|
Na.175 Rajab 1419, Novemba 13 - 19, 1998 |
WAKATI Waislamu mjini Morogoro wakiwa usingizini na Masheikh wao wakiwa katika mizozo ya kiitikadi na kugombania ukubwa Misikitini, huko Uluguruni Waislamu wamezama kwenye ibada za matambiko katika mizimu, gazeti hili limeelezwa hivi karibuni. Wakiongea na AN-NUUR mjini hapa, Waislamu kadhaa wa Morogoro vijijini wamewalaumu vijana ‘wanaharakati’ wa Kiislamu, wasomi na Masheikh ambao wamejazana mjini wakinyoosheana vidole huku Uislamu ukididimia vijijini. Waumini hao kutoka milima ya Kibogwa, Tawa, Kinole, Kibungo juu na Tegetero walisema kwamba licha ya kuwa Waislamu ndio wengi Uluguruni, lakini ni kama povu. Baadhi ya Msikiti hutumika kuratibu ibada za matambiko kwenye mizimu, ngoma za kurithi majina na kushadidia mambo kama hayo. "Hadi hivi sasa Salatu Dunale (mzimu wa wachuma au wavigunga ulioko Kibungo juu), Kingalu ulioko Kinole, Matotola, Lubandile (mizimu ya Mgeta), Mwenyedibwaya, Dihimbwa na Korelo (iliyoko Kihunza na Korelo), Nyaluwela (mzimu wa Lumba), Salambwe (Mziladongo), Mangalugome "tetemeko la nchi" (Kibungo) na Ngulu imekuwa ndio ibada ya Waislamu Uluguruni", ameeleza Mzee Juma Saidi Mwanamihule mkazi wa Kibungo. Aliongeza kusema kuwa "si ajabu leo hii kumsikia Muislamu khamsa swalawat akiapa kwa jina la mzimu - Mangalugome sasa si khatari hii bwana mdogo?" alihoji Mzee Mwanamihule. Naye Bwana Athman Khamis Mowele "Mlamlali" mkazi wa Tawa alisema kwamba hali ya Waislamu na Uislamu huko vijijini inatisha mno, hivyo zisipochukuliwa hatua za makusudi kabisa kuleta nusra, Misikiti itakuwa vitengo vya kutambikia mizimu na mababu waliopita. Na Mwandishi Wetu, Dodoma MHESHIMIWA Profesa Sheikh Juma Mikidadi amewataka Waislamu waige tabia za Mtume Muhammad (s.a.w.) kwa kujenga shule kwa wingi ili kufuata agizo la Allah (s.w.) juu ya amri ya kusoma. Mheshimiwa Prof. Mikidadi aliyasema hayo wakati alipokuwa akiwahutubia mamia ya Waislamu waliokusanyika katika hafla ya Maulidi iliyofanyika Masjid Qubaa mjini Dodoma Novemba 7 mwaka huu. Aliwataka Waislamu kuitafakari sana Maulidi na kuielewa vizuri kwani yote yaliyomo ndani ya Maulidi ni sifa na tabia za Mtume (s.a.w) ambazo Waislamu wanapaswa kujipamba nazo. Alisema kuwa Mtume (s.a.w.) alipofikia umri wa miaka 40 alipewa amri ya kusoma, amri hii pia inawahusu Waislamu wote, hivyo suala la kujiingiza katika taaluma mbalimbali na kujenga mashule ni moja ya utekelezaji wa amri hii tukufu ya Allah (s.w.) Aliwaeleza Waislamu kuwa historia inajieleza jinsi gani Waislamu wa karne ya saba walivyotoa mchango katika elimu za hisabati, kemia, jiografia na fizikia na hata katika elimu za tiba, pia walifikia kutoa huduma za upasuaji, na utengenezaji wa vifaa vya kupasulia na dawa za nusu kaputi. Alisema Mheshimiwa Prof. Mikidadi kuwa leo hii maendeleo haya hayapo kwa Waislamu, hvyo aliwasisitiza Waislamu kutafakari juu ya mtandao mzima wa kuleta maendeleo kwa vizazi kwa kuanzisha taasisi za elimu na kuimarisha zilizopo. Wakati huo huo, Imam wa Masjid Manyema mjini Dodoma Sheikh Ahmed Saidi amewataka Waislamu watekeleze ibada ya sala kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Allah (s.w.) nao ni kuswali kwa nyakati zake. Sheikh Ahmed Saidi aliyasema hayo alipokuwa akiwahutubia mamia ya Waislamu waliokusanyika katika swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Manyema Mjini Dodoma Novemba 6, mwaka huu. Sheikh Ahmed aliwaeleza Waislamu kuwa nyakati za swala zimewekwa na Allah (s.w.) hivyo mja hana budi atekeleze ibada hiyo, na kupata malipo kwa namna Allah (s.w.) alivyoamrisha. Alisema kutekeleza ibada kwa kufuata matamanio ya nafsi ni kujiingiza katika shirk. Aidha, aliwaonya Waislamu tabia ya kuzikusanya swala zote kwa wakati mmoja. Sheikh Ahmed aliwasisitiza Waislamu juu ya kuwa na msimamo katika kutekeleza sheria za Allah (s.w.). Aliwaonya baadhi ya Waislamu wenye tabia ya kuswali kwa msimu Ijumaa hadi Ijumaa. Alisema kuwa ibada hii ya swala alikabidhiwa Mtume (s.a.w.) na Allah (s.w.) mwezi huu wa Rajabu 27. Katika hotuba hiyo Sheikh Ahmed pia aliwaomba Waislamu kuimarisha michango ili waweze kumalizia ujenzi wa uzio wa Msikiti pamoja na ununuzi wa kipaza sauti. |
YALIYOMO
Maoni Kuvuja kwa mitihani: Tuweni wakweli kwa nchi yetu Katibu
wa Baraza Kuu azikwa Dar
Ubabe
wa madhalimu kuzimwa:
MACHO
YA SHUTUMA
Wazo
mpachiko (Programmed mind)
Ta'azia: Abbas Shaaban Kilima 1938-1998 Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 4
Siri
ya Miujiza
Umuhimu
wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo
Ifahamu
Madrasat Ghazal Muslim - Moro
Pamoja
na sala, tusimamishe zakah
Aina
za maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu
Israi
na Miiraji ni miujiza
Pamoja
na ahadi ya Serikali kuzifuta: kesi za mihadhara zaendelea mahakamani
Waislamu Uluguruni Moro wazama kwenye matambiko Imarisheni
miradi ya elimu - Prof. Mikidadi
Teknologia:
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (5)
Mafunzo
ya Qur'an
Chakula
na lishe
|