AN-NUUR 
Na.172 Rajab 1419, Oktoba 23 - 29, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Mahafali ya AMSIR Iringa
Na Mwandishi Wetu

Jumuiya ya Kiislamu inayounganisha Waislamu waliopo mashuleni na vyuoni katika mkoa wa Iringa yaani AMSIR (Association of Muslim Students in Iringa Region) imefanya mahafali siku ya Jumamosi iliyopita tarehe Septemba 10, 1998, ya kuwaaga wanafunzi Waislamu wanaomaliza kidato cha nne, mwaka wa kwanza na wa pili katika shule mbalimbali na vyuo hapa Iringa. 

Shule zilizoshiriki katika mahafali hiyo ya aina yake zilikuwa ni Lugalo (Mwenyeji wa sherehe), Caglielo, Mwembetogwa, Ifunda Technical School, Tosamaganga, Ruaha Tech. School, Kalenga Sekondari, Kawawa na vyuo vilivyoshiriki ni pamoja na Veta Iringa, Chuo cha Maendeleo Rungemba, na Chuo cha Afya Iringa, bila kuwasahau wanafunzi Waislamu kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini kinachomilikiwa na Lutheran Mission. 

Katika mahafali hiyo mgeni rasmi alikuwa ni Sheikh Said Abri ambaye ni Mdhamini wa Taasisi ya Kiislamu Dhi-Nurayn ya hapa mjini Iringa. Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Ust. Swai kutoka Ofisi ya Kilimo Mkoa, Ust. Dhul-Kifki na Ust. Shaaban ambao ni Madaiya wa hapa mjini Iringa na pia Walimu walezi wa Waislamu katika shule mbalimbali pia walipata nafasi ya kuhudhuria hafla hiyo. 

Sherehe zilianza kwa dua, kufuatiwa na Qur’an, kisha wageni walitambulishwa na Makamu Mwenyekiti Ust. Mohamedi Taher kutoka VETA. Kisha ilifuata mada iliyolewa na Katibu Mtendaji wa kudumu wa AMSIR Ust. Seif. 

Wakitoa nasaha zao kwa wanaomaliza masomo yao, waalimu walezi na wanafunzi wanaobaki walisisitiza kuwa kumaliza kidato cha nne, mwaka wa kwanza au wa pili haina maana kuwa ndio mwisho wa kusoma bali wawe na moyo wa kuendelea zaidi na masomo. 

Akitoa nasaha zake Ust. kutoka Tosamaganga alitoa historia ya Waislamu na namna gani waliweza kuchangia katika maendeleo ya sayansi na elimu mbalimbali. Aliwakumbusha wale wanaomaliza kuwa na mwenendo mwema ili kuinua hadhi ya Uislamu huko waendeko. Aliwataka akina dada na Waislamu kwa ujumla kufuata utamaduni wa Kiislamu katika tabia zetu na hasa vazi la Hijabu kwa akina dada. 

"Hijabu zisivaliwe kwenye mahafali tu", alisisitiza. Ust. kutoka Lugalo yeye aliwataka Waislamu kutojihusisha na maovu kama vile uvutaji wa bangi, kunywa pombe, uasherati na uzinifu na pia wizi na uongo. 

Ust. Msumi ambaye ni mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini kitengo cha sheria yeye aliwaasa Waislamu kutoridhika na elimu kidogo waliyoipata. Aliwahamasisha waagwa kujitahidi kwa muda uliobaki ili wote wafanye vizuri kwenye mitihani yao. 

Akitoa mfuno wa namna gani Waislamu tunavyopata taabu kwa kutokujitegemea, alisema pale Tumaini matangazo yote muhimu yanatolewa baada ya salat ya Bwana na ni lazima Muislamu uhudhurie. 

Mwalimu mlezi wa Ifunda Sekondari aliwaasa Waislamu kufuata maadili mema. Kisha akafuata mwalimu mlezi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Ust. Salama ambaye yeye alianza nasaha zake kwa kuhoji kuwa kwa nini hivi leo licha ya wingi katika nchi bado Waislamu ni wachahce katika taasisi mbalimbali. Alitoa mfano shule ya Iringa Sekondari inachukuwa wanafunzi zaidi ya 500 lakini Waislamu hawazidi 50. Walimu waliopo pale ni 40 lakini Waislamu ni 3 tu. "Lazima kuna kitu", alionyesha wasiwasi wake. Suala la pili alilohoji lilikuwa ni suala la Waislam kukosa masomo muhimu wakati wakienda misikitini siku ya Ijumaa, mwalimu alisema hakuna sababu za msingi zinazowafanya wakuu wa shule kung’ang’ania ratiba zilizopo wakati inawanyanyasa Waislamu." Lazima tudai haki yetu hii alitilia mkazo suala hili. Waalimu walezi wa Lugalo na Fosa Maganga, Ust. Mbilili (Lugalo), waliwaasa wanafunzi kufuata mwenendo mwema popote wanapokuwa. 

"Tufuate na kuyaingiza katika Uislamu yale tu yanayokubalika katika Uislamu kutoka katika elimu hizi tunazopata mashuleni, kwani mfano huu wa elimu ni wa kimagharibi ambao ni maadui wa Uislamu", maneno haya yalisemwa na mlezi wa Waislamu wa shule ya wasichana wa Caglielo inayomilikiwa na Kanisa Katoliki. Ust.Shaabani yeye alitoa usia kuwa elimu iliyopotoea ni haki kwa Muislamu hivyo ichukuliwe pote inapopatikana.Ust.Swai alisisitiza ucha Mungu na kutubia makosa yetu. 

Akisoma risala kwa mgeni rasmi Mwenyekiti wa AMSIR Mkoani Iringa Ust. Sadick Suleimani Gogo alisema licha ya AMSIR kupata mafanikio kidogo ya kuziunganisha shule na vyuo na kuwa pamoja kwa mawasiliano ya mara kwa mara, kuhusu matukio mbali yanayohusu Uislamu, AMSIR ina matatizo kadha wa kadha. Kwanza ni suala zima la uchumi. AMSIR inategemea michango ya wanafunzi walioko mashuleni ambayo ni fedha kidogo na hazitoshelezi kuendeshea shughuli mbalimbali za AMSIR. 

Shughuli hizo ni pamoja na kuhakikisha kuwa AN-NUUR linaifikia kile shule yenye Waislamu hapa Iringa na kununua vitabu vya Elimu ya Dini ya Kiislamu. Tatizo lingine ni ukosefu wa Waalimu wa kufundisha somo la Maarifa ya Uislamu mashuleni na pia ukosefu wa vifaa vya kufundishia na vitabu vya rejea kwa wanafunzi wanapotaka kusoma wenyewe. Sasa hivi kuna waalimu wachache wa kujitolea wanaofanya jihadi katika baadhi ya shule za Sekondari kama vile Ifunda, Mkwawa na Chuo cha Ualimu cha Krelu. Hata hivyo katika muhula ujao AMSIR imeandaa utaratibu wa kuwafanya wanachama wake ambao ni wanafunzi wote Waislamu kutoa michango kila mwezi ili kufanikisha shughuli zake. 

Akijibu risala ya Mgeni rasmi Sheikh Abri alisema, tatizo la uchumi linaweza kutatuliwa na sisi wenyewe kwa mipango tu. 

Alitoa mfano kuwa Waislamu tumejisahau mno kwani tunafikiri kuwa anayewajibika kutoa zaka ni tajari tu, kumbe zaka ni faradhi kwetu. 

Aliwataka waalimu walezi kushirikiana na taasisi zilizopo Mkoani hapa kutatua baadhi ya matatizo ya wanafunzi. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 

TAHARIRI 
Kuangukia makaa hakuna nafuu kwa aliye kikaangoni 

Wanawake Dodoma wataka mtoto aliyepigwa risasi akatibiwe nje 

Kesi za Mwembechai zaanza kusikilizwa 

Fitna ya Bakwata 

Dondoo za saikolojia: Tuonavyo mambo 

Waraka wa Baraza Kuu kuhusu Parole 

Inawezekana kufanyika mdahalo kati ya Waislamu na wasio Waislamu? 
Na Nandenga wa Mkomidachi 

Teknologia 
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (2) 
Na Hassan Omar 

Serikali ihamie Dodoma kwanza ! 
Na. Said Rajab 

Mahafali ya AMSIR Iringa 
Na Mwandishi Wetu 

Madrasatul Nnajjary Islamiya 

Ijue Madrasatul Riyaadh 

Bihawana Sekondari wafungua Ijumaa 

Vijana Shinyanga watakiwa kuwa mfano mwema 
Na Jihad R. Saballa, Shinyanga 

Vyeo visiwasahaulishe majukumu yenu- Sheikh Abri 
Na Mwandishi Wetu, Iringa 

Jiandaeni na kifo – Sheikh Abdallah 
Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

Semina zawazindua wanawake Bukoba 
Na Nadhiru Ishengoma 

Waislamu wanaomaliza Kidato cha Nne Tanga waaswa 
Na Ibn Mohamed 

Ndugu Kamuhabwa ndiye mwenye chuki na AN-NUUR 
Mwandishi: Maalim Bassalah 

'Ukombozi wa mwanamke si kugeuzwa biashara huria' 
Na Japhary Lemah, Arusha 

Polisi walinda amani katika muhadhara wa Wakristo 
Na Badru Kimwaga 

Mazengo wapewa uwanja wa kujenga Msikiti 
Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

'Ajiengua Chuoni Z'bar kwa kutoruhusiwa kuvaa hijab' 
Na Seif Hamad Suleiman, Zanzibar 

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Shairi 
Simlazimishe Yesu ukombozi wa ulimwengu (jibu)  

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita