|
Na.175 Rajab 1419, Novemba 13 - 19, 1998 |
|
Kuvuja kwa mitihani: HABARI za mitihani kuvuja katika shule au vyuo vya elimu ya juu, si mpya hapa kwetu Tanzania. Hali hiyo tumekuwa tukisikia ikitokea kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu; miaka nenda-rudi. Lakini suala la kuvuja mitihani ya Kidato cha Nne mwaka huu limekuja na kishindo kikubwa, ambacho tayari kimeisha zua maoni tofauti miongoni mwa wananchi nchini. Pengine kishindo hicho hakitokani na sababu za mitihani hiyo kuvuja, bali kutokana na hatua za kuifuta mitihani hiyo nchi nzima. Hatua hii ya kufuta mtihani kitaifa ni ya mara ya kwanza kuchukuliwa na serikali. Nayo imetajwa kwa kishindo kikubwa vile vile kutokana na hasara na gharama kubwa ambazo Serikali itaingia katika kuiandaa upya mitihani mingine katika muda wa siku zipatazo 60. Katika mtazamo huu wa hasara na gharama, upo pia mtazamo wa watahiniwa wanaolalamika kuwa ni hasara na gharama kubwa kwao kupoteza muda, nguvu za maarifa na juhudi kwa ajili ya kujiandaa upya kwa mtihani mwingine. Vilevile ipo gharama nyingine ya kisaikolojia, hali na mali kutokana na kuvurugika kwa mipango na mategemeo ya kukamilisha ngwe ya masomo ya miaka minne. Hii itawaathiri pia, wanafunzi, wazazi, walezi na hata waalimu. Pamoja na hasara kuna gharama kubwa ambazo idadi ya wananchi wamekuwa wakizijadili na sisi tungependa kuzitolea maoni yetu. Kuvuja kwa mitihani kulikofurutu ada mwaka huu ni dalili ya kushitadi kwa maradhi mazito yanayolikabili taifa letu. Tusipokuwa na ujasiri wa kuukabili uso kwa macho ukweli uliojidhihirisha mwaka huu, maradhi yanaweza kuliangamiza taifa letu. Gharama ya kuyafuga maradhi haya ni zaidi ya shilingi milioni 550 za kodi zetu zitakazotumika tena na serikali. Kwanza ni vigumu sana kuweza kukadiria kwa ukamilifu maafa yanayoweza kutufika kwa kuwategemea "wataalamu" wanaokabidhiwa dhamana nzito na nyeti kwa vyeti walivyovipata kwa wizi wa mitihani. Ni sawa na abiria wanaoendeshwa na dereva asiyejua chochote kuhusu udereva lakini mwenye leseni C aliyoipata kwa kufanyiwa mtihani. Mamia ya abiria hupoteza maisha yao kutokana na "madereva" wa aina hii. Gharama ya roho hizo zinazopotea ni shilingi ngapi? Ni hasara ilioje ikiwa kwa mfano "msomi" huyo mwenye vyeti na shahada alizozipata kwa kufaulu vizuri mitihani iliyovuja atapewa dhamana ya kuwanunulia wananchi meli au kivuko na "msomi" huyo hajui ni ipi tofauti ya meli nzima na mbovu? Ni mateso kiasi gani yatawafika raia ikitokezea (na Mwenyezi Mungu atuepushe na hilo) kuwa "mtaalamu" wa aina hii kateuliwa kuwa mshauri wa Rais? Ole wenu itokezee kuwa kwa shahada zake za mitihani iliyovuja apewe fursa ya kugawa viwanja na maeneo ya hifadhi za misitu! Ni usumbufu ulioje kwa wananchi iwapo kwa mfano ataamua kuhamisha maboya ya mipaka kila baada ya muda fulani? Gharama ya usumbufu huo ni shilingi ngapi? Hali itakuwaje ikiwa sekta ya afya itakuwa na "madaktari" waliofaulu mitihani iliyovuja? Je, katika hali kama hiyo wale wenye uwezo kifedha au wenye madaraka serikalini watakubali kutibiwa nchini? Lakini gharama nyingine kubwa inayotokana na kuwapa dhamana kubwa watu waliofaulu mitihani iliyovuja ni kuistawisha rushwa nchini. Huwezi kumtazamia mtu aliyepata madaraka yake kwa rushwa awe ni askari wa kupambana na rushwa? Mtu wa aina hii hana hata uso wa kuwataja wala rushwa. Kwa sababu yeye mwenyewe ananuka rushwa, ataitumia pia dhamana aliyopewa kwa kudai rushwa, ndio maana alitoa rushwa ili kuipata fursa hiyo. Je, dhulma wanayoipata wananchi kutokana na rushwa, gharama yake ni shilingi ngapi? Janga jingine kubwa ambalo lazima litokee katika mazingira ya kuwa na "wataalamu" bandia ni kujenga na kuimarisha tabaka la madhalimu na wadhulumiwa. Kwani ni jambo linalojulikana wazi kuwa rushwa na haki havitangamani. Kinadharia, katika nchi yetu watu hupata fursa ya kuendelea na masomo ya sekondari na elimu ya juu na hatimaye kupewa dhamana kubwa serikalini si kwa sababu nyingine yeyote isipokuwa uwezo na ujuzi wao. Na kwamba nchi yetu inaendeshwa bila ubaguzi wowote wa dini au kabila. Lakini kihistoria, wakoloni waliiendesha nchi hii kwa misingi ya ubaguzi mkubwa wa kidini dhidi ya Waislamu hasa katika elimu. Ni mara baada ya uhuru kwa mfano katika waraka wa Agosti 26, 1963 wa kurasa 15 wa marehemu Sheikh Hasssan bin Amiri, Waislamu walionyesha wasiwasi wao juu ya jinsi ubaguzi wa kidini dhidi yao ulivyokuwa unaimarishwa ndani ya serikali pamoja na kuchukua ahadi ya kuifanya nchi hii kuwa ya Kikristo. Nafasi karibu zote za masomo ya nje ya nchi walipewa Wakristo kwa madai kuwa ndio wanaostahiki kupewa. Nafasi karibu zote serikalini pia walipewa wao kwa madai hayo hayo. Karibu miaka 40 sasa baada ya uhuru, uwiano wa kielimu na kimadaraka baina ya Waislamu na Wakristo unatisha. Umefikia kiwango ambacho unaweza kusema kuwa kwa wastani Wakristo ndio watawala na Waislamu ndio watawaliwa. Na hoja bado ile ile kuwa Wakristo wanapewa nafasi hizo kwa sababu ya uwezo na ujuzi wao. Hata hivyo, wananchi hawajaweza kuthibitisha umadhubuti wa hoja hii wanaipoipima na kiwango cha maendeleo nchi yetu iliyoyafikia kwa miaka 37 sasa! Na hata katika Bodi ya Parole iliyovunjwa na Mheshimiwa Rais bado wanaopinga kuvunjwa kwa Bodi ile wanadai suala la uwezo ndilo lililozingatiwa. Kwa ushahidi kabla na baada ya uhuru Waislamu wamekuwa wakidai kwa ushahidi kuwa kubakia kwao nyuma kielimu na kimadaraka si jambo la bahati mbaya. Lakini siku zote madai hayo yamekuwa yakipuuzwa. Miaka 11 iliyopita, Marehemu Profesa Kighoma Malima alizigundua njama nzito dhidi ya Waislamu zilizokuwa zikipangawa na kutekelezwa na Wizara ya Elimu na Utamaduni. Aliandika dokezo rasmi kwa Rais ili uchunguzi wa kina ufanywe ili kuliondoa tatizo hilo ambalo alisema linaweza kulitumbukiza taifa letu katika maafa katika siku zijazo. Alishutumiwa kuwa anataka kuwapendelea Waislamu na akaondolewa katika wizara hiyo ambayo katika kipindi chote cha utawala wa Mwalimu Nyerere alipewa Waziri Mkristo kuiongoza, kama ambavyo Nyerere siku zote aliteua Muislamu kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Mwaka 1995 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Dar es Salaam, Marehemu Profesa Malima alizieleza njama hizo za kuwanyang’anya nafasi za masomo watoto wa Kiislamu waliofaulu na kuwapa Wakristo, kwa kutokutumia namba wakati wa kutangaza matokeo. Alipouziba mwanya huo mwaka huo Waislamu waliopata fursa ya kuendelea na masomo waliongezeka kwa asilimia 40! Na kwamba alipoondoka tu wizarani hapo mtindo wa kubana Waislamu ukaendelezwa. Haya ni madai mazito sana kutolewa na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo nyeti. Mtu angetegemea kuwa angalau serikali ingekanusha au kuunda tume ya uchunguzi. Yote hayo hayakufanywa. Lakini kwa bahati njema safari hii ukweli umedhihiri. Sio kila aliyepewa dhamana na madaraka ameyapata madaraka hayo kwa sababu ya uwezo na ujuzi wake. Na siyo wote wanaokosa fursa za kuendelea na masomo ya juu wanazikosa fursa hizo kwa sababu hawana uwezo kimasomo, bali kwa sababu hawana uwezo wa kununua mitihani. Katika Urusi ya zamani viongozi wa Kikomunisti waliokuwa katika Baraza Kuu la Siasa (Polit Bureau) walijilimbikizia marupurupu mengi sana yaliyowatofautisha sana na raia wa kawaida. Kwa sababu ya uhondo huo kila mmoja wao alifanya kila njia kuhakikisha kuwa mwanawe anaingia katika Baraza hilo. Hivyo wakawa wanarithishana bila kujali uwezo wao. Hiyo ni hulka ya kibinadamu. Hapa kwetu wapo watu ambao kwa kuiona shida wanayoipata raia wa kawaida na starehe za walioshika madaraka serikalini wanafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa watu wao wanaendelea kuhodhi nafasi hizo hata kama hawana uwezo! Na kwa mtindo huu ikiwa waliozishika mwanzo walikuwa ni watu wa dhehebu fulani hali hiyo itadumishwa hata kama itabidi kuiiba mitihani yote na majibu yote! Hatari ya kuiruhusu hali hii kuendelea katika mazingira ya Tanzania ya leo ni kuwa inajenga na kuimarisha uhasama wa kidini na kuididimiza nchi kimaendeleo. Na vile vile kuwafanya wananchi wadhanie kudidimia kwa nchi katika kila eneo hivi sasa kunatokana na watendaji wake wa ngazi za juu kuwa wale "waliofaulu" kwa upendeleo na kuvujishiwa mitihani! Ikifikia hatua ya watu kupewa vyeo kwa sababu ya dini zao watu hao baadaye hawataweza kusimamia haki au kuwatendea haki watu wasiokuwa wa dini zao. Kwa dhulma kabisa, kinyume na Katiba na sheria za nchi Waislamu wameuliwa kama kuku katika Msikiti wa Mwembechai. Waislamu wamekuwa wakiiomba serikali japo iunde tume ya kuchunguza mauaji hayo. Hili halijafanyika, kilichofanyika ni kuwapongeza askari kwa kazi nzuri waliyoifanya na wengine kupandishwa vyeo. Mwaka huu pia yupo Muislamu aliyekamatwa na kutiwa ndani kwa kusema Yesu si Mungu! Mtu angetegemea mabingwa wa sheria wa serikali wangeishauri serikali. Hilo halikutokea. Ikiwa sehemu kubwa ya watendaji hao pia ni wa dini nyingine ni rahisi kwa raia kudhani kuwa watu wanabaguliwa kwa sababu ya dini zao. Maadamu safari hii serikali imekiri kuwa kuna udanganyifu mkubwa katika mitihani ni vyema basi fursa hii itumike siyo tu kuwatafuta waliosababisha kuvuja kwa mitihani hiyo, bali kuyatazama kwa kina madai yote yanayohusu kudhulumiwa kwa baadhi ya raia katika suala hili la elimu. Pengine njia nzuri siyo kuituma wizara yenyewe kulichunguza suala hili, bali kuunda tume huru itakayotizama masuala yote. Kwa mfano Tume hiyo inaweza kuchunguza madai kuwa zipo shule za serikali zinazopewa upendeleo maalumu na Wizara ya Elimu kwa kupatiwa vifaa vingi na bora, vitabu na waalimu wa kutosha. Na kwamba watoto wa wakubwa ambao hawajapatiwa fursa ya kwenda kusoma nje ya nchi hupelekwa katika shule hizo. Na zipo shule za wanyonge ambazo zina upungufu wa kila kitu. Tume hiyo pia ichunguze ukweli wa madai kuwa zipo shule maalum ambazo hazipelekewi wasimamizi wa mitihani wa kutoka nje, na iwapo itasadifu pia kuwa shule hizo zina ada ya kufanya vizuri au vibaya katika mitihani Tume hiyo pia ichunguze ukweli wa madai kuwa fursa za kwenda kusoma nje ya nchi hazitolewi kwa uadilifu. Yapo madai kuwa nafasi hizo hutangazwa makanisani kabla au bila ya kutangazwa magazetini. Yapo madai pia kuwa upo udini katika Wizara ya Elimu. Na miaka 12 iliyopita warsha ya waandishi wa Kiislamu ilipeleka rasmi kwa Mheshimiwa Spika wa Bunge la Muungano ombi la kutaka suala la udini katika Wizara hiyo uchunguzwe kama ambavyo Bunge hilo lilivyounda Tume kuchunguza ukabila katika Bodi ya Biashara ya Nje (BET). Yawezekana kuwa madai yote haya yakawa ni uzushi mtupu usiokuwa na ukweli wowote. Lakini ni vema hilo lithibiti baada ya uchunguzi huru. Madai haya hayawezi kupuuzwa baada ya ukweli wa kuvuja mitihani kwa kiwango cha kutisha kudhihiri. "Inasikitisha". Inasikitisha kuwa kufutwa kwa mitihani yote ya kidato cha nne kumekuja katika kipindi ambacho wananchi bado wanajadiliana kuhusu ripoti ya Transprancy International inayodai kuwa Tanzania inachuana na Nigeria kwa rushwa. Na kumekuja pia katika kipindi ambacho Mheshimiwa Rais ameomba wananchi wamtajie wala rushwa. Tutakuwa tumeitumia vizuri fursa hii ya kuvuja kwa mitihani ikiwa tutaitumia kuuchunguza ukweli wote bila woga ikiwa ni pamoja na madai ya Waislamu ya kubaguliwa kielimu ili kuhakikisha kuwa dhulma inaondoka na haki inatendeka kwa raia wote. Tukifanya hivyo, tutakuwa wakweli kwa nchi yetu. |
YALIYOMO
Maoni Kuvuja kwa mitihani: Tuweni wakweli kwa nchi yetu Katibu
wa Baraza Kuu azikwa Dar
Ubabe
wa madhalimu kuzimwa:
MACHO
YA SHUTUMA
Wazo
mpachiko (Programmed mind)
Ta'azia: Abbas Shaaban Kilima 1938-1998 Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 4
Siri
ya Miujiza
Umuhimu
wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo
Ifahamu
Madrasat Ghazal Muslim - Moro
Pamoja
na sala, tusimamishe zakah
Aina
za maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu
Israi
na Miiraji ni miujiza
Pamoja
na ahadi ya Serikali kuzifuta: kesi za mihadhara zaendelea mahakamani
Waislamu Uluguruni Moro wazama kwenye matambiko Imarisheni
miradi ya elimu - Prof. Mikidadi
Teknologia:
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (5)
Mafunzo
ya Qur'an
Chakula
na lishe
|