|
|
|
Kwenye makala yetu iliyopita kuhusiana na mada iliyopo hapo juu, tulieleza kwa ufupi na kwa ujumla mambo yote ya kawaida yanayoandamana na kuunganisha kompyuta mbili kwa kutumia programu iliyo kwenye Windows 95 inayoitwa Direct Cable Connection (DCC). Tulitoa maelezo ya jumla kwa makusudi kabisa ili wasomaji wapate kuyafuatilia na kuyaelewa maelezo hayo kwa urahisi zaidi. Katika sehemu hii ya pili ya makala yetu, tutakita zaidi kwenye yale mambo ambayo si ya kawaida ingawa ni muhimu kuyaelewa ili kuweza kukabiliana na hali mbali mbali zinazoweza kutokezea mtu anapohitaji kuunganisha kompyuta mbili kwa kutumia DCC. Kitu cha kwanza ambacho ni muhimu ila kwa bahati mbaya hatukukieleza kwenye makala yetu iliyopita, ni kuwa ni lazima ile kompyuta ambayo utaifanya kama "Host", iwe inaruhusu kompyuta nyengine kuona na kuyanakili majadala yake. Ili kuwezesha hivyo, tumia Start -> Settings -> Control Panel -> Network -> File and Print Sharing na uweke tiki kwenye sehemu yenye "I want to be able to give others access to my files". Kwenye sehemu ya kwanza ya makala hii pia tulieleza kwamba inaweza kutokezea kuwa programu ya DCC haikuwekwa kwenye kompyuta yako. Kama hali ni hiyo, itabidi uiweke ama kwa kutumia CD ya Windows 95 (kama kompyuta yako inayo CD-ROM drive), au kwa kutumia diskette za Windows 95. Lakini, watumiaji wengi wa kompyuta huwa hawana CD au diskette zilizotumiwa kuweka Windows 95 kwa mara ya kwanza kwenye kompyuta zao. Inabidi waazime kutoka kwa watu wengine. Ikitokezea hivyo, wakati wa kuiweka DCC kwa kutumia Start -> Settings -> Control Panel -> Add/Remove Programs -> Windows Setup na kuendelea kama tulivyoeleza kwenye sehemu ya kwanza ya makala hii, yanaweza kutokezea matatizo kidogo ya kutoafikiana kati ya Windows 95 iliyo kwenye CD au diskette, na Windows 95 iliyo tayari kwenye kompyuta. (ANGALIA: Maelezo ya kuiweka DCC yaliyotolewa kwenye makala iliyopita kimakosa hayakutaja hatua ya "Add/Remove Programs" kama ilivyo hapo juu. Tafadhali fanya masahihisho). Kama Windows 95 ya kwenye diskette haiafikiani na Windows 95 iliyo kwenye kompyuta, kwa mfano, kompyuta inaweza kutoa agizo uweke diskette nambari 12, na ukiiweka ikakwambia tena uiweke diskette nambari hiyo hiyo. Ikitokezea hivyo usishituke. Wewe jaribisha tu kuweka diskette nambari 2, na ikigoma weka nambari 3, na kuendelea hivyo hivyo mpaka faili linalohitajika litakapoonekana. Kazi hiyo si rahisi na inachukua muda mrefu. Kupunguza kazi, na kunusuru muda, kama kompyuta yako ina nafasi ya kutosha, basi tengeneza jalada jipya lenye jina "win95disks" na zinakili diskette zote, moja baada ya nyengine, kwenye jalada hilo. Wakati unapoiweka DCC kwa kutumia utaratibu tuliouleza hapo juu, chagua "Have Disk" kwenye kidirisha kitakachojitokeza, na kisha ieleze kompyuta wapi ilipo Windows 95 kwa kuandika, kwa mfano, C:\win95disks kwenye kisanduku kilicho chini ya maandishi "Copy manufacturer’s files from:". Kitu chengine ambacho hatukukieleza kwa kina kwenye sehemu ya kwanza ya makala hii ni kuwa, ili DCC ifanye kazi, ni lazima kila kompyuta iwe na jina, yaani "Share name", na pia ni lazima iwe na jina la "Workgroup". Kama kompyuta yako haina taarifa hizo, basi unaweza kuziweka kwa kutumia Start -> Settings -> Control Panel -> Network -> Identification. Unaweza kuzipa kompyuta zako majina yoyote yale, kwa mfano kompyuta moja unaweza kuipa jina, (yaani Share Name), "MYPC1", na nyengine ukaipa jina "MYPC2". Lakini, Workgroup ni lazima iwe hiyo hiyo kwenye kompyuta zote mbili. Kwa urahisi, kwenye sehemu ya Workgroup, unaweza kujaza neno "WORKGROUP", kwenye kompyuta zote mbili. Jambo jengine muhimu ni kuwa, DCC inahitaji kompyuta zako mbili ziwe na uwezo wa kutumia protokali za utando (network protocols) zinazofanana. Ukitaka kujua protokali zinazotumia na kompyuta zako, bonyeza Start -> Settings -> Control Panel -> Network -> Configuration. Kama angalau protokali moja kati ya Microsoft IPX/SPX-compatible, NetBEUI, na TCP/IP, inaonekana kwenye kompyuta zote mbili, basi mambo mazuri. Kama hakuna protokali hata moja ambayo iko kwenye kompyuta zote mbili, itabidi uziingize protokali zinazohitajika kwa kubonyeza Add -> Protocol -> Add. Chagua "Microsoft" kwenye upande wa "Manufacturer", na uchague protokali unayoitaka kwenye upande wa "Network Protocol". Tunapendekeza kwenye kompyuta zote mbili uziweke protokali zote tatu tulizozitaja hapo juu. Protokali ya NetBEUI (Network Basic Input/Output System Extended User Interface), inahitajika kama utapenda kuwa na uwezo sio wa kupeleka majalada tu kutoka kwenye kompyuta moja kwenda nyengine, bali pia kuweza kuanzisha programu zilizo kwenye kompyuta ya pili. Kama haja yako ni kupeleka mafaili tu kati ya kompyuta mbili, basi protokali ya Microsoft IPX/SPX-compatible inatosha. Tulieleza kwenye sehemu ya kwanza ya makala hii kuwa ama unaweza kutumia parallel cable au serial cable. Ukienda kwenye maduka ya vifaa vya kompyuta, baadhi ya waya hizo utaziona kabisa zimeandikwa kuwa zinaweza kutumiwa kuunganishia kompyuta mbili. Hata hivyo, baadhi ya parallel ports, hasa za kompyuta za siku hizi, huwa zinahitaji parallel cables za aina maalum. Kwa hivyo, ikitokezea kuwa umefuata taratibu zote kama zilivyoelezwa kwenye makala hii, lakini bado ikashindikana kompyuta zako mbili kuunganishika, basi unaweza kuutuhumu waya ulioutumia. Ni vyema kama ni parallel cable ukaupata ule unaoweza kutumika kupelekea data pande zote mbili, yaani "bidirectional". Kuna baadhi ya nyaya siku hizi zinaandikwa hasa kuwa unaweza kuzitumia pamoja na Direct Cable Connection. Hizo ni za uhakika na ni vyema ukazitumia hizo. Tuliwahi kueleza kwamba kwa kutumia DCC, unaweza kuingiza programu kwenye kompyuta moja kwa kutumia CD iliyo kwenye kompyuta nyengine. Hiyo ni sahihi kabisa na inawezekana kwa programu nyingi sana. Lakini zipo baadhi ya programu ambazo wakati unapoziingiza kwenye kompyuta huhitaji kuianzisha upya (restart) kompyuta. Kama kompyuta inaanzishwa upya kama ni hatua ya mwisho kabisa ya kuingiza programu kwenye kompyuta ili tu kompyuta hiyo iweze kufanyakazi kwa kutumia mabadiliko yaliyofanywa, basi hakuna neno. Ile kompyuta isiyo na CD, yaani iliyofanywa kuwa "Guest", ndiyo itakayoanzishwa na mambo yatakamilika bila ya tatizo lolote. Lakini, kama kompyuta inaanzishwa mwanzoni kabisa au katikati, kabla ya kumalizika kwa hatua zote za kuiingiza programu mpya kwenye kompyuta, hapo kidogo kuna ugumu. Hiyo ni kwa sababu, unapotumia DCC, kompyuta ikianzishwa, kiungo cha Direct Cable Connection nacho hukatika. Sasa, kuna namna mbili. Wakati kompyuta itakapoanzishwa upya, kwa vile kiungo cha DCC kimekatika na CD iliyo kwenye kompyuta ya pili (yaani "Host"), haionekani tena, programu yako italalamika na kukueleza kuwa hailioni jalada lenye programu unayotaka kuiingiza. Hapo sasa, utahitaji kuanzisha tena DCC na kuziunganisha kompyuta zako kabla hujaendela na hatua zilizobakia. Lakini, kwa programu zenye tabia hiyo, tunashauri, kama unayo nafasi ya kutosha kwenye kompyuta yako, basi tumia DCC kuinakili CD yote kwenye jalasa moja kwenye ile kompyuta isiyo na CD, kisha uiingize hiyo programu moja kwa moja kwa kutumia jalada hilo badala ya CD iliyo kwenye kompyuta ya pili. Na programu nyengine zozote zile, hata zisizokuwa na tabia ya kuianzisha upya kompyuta, unaweza kuziingiza kwa haraka zaidi ukitumia njia hiyo. Kama CD umeinakili kwenye jalada C:\CDROM, basi kuingiza programu yako utatumia Start -> Run, na utaandika jila la programu ya kuanzishwa kama C:\CDROM\SETUP.EXE au mara chache, C:\CDROM\INSTALL.EXE. Liangalie hilo jalada uone kama kuna faili SETUP.EXE au INSTALL.EXE na tumia utakaloliona. Kunakili CD yote kuingia kwenye jalada fulani ni kazi rahisi sana. Kwanza tumia Windows Explorer -> New -> Folder kutengeneza jalada jipya - tuseme jina lake ni "CDROM" na liko chini ya "C:". Kisha kwenye hiyo hiyo Windows Explorer au My Computer, bonyeza kifungo cha kulia cha mouse juu ya jina, yaani "Share Name", ulioipa CD-ROM drive ya kompyuta ya pili. Kwenye kidirisha kitakazhotokezea chagua "Copy". Kisha bonyeza kifungo cha kulia cha mouse kwenye lile jalada jipya ulilolitengeneza, yaani C:\CDROM, na uchague "Paste". Ukifanya hivyo CD yote itanakiliwa kwenye jalada lenye jina C:\CDROM, na kuanzia hapo unaweza kulitumia jalada hilo kama ambavyo ungeweza kuitumia CD. Jambo jengine muhimu ni kutahadharisha tu kwamba, ingawa unaweza kutumia DCC kunakili majalada kutoka kwenye kompyuta moja ("Host") Kuingia kwenye kompyuta nyengine ("Guest"), kama majalada hayo ni ya programu iliyowekwa tayari na inafanyakazi kwenye kompyuta ya "Host", haina maana kuwa ukishayanakili majalada ya programu hiyo, utaweza pia kuitumia programu hiyo kwenye kompyuta ya "Guest". Hiyo ni kwa sababu, kuna mafaili mengine kadhaa, hasa yanayoishia na .DLL, .VBX, .OCX, .VXD, .DRV, n.k, ambayo huwekwa kwenye jalada C:\WINDOWS\SYSTEM, hayo yanahitajiwa pia kuwezesha programu mbali mbali kufanyakazi. Kama hukuyaingiza kwenye kompyuta ya "Guest", programu husika itakuwa haikukamilika na haitaweza kufanyakazi. Hata hivyo, si jambo la busara kuyanakili mafaili hayo kutoka kwenye "Host" kuingia kwenye "Guest" kwani kuna hatari ya kuweza kuharibu mambo. Vyema zaidi, kama inawezekana, uingize programu unayoitaka upya kabisa kwa kutumia CD ya programu hiyo.Kituchengine ambacho hakikutajwa kwenye sehemu ya kwanza ya makala hii ni kwamba, baada ya kuiingiza DCC kwenye kompyuta, mara nyengine ukiitumia DCC kunganisha kompyuta ni kiasi cha kubonyeza "Listen" kwenye kompyuta ya "Host" na kubonyeza "Connect" kwenye kompyuta ya "Guest". Ukibonyeza "Change" unapata nafasi ya kubadilisha kompyuta iliyokuwa "Host" kuwa "Guest" na iliyokuwa "Guest" kuwa "Host". Mwisho tungependa kueleza kwamba sio programu ya Direct Cable Connection tu inayoweza kutumiwa kuunganishia kompyuta mbili. Ziko programu nyengine kadhaa zinazouzwa, kama vile Laplink, au PcAnywhere, unazoweza kuzitumia badala ya Direct Cable Connection. Lakini kama cha "bure" kipo kuna haja gani ya kutumia cha kununua!? |
YALIYOMO
Wanawake Dodoma wataka mtoto aliyepigwa risasi akatibiwe nje Kesi za Mwembechai zaanza kusikilizwa Dondoo za saikolojia: Tuonavyo mambo Waraka wa Baraza Kuu kuhusu Parole Inawezekana kufanyika mdahalo kati
ya Waislamu na wasio Waislamu?
Teknologia
Serikali ihamie Dodoma kwanza !
Mahafali ya AMSIR Iringa
Bihawana Sekondari wafungua Ijumaa Vijana Shinyanga watakiwa
kuwa mfano mwema
Vyeo visiwasahaulishe majukumu
yenu- Sheikh Abri
Jiandaeni na kifo – Sheikh
Abdallah
Semina zawazindua wanawake
Bukoba
Waislamu wanaomaliza Kidato
cha Nne Tanga waaswa
Ndugu Kamuhabwa ndiye mwenye
chuki na AN-NUUR
'Ukombozi wa mwanamke si kugeuzwa
biashara huria'
Polisi walinda amani katika
muhadhara wa Wakristo
Mazengo wapewa uwanja wa
kujenga Msikiti
'Ajiengua Chuoni Z'bar kwa
kutoruhusiwa kuvaa hijab'
Shairi
|