|
|
| Ujumbe wa
waandishi kwa Bw. Batendi, Wakristo:
Isaya 9:6 hakuagiza Yesu aitwe Mungu
Na Muhibu Saidi KUPITIA gazeti hili toleo la Agosti 28, hadi Septemba 3, 1998 nilipokea ujumbe kutoka kwa rafiki yangu (Mkristo), Bw. Elia Batendi ndani ya barua yake iliyokuwa na kichwa "ujumbe kwa waandishi". Pamoja na kuhitaji tumsaidie kujibu maswali yake kdhaa, ametumia fursa hiyo (ya ujumbe) kutushutumu mimi, Bw. Abdul Ghulam na Waislamu wengine kwa ujumla kwamba ni wanafiki kwa kile alichodai kuwa tumekuwa tukiisoma Biblia kwa kuchagua aya tunazotaka kuzisikia, lakini aya ambazo ni kali kwetu hatuthubutu kuzisoma! Akitoa shutuma hizo, Bw. Batendi anasema Bw. Muhibu aliandika kuhusu Yesu au Isa na Bw. Gullam aliandika kuhusu Ukristo na Ujamaa vimeshindwa. Akaendelea kusema mabwana hawa wawili wamejitahidi kunukuu aya mbalimbali za Biblia ili kutetea hoja zao, pia wote wawili wamemshambulia Mtume Paulo. Bw. Gullam anadai Ukristo uliasisiwa na Paulo na Bw. Muhibu anadai Paulo ndiye aliyezua kuwa Yesu alikufa kisha kufufuka. Huku akimsisitizia Mhariri wa gazeti hili kutufikishia ujumbe wake huo, Bw. Batendi alitoa aya ya Mathayo 15:24 Yesu aliyosema "Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli" aliyodai sisi kupenda kuinukuu na kuacha nyingine ya Yohana 10:16 aliyodai inaendeleza kuwa Yesu alisema anao kondoo wengine ambao siyo wa zizi hili (Waisraeli). Aya nyingine aliyodai kuwa Waislamu hatuinukuu ni Isaya 9:6 inayosema: "Tumepewa mtoto mwanaume, ataitwa Mshauri wa Ajabu, Mungu mwenye Nguvu", badala yake tunazua uongo kuwa Wakristo ndio walioanza kumwita Yesu ni Mungu. Aidha, akishutumu tabia ya kuchagua maandiko ya Biblia, Bw. Batendi alisema hiyo ni sawa na Mkristo anukuu Qur'an Suratu An Nah 16:81 kuwa Mwenyezi Mungu amekufanyieni kanzu zinazowakingeni na joto (na baridi) na kisha Mkristo huyo atafsiri kuwa kumbe Mungu wa Waislamu ni fundi cherehani anawashonea Waislamu kanzu - ni vyema? Pamoja na hayo, itakuwa si Akhlaq uelee hewani. Kwa mantiki hiyo, binafsi yangu kwanza napenda kukiri rasmi kupokea ujumbe huo (wa Bw. Batendi) kwa moyo mkunjufu wa kiungwana (Uislamu). Hata hivyo, kabla sijaingia katika mjadala huu husika ningependa awali ya yote kumsihi Bw. Batendi jambo muhimu. Katika ujumbe wake huo amezitaja aya zilizomo katika Suratul Araaf: 203 na Suratu Tawba :64 kama ushahidi unaounga mkono kile alichodai "unafiki wetu" wa usomaji wa kuchagua aya tunazotaka kuzisikia. Kwa faida ya wasomaji ningeomba nizinukuu hapa chini aya hizo kama zilivyo: "Na usipowaletea aya (wazitakazo) husema kwanini hazizuii (mwenyewe)? Sema nayafuata yaliyofunuliwa kwangu kutoka kwa Mola wangu. Hizi (aya za Qur'an) ni dalili (kubwa za ukweli wangu) zitokazo kwa Mola wenu na ni uongofu na rehema kwa watu wanaoamini"" (7:203). "Wanafiki wanaogopa kuteremshiwa sura itakayowatajia (unafiki wao) uliyomo katika nyoyo zao. Sema fanyeni tu mzaha, hakika Mwenyezi Mungu atayatoa nje hayo mnayoyaogopa". (9:64) Kwa kweli mtu kama Batendi ambaye anaonekana dhahiri kuwa mstari wa mbele katika mambo ya dini na kutazamiwa kuwa na mafundisho ya busara kwa watu, hastahili kutoa shutuma hizo hasa katika hali ambayo inaonyesha wazi binafsi yake hajiamini na anayoyadai. Tena wakati huo huo anataka ajibiwe maswali yake! Baya zaidi ni kule kutumia aya hizo za Qur'an Tukufu hapo juu kama ushahidi wake wakati aya hizo kamwe hazihusiani kabisa na madai yake hayo potofu. Aya hizo zinachoeleza ni kuhusu aya ambazo zilikuwa bado hazijateremshwa kabisa. Ndio Makafiri na Wanafiki wa zama za kuteremka kwa Qur'an wakawa wakimghasi Mtume (saw) wakitaka zishuke aya zile tu zitakazokidhi mahitaji yao (Al- Araaf :203). Pia Wanafiki wakawa wanaogopa zisishuke aya zitakazofichua unafiki wao walioficha (Atawba :64). Tofauti na ukweli huo juu, aya hizo za Biblia ambazo Bw. Batendi anadai eti hatuthubutu kuzisoma, kwa kweli hizo tayari zipo. Isipokuwa Wakristo wameshindwa kuzielewa. Pili, kuibua madai haya mapya, kunadhihirisha wazi kwamba Bw. Batendi ambaye ndiye mwanzilishi wa mjadala wa Yesu na Isa kupitia gazeti moja la kidini (siyo ANNUUR) litokalo kila wiki mara moja hana tena hoja za kutofautisha historia ya Yesu na Isa. Tatu, pamoja na kumfanyia Mwenyezi Mungu istihzai (mchezo, kwa kweli maneno kwamba "Mungu wa Waislamu ni fundi cherehani anayewashonea Waislamu kanzu" hayadhihirishi isipokuwa ni kwa kiasi gani Bw. Batendi amedhamiria makusudi kumkejeli Mwenyezi Mungu, kwani maneno hayo hayamo kabisa katika aya ile ya Qur'an (An-Nahl: 81) aliyoitaja mapema na wala hayahusiani kabisa na lawama anazowatwika Waislamu kuhusiana na madai yake hayo. Tunachokifanya Waislamu ni kuzitaja aya za Biblia na Qur'an zinazothibitisha waziwazi mambo tofauti kama vile upweke wa Mwenyezi Mungu katika Uungu wake (Qur'an 112:1 na Marko 12:29), Utume wa Yesu kwa wana wa Israeli (Qur'an 3:49 na Mathayo 15:24) n.k. Wanachotakiwa Wakristo nao kukifanya ni kuvunja hoja zetu hizo na siyo kukejeli kama anavyofanya Bw. Batendi hapo juu. Nne, madai yake (Bw. Batendi) kuwa ndani ya Biblia kuna aya ambazo sisi tunapenda kuzisikia na nyingine ni kali kwetu ambazo amedai hatuthubutu kuzisoma, yanadhihirisha kwamba kwenye Biblia kuna maneno yanayopingana. Na sababu yake kubwa ni kama ile aliyosema Bwana Paulo kwenye waraka wake kwa Wagalatia kwamba kuna "Injili ya waliotahiriwa" na "Injili ya wasiotahiriwa" (Wagalatia 2:6-8). Sisi Waislamu mara kwa mara tunazingatia Injili ile ya Waliotahiriwa aliyoiacha Bwana Yesu. Kwa mfano Bwana Yesu katika Injili ya Waliotahiriwa alisema: "Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli" (Mathayo 15:24). "Yesu akamjibu, sikia Israeli Bwana Mungu wetu ni Bwana Mmoja". (Marko 12:29) n.k. Lakini wengine kwa kuzingatia Injili ya Wasiotahiriwa ndio wanaotoa madai kama hayo ya akina Batendi. |
YALIYOMO
TAHARIRI Hakuna Muislamu aliyekufa kutokana na vurugu Mgogoro wa kiwanja Duma: Wakatoliki wasema kuna njama za Waarabu Same Na Mwandishi Wetu Wanawake wakutana Mwanza na kusema: Kunyanyaswa sasa basi Na Mwandishi Wetu, Mwanza Sheikh Omar Bashir ataka Waislamu waimarishe mshikamano Na Said Sharif Ustaadhi Abdallah Mfoyi afariki Na Muhibu Saidi Baraza Kuu halina Katibu Nguruka - Sheikh Kilima Na Abu Adli Viongozi Msikiti wa Ubungo Darajani waitwa polisi Na Kassim Juma Marekani `ilivyosaidia' Mujahidiin Barua ya mtoto wa miaka minne toka Lebanon kwa Bibi Hillary Clinton Ujumbe wa waandishi kwa Bw. Batendi, Wakristo Na Muhibu Saidi Waislamu wanadhalilishwa au wanajidhalilisha Tusiwe Jogoo wa Esopo na Almasi Na MAALIM ALI BASSALEH Sherehe za wiki ya usalama barabarani: Kauli nzito za waheshimiwa zimekalia kuti kavu Na Said Omar Mwanasayansi Avicenna: Tabibu bingwa. Na Dk. A. A. Amur Ujenzi wa Msikiti wa Ijumaa Mriti waanza Na Nasib A. Mziray Kutoweka kwa hazina adimu za kimazingira Na Yassir Salim Mfalme Najashi ni mfano bora wa kuigwa kwa watawala Na Idi Kikong'ona Waislamu Moro wasaidia wagonjwa Na Mwandishi Wetu, Morogoro KUFUATIA KUTISHIA MAGAZETI: Sheikh Ayoub amjibu Askofu Rajab Rajab Na Mussa Ally TAMSA Tanga waahidi kuendeleza mema Na Ibn Mohammed, Tanga Ufugaji, uuzaji nguruwe wakera wananchi Dar Na Mwandishi Wetu Mafundisho ya Quran Kuwepo kwa ufufuo Barua za wasomaji
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org