|
Na.175 Rajab 1419, Novemba 13 - 19, 1998 |
Ifahamu
Madrasat Ghazal Muslim - Moro
"HUWEZI kujenga msikiti kabla hujawapa elimu watakaoingia humo". Hiyo hi kauli ya Bw. Ally Suleyuum kiongozi mwandamizi wa Jabal Hira Islamic Center na mmoja wa waasisi wa Ghazal Muslim Madrasat, Morogoro. Ghazal Muslim ilianzishwa rasmi mwaka 1974 na Sheikh Suleyuum akishirikiana na Bw.Ahmed Abdallah Pinto pamoja na Bw. Mohamed Ramadhan aliyejitolea kujenga jengo la Madrasa hiyo miaka minane baadaye (1982) kwa gharama ya shilingi laki moja wakati huo, chini ya Mwalimu Shaaban Khamis. Madrasa hii awali ilikuwa mahali ilipokuwa Muslim Madrasa ambayo ilianzishwa na East African Muslim Welfare Society chini ya usimamizi wa tawi la Morogoro. Muslim Madrasa iliwaandaa watoto wa Kiislamu kabla ya kuanza elimu ya msingi. Watoto waliolelewa hapa baadae walipelekwa Muslim Primary School iliyochukuliwa na serikali mara baada ya kuvunjwa EAMWS (1968). Shule hii ya msingi hivi sasa inaitwa Uhuru Primary School iko eneo la Kiwanja cha Ndege mjini hapa. Tangu mwaka huo hadi sasa madrasa ya Ghazal imepitiwa na waalimu kadhaa kwa nyakati tofauti, waalimu hao ni pamoja na Mwalimu Barton, Yusufu Bakari Kwangaya, Sakina Salum Muwinge, Pili Kizeluze, Bahati Nasoro na Mariam Juma "au Mwalimu Mama". Wengine walioacha mchango mkubwa kitaaluma ni Ahmed Rubajuma, Ally Omary Ngalawa, Mwalimu Maftah, Ally Kwembe na Mwalimu Mohamed Saidi (38) Mudir wa hivi sasa akisaidiwa na Abdulrahim Dianga. Ghazal Muslim ni moja ya Madrasa kadhaa za mjini Morogoro zilizopata mafanikio kitaaluma. Kwa miaka 24 sasa shule hiyo imetoa zaidi ya wahitimu 1,000 wengi wao wakiwa ni Maimamu wa Misikiti, viongozi wa dini katika taasisi kadhaa za Waislamu ndani na nje ya nchi, waalimu wa maarifa ya Kiislamu na walezi wa vituo vya Kiislamu vya malezi ya watoto wadogo na mayatima. Kwa mujibu wa Mudir wa Madrasa hiyo Maalim Mohamed Saidi, shule hiyo hutoa wahitimu zaidi ya 30 kila mwaka tangu mwanzoni mwa miaka ya tisini. Kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 96 wa madarasa yote matatu. Shule hiyo inafundisha maarifa ya Kiislamu, lugha ya Kiarabu, kuandika, kuhesabu, Kiswahili na Kiingereza. Tatizo kubwa la Madrasa hiyo ni pamoja na vifaa vya kufundishia, samani hususan madawati na posho duni za walimu. Akilidokeza AN-NUUR , Sheikh Suleyuum alisema kuwa huenda mwakani 1999 madrasa hiyo ikageuzwa kuwa shule ya msingi bila kuvunja programu ya sasa. "Mradi huo wa shule ya msingi utagharimu zaidi ya shilingi milioni hamsini kama gharama za ujenzi wa madarasa mapya. Kwa kuanzia madarasa tulionayo yanakidhi haja kwani ndio haya haya waliyoanzia Tabal Hira High School mwaka 1983". Anasema kiongozi huyo. Aidha amewaomba Waislamu kuchangia kwa hali na mali mradi huo ili kuboresha elimu kwa jamii ya Kiislamu na kuleta mapinduzi ya maendeleo. "Ni vyema Waislamu waone umuhimu wa kujenga shule na vyuo vya elimu ya juu, hususan shule za watoto wadogo (Nursery Schools), za msingi na vyuo, kama wanavyoona umuhimu wa kujenga misikiti." Akatoa changamoto Sheikh Suleyuum, "Huwezi kujenga msikiti kabla hujawapa elimu watakaoingia humo, hilo ni jambo la msingi kabisa", anasisitiza. Kwa upande wa Mitaala mipya ya elimu ya dini katika shule za msingi na madrasa za mitaani, uongozi wa Ghazal Muslim umeipongeza taasisi ya Kiislamu ya IPC kwa kuwaandalia dira hiyo. "Tunaipongeza hatua hiyo si kwa maneno bali kwa kukifanyia kazi kile tulichoandaliwa kivitendo." Anasema Mwalimu Mohamed Saidi na kuwaomba walimu wote wa Madrasa za Mtaani Mkoani Morogoro, pamoja na wale wanaofunza maarifa ya Kiislamu katika shule za msingi kuhakikisha kuwa wanapata mitaala hiyo, na vitabu vya kiada kisha kuvifanyia kazi haraka iwezekanavyo. "Wakati wa kutilia mkazo" "dufu" na kaswida umekwisha, tufungue ukurasa mpya sasa, hasa katika mbinu za ufundishaji. Huwezi kumuweka mwanafunzi miaka kumi madrasa wakati uwezo wa kumfunza kitu hichohicho kwa miaka isiyozidi mitatu upo, kutokuwa na silabasi wala kuhitimu si ufundishaji." Anasisistiza Mwalimu huyo. |
YALIYOMO
Maoni Kuvuja kwa mitihani: Tuweni wakweli kwa nchi yetu Katibu
wa Baraza Kuu azikwa Dar
Ubabe
wa madhalimu kuzimwa:
MACHO
YA SHUTUMA
Wazo
mpachiko (Programmed mind)
Ta'azia: Abbas Shaaban Kilima 1938-1998 Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 4
Siri
ya Miujiza
Umuhimu
wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo
Ifahamu
Madrasat Ghazal Muslim - Moro
Pamoja
na sala, tusimamishe zakah
Aina
za maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu
Israi
na Miiraji ni miujiza
Pamoja
na ahadi ya Serikali kuzifuta: kesi za mihadhara zaendelea mahakamani
Waislamu Uluguruni Moro wazama kwenye matambiko Imarisheni
miradi ya elimu - Prof. Mikidadi
Teknologia:
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (5)
Mafunzo
ya Qur'an
Chakula
na lishe
|