|
Na.175 Rajab 1419, Novemba 13 - 19, 1998 |
WIKI moja baada ya kuikumbusha serikali ijiunge na Shirika la OIC, Katibu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Abas Kilima amefariki dunia katika ajali ya gari alfajiri ya Jumamosi Novemba 7, mwaka huu. Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Bw. Ali Kilima, ajali hiyo ilitokea Chalinze mkoa wa Pwani ambako marehemu alikuwa njiani kurejea Jijini akitokea Kondoa kuhudhuria mazishi ya mwanawe aliyefariki dunia mwanzoni mwa wiki iliyopita. Katika ajali hiyo, mke wa marehemu Bi. Rukia Fundi pia alifariki dunia papo hapo. Akisimulia jinsi ajali hiyo ilivyotokea, Bw. Ali Kilima alisema gari walilokuwa wakisafiria lilianza kuyumba kabla ya kupinduka mara kadhaa na kusababisha vifo hivyo. Katika gari hilo walikuwemo pia ndugu, mtoto na mjukuu wa marehemu pamoja na dereva ambao walisalimika bila kupata majeraha yeyote. Marehemu wote wawili walizikwa siku ya Jumapili Novemba 8, 1998 katika makaburi ya Kisutu katikati ya Jiji. Siku chache kabla ya safari yake Alhamisi jioni, Sheikh Abas Kilima aliandaa kongamano lililowakusanya Waislamu kutoka sehemu mbalimbali nchini. Kongamano hilo lililofanyika Novemba 1, mwaka huu Temeke Jijini Dar es Salaam, lilizungumzia pamoja na mambo mengine hali ya Waislamu nchini na uadui ulio dhidi yao katika nyanja mbalimbali. Wakati akiwasilisha taarifa ya Baraza Kuu katika kongamano hilo, marehemu Sheikh Abas Kilima aliikumbusha serikali kutimiza ahadi iliyotoa ya kujiunga na Shirika la OIC. Alieleza kunyong’onyea kwa nchi kiuchumi kwamba ni mojawapo ya sababu zilizolifanya baraza lake kuikumbusha serikali ahadi yake iliyotoa. Aliwaondoa wasiwasi wale wenye madai kwamba OIC ina malengo ya kuwasilimisha wasio Waislamu, kwa kuwaeleza kwamba ingawa shirika hilo ni la kidini (Islamic Organization) lakini malengo yake ni kuboresha hali za kijamii za nchi wanachama wake kwa kuzipa misaada na mikopo isiyo na riba. Wakati huo huo, maelfu ya waumini wa dini ya Kiislamu Jijini Dar es Salaam walishiriki mazishi ya marehemu Abasi Kilima na mkewe. Kuanzia nyumbani kwa marehemu Kijitonyama, waumini hao walifurika jioni ya Jumamosi hadi majeneza yanaondoka mahala hapo kuelekea Msikiti wa Tanzania Islamic Centre Magomeni kulikotolewa nasaha mbalimbali kabla ya swala ya Jeneza. Mwandishi wa habari hizi alishuhudia umati wa waumini ukifunga barabara ya Morogoro na kusababisha magari yaliyotokea Ubungo na Mwenge na yale ya Kariakoo kusimama kwa masaa kadhaa wakati majeneza yakisindikizwa kuelekea makaburi ya Kisutu. |
YALIYOMO
Maoni Kuvuja kwa mitihani: Tuweni wakweli kwa nchi yetu Katibu
wa Baraza Kuu azikwa Dar
Ubabe
wa madhalimu kuzimwa:
MACHO
YA SHUTUMA
Wazo
mpachiko (Programmed mind)
Ta'azia: Abbas Shaaban Kilima 1938-1998 Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 4
Siri
ya Miujiza
Umuhimu
wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo
Ifahamu
Madrasat Ghazal Muslim - Moro
Pamoja
na sala, tusimamishe zakah
Aina
za maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu
Israi
na Miiraji ni miujiza
Pamoja
na ahadi ya Serikali kuzifuta: kesi za mihadhara zaendelea mahakamani
Waislamu Uluguruni Moro wazama kwenye matambiko Imarisheni
miradi ya elimu - Prof. Mikidadi
Teknologia:
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (5)
Mafunzo
ya Qur'an
Chakula
na lishe
|