|
|
|
TUKIO la Nzasa ni mfululizo tu wa matukio ya serikali yetu kutumia vibaya nguvu za dola. Serikali ya awamu hii iliwahi kutumia jeshi la wananchi kuchoma moto ngano iliyodaiwa kuwa haifai kwa matumizi ya binadamu wala mifugo. Licha ya mahakama kutoa pingamizi kuzuia ngano hiyo isiteketezwe mpaka ufumbuzi wa kisheria utakapopatikana, serikali kama kawaida yake ikakwepa kutatua tatizo hilo kwa njia za kiungwana na kiuadilifu. Ikapuuza amri ya mahakama na kutumia rungu la dola visivyo. Sijui kama nia na madhumuni ilikuwa kumkomoa mwenye ngano ile ile kweli akakomolewa bila hata kuzingatia taratibu za kisheria. Sheria inakuwa na maana pale tu inapoilinda serikali. Wanyonge hawana haki ya kulindwa na sheria. Tatizo jingine ni hili la Wamachinga. Vijana hawa wanatokea kwa sababu serikali imeshindwa kuandaa mazingira mazuri ya ajira kwa vijana. Vijana hawa wametelekezwa na serikali yao na wakaamua kujitafutia riziki zao halali kwa kufanya biashara ndogo ndogo. Serikali badala ya kuangalia kiini hasa cha tatizo hili, imekuwa ikitumia POLISI bila mafanikio kuwafukuza Wamachinga Jijini. Eti! Wanadai wamewakatia maeneo ya biashara Mbagala ! Mbagala kuna masoko ya biashara za kimachinga ! Biashara hizi zinafanyika mijini kwenye watu wengi. Kuwapeleka Wamachinga Mbagala nikuwalazimisha wavunje amri ili upate sababu ya kuwaadhibu. Huu ni udhalimu na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Janga lililotokana na mihadhara inayodaiwa ya kashfa bado halijafutika katika kumbukumbu zetu. Baada ya serikali kubaini kuwa wanaodai kukashifiwa na wahadhiri wa Kiislamu hawana hoja wala ushahidi wa kutosha mbele ya sheria, ikawa inakwepa kulitatua tatizo kama sheria na taratibu za nchi zinavyotaka. Kwa sababu kwa njia ya kisheria na kiadilifu, "agenda" dhidi ya Waislamu hazitokamilika. Mabavu yakatumika na damu ya Waislamu ikamwagwa Mwembechai. Wananchi wa kijiji cha Nzasa wameishi kwa miongo mingapi ? Serikali ilikuwa wapi muda wote huo ? Kwanini hawakuwaondoa watu wa mwanzo kabisa kuvamia eneo hilo ? Serikali imelifanya suala la Nzasa kuwa maafa kwa wananchi kwa kuchelewa kwake kulidhibiti tangu lilipoanza. Na hii ndiyo faida ya kutokuwa na mipango ya muda mrefu na kutegemea sera za "ghafla" kuendesha nchi. Lazima tukukubali ukweli, zoezi la kuhama makazi ni zito na lina gharama kubwa. Hasa ukizingatia hulipwi fidia wala hukuandaliwa makazi mapya. Serikali inatoa matamko tu: "Hameni mabondeni, hameni kwenye hifadhi ya taifa" ! Lakini haizingatii ugumu wa kuhama wala haitoi msaada unaohitajika. Huwezi kuhamisha binadamu kama unavyohamisha kikapu cha mihogo ! Binadamu ana uhai na maisha ambayo yana thamani kubwa zaidi kuliko hifadhi ya taifa. Serikali yenyewe imeshindwa kuhamia Dodoma mpaka leo kwa nini ? Tangu tuambiwe mji wa Dodoma unaandaliwa kuwa Makao Makuu ya Chama na Serikali, leo mwaka wa ngapi ? Ukumbi wa Bunge, makazi ya mawaziri na kadhalika, lakini suala la kuhamia Dodoma ni msamiati kwa serikali. Serikali haitaki kuhamia Dodoma. Sijui inaona ugumu gani. Kama serikali inashindwa kuhamia Dodoma, basi suala la kuwahamisha wananchi kwa nguvu lisiwe mkuki kwa nguruwe. Serikali inadiriki kuwahamisha wananchi wa kijiji cha Nzasa utadhani inapambana na wadudu waharibifu ! Maana ukishaharibu makazi yao na rasilimali zao basi hawatakuwa na sababu ya kuishi pale. Inashangaza sana kumsikia Waziri wa Mali Asili na Utalii akijisifu kwamba zoezi la kuwachomea nyumba na vyakula wananchi wa kijiji cha Nzasa litafanywa kwa uangalifu mkubwa ili kuhakikisha hakuna mtu anayeumia ! Yaani kule mwanamke kujifungulia kwenye matuta ya viazi, vyakula kuchomwa moto, na wananchi kulala juu ya miti kama tumbili si maumivu kwa tafsiri ya Bi. Zakia Meghji ! Nadhani Watanzania tumekuwa wapole sana kwa serikali yetu. Serikali imejaa kibri na inajiona inaweza kufanya lolote kwa wananchi na bado inategemea kuwepo madarakani. Siyo tabia ya serikali inayokuwa madarakani kwa kukubaliwa na wananchi kufanya ukatili huu. Hivi Watanzania hatuna namna ya kuiwajibisha serikali yetu ! Dola inapaswa kutulinda siyo kutunyanyasa kwa visingizio mbalimbali. Napenda kuchukua fursa hii kuwaomba Watanzania wote kwa ujumla tuwasaidie ndugu zetu hawa wa Nzasa. Maafa yaliyowakuta ni makubwa sana na serikali haionyeshi dalili yoyote ya kuwahurumia. Tusipumbazwe na propaganda za kuwatia hatiani wananchi hawa ili ikosekane sababu ya kuwalipa fidia. Binadamu pia ni sehemu ya mazingira. Kumhamisha binadamu ‘kihuni’ namna ile ni uharibifu mkubwa zaidi wa mazingira kuliko ule tunaotaka kuulinda. Sera mbovu na mgawanyo wa choyo wa maliasili ndiyo wa kulaumiwa siyo wananchi wasiokuwa na hatia. Sheria isitumike pale tu inapokuwa na manufaa kwa serikali. Sheria hiyo hiyo inawapa haki wananchi wa kijiji cha Nzasa ya kulindwa, kuthaminiwa utu wao, na kujaliwa na serikali yao kama raia. Serikali itawasaidiaje wananchi hawa waliokumbwa na ‘El-Nino’ hii ya aina yake ? |
YALIYOMO
TAHARIRI
Wanawake Dodoma wataka mtoto aliyepigwa risasi akatibiwe nje Kesi za Mwembechai zaanza kusikilizwa Dondoo za saikolojia: Tuonavyo mambo Waraka wa Baraza Kuu kuhusu Parole Inawezekana kufanyika mdahalo kati
ya Waislamu na wasio Waislamu?
Teknologia
Serikali ihamie Dodoma kwanza !
Mahafali ya AMSIR Iringa
Bihawana Sekondari wafungua Ijumaa Vijana Shinyanga watakiwa
kuwa mfano mwema
Vyeo visiwasahaulishe majukumu
yenu- Sheikh Abri
Jiandaeni na kifo – Sheikh
Abdallah
Semina zawazindua wanawake
Bukoba
Waislamu wanaomaliza Kidato
cha Nne Tanga waaswa
Ndugu Kamuhabwa ndiye mwenye
chuki na AN-NUUR
'Ukombozi wa mwanamke si kugeuzwa
biashara huria'
Polisi walinda amani katika
muhadhara wa Wakristo
Mazengo wapewa uwanja wa
kujenga Msikiti
'Ajiengua Chuoni Z'bar kwa
kutoruhusiwa kuvaa hijab'
Shairi
|