|
|
|
KATIKA makala iliyotangulia, nilizungumzia unyonge unaotukuta Waislamu, katika kupuuzwa, kudharauliwa na kunyanyaswa na vyombo vyetu wenyewe vya vyama na serikali nchini mwetu. Pia nikasisitiza umuhimu wa kutafuta kwanza na kushika barabara Ufalme wa kisiasa, ili tuweze kwa uhakika kulinda, kukuza na kuimarisha maslahi yetu bila ya kukiuka maadili ya Uislamu kwa kuwadhalilisha wananchi wenzetu wasiokuwa Waislamu. Waislamu tuna bahati nzuri kubwa sana ya kuwa na mwanga (sio mwenge) katika Qur’an na Sunnah. Kama tungezingatia mwanga huu, haya yote yanayotukabili hii leo yasingekuwepo. Tunaambiwa katika Suratul-Al-Imraan, aya ya 103 "Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote, wala msiachane, na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu, mlikuwa maadui, naye akaziunganisha nyoyo zenu, hivyo mkawa ndugu, na mlikuwa ukingoni wa shimo la jahanamu, naye akakukoeni nalo. Nanma hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni aya zake ili mpate kuongoka". Tumeagizwa Waislamu kupendana, kuhurumiana, kushirikiana, kulindana, kusaidiana na mengi yaliyo mazuri na mema. Na huo ndio msingi wa kuwa kila Muislamu ni ndugu wa Muislamu mwenzake. Tukihimizana na kuyafuata hayo, kwa haki Lillah, haitakuwa kazi nzito kwetu kuupata ufalme wa kisiasa. Waislamu hatuna haja ya chama (kwanza wala hakitaandikishwa na wahusika). Uislamu wenyewe ni chama tosha. Hatuna haja ya kadi (La illah il Allah, Muhammad rasul Allah), inatosha kuwa kadi yetu. Hatuna haja ya michango ya kila mwezi, sadaka zetu zinatosha kuwa michango yetu ya kila siku. Hatuna haja ya nyumba kumi kumi, Misikiti yetu inatosha kuwa matawi yetu. Hatuna haja ya mikutano ya hadhara Jangwani wala kule kidongo chekundu au Mnazi Mmoja (hatutapewa vibali), mikutano yetu mitano ya kila siku na mkutano wetu mkubwa wa kila Ijumaa, tuliyopangiwa na Mwenyezi Mungu (s.w) inatutosha. Hiki si chama, hii ni Dini yetu. Kuitangaza ni wajibu wetu, kuipenda, kuifuata na kuitekeleza ni lazima kwetu. Kupata maslahi ya Waislamu na Uislamu wenyewe ni haki yetu. Hatuiombi wala hatumwombi mtu radhi kuwa na haki hiyo. Katika hali hii tuliyonayo leo, ngao yetu ni umoja wetu na silaha yetu ni kura ya pamoja (block vote), katika kila uchaguzi. Iwe ni uchaguzi wa wajumbe wa nyumba kumi kumi, wa kata, wa tawi, wa madiwani, wa taasisi, wa chama, wa wabunge mpaka ule wa Rais. Hatumchagui mtu kwa kuwa ana jina la Kiislamu, la hasha. Lazima tunahikishe kuwa anatuthamini, anatuheshimu, anatulindia maslahi ya Waislamu na Uislamu wenyewe. Waislamu wachangamkie uanachama na uongozi wa vyama vyote vya siasa, tusingojee kupewa, tuchukuwe! Katika hali hiyo, tutaacha kupuuzwa na Insh-Allah, Ufalme wa kisiasa tutautia mikononi mwetu na dhima ya kuomba omba itatutoka. Viongozi wa serikali yetu, waliokalia viti vya dola kwa kura zetu ni watumishi wetu. Sioni sababu ya kwenda kuwaomba, huku mikono yetu iko nyuma, eti watufanyie hiki au kile. Hao tunawatuma tu watufanyie tunayowachagulia watufanyie. Kama wanaonyesha jeuri, basi kazi yetu inakuwa moja tu, kuwatoa katika viti vya dola yetu. Kinachohitajika katika kutimiza hayo ni uongozi bora na wafuasi bora walioshiba Uislamu kikweli kweli. Na kuushiba Uislamu ni jukumu na wajibu wa kila mmoja wetu. Hapa panahitajika kumwogopa na kumtii Mwenyezi Mungu (s.a.w) na Mtume wake Muhammad (s.a.w.). Kwa maneno mengine, tunahitajika kupigana jihadi kubwa, kila mmoja wetu na nafsi yake mwenyewe kwanza. Viongozi wa Uislamu na wale wa Kiislamu, ili kufanikisha, lazima wajizatiti na kuwa majasiri. Na kuwa pamoja katika malengo yao na uongozi wao. Ni muhimu kwao kuondoa matatizo yao ya kibinafsi ndani ya Misikiti yao na majumba yao kwa faragha, hekima na taadhima. Kinyume cha hayo, watakuwa viongozi bandia wasiokomaa vichwani mwao na hivyo watakuwa wameshindwa kuonyesha sifa za uongozi wa Uislamu na waumini wake. Na wafuasi wa Kiislamu na Uislamu wanatakiwa kuwa na sifa na tabia hizo hizo. Katika harakati za kujitafutia Ufalme wa kisiasa, lazima kuna matatizo yatakayojitokeza. Yale tunayoyategemea ni lazima tuyazungumze kabla ya kujitokeza kwake. Linalokuja haraka akili ni lile la Waislamu wasaliti (ndumilakuwili), waoga (watetea matumbo na vyeo vyao), wanafiki (akina popo hao) na wale waliochanganyikiwa (hawajui wayafanyayo). Hao hatuna haja ya kuwapiga pande na kuwasusa. Tuukumbuke mfano wa Sayidna Omar, huenda katika hao pakapatikana askari wazuri wa Uislamu. Chuki, husda, visasi, kukomoana na choyo kamwe havitatusaidia. Tujifunze kuvumiliana, kusameheana, kufundishana na kuaminiana. Lipo pia tatizo la huyu Suni, yule Maliki na wale hivi na hao vile. Tujiulize kwanza, Mtume wetu mpendwa alikuwa kundi gani katika makundi hayo? Aliye bora kati yetu ni yule amchae Mwenyezi Mungu (s.w) na hakuna kati yetu anayemjua au anayejijua. Kwa hiyo tusipoteze malengo yetu katika kushughulikia yaliyokuwa juu ya uwezo wetu. Kazi yetu kubwa ni kujiombea nafsi zetu wenyewe na kuombeana kati yetu. Kukosoana ni wajibu, lakini tunawajibika kuwa na hekima na taadhima, siyo kudharauliana, kukebehiana. Itakuwa tunalikataa lipi na tunalifanya lipi. Mbali ya hayo na mengine kama hayo, kuna suala la Misikiti. Sheikh au Imamu wa Msikiti huu hasemi na Sheikh wa Msikiti ule. Mimi Msikiti wangu ule, si swali Msikiti huu na yanayofanana na hayo, wallahi, mimi bado sijajua vigezo kama hivi vinatoka wapi. Mambo kama hayo tunahitajika kujihadhari nayo sana, ndiyo yanayochangia kutuletea unyonge huu tulionao hivi sasa. Ili kujikomboa tujiepushe nayo. Viongozi wa Misikiti, Madrasa, taasisi na vyombo vingine vya Kiislamu
kama vile Baraza Kuu, Tabligh, Warsha, Ansaar kwa mfano, lzima vijishughulishe
katika ngazi kuanzia mashina, kata, matawi, wilaya, mikoa na kitaifa. Na
katika ngazi zote hizo kuwepo chombo kinachowawakilisha wote katika mfumo
wa "United Front" au "Coalition" ya namna moja au nyingine. Kupitia umoja
huo, uamuzi ukitamkwa unakuwa wa sauti moja kwa vile kila chombo kina uwakilisho
katika hiyo "United Front" au "Coalition" inayohusika. Nadhani sote tunaelewa
kuwa Roma haikujengwa siku moja. Hebu tujaribu katika uchaguzi unaokuja
mwaka 2000. Tukipata mafanikio hata kidogo tu, kazi yetu inabakia pale
pale kutumia akili zetu. Daima mbele, nyuma katu. Tumedhalilishwa vya kutosha,
tumetumiwa vya kutosha, lazima sasa tuseme sasa basi.
|
YALIYOMO
Maoni Kuwa na mawazo ya kufugwa tunajidharaulisha Sakata la
mabucha ya Nguruwe kuibuka upya
Bakwata yairushia polisi makombora Ngaramtoni MACHO YA
SHUTUMA
Serikali
yatakiwa iwachukulie hatua wauaji
Historia ya Msikiti wa Ngaramtoni Silaha yetu
ni kura ya pamoja
Anuani
ya fikra
Tunahitaji
"UN' ya Waislamu!
Kongamano la wanawake wa Kiislamu Newala lafana Umuhimu
wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo - 2
Kesi mojawapo ya mihadhara yafutwa Wasaidieni watoto wenye vipaji - Prof. Kilonzo Mahafali ya kidato cha nne Thaqafa: Wazazi wakumbushwa wajibu wao Wanafunzi
Mwanza wadai haki za kuabudu mashuleni kwa usawa
Saidianeni katika shida - Sheikh Abdallah Waislamu, Wakristo Rufiji watakiwa kuunda umoja Someni muiokoe jamii kimaadili Kesi
nyingine ya Waislamu Mwembechai yaahirishwa
Kusilimu kwa Wakristo kwaleta kero Mwanza Nzasa waomba msaada wa chakula, madawa Katibu wa Bakwata Moro ang'olewa Msikitini Chakula
na lishe
|