|
Na.175 Rajab 1419, Novemba 13 - 19, 1998 |
|
NI nani anaeweza kuitwa kiongozi wa Waislamu katika Tanzania. Je, ni yule ambaye anatambulikana na dola kama kiongozi wa Waislamu, akakumbatiwa na viongozi wa dola na chama tawala, akapewa fursa katika magazeti na radio, akakaribishwa katika dhifa na sherehe za serikali. Ni nani kiongozi wa Waislamu, Je ni yule anayealikwa kwa jina la Uislamu kula na kunywa katika nyumba za viongozi na akapigwa picha nao; na picha hizo zikatawanywa katika magazeti siku ya pili yake. Je ni nani kiongozi wa Waislamu, je ni yule ambae hotuba zake hupeperushwa hewani moja kwa moja au ni yule ambaye yupo mbali na haya yote, akiutumikia Uislamu kimya, kimya huku akikutwa na kila masahibu yamkutayo kiongozi wa kweli wa Waislamu katika historia ya Waislamu wa Tanganyika. Je uongozi maana yake ni kujikurubisha kwa wafalme na kujinufaisha binafsi. Kiongozi wa kweli wa Waislamu hana fursa ya radio wala magazeti, haalikwi kwenye dhifa wala nyumbani kwa wakubwa. Hawa kwao wao uongozi ni jukumu la kumtumikia Allah (s.w.) pekee. Marehemu Abbas Kilima ni katika viongozi hawa. Hakupewa fursa katika radio au gazeti. Abbas Kilima hata siku moja hakupata kufanya kampeni ya kuomba uongozi. Waislamu wenyewe kwa ridhaa yao ndiyo siku zote walikuwa wakimtwisha mzigo huo. Na yeye aliwatumikia Waislamu na Uislamu si kwa jingine ila katika kutafuta radhi za Allah. Hakuwa na shauku, maneno yake yaandikwe gazetini au sauti yake isikike radioni kiasi kwamba kwake yeye utumishi kwa Waislamu ilikuwa hata kufanya kazi ambazo wengi wanaziona dhalili, kama kuwatengea watu chakula. Ukitaka ukweli ya haya angalia mwendo wa marehemu hadi umauti ulipomfika. Sheikh Abbas Shaaban Kilima alizaliwa huko Tabora Mtaa wa Usagara Mwezi 26 Rajab, 1358 H sawa na tarehe 29 Septemba, 1938. Ndoa yake ya kwanza ilikuwa mwaka 1958. Miaka 40 baadae amefariki siku moja yeye na mkewe huyo Rukia binti Fundi. Alipata elimu yake ya msingi katika Shule za Town School (Tabora mjini) na Mwanhala (Nzega). Wakati elimu ya msingi ya Uislamu aliipata katika chuo kilichoitwa Anjuman Muslim School cha Sheikh Ali Abeid. Baadaye alijiunga na Tabora Boys na kisha shule ya Ufundi Ifunda. Baada ya kujiunga na Shirika la Reli la Afrika Mashariki alihudhuria kozi mbalimbali hadi kupata Stashahada ya Uhandisi wa Mashine (Mechanical Engineering). Vituo vyake vikuu vya kazi akiwa katika Shirika la Reli vilikuwa Dar es Salaam, Nairobi, Voi na Nakuru. Hadi anaacha kazi alikuwa Senior Mechanical Inspector. Marehemu Abbas Kilima alikuwa ni mmoja wapo katika wana Warsha ya waandishi wa Kiislamu (Muslim Writers Workshop). Hapa si mahali pake kueleza umuhimu wa Warsha katika harakati za kuuhusisha Uislamu Tanzania. Kipaji cha uongozi wa Abbas Kilima kilianza kuonekana mwaka 1981 kwakati Warsha kupitia utafiti walioufanya na wana taaluma ya elimu walipowatanabaisha Waislamu na Serikali kuwa kuna njama dhidi ya Waislamu ndani ya Wizara ya Elimu, njama ambayo ilikuwa ikiendeshwa kwa makusudi kuwanyima nafasi za elimu vijana wa Kiislamu. "Hoja ya Kuchunguza Dhulma dhidi ya Waislamu wa Tanzania Katika Elimu ya Juu", 18 Julai, 1991. Warsha ilisambaza matokeo ya utafiti huu kwa Waislamu wote wa Tanzania Bara na Visiwani. Utafiti uliofanywa Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa ukionyesha kuwa ingawa wakazi wengi wa Dar es Salaam ni Waislamu kufikia asilimia 67 na idadi ya wanafunzi katika shule za msingi wengi ni Waislamu, idadi hiyo haijionyeshi katika uwiano na Wakristo katika uchaguzi wa kuingia kidato cha kwanza. Uchunguzi ulionyesha jinsi idadi ya wanafunzi Waislamu ilivyokuwa ikipunguka kadri hadi kufikia chuo kikuu. Uchunguzi ulidhihirisha kuwa kulikuwa na njama mahsusi ya kuwadhulumu Waislamu. Wizara ya Elimu ilikuwa ikikiuka maadili ya taifa ya kutobaguana kwa misingi ya dini. Serikali ilishtushwa sana na taarifa ile na ikataka kujua kwa uhakika ni akina nani hasa waliofanya uchunguzi ule. WARSHA iliamua kuchukua hatua mbili kwa pamoja. Kwanza iliamua kuwatahadharisha Waislamu pamoja na Serikali kuhusu ugunduzi huo; na pili WARSHA ilianza bidii ya kuzibadili shule zilizokuwa mikononi mwa BAKWATA kuwa seminari za Kiislamu. Kufuata hatua hii ikaamuliwa pia shule hizo kuanzia hapo ziwe mahsusi kwa ajili ya vijana wa Kiislamu na ziendeshwe katika misingi ya Kiislamu. Utafiti huu ulikuwa unatishia umoja wa taifa. Kuwepo na kundi la waumini wa dini moja katika wizara ya serikali wakifanya maamuzi kwa ajili ya faida ya Imani zao ilikuwa jambo la hatari sana. Bila kutangazwa wazi Serikali iliamua kwanza wasakwe ijulikane Warsha ni nani na wote waliofanya utafiti ule; na pili shule hizo za Kiislamu zilizobadilishwa kuwa seminari zifutwe na kurejeshwa katika hali yake ya awali. Katika kadhia hii Mwenyezi Mungu alitoa mtihani wa kupambana na viongozi wanaojilazimisha uongozi wa Uislamu kwa manufaa yao na wale wanaoshughulikia manufaa ya Uislamu kwa kutaka radhi za Allah. Tuanzie hapa katika kumkumbuka marehemu Abbas Kilima. Uongozi wa BAKWATA ulikubali kutii amri ya kuvunja seminari za Kiislamu na kuwavua mabinti hijab zao. Wazazi wa Kiislamu mmoja wapo akiwa Abbas Kilima alipinga kitendo cha kuirejesha shule ya Kinondoni katika hali yake ya zamani. Kamati iliundwa ili ishughulikie tatizo hilo. Abbas Kilima alichaguliwa kuwa mmoja wa wana kamati ya wazazi wa shule ya Kinondoni. Abbas Kilima ingawa wengi hawakuwa wanalijua hilo alikuwa ni mmoja wa viongozi wa Warsha waliofanya uamuzi wa kufanya utafiti kuhusu kupunjika kwa elimu kwa vijana wa Kiislamu. Kwa hiyo basi kuwa na mwana kamati kama yeye katika kamati ile ya wazazi ilikuwa imempata mtu mjuzi wa hila na njama za Serikali. Uongozi wa BAKWATA katika kutii amri ya Serikali ilianzisha kampeni dhidi ya Warsha waliokuwa ndani ya BAKWATA. Serikali ikaweka vyombo vya habari wazi kwa BAKWATA kueneza propaganda dhidi ya Waislamu waliokuwa wakitaka haki itendeke katika utoaji wa elimu. Abbas Kilima na kamati yake waliitwa Wizara ya Mambo ya Ndani mara kadhaa kuhusu shule ya Kinondoni. Mambo yaliyokuwa yakielezwa huko yangeli mtisha mtu yeyote yule na kumfanya aache kabisa kuwashughulikia Waislamu. Kwa ustadi mkubwa sana Abbas Kilima alihakikisha Waislamu wa nchi nzima wanafahamishwa kila kauli ya serikali kuhusu wao. Msimamo wa Abbas Kilima ulikuwa kuwa uamuzi wa hatima ya shule ya Kinondoni utatolewa na Waislamu wenyewe na BAKWATA hawana haki ya kuwavulia Waislamu mipango yao ya maendeleo na kuwavua mabinti zao vazi lao la stara. Serikali ikajikuta ina wakati mgumu sana kujieleza kwa umma wa Kiislamu kuwa ilikuwa ikifanya haki na kwa maslahi ya taifa na siyo kwa maslahi ya kanisa. Baada ya kuvutana kwa muda mrefu na muafaka kushindwa kupatikana nyuma ya milango ya siri katika Wizara ya Mambo ya Ndani, Abbas Kilima na wenzake waliamua kuitisha mkutano shule ya Kinondoni na ili Waislamu wapewe taarifa na wajadili hatua itakayofuatia katika kupambana na udhalimu. Bwana Abbas kwa masikitiko makubwa alipata kuhadithia kuwa, siku kabla ya mkutano ule muhimu serikali ikatoa tangazo la vitisho lililosomwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Radio Tanzania, David Wakati, kuwa mkutano wa Waislamu katika shule ya Kinondoni si halali na yeyote atakayehudhuria atachukuliwa hatua za kisheria. Serikali haikukomea hapo walituma kikosi cha askari kutoka kituo cha polisi cha Oysterbay kuja kuhakikisha kuwa Waislamu hawakutani kujadili matatizo ya elimu ya vijana wao. Abbas Kilima hakutishwa na tangazo hili na siku ya pili alifika kuwatumikia Waislamu kama ada yake. Halikadhalika Waislamu walifika shule ya Kinondoni kuitika mwito bila ya kuhofu serikali na tangazo lake. Waislamu waliamua kufanya mkutano litakalotokea na litokee. Kamanda wa kikosi cha askari alikuwa kijana wa Kiislamu, aliwasihi sana Waislamu kwa maneno mazuri kuwa wasifanye ule mkutano pale. Abbas Kilima aliwashauri Waislamu wafanye shura ili upatikane uamuzi wa nini la kufanya. Waislamu wapambane na askari au waepushe shari. Na hii ndiyo ilikuwa sifa kubwa ya marehemu, alikuwa kiongozi mwenye busara sana. Hakuwa kiongozi aliyefurahishwa na mafanikio ya haraka haraka. Wala hakuwa kiongozi atakaesusa iwapo kutakuwa na kikwazo katika uongozi wake. Shura iliamua Waislamu watawanyike kwa amani. Abbas Kilima alijua kuwa siku ile pale shule ya Kinondoni Waislamu walikuwa wamefikishwa kwenye sulhu ya Hudaibbiya. Hiki ndicho kile kipindi ambacho serikali ilijitokeza waziwazi na kufanya mabadiliko ya uongozi katika BAKWATA katika mkutano uliofanyika Chuo Cha Ardhi, Dar es Salaam. Serikali bila shaka ilifurahi kuwa imewashinda Waislamu, lakini je ni kweli ilikuwa ameshinda? Miaka kumi baadae Abbas Kilima ndiye atakaekuwa na kicheko cha mwisho. Atakuwa amesaidia kuwavusha Waislamu katika maji marefu sana na kuanzia hapo historia ya Waislamu wa Tanzania itakuwa nyingine. Watakuwa na nguvu na ari ya kupambana na chochote. Insha Allah tutahadithia kipindi hicho cha kihistoria baadae. Marehemu Abbas Kilima ni katika mmoja wapo wa watu walioshughulika sana katika kuzifichua njama dhidi ya Waislamu kwa kufanya kazi kimya na kuelimisha. Mkakati uliofuatia ulikuwa ni kuwaamsha Waislamu popote walipo ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kuhusu dhulma inayowakabili Waislamu wa Tanzania. Katika hili Abbas Kilima alishiriki kikamilifu. Alikuwa ni amiri jeshi aliyeamini kuwa vita ili vifanikiwe vinahitaji maandalizi ya silaha kali na mikakati. Kwa kipindi cha takriban miaka kumi kuanzia sakata ya seminari za Kiislamu Abbas Kilima alijitupa katika kuutumikia Uislamu akifanya kazi zake kimya kimya. Waislamu walikuwa wamejifunza somo muhimu sana. Waliamua kuanzisha seminari zao hata kama serikali itakuwa haitaki. Mantiki yenyewe ilikuwa ni kuwa haiyumkiniki na ni muhali hasa kwa Muislamu kutaka idhini kwa yeyote ya kumtumikia Allah. Ujumbe huu ulisambazwa kwa Waislamu wa nchi nzima na ukaeleweka. Semina nyingi zilifanyika kusambaza ujumbe huu na Abbas Kilima akishiriki. Waislamu walihamasika na vikundi vingi vya kusaidia Waislamu vilianzishwa. Kufikia mwaka wa 1990 viongozi waliokuwa wanajiita viongozi wa Waislamu wakawa kama vile hawapo. Waislamu wakijifanyia mambo yao kwa ufanisi ambao haukuwepo hapo zamani. Katika Baraza la Idd Ukumbi wa Arnautoglo, Dar es Salaam tarehe 17 Aprili, 1991 BAKWATA ilitoa hotuba ya kulaumu serikali kwa kuwaachia Waislamu wafanye mambo yao wenyewe nje ya BAKWATA. Haya yalisemwa mbele ya mgeni wa heshima, Rais Ali Hassan Mwinyi. Jibu la Mwinyi lilikuwa BAKWATA zungumzeni na Waislamu. Mwaka wa 1991 utakumbukwa katika historia ya harakati za Waislamu katika kupambana na dhulma. Hali ya Waislamu katika ufahamu ilikuwa nzuri sana. Waislamu walikuwa wameshatambua kuwa serikali yao haikuwa ya kisekula kama ilivyokuwa ikidai. Waislamu walikuwa wameunda taasisi nyingi, nyingine zilikuwa na usajili na nyingine hazikuona haja wala umuhimu wa kufanya hivyo. Wakati ulikuwa umefika sasa wa kufanya mapinduzi makubwa katika uongozi wa Waislamu wa Tanzania, kung’oa wanaojiita viongozi wa Waislamu ndani ya BAKWATA na kuweka viongozi wa kweli wa Waislamu. Harakati za Kiislamu zilikuwa zikisikika kila mahali. Katika mwezi Julai na Septemba, 1991 baadhi ya viongozi wa Waislamu kutoka kamati maalum iliyoundwa kufuatia kikao cha baadhi ya taasisi zilizoko jijini Dar es Salaam walitembelea mikoa ya Tanzania kukutana na Waislamu. Madhumuni yakiwa ni kwanza kupata ridhaa yao na kuwaalika Dar es Salaam katika mkutano wa kitaifa wa Waislamu kujadili matatizo ya uongozi katika BAKWATA ili chombo hicho kimtumikie Allah kama kilivyoazimiwa. Mmoja wa wana kamati iliyopita mikoani kuwatembelea Waislamu kuwaalika kuja kuijadili BAKWATA alikuwa Abbas Kilima. Tarehe 15 Septemba, 1991 mkutano wa Kitaifa wa Waislamu wa Tanzania (National Muslim Conference) ulifanyika Ukumbi wa Nkrumah Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Serikali haikuwa na nguvu ya kuwazuia Waislamu kufanya mkutano kama walivyowaonea wakati wa sakata ya shule ya Kinondoni. Sauti ya umma wa Kiislamu ilikuwa kubwa. Serikali ilimtuma aliyekuwa Waziri Mdogo wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Abdulrahman Kinana aje aufungue mkutano ule. Kinana alileta ujumbe kwa Waislamu kuwa serikali ipo tayari kushirikiana nao katika kutatua matatizo yanayowakabili. Wengi hawakuwa wanafahamu mchango wa marehemu. Ilikuwa ni safari ndefu kutoka siku ile Abbas Kilima alipoongoza shura pale shule ya Kinondoni na kuwaomba Waislamu wasipambane na serikali bali watawanyike kwa amani. Abbas Kilima hakuwa mtu wa kujikweza, katika mkutano ule yeye alikuwa pembeni akitumika katika kamati mbali mbali za mapokezi ya wajumbe na chakula. Ni vigumu kwa mtu aliyekuwa hamfahamu kuamini kuwa mtu yule anaonekana wa kawaida sana ndiye mmoja katika vichwa nyuma ya ufanisi wa hadhara ile. Katika historia ya harakati za Kiislamu hapajatokea kwa wakati mmoja viongozi wa kweli wa Waislamu kukutana mahali pamoja kama vile. Mkutano ule uliamua kuwa katiba ya BAKWATA ipitiwe upya kwa ajili ya marekebisho na jina jipya kwa ajili ya umoja wa Waislamu litafutwe. Haya yalikuwa maamuzi ya kihistoria toka Waislamu walipovunjiwa umoja wao wa EAMWS na Serikali ya Nyerere mwaka 1968. Msomaji na aunganishe hapa na ile sulhu iliyopitishwa shule ya Kinondoni na Abbas Kilima, iliyoamua Waislamu wasipambane. Kwa hakika haihitaji akili nyingi sana kutambua busara ya uamuzi ule na matunda yaliyopatikana baadae. BAKWATA ilikataa kuitika mwito wa Waislamu waliokutana Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, ikaendelea kung’ang’ania madaraka. Kilichofuatia yalikuwa ni mapinduzi. Tarehe 4 Januari, 1992 mkutano mwingine wa Kitaifa wa Kiislamu ulifanyika Ukumbi wa Diamond. Wakiwa katikati ya mkutano ghafla mkutano ulisimamishwa na wajumbe wakapewa taarifa kuwa wakati mkutano ukiendelea Waislamu wamefanya mapinduzi na kupindua uongozi kibaraka wa BAKWATA kwa kuteka makao makuu, ofisi ya mkoa na shule ya Al Haramain. Ni wachache katika Waislamu wenye kufahamu mchango wa Abbas Kilima katika haya yote. Na ni wachache wenye kujua maamuzi haya yalipelekea matokeo gani katika harakati za Waislamu kudai haki zao kuanzia mwaka 1992. Waislamu walikuwa sasa wamejifunza nguvu za Ukristo ndani ya Serikali na uwezo wake. Ni lipi wanaweza kulifanya kupambana na Waislamu na ni lipi linawatia hofu. Serikali iliamua kukaa uso kwa uso na viongozi wa kweli wa Waislamu. Kwa muda serikali ilibidi ijitenge na BAKWATA. Kwa mara ya kwanza serikali iliamua kuzungumza na viongozi wa kweli wa Waislamu. Katika mambo ambayo viongozi wa Waislamu waliyoomba serikali isaidie ni kutaka Wizara ya Mambo ya Ndani na Msajili wa Vyama (Registrar of Societies) watoe ushirikiano ili mabadiliko katika uongozi wa BAKWATA yafanyike bila vurugu. Kilichomdhihirikia Abbas Kilima ni kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani na Msajili wote walikataa kutoa ushirikiano na badala yake kuikumbatia BAKWATA ambayo Waislamu walikuwa wanataka kuifanyia mabadiliko. Kwa kuwa Waislamu walikuwa na uongozi thabiti na watu waliojitolea kumtumikia Allah kama Abbas Kilima, akifanya kazi kwa kutaka radhi zake, Mwenyezi Mungu alitia taufiki katika mambo yake. Tetesi zilikuwa zikisikika kuwa serikali inashangazwa na ufanisi wa hali ya juu wa mambo ya Waislamu katika kuendesha mijadala na serikali hata kufikia kusema kuwa hawa si Waislamu kwani Waislamu tunawafahamu. Hawa si wao bali wanatumiwa. Kutokana na ukaidi wa BAKWATA kutaka uongozi wa Waislamu kwa nguvu bila ridhaa yao na kutokana na serikali kuipa nguvu BAKWATA. Abbas Kilima alipewa jukumu la kushughulikia tasjila ya Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu. Serikali ilikalia usajili wa Jumuia hii kwa mwaka mzima na katika kutaka kuihuisha BAKWATA, tarehe 28 Aprili, 1993 Waziri wa Mambo ya Ndani aliitisha mkutano wa BAKWATA na Kanisa. Katika mkutano ule Kanisa lilijitolea kutoa fedha kuipa BAKWATA ili iweze kujikimu, ifanye uchaguzi na iendelee kuwepo madarakani kama kiongozi wa Waislamu. Hiki kilikuwa kipindi kigumu sana kwa Ab bas Kilima. Baadhi ya Waislamu walitafsiri hatua ile kama ni tangazo la vita dhidi ya Waislamu. Ilikuwepo fikra kwa baadhi ya Waislamu kuwa njia pekee ya Waislamu kupata haki zao kuanzia taswira ya Jumuia yao dhidi ya BAKWATA ni mapambano ya ana kwa ana yaani civil disobedience. Abbas Kilima alikuwa na muda mgumu sana kuwatuliza Waislamu wa Dar es Salaam na mikoani waliokuwa na fikra hizo. Si wengi wanaojua kuwa damu ingelimwagika siku nyingi sana hata kabla ya Mwembe Chai. Inasemekana ni kwa kuhofu jaribio hilo ndipo serikali ikaja kutoa usajili wa Baraza Kuu kwa ghafla. Katika utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi ndani ya Bunge la Muungano kilizuka kikundi cha Wabunge kilichokuwa kikipinga Zanzibar kujiunga na Organisation of Islamic Conference (OIC). Kikundi hiki kikisaidiwa na vyombo vya habari pamoja na vile vya serikali na CCM ilisimama kidete kutaka kuvunja katiba. Pamoja na kujiunga na OIC ilidaiwa kuwa ilikuwapo halikadhalika njama kupitia Islamu in Africa Organisation (IAO) kuupiga vita Ukristo Tanzania. Nusra ya rais na mustakbali wa Uislamu Tanzania ulitegemea sana jinsi uongozi wa Waislamu utakavyojibu mapigo ndani ya Bunge. Abbas Kilima alishughulika sana katika kipindi hiki kwa kutayarisha mswada wa Waislamu kwa Spika wa Bunge kuhusu OIC. Mswada ambao ulitayarishwa kitaalamu kiasi kuwa Mwenyekiti wa Baraza Kuu, Sheikh Salum Khamis aliitwa na Kamati ya Bunge ya Katiba aje aeleze masimamo wa Waislamu. Mbele ya Kamati ya Bunge ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Philip Marmo, kwa mara ya kwanza Bunge lilizungumza na viongozi wa kweli wa Waislamu. Huu ulikuwa ushindi mkubwa. Bunge lilitambua ukweli kuwa uongozi wa Waislamu hauko BAKWATA bali kwa viongozi kama Abbas Kilima. Si wengi waliokuwa wanajua mchango wa Abbas Kilima katika kuwatafutia nusra Waislamu wa leo na hao watakaokuja baadae katika Tanzania. Waislamu watakikumbuka kipindi hiki kwa ile mikutano mingi na iliyokuwa ikihudhuriwa na Waislamu toka kila pembe ya Dar es Salaam na bila shaka wana kumbukumbu nzuri sana ya marehemu akiwa anatoa taarifa jinsi Baraza Kuu lilivyokuwa likishughulikia mambo kama haya. Hiki ni kipindi ambacho hisia za kidini zilikuwa juu sana. Katika hijja ya mwaka huu Abbas Kilima akiwa mmoja wa wanakamati ya Tanzania Muslim Haj Trust aliweza kushirikiana na Waislamu wengine kuifanya hija ichukue sura mpya kabisa. Kuanzia mwaka 1990 Waislamu walikuwa wamefikwa na madhila mengi na halikadhalika walikuwa wamepiga hatua kubwa ya maendeleo. Kuwekwa ndani viongozi wa kweli wa Waislamu, kufungwa na mauaji ya Mwembe Chai kulikuwa kumewakomaza Waislamu. Ilionekana kuwa litakuwa jambo jema kama Waislamu waliotoka sehemu tofauti za Tanzania watakuwa na darsa baada ya sala ya Fajr ili waelimishane kuhusu madhila hayo, kuangalia walikotoka, kupeana majukumu na kuweka mikakati ya baadae. Abbas Kilima aliwahamasisha sana vijana hasa wale waliokuwa masomoni Saudi Arabia kuhusu hali ya Uislamu Tanzania. Darsa hizi zilifana sana na ikaazimiwa kuwa kila mwaka iwekwe ratiba kama hii. Kila dhila lililowakuta Waislamu, marehemu alishughulikia, kuanzia seminari za Kiislamu, kuchanwa Qur’an Buzuruga, kuvamiwa kwa msikiti wa Kiwanja cha Ndege Morogoro, kesi za bucha ya nguruwe, OIC, kusajili Baraza Kuu, Mwembe Chai, semina na kongamano za Waislamu, mihadhara; kwa hakika maisha ya Abbas Kilima yanakwenda sambamba na harakati za Uislamu katika Tanzania. Ni vigumu sana katika Taa’zia kuweza kumweleza marehemu Abbas Kilima ukammaliza. Uongozi wake ni mfano wa kuigwa. Hakudai ukubwa kwa Waislamu. Marehemu Abbas alikuwa hana muda wa kukaa kupanga ajitafutie cheo. Siku zote yeye aliona ni mtumishi wa Waislamu. Waislamu walilitambua hilo na kila ikiwepo kazi basi utasikia, mpeni Abbas Kilima. Wale wake ambao waume zao walikuwa jela kwa ajili ya Uislamu watamkumbuka marehemu kwa juhudi zake za kuwatembelea na kuwafariji katika kipindi kile cha mashaka. Wakati mwingine ni vigumu hata kujua ni wakati gani alikuwa akifanya kazi zake za kupata rizki na ni wakati gani alikuwa akiwatumikia Waislamu. Wakati wa hija alikuwa yeye mstari wa mbele kuwahudumia mahujaj kwa kila jambo. Wakati wa chakula utamwona yupo amebeba sahani anagawa. Huu ndio mfano wa kiongozi. Upo uhakika kuwa wakati wanahistoria watapoandika historia ya harakati za Waislamu dhidi ya dhulma kama zilivyojitokeza katika Tanzania, hawataacha kuinukuu barua yake aliyowapelekea wabunge pale Waziri wa Mambo ya Sheria na Katiba wakati ule Samuel Sitta alipotaka kupeleka Bungeni muswada wa kupiga marufuku mihadhara. Katika barua hiyo Abbas Kilima alisema kuwa mafundisho ya Uislamu na Ukristo yanapingana kwa kila hali. Katika Ukristo kuamini kuwa Yesu Kristo ni Mungu au mtoto wake Mungu, alikufa msalabani, katika Uislamu kuamini hivyo ni kufru. Kupitisha sheria kama hiyo ni kuwazuia Waislamu kumtakasa Allah. Kupitisha sheria kama hiyo ni kinyume cha katiba kwani sheria itakuwa inaulinda Ukristo. (Abbas S. Kilima to Members of Parliament, BK 1.5/39/94 20 Augusti, 1994). Barua ile iliwatisha Wabunge, wakaona ukweli uliokuwa katika barua ile na shida itakayokuwa mbele yao. Mswada ule hadi Samuel Sitta anatoka Wizara ya Sheria haukuwasilishwa Bungeni. Itakuwa kazi kubwa sana kumpata mtu wa kujaza pengo aliloacha Abbas Kilima. Kwani nafasi yake haikuwa ya kupata ukubwa na starehe za dhifa. Nafasi yake ilikuwa nafasi ngumu ya utumishi kwa Allah, iliyojaa kila aina ya shida. Haiwezekani kamwe kiongozi wa kweli akautumikia Uislamu na akapendeza machoni mwa wale wanaoupinga Uislamu. Haiwezekani malipo ya kumtumikia Allah yawe mialiko ya kula na kunywa meza moja na wale wanaompinga Allah. Ni muhali kumtumikia Allah na malipo yake yakawa dhifa na kushehenezwa na mapicha magazetini na hotuba kurushwa maredioni. Anaemtumikia Allah malipo yake si dhifa za kula na kunywa na wakubwa, malipo yake hapa duniani ni vitisho, dhiki, na mateso ya kila aina. Faraja kubwa aliyokuwanayo marehemu Abbas Kilima ni kule kutambua kuwa Allah alimwepusha na fedheha hii na alikuwa akijua kuwa alilokuwa akifanya ni kwa maslahi ya Uislamu na akatarajia malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wakati jeneza lake linatolewa msikitini likiwa limetangulia mbele na la mke wake likifuatia, kamati ya mazishi kwa nia njema kabisa ilipanga usafiri ili kuwapunguzia safari Waislamu. Waislamu walikataa kata kata majeneza hayo kuingizwa ndani ya gari, wakasema Abbas Kilima na mkewe watakwenda juu ya mabega yetu hadi makaburini Kisutu. Kutokea Msikiti wa Tanzania Islamic Centre Magomeni maelfu ya Waislamu walibeba jeneza la Abbas Kilima na lile la mkewe Rukia Bint Fundi bega kwa bega, mkono kwa mkono kupitia Morogoro Road hadi katika makaburi ya Kisutu. Sheikh Abbas amekufa wakati akihangaikia kuanzishwa kwa Redio Kheri. Sheikh Abbas Kilima amekufa wakati akishughulikia taratibu za kumtibia Mwanafunzi Chuki Athumani Nje ya Nchi. Yuwapi Abbas Mwingine wa kuyabeba majukumu haya? Innalilaahi wainna ilahi raajiuun
|
YALIYOMO
Maoni Kuvuja kwa mitihani: Tuweni wakweli kwa nchi yetu Katibu
wa Baraza Kuu azikwa Dar
Ubabe
wa madhalimu kuzimwa:
MACHO
YA SHUTUMA
Wazo
mpachiko (Programmed mind)
Ta'azia: Abbas Shaaban Kilima 1938-1998 Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 4
Siri
ya Miujiza
Umuhimu
wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo
Ifahamu
Madrasat Ghazal Muslim - Moro
Pamoja
na sala, tusimamishe zakah
Aina
za maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu
Israi
na Miiraji ni miujiza
Pamoja
na ahadi ya Serikali kuzifuta: kesi za mihadhara zaendelea mahakamani
Waislamu Uluguruni Moro wazama kwenye matambiko Imarisheni
miradi ya elimu - Prof. Mikidadi
Teknologia:
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (5)
Mafunzo
ya Qur'an
Chakula
na lishe
|