tunataka utueleze kwa kina juu ya dhuluma mliyowafanyia watoto wetu kwa kuigeuza shule yao kuwa nyumba ya kupanga pia utupe maelezo ya kukinaisha kuhusu nyumba za Wakfu za Msikiti huu ambazo waumini hawaoni matunda yake na mwisho utupe ripoti halisi na sahihi ya mapato na matumizi ya Msikiti tangu ulipoingia madarakani hadi sasa", alisema Bw. Amani Kasanga. 

"Ni aibu kwa Msikiti mkubwa kama huu kutokuwa na maendeleo yoyote ya maana", alisema mzee Salim Said Makelele wakati akiuliza swali uongozi uliomaliza muda wake. 

Wakionyesha uchungu wao, waumini waliomng’oa madarakani Bw. Mkambala na kamati yake na kuchagua uongozi mpya utakaowaongoza kwa kipindi kijacho cha miaka mitano. 

Waliochaguliwa ni Bw. Bene Omar Lukwele kama Katibu na wajumbe wananae wa kamati ya Msikiti. 

Wajumbe hao ni Bw. Salum Sudi Makelele, Ally Omar Ngalawa na Juma Yusuf. 

Wengine ni Aboubakar Ally, Rashid Othman, Nasoro Mbega, Hamis Sengo na Shaaban Viguro. 

Wakati Sheikh Mohamed Kairo anaendelea na nafasi yake ya uimamu. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
Maoni 
Kuwa na mawazo ya kufugwa tunajidharaulisha 

Sakata la mabucha  ya Nguruwe kuibuka upya 
Na Mwandishi Wetu  

Kondom sio kinga ya Ukimwi 

Bakwata yairushia polisi makombora Ngaramtoni 

MACHO YA SHUTUMA 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Serikali yatakiwa iwachukulie hatua wauaji 
Na Mwandishi Wetu 

Historia ya Msikiti wa Ngaramtoni 

Silaha yetu ni kura ya pamoja 
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC  U.S.A 

Anuani ya fikra 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Kuukaribisha mwezi mtukufu 

Tunahitaji "UN' ya Waislamu! 
Na Said  Rajab 

Kongamano la wanawake wa Kiislamu Newala lafana 

Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo - 2 
Na Ustaadh Kupa Pazi Said 

Kesi mojawapo ya mihadhara yafutwa 

Wasaidieni watoto wenye vipaji - Prof. Kilonzo 

Mahafali ya kidato cha nne Thaqafa: Wazazi wakumbushwa wajibu wao 

Wanafunzi Mwanza wadai haki za kuabudu mashuleni kwa usawa 
Na Iddi M. Katiba, Mwanza 

Saidianeni katika shida - Sheikh Abdallah 

Waislamu, Wakristo Rufiji watakiwa kuunda umoja 

Someni  muiokoe jamii kimaadili 

Acheni Shirki 

Kesi nyingine ya Waislamu Mwembechai yaahirishwa 
Na Muhibu Said 

Kusilimu kwa Wakristo kwaleta kero Mwanza 

Nzasa waomba msaada wa chakula, madawa 

Katibu wa Bakwata Moro ang'olewa Msikitini 

Masomo ya Dini ya Kiislamu  

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Umuhimu wa chakula katika shule za awali]  

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita