|
|
| Barua
Meghji ametoa mpya ! Ndugu Mhariri NIMESHINDWA kuvumilia upotoshaji wa ukweli unaofanywa na serikali kuhusu yale yaliyofanyika katika kijiji cha Nzasa. Akijihojiwa na waandishi wa habari Oktoba 12, 1998, Waziri wa Maliasili na Utalii, Bi. Zakhia Meghji ameitetea hatua ya serikali ya kuwachomea makazi na rasilimali zao wananchi wa kijiji cha Nzasa. Waziri Meghji anadai kwamba vilivyochomwa ni vibanda tu na wala siyo nyumba na wanaolalamika ni wale wafanya biasharaya mkaa walioko mijini. Vibanda hivyo vilikuwa vinatumika kuhifadhia wachoma mkaa ! Alidai pia kwamba hata wananchi wengine wa kijiji hiki walishiriki katika zoezi hilo ! Bi. Meghji alisisitiza kwamba zoezi la kuwahamisha "wavamizi" katika hifadhi za taifa litaendelea. Jamani ! Hawa watu wanakosa huruma kiasi hiki ! wanabadilisha tafsiri ya maneno na matukio utadhani walioshuhudia dhulma hii wamekufa ! Kibanda nacho ni nyumba Mheshimiwa Waziri, ingawa si kila nyumba ni kibanda. Labda kwa sababu "vigogo" mnaishi katika makasri ndiyo maana mnaona nyumba za wanakijiji wa Nzasa ni "matundu ya panya". Yaliyochomwa moto ni makazi ya wana Nzasa; yawe vibanda au viota si hoja ya msingi hapa. Kitendo cha kinyama cha askari wa POLISI na wa Maliasili kuwalazimisha wananchi wachome nyumba zao kwa mikono yao ndiyo kushiriki katika zoezi hilo haramu ! Ama kweli dunia inakwisha sasa ! Kama huo ndiyo uzalendo basi wengine umeshatushinda. Mtu yeyote mwenye akili yenye kutuama hawezi kuchoma nyumba yake kimasihara namna hii. Wananchi hawa wameshurutishwa kuchoma nyumba zao kwa mikono yao wenyewe ili wapate mateso ya kisaikolojia kwa kipindi chote watakachokumbuka Nzasa. Kuwasimanga Watanzania wengine wanaowahurumia wananchi wa Nzasa kwa kuwasingizia ni wafanyabiashara ya mkaa unaokatwa katika misitu ya Kazimzumbwi ni na kuwavunjia heshima wananchi hawa. Kanuni ya maumbile inawabana binadamu kusaidiana na kuhurumiana kama walivyo wanyama wengine wa jamii moja. Ukijiona huna huruma na binadamu wenzio basi ubinadamu wako una dosari. Bisura Waziri,
Nyumba ya Wakfu kugeuzwa baa Ndugu Mhariri NAOMBA unipelekee huu ujumbe wangu kwa Waislamu wa Masjid Mwinyi kutokana na dhulma wanayofanyiwa. Mimi sina mengi ninachosema ni kuwa, kama kweli nyinyi mna ushahidi wa kutosha kuwa nyumba hizo mliandikiwa na almarehemu Hajat Aziza, basi mimi ninachosema kwa hakika Muislamu harithiwi na Mkristo kwa hali yoyote ile iwayo. Suala lililopo ni kuchukua nyumba zetu. Hakuna mtu atakae tusikia na nyumba tutazikosa hivi hivi. Shime Waislamu wote tutokeni wote tutakapoitwa tukachukue mali za Muislamu mwenzetu. Alhaj M.M. Mattaka,
Wasiotekeleza ibada tusishirikiane nao Ndugu Mhariri WALE ambao si Waislamu hudhania kuwa Uislamu ni kuvaa kanzu na ‘baragh shia’ au kuwa na jina fulani. Na wakati Uislamu ni mfumo mzima wa maisha ambapo huanzia kwa kumuamini Allah na Mitume yake na yote ambayo wameteremshiwa kwao. Ama baada ya nayo: Ninachotaka kukizungumza ni wale wenzetu ambao wamejaaliwa kuwa Waislamu lakini kwa makusudi wanashindwa kutekeleza ibada yaani lengo la kuletwa hapa duniani. Ingawa kila siku wanakumbushwa. Tunaishi na watu kwa muda mrefu tunashindwa kujuana ni dini gani, ingawa wana majina ya Kiislamu lakini hawana hata dalili moja ya kuwa wao ni Waislamu. Ukimtolea salamu anashindwa vya kuijibu, ukiyatizama hayo maisha anayoishi yeye na familia yake hayana tofauti na maisha ya watu wa dini nyingine. Watoto hakuna hata mmoja aliyempeleka madrasa. Ukifika mwezi wa Ramadhani hana habari kabisa kuwa mwezi huo watu wanajizuia kula, kunywa pamoja na yale yote yanayobatilisha swaumu. Wanajilia mchana hadharani bila ya kuwa na wasiwasi wowote. Mwezi wa Ramadhani ukimalizika tu (ukiindama shawali) yeye huwa wa mwanzo katika kuhudhuria sala ya suna. Na kuku kama hajachinjiwa na Sheikh kwkae ni haramu kumla wakati mwezi mzima wa Ramadhani alimuasi Allah (s.w.). Ndugu Waislamu ninatoa wito, watu hawa tuwatenge tusishirikiane nao katika shughuli zao iwe ni harusi, msiba, karamu au hitima. Tuwaachie wafanye wenyewe kwani si wenzetu katika mambo yanayohusu Uislamu. Na Masheikh muwe mstari wa mbele katika kusimamia haya. Anapokujia mtu ambaye mwezi wa Ramadhani akila mchana na kukutaka ukamchinjie kuku wake au chochote kile chenye kuchinjwa ukatae na umuulize kuwa mwezi wa Ramadhani alimuasi Allah (s.w) basi kwa hivyo aendelee kula kibudu. Ni mategemeo yangu msimamo huo tutakuwa ni wenye kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu kwa kurukuu na kusujudi pamoja ili kutafuta fadhila za Allah (s.w.) Na pia ile tofauti kati ya Muislamu na asiye Muislamu itakuwepo. Ali Baraka Khamis,
Afya zetu zipo hatarini kutokana na ufugaji ovyo wa wanyama haramu nguruwe Ndugu Mhariri NAOMBA nafasi katika gazeti lako la kila wiki la AN-NUUR ili nitoe malalamiko yetu sisi wananchi wa Karakata kutokana na hatari iliyopo kuhusu afya zetu na hali mbaya ya eneo hili linalofugwa nguruwe. Hapa Karakata katikati ya makazi ya watu wanafugwa nguruwe wengi ambao wakati mwingine huonekana wakiranda randa ovyo barabarani huku watu wengi wapitao kwa miguu. Kinyesi cha wanyama hawa haramu hutupwa nje kwa makusudi na Bwana mmoja ambaye ni mstaafu jeshini akisaidiana na mwenzake ambaye ni bado ni mtumishi huko jeshini (ofisa). Kinyesi hiki husambazwa kipindi cha mvua na kuenea kilomita nyingi tu hadi kwenye kisima ambacho wananchi wa Karakata nzima huchota maji hapo. Juhudi zimefanyika kutoa taarifa kuanzia Mwenyekiti wa Tawi la Mogo (CCM), Bwana Afya Ilala hata Mkuu wa Wilaya anazo habari hizi. Vyombo vya habari kama ITV, Mtanzania wanafahamu vyema eneo hili linavyotisha kinachoendelea siku hadi siku ni chuki baina ya mtu huyu jeuri na raia wema wasiopenda taabu na kuvunjika amani. Serikali yetu imetuweka mahali ambapo tunadhani mambo haya yanapata baraka zake kutokana na mradi wa SUKITA uliokufa. Wazee wa mazingira Dk. Omari Ali Juma na mwenzake Bw. Reginald Mengi mpo wapi ? Ikiwa kweli lengo lenu watu wa mazingira ni zuri, njooni haraka muone hali hii ya kutisha msisubiri mpaka watu wakaanza kukwaruzana. Nguruwe wanafugwa kama mbuzi na nyama yake huuzwa katika barabara ya miguu ambapo kila apitaye hapo husikitika. Watu wa mazingira njooni upesi muone watu wengine jinsi wanavyoweza kuwapuuza watu wengine na kuwaletea madhara ya afya raia wema kwa ulafi tu wa nyama na fedha haramu. Na wewe mwandishi njoo ujionee kila Jumapili. Raia wema,
Kuadhini kwa kubadilisha maneno ni halali? Ndugu Mhariri NAPENDA japo nami nipate nafasi ya kusema kinachonikera kupitia gazeti hili lenye utukufu mkubwa kwa kutufunza mengi tusiyoyajua na sasa tunayajua. Kama tunavyoelezwa kwenye Qur’an kuwa "Tufundishane yaliyo mema na tukatazane mabaya". Naomba nitumie nafasi hii kuuliza jambo ambalo kwangu mimi hunikera sana pale mtoa adhana anaposema "Hay-ala-l-bala" badala ya kutamka "Hay-ala-lfala" kama tulivyofundishwa. Au wakati mwingine huchanganya yote mawili kwa vile huwa inasomwa mara mbili basi mtoa adhana huyo naye huyasema au yote mawili kwa bahati mbaya hutamka mara moja moja kwa kila neno katika hayo. Imekuwa ni jambo la kawaida katika Msikiti wa Masjid Jabal Hirra – Mabibo kusikia baadhi ya watu wanaoadhini kubadili sehemu hiyo. Kwa hiyo naomba nifafanuliwe kupitia gazeti hili ikiwa hayo matamshi ni sawa. Vile vile ningeomba kama itawezekana wahusika wautembelee Msikiti huo ili wasikie wao wenyewe na kuchukua hatua inayofaa juu ya suala hili. Muulizaji,
Kutolewa kwa kibali cha kuuza silaha, Waislamu lazima tuelewe uzito wake Ndugu Mhariri NAOMBA nafasi ndogo katika gazeti lako tukufu ili niweze kutoa nasaha zangu kwa jamii ya Kiislamu nchini juu ya biashara ya silaha nchini kwetu. Naomba tujiulize maswali haya mawili; hivi kwa nini uamuzi huu mzito usiwashirikishe wananchi moja kwa moja au kupitia wawakilishi wao bungeni ? Na pili, hivi hii ilikuwemo katika sera tulizokuwa tunapumbaziwa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 1995 ? Kama hii haikuwemo kwanini tendo hili zito lizuke ghafla na bila ya maelezo ya kutosha kutolewa ? Waislamu tunaelewa kuwa kuna dhehebu la dini ya Kikristo linamiliki tume ya Majeshi ya kivita, na hakuna maelezo yaliyotolewa na serikali juu ya tume hiyo. Chukueni hadhari wananchi. Abdul Omar,
Tusijenge mazingira ya chuki kati ya wananchi na serikali Ndugu Mhariri TANZANIA ni nchi ya amani na inasifika kwamba ni kisiwa cha amani. Pamoja na hivyo nimesikitishwa sana niliposoma gazeti la AN-NUUR toleo Na. 171 la Oktoba 16 – 22 ambalo linaonyesha hali halisi ya wananchi wa Tanzania wanavyonyanyasika huko Nzasa. Kwa kweli ni aibu kuona kwamba nchi yetu inashughulikia wakimbizi kutoka nje ya nchi lakini wakati huo huo ikiangamiza makazi ya raia wake. Hali halisi ya Watanzania waliochomewa moto nyumba zao huko Nzasa ni ya kutoa machozi, kwani kuna Ajuza hadi wa miaka 90 amekalia kitanda chake nje kabisa na habari za kuaminika zinaeleza kwamba wananchi hao wanalala nje kabisa na kuathirika vibaya na baridi kali la usiku. Hivi kweli hii ndio demokrasia, sheria na haki ambayo viongozi wetu waliahidi kutuletea. Hivi kweli huku ndio kuondoa kero za wananchi. Kuwafukuza wananchi chini ya miembe, kuwakataza kung’oa mihogo yao ndio haki na uadilifu ? Cha aibu mno ni pale zinapotolewa kashfa kwamba hizo sio nyumba bali ni vidungu yaani nyumba za kuhamia ndege au za kujihifadhi wakati wa kilimo. Stara ni stara anayelala kwenye (kasri) nyumba ya fakhari na halikadharika ni sawa na yule anayelala kwenye kidungu alikadhalika. Ili kuonyesha ukosefu wa haki na uhuni, wale waliochomewa nyumba zao wala hawajafikiriwa chochote kuhusu makazi mengine. Vile vile wananchi hawa wanapojaribu kutaka kuwasiliana na vyombo vya juu wanafanyiwa urasimu. Ninawapongeza sana DUMT (Dar es Salaam University Muslim Trusteeship) kwa msaada wao na wale wote ambao wamewasaidia wananchi hao. Inabidi serikali itafakari kuhusu suala hili na iwapatie makazi na kuwalipa wananchi hasara walizozipata kwani tusipoziba ufaa tutajenga ukutaa. Tunajenga mazingira ya chuki baina ya wananchi na serikali, wananchi hawa watakapodai haki yao kwa nguvu, watauliwa. Serikali isinyang’anye haki za watu kwa mabavu. Mariam U.,
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Wanawake Dodoma wataka mtoto aliyepigwa risasi akatibiwe nje Kesi za Mwembechai zaanza kusikilizwa Dondoo za saikolojia: Tuonavyo mambo Waraka wa Baraza Kuu kuhusu Parole Inawezekana kufanyika mdahalo kati
ya Waislamu na wasio Waislamu?
Teknologia
Serikali ihamie Dodoma kwanza !
Mahafali ya AMSIR Iringa
Bihawana Sekondari wafungua Ijumaa Vijana Shinyanga watakiwa
kuwa mfano mwema
Vyeo visiwasahaulishe majukumu
yenu- Sheikh Abri
Jiandaeni na kifo – Sheikh
Abdallah
Semina zawazindua wanawake
Bukoba
Waislamu wanaomaliza Kidato
cha Nne Tanga waaswa
Ndugu Kamuhabwa ndiye mwenye
chuki na AN-NUUR
'Ukombozi wa mwanamke si kugeuzwa
biashara huria'
Polisi walinda amani katika
muhadhara wa Wakristo
Mazengo wapewa uwanja wa
kujenga Msikiti
'Ajiengua Chuoni Z'bar kwa
kutoruhusiwa kuvaa hijab'
Shairi
|