|
Na.175 Rajab 1419, Novemba 13 - 19, 1998 |
| Pamoja
na sala, tusimamishe zakah
MWENYEZI Mungu ameizungumza zakah katika Qur’an takatifu zaidi ya mara sabini na mbili. Tamko la zakah linatanguliwa na tamko la swalatu. Wakati ni huu kwa sisi Waislamu kujiuliza kwa nini Mwenyezi Mungu amezungumzia zakah zaidi ya mara sabini na mbili katika Qur’an? Bila shaka somo hili lina umuhimu wake wa pekee na nafasi yake ya pekee. Katika Surat ya Baqara aya ya kwanza mpaka ya tatu, anasema: "Hiki ni kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake, ni mwongozo kwa wamchao Mwenyezi Mungu. Ambao huyaamini yasioonekana na husimamisha sala na hutoa katika yale tuliyowapa. Ebu tuangalie jamii yetu ya Waislamu kama ina kwenda sambamba na aya tuliyoitaja hapo juu. Waislamu tumeweka mkazo zaidi juu ya salah kuliko zakah au kutoa mali zetu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Mtindo huu hautusaidii hata kidogo kujenga udugu wa Kiislamu. Muislamu tajiri hata kama ana sali kupindukia na upande mwingine anaacha au anapuuzia kutoa zakah, basi huo si ndugu katika jamii ya Kiislamu. Ushahidi wa jambo hili unapatikana katika sura ya 9 aya ya 11 ambayo inasema: Kama wakitubu na wakasimamisha salah na wakatoa zakah, basi ni ndugu zenu katika dini. Na tunazielezea aya zetu vizuri kwa watu wanaojua. Baadhi ya Waislamu walikataa kutao zakah mara tu kifo cha Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) kilipotokea. Khalifa Abubakar (r.a.) hakukubaliana na hali hii iliyojitokeza. Hatua aliyoichukuja ni kuwatumia jeshi kuwalazimisha kutoa zakah na kupigwa vita kama hilo litashindishwa. Lakini hatua hii ilichukuliwa baada ya Khalifa Abubakari (r.a.) kuwasomea aya hii iliyotajwa hapo juu, maswahaba na kisha wote wakamuunga mkono kufanya hivyo. Hali ilivyokuwa wakati wa utawala wa Khalifa Abubakari na hali tuliyokuwa nayo wakati huu ni tofauti sana. Sababu ni kwamba Waislamu hatuna utawala wala hatuna jeshi dhidi ya wanaokataa kulipa zakah. Tunachoweza kufanya ni kuwaelimisha matajiri na kadhalika juu ya umuhimu wa zakah na faida zake katika jamii. Hili lifuatiwe na kuwepo kwa utawala mzuri wa zakah na watendaji wake, na mabingwa wa zakah. Historia ya Kiislamu inafundisha kuwa chombo cha zakah si chombo cha kuachwa na kina faida ambazo zinastahiki kuandikwa kwa wino wa dhahabu. Waislamu wa wakati ule walifanikiwa kiasi kikubwa kufuta shida na mahitaji mbalimbali ya kiuchumi na ya kifedha katika jamii zao, Hata ikaanzwa kufikiriwa kuhamisha zakah kwa watu wasiokuwa Waislamu. Mafanikio haya ya kiuchumi na ya kifedha hayawezi kupatikana katika jamii mbalimbali kwa kutumia mifumo ya fedha na ya kiuchumi ya wakati huu, iwe wa kijamaa, wa kibepari au wa demokrasia. Sababu mifumo hii ina lengo kuu la kunyonya nchi au jamii dhaifu. Waislamu tumeathirika sana na mifumo hii. Hivi sasa Waislamu tumeshindwa kuwasaidia mafakiri, masikini, wanaotiwa nguvu nyoyo zao juu ya Uislamu, kuwapa uungwana watumwa (mateka wa vita), wenye madeni, mambo aliyoamrisha Mwenyezi Mungu,wasafiri walioharibikiwa, kujenga mashule, hospitali, barabara, visima, madaraja, vyuo vikuu, vyuo vya waalimu, madarasa, vyuo vya utafiti, mashamba ya kilimo, mifugo, miti na kadhalika. Wasiokuwa Waislamu wanayaendea mbio kuyafanya baadhi ya mambo yaliyotajwa. Nguvu hii wanaipata wapi? Wanapata nguvu hii kutokana na kodi ya serikali na mifuko ya fedha waliyoiunda ambayo inachangwa na Waislamu na wasio Waislamu. Pia kodi zao na mifuko haina mipaka ya uhalali na uharamu. Hivyo hawana malipo yoyote mbele ya Mwenyezi Mungu. Wakati umefika kwetu kubadilisha mwenendo wetu ili kusimamisha asasi ya zakah kwa faida ya jamii ya sasa na jamii inayokuja. Mwenyezi Mungu hayuko tayari kubadilisha hali zetu kama sisi wenyewe hatujawa tayari. Na Mtume anasema katika mafundisho yake kwamba ni lazima Waislamu tuwe ni watu wa manufaa kwa binaadamu wenzetu. Tukiambatana na binadaamu katika kuwafanyia maendeleo yao na ihsani mbalimbali, basi tufahamu kuwa Uislamu utakuwa katika nafasi ya pekee katika maisha yetu ya kila siku. Ebu tuazimie kuingia katika karne ya ishirini na moja kwa kuunganisha salah na zakah, na nguzo hizo mbili kuzisimamisha barabara katika maisha yetu. Hii ndiyo njia ya kupata pepo ya Mwenyezi Mungu hapa duniani na huko akhera. Hili linawezekana, tuanze na tuendeleze. |
YALIYOMO
Maoni Kuvuja kwa mitihani: Tuweni wakweli kwa nchi yetu Katibu
wa Baraza Kuu azikwa Dar
Ubabe
wa madhalimu kuzimwa:
MACHO
YA SHUTUMA
Wazo
mpachiko (Programmed mind)
Ta'azia: Abbas Shaaban Kilima 1938-1998 Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 4
Siri
ya Miujiza
Umuhimu
wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo
Ifahamu
Madrasat Ghazal Muslim - Moro
Pamoja
na sala, tusimamishe zakah
Aina
za maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu
Israi
na Miiraji ni miujiza
Pamoja
na ahadi ya Serikali kuzifuta: kesi za mihadhara zaendelea mahakamani
Waislamu Uluguruni Moro wazama kwenye matambiko Imarisheni
miradi ya elimu - Prof. Mikidadi
Teknologia:
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (5)
Mafunzo
ya Qur'an
Chakula
na lishe
|