|
|
| Ujenzi
wa Msikiti wa Ijumaa Mriti waanza
Na Nasib A. Mziray KIJIJI cha Mriti kiko katika tarafa ya Ugweno wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, kina jumla ya kaya 396, katika kaya hizo kaya kumi na moja ndizo za Wakristo tu, kaya 385 ni za Waislamu. Waislamu wa kijiji hicho wamekuwa wakisali sala ya Al-Ijumaa katika kijiji cha Kifula na Mwaniko kwa miaka mingi, vijiji ambavyo viko mpakani na Mriti. Ila Misikiti imejengwa katikati ya vijiji hivyo. Hii kufanya mtu kutoka Mriti kwenda Mwinuko kusali Aljumaa kuwa mbali na kutoka pia Mriti kwenda Kifula pia kuwa mbali. Hali hiyo huwafanya wazee wa Kiislamu kukosa sala ya Aljumaa kwa sababu ya umbali huo. Katika kijiji cha Mriti kuna Msikiti mdogo ambao Waislamu wameamua kuanzisha sala ya Aljumaa tangu mwezi Oktoba, 1997. Pamoja na kwamba Waislamu wanaosali nje ya Msikiti huo ni wengi kushinda wanaosali ndani kutokana na udogo wa Msikiti huo, mvua huwanyeshea waumini mara kwa mara lakini huendelea kufanya ibada hiyo bila matatizo kwani wameazimia kwamba watakapokuwa wanasali hapo kwa tabu ya mvua na jua ndipo watapata moyo wa kujitolea mali zao na nguvu zao ili kujenga na kuepukana na hiyo adha. Pia Waislamu hao wameazimia kwamba baada ya Msikiti kukamilika wataanza ujenzi wa Chuo cha Ufundi na Qur'an. Sababu hasa ya kutaka kujenga hicho chuo ni ili kumuandaa kila kijana atakayesoma hapo awe amepata elimu na ujuzi na kumfanya aweze kumudu maisha yake vizuri na kutumia jasho lake mwenyewe. Waislamu wa kijiji cha Mriti wanaomba msaada kwa Muislamu yeyote kwa ajili ya kumaliza ujenzi wa Msikiti na ujenzi wa Chuo. Msaada huo upitishwe kwenye ofisi za gazeti la ANNUUR Dar es Salaam.
Kutoweka kwa hazina adimu za kimazingira Na Yassir Salim MAUMBILE ya dunia, misitu, mimea na mfumo mzima wa ikolojia hutoa tafsiri ya maneno ya Muumba pale aliposema: "Litukuze jina la Mola wako aliye Mtukufu. Aliyeumba (kila kitu na) akazitengeneza. Na akakikadiria (kila kimoja jambo lake) na akakiongoza (kufanya jambo hilo)" (87:1-3) - (Angalia pia 32:7. 25:2, 54:49). ALLAH (sw) amezitengeneza mizani asilia za kimaumbile kwa lengo la kusahilisha maisha yetu ya kila siku. Mizani asilia (maumbile) karibu zote hutulinda na maafa ya kimazingira. Maafa mengi huzuiwa na kazi nyeti zisizoonekana kirahisi zinazofanywa na milima, misitu, bahari, ozoni leya n.k. Kazi nzuri za baadhi ya maumbile haya huonekana na zingine si rahisi kuonekana kwa macho. Katika mfumo wa maumbile aliouweka Allah (sw) kila kiumbe kina nafasi yake na lengo lake. Kila kimoja huongozwa na Allah (sw) katika kufikia lengo la kuumbwa kwake. Binadamu kwa njia ya utafiti na kuelimishwa, polepole anaanza kutambua umuhimu wa kuwepo maumbile haya katika maisha yake ya kila siku; na anaanza kufahamu kuwa Allah (sw) ameumba kila kiumbe kwa lengo maalumu. Ni ukweli uliowadhihirikia hivi sasa wanasayansi kuwa bila msaada wa maumbile asilia naviumbe hai binadamu hataweza kuishi maisha ya salama. Kulingana na utafiti uliofanywa na wanasayansi, " viumbe vyote hai huhitajiana katika kuendeleza na kudumisha uhai na maisha yao asilia". (Angalia Sayyid Qutb, Fy Dhilali al Qur'an, Sherehe ya Suuratul A'la). Sisi sote tunahitaji msaada wa kimazingira na pia tunahitaji zawadi asilia zenye kutokana na mazingira na viumbe hai kama ngozi, mbolea, asali, chakula na madawa. Uharibifu wa misitu ya mvua ya kitropiki, misitu asili na misitu ya kuotesha unaleta taathira kwa ikolojia, mazingira na binadamu. Hivyo kuingilia kati malengo maalumu ya maumbile yaliyowekwa na Muumba yenye kufanikisha uhai wa binadamu na lengo la kuumbwa kwake. Baadhi ya taathira zinazoletwa na uharibifu wa Misitu ni: Kwanza, kunyima na kudhulumu jamii asili (tribal communities) zenye kuishi na kutegemea misitu hii katika kutosheleza mahitaji ya maisha yao ya kila siku. Hivyo uharibifu wa misitu unaidhulumu jamii asili haki zao za kijamii za kupata ardhi salama, chakula na makazi mazuri. Pili, uharibifu wa misitu unasababisha mmomonyoko mkubwa wa ardhi na kupotea kwa udongo mwingi wenye rutuba. Kuondoka kwa uto wa asili na utando wa mimea katika ardhi ni sababu kuu za kupatikana mmomonyoko wa ardhi. Kuja kwa mvua kali au za kawaida kutasababisha kuchukuliwa udongo wenye rutuba na kutupwa kwenye mito au maziwa; hivyo kupelekea uharibifu wa ardhi zinazofaa kwa kilimo na mashamba. Tatu, uharibifu wa misitu unaleta mabadiliko ya hali ya hewa ya muda mrefu. Misitu, miti, mimea na uoto wa asili imeumbwa na Mjuzi Mwingi wa Rehema kwa lengo maalumu. Kuharibiwa kwa maumbile haya kunaleta mabadiliko hatari ya kimazingira. Kwa mfano, misitu hupeleka maji angani kwa njia ya mvuke na hivyo kutuletea mvua zenye manufaa makubwa kwetu. Hivyo, vyanzo vya maji vinapotea, mvua zitapungua, mimea na dawa adimu za mitishamba. Misitu na mimea yenye hunyonya hewa chafu "kabondaioksaidi" kutoka angani na kuihifadhi. Ukataji miti na utowekaji wa asili kwa njia ya mmomonyoko wa ardhi unapeekea kabondaikoksaidi kuongezeka angani. Kuongezeka kwake kupita kiwango asilia japo kwa kiasi kidogo kutasababisha wastani wa kiwango cha joto cha dunia kupanda. Hivyo kuyeyusha mabarafu (visiwa vya barafu vilivyopo hapa duniani) na kuleta mabadiliko hatari katika usawa asilia wa bahari. Nne, uharibifu wa misitu kwa njia ya ukataji miti na uchomaji moto hupelekea kupunguka na kupotea kwa aina mbalimbali za mimea, mbegu asili na viumbe hai ambayo vyote ni muhimu kwa kuhifadhi maisha na uhai wa binadamu. Taathira inayopatikana kwa kupotea mimea na mbegu asilia ambayo idadi kubwa bado haijafanyiwa utafiti inaitwa `genetic erosion'. Inakisiwa itakapofika katikati ya karne inayokuja, robo ya 250,000 ya aina ya mimea yenye kujulikana na yenye manufaa kwa binadamu itapotea kwa njia mbalimbali. Zikiwemo za ukataji miti, uchomaji moto misitu, mabadiliko ya wakulima kwenda kwenye zao moja, ufugaji wa wanyama wengi kwenye eneo moja lisiloweza kuhimili wingi wa wanyama na vijiji kugeuka kuwa miji. Taathira yenye kupatikana japokuwa misitu itakatwa kwa malengo mazuri ya kiuchumi kama kupata mbao, kutengeneza njia za usafirishaji; au kwa ajili ya fanicha na vifaa vya nyumbani au ujengaji wa makazi ya watu. Malengo haya yenye kuonekana mazuri kiuchumi pamoja na uchomaji moto misitu ndio sababu kuu ya upoteaji mkubwa wa hazina adimu alizoweka Muumba katika mazingira. Hapa tutajaribu kiundani kuangalia upoteaji wa hazina adimu na taathira tunayopata katika kilimo na tiba. Taathira katika kilimo Ukataji miti na uchomaji moto misitu unasababisha kupotea kwa mimea na mbegu zenye faida za kiajabu katika kilimo. Uwezekano wa kuwa moja ya mbegu au mmea unaopotea kuwa na sifa ya kiasili `gene' ambayo huweza kuleta mapinduzi ya aina fulani ya kilimo. Mifano hai yenye kuthibitisha ukweli huu ipo mingi. Mfano, mpunga unaoitwa `wheatland rice' kutoka Uturuki umethibitika kuwa na kinga ya maradhi yenye kuigharimu Marekani dola 50 milioni kila mwaka. Mfano mwingine ni mtama unaoitwa `Ethiopian barley' wenye kutoa kinga dhidi ya virusi vyenye kuogopwa vya rangi ya njano kwa zao la thamani ya dola milioni 160 la California. Kwa mifano hii, tunaweza kusema kila mmea au mbegu inayopotea ni sawa sawa na kupoteza hazina moja adimu ya kimazingira. Taathira katika tiba Allah (sw) hajajalia ugonjwa usiokuwa na tiba. Haya ni maneno ya Mtume (saw) ambayo ni changamoto yenye kutoa mwanga kwa watafiti na wanasayansi wote duniani hasa katika utafutaji wa tiba ya maradhi yasiyokuwa na dawa. Kwa sera hii ya Mtume (saw) tunaweza kusema kila mmea, mbegu au kiumbe kinachoondolewa katika uso wa ardhi ni sawasawa na kuipunguzia dunia uwezo wa kutibu maradhi. Tunapoharibu makazi ya mimea, mbegu na viumbe hai (misitu) tujuwe tunaharibu na kuua vitu vyenye manufaa makubwa katika kilimo na tiba. Baadhi ya chembechembe zinazotolewa kwenye mimea zinatumiwa katika kutengeneza madawa ya aina mbalimbali ikiwemo asprin. Katika Marekani peke yake imekadiriwa karibu asilimia ishirini na tano ya madawa yote wanayoandikiwa wagonjwa kila siku asili yake ni mimea. Mfano, atropine kutoka mmea unaoitwa Atropa belodona. Cadeine na Morphine kutoka Opium poppy, Paparem Somniferum. Quinine dawa maarufu yenye kutibu malaria inatoka kwenye magome ya mti unaoitwa Cinchoma. Imegundulka karibu asilimia thamanini ya madawa muhimu yanaweza kupatikana kutoka kwenye mimea tena kwa gharama ndogo kuliko kutengenezwa kwenye maabara. Mmea aina yoyote ile si vizuri kudharauliwa. Hata mmea unaoonekana hauna umuhimu siku moja unaweza ukaonyesha maajabu katika maduka ya dawa kadri sayansi na teknolojia vitakavyoendelea kupiga hatua. Mfano watafiti wa magonjwa ya ukimwi wamegundua aina ya dawa katika mizizi ya tango la Kichina ambayo inaweza kufanya kazi dhidi ya Ukimwi. Dawa ingine ambayo inafanyiwa uchunguzi yenye uwezo wa kutibu ugonjwa wa kansa ya damu kwa watoto na melanoma inatoka katika miti inayostawi hasa katika misitu ya mvua. Mimea muhimu ya aina mbalimbali yenye kutarajiwa katika utafiti wa madawa ipo hatarini kupotea hata kabla binadamu hajajua namna ya kuzifanyia kazi sifa pekee za mimea hiyo. Mfano hai ni mmea wa familia ya Periwinkle Aprocynaceae kwa jina la kitaalamu Cahtaranthus Coriaceus unapatikana kwa idadi ndogo Madagascar ni wenye kutishiwa kupotea kwa kuchomwa moto na kuliwa na wanyama. Mmea huu unaweza kuleta mapinduzi makubwa katika tiba ya kansa ijapokuwa tiba inayotokana nayo bado haijathibitishwa. Ni jukumu letu kulinda urithi wetu asili wa mazingira, kwa ajili ya manufaa yetu na vizazi vijavyo. Kama Makhalifa waadilifu tusikubali kushiriki au kuchangia katika dhulma ya kimazingira inayoendelea kufanyika dhidi ya jamii duniani na hapa nchini. Pia hatuna budi tuanze kutambua na kuthamini kazi zinazofanywa na misitu, maumbile asilia na msaada tunaopata kutokana na mazingira salama.
Mfalme Najashi ni mfano bora wa kuigwa kwa watawala Na Idi Kikong'ona KUTOKA kwenye historia ya Mfalme Najashi wa Ethiopia kuna mafundisho mengi yaliyo bora na yanastahiki kuigwa na watawala wa sasa, hasa wale wanaongoza serikali zisizokuwa na dini ya taifa. Najashi alikuwa mfalme Mkristo mpenda haki, muadilifu, aliyejali na kuheshimu uhuru wa kuamini, kufuata na kutangaza dini. Alichukizwa na kitendo cha watu kuteswa na kuuawa kwa ajili ya kuamini kwao Mungu moja na kuitangaza imani hiyo kwa walimwengu. Japo walikuwa si raia wa nchi yake na vile vile ni watu walioamini kinyume na aaminivyo yeye, Najashi aliwalinda na kuwapa hifadhi watu hao kwa sababu tu ya kujali na kuthamini uhuru aliopewa binadamu na Muumba wake, wa kuamini, kufuata na kuitangaza anayoamini kwa walimwengu. Hebu tusafiri kidogo ili tuone katika historia ya utawala wa Mfalme Najashi wa Ethiopia wakati wa zama za Mtume Muhammad (saw) mambo yalikuwaje. Wakati binadamu walipoacha muongozo wa Allah (sw), kubobea na kuzama katika mamlaka ya Shirk, na binadamu wachache kujipachika mamlaka ya Allah (sw) kwa kuwatungia wengine sheria zilizowagawanya katika matabaka na kuwakandamiza waliochini, Allah (sw) kwa Rehema zake akamteua na kumtuma Mtume Muhammad (saw) kuja kuwatoa na kuwakomboa binadamu katika Shirk pamoja na dhulma waliyokuwa wakifanyiwa. Mtume (saw) alianza kuondoa utumwa wa kifikra kwa kufundisha binadamu ni nani hasa Muumba wao, mamlaka yake na haki zake kwa viumbe. Kisha akawafahamisha binadamu kuwa lengo la maisha haya ni kutii na kufuata sheria za Muumba. Ni wale tu watakaofuata sheria za Muumba watakaopata maisha ya amani na utulivu hapa duniani pamoja na maisha ya furaha yenye kudumu huko Akhera. Na wale watakaofuata sheria zilizo kinyume na zile za Muumba, wataishi maisha ya dhiki hapa duniani na adhabu zisizokwisha huko akhera. Watu wakatanabahi, kwa hiari yao wakaanza kujitoa katika makucha ya madhalimu na kuufuata muongozo wa Mola wao. Watawala wa Kikuraish wakaona kuwa maslahi yao yako hatarini, na hawatopata tena nafasi ya kuwagawa watu katika matabaka na kuwanyanyasa. Wakaanza kuwatesa na kuwaua wale waliofuata ujumbe wa ukombozi. Mateso yalipozidi kwa Waislamu kwa sababu tu ya kuamini kwao umoja wa Allah, kuyakubali mamlaka yake na kuitafsiri imani yao kivitendo, Mtume (saw) akawaruhusu Waislamu kuhamia Ethiopia (Uhabeshi) na kuwaambia kuwa: "Huko kuna mfalme asiyedhulumu na kumnyanyasa mtu kwa sababu ya imani yake. Chini ya uongozi wa Bwana Jafari bin Abitalib (ra) Waislamu wakafunga safari kuelekea Ethiopia na kuyaacha makazi yao na baadhi ya ndugu zao Waislamu. Watawala wa Kikuraish walipopata habari wakawatuma vijana wenye silaha ili kuwazuia Waislamu, lakini hawakufanikiwa. Kana kwamba haikutosha, wakawatuma vijana maarufu na walio weledi wa kupandikiza fitna huko Ethiopia. Wakawapa na zawadi zenye thamani kubwa ili kuwashawishi viongozi wa Ethiopia pamoja na Mfalme wawakubalie matakwa yao. Walipofika wakazigawa zawadi kwa wale wasaidizi wa Mfalme na kuwaambia: " Hivi karibuni baadhi ya vijana wetu wasiofahamu na wasio na uzoefu wameacha dini yetu na wala hawakuingia katika dini yenu na sasa wamekuja katika nchi yenu. Viongozi na wakubwa wetu wametutuma kuja kwenu na kuwaombeni muwafukuze na kutukabidhi sisi. Tunawaomba mtuunge mkono pindi tutakapofikisha suala hili kwa Mfalme". Wakafika kwa Mfalme, wakampa zawadi na kumueleza shida yao. Viongozi wote waliomzunguka Mfalme wakaunga mkono madai ya wajumbe wa Kikuraish na kusisitiza kuwa Waislamu wafukuzwe. Najashi, Mfalme Mkristo aliye muadilifu akasema: " Si sawa nitoe hukumu ya kuwafukuza watu waliokilimbia nchini mwangu. Kwa kuwa watu hawa wanaweka imani na tumaini katika nchi yangu, nitawaita na kufanya uchunguzi kisha nitahukumu". Wakiongozwa na Jafar (r.a) Waislamu wakaingia Ikulu kuitikia wito wa Mfalme. Mbele ya jopo la viongozi waliopokea zawadi na wajumbe wa Makuraish, Mfalme akawauliza Waislamu: "Hii dini yenu mpya ni dini gani ambayo inatofautiana na dini yenu ya zamani na dini yetu?" Jaafar akajibu: "Sisi tulikuwa watu wajinga, tukiabudu masanamu, tukila mizoga, tukifanya uasherati, tukiwatendea vibaya majirani na wenye nguvu kati yetu walikuwa wakiwanyanyasa na kuwakandamiza wanyonge. Mwenyezi Mungu akamteua Mtume miongoni mwetu ambaye tunaujua ukweli wake na uaminifu wake. Yeye akatufundisha kumwabudu Mungu mmoja tu na kutukataza kuyaabudu masanamu, ametuamrisha tusema kweli, tuhifadhi amana, tuwapende majirani na tuwaheshimu watu. Ametukataza kusema uongo, tusitende maovu, tusiwanyanyase yatima na kuwadhalilisha wanawake. "Sisi tumemwamini yeye, tumesadiki na kufuata maamrisho yake. Lakini wakubwa wetu wakatupinga na kutuamuru tuyaache maamrisho hayo na turejee kwenye kufru. Kwa kuwa tulikataa na tukaendelea kuwakumbusha, wakatuadhibu na kuwaua baadhi yetu. Hii ndiyo sababu ya kuhamia nchini kwako". Mfalme Najashi akauliza: "Je, unaweza kutusomea chochote alichoamrisha Mtume wenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu?" Jafar akasoma baadhi ya aya katika sura ya 19. Najashi, viongozi pamoja na watalaamu wa Kikristo wakatokwa na machozi bila ya kujizuia. Mfalme Najashi akasema: "Naapa kwamba ukweli aliousema Isa (as) ndiyo huu, na kwamba maneno haya na maneno ya Isa yanatokana na chimbuko moja! Na sitawakabidhi ninyi ( Waislamu) katika mikono ya watu hawa". Kisha akawageukia wajumbe wa Makuraish: "Sichukui rushwa! Chukueni zawadi zenu muondoke!" Hapa kwetu Tanzania, nchi isiyokuwa na dini ya taifa, yenye kufuata Katiba inayompa kila raia uhuru wa kufuata dini anayoitaka na kuihubiri kwa wengine' Waislamu wanateswa, kudhalilishwa na kuuawa kwa sababu yaliyotolewa na Paroko dhidi ya Waislamu inayodaiwa kukashifu dini ya watu wengine. Najash alikuwa Mfalme Mkristo na Ukristo ulikuwa ndiyo dini ya Taifa; Waislamu hawakuwa raia wa nchi yake, pamoja na kufikishiwa madai kutoka kwa wajumbe wa Makuraishi ya kwamba Waislamu waliokimbilia nchini kwake, walikuwa wanaamini na kuhubiri imani iliyo kinyume na ile aliyonayo yeye, bado aliona umuhimu wa kuyafanyia uchunguzi wa kina madai hayo. Alipopata uhakika na yakini ya mambo hakusita kutoa hukumu ya haki kwa Waislamu. Najashi hakudanganywa kabisa katika hukumu yake na propaganda za Makuraishi wala za wasaidizi wake waliopokea zawadi za Makuraishi. Aliona thamani na ubora wa kuwatendea haki Waislamu na kuwalinda na udhalimu wa Makuraishi. Huu ndiyo ukweli, uwazi na uadilifu unaostahiki kuigwa na watawala na ndiyo hasa `Religious tolerance'. Hapa kwetu Tanzania Ukristo siyo dini ya taifa, na Waislamu siyo wakimbizi, bali ni wananchi na kwa uananchi huo ndio maana wakapigania uhuru wa nchi hii, na hasa ukiwalinganisha na wale raia waliopokea mafundisho kutoka kwa wakoloni ya kuwa "Adui yako mpende! Mtu akikupiga shavu la kulia, mpe na la kushoto". Waislamu wamesakwa majumbani mwao, wakatiwa rumande, wakauawa hadharani! `Piga yule! Muongeze! Wazee na akina mama wa Kiislamu wakadhalilishwa. Mhe. Rais kimya! Imekuwa uwazi na ukweli kizani. Eti hakuna haja ya kuunda tume ya kuchunguza suala la Mwembechai. Kuna `Slogans' kama: Mulism Fundamentalist" "Siasa kali" zinazoenezwa na maadui wa Uislamu kupitia vyombo vya habari ili kuuhujumu. Wengi kati ya viongozi wetu wameathiriwa na propaganda hizi kwa kiwango kikubwa, jambo ambalo huwafanya wao kuyatumia maneno haya dhidi ya Waislamu pindi wanapodai haki zao. Chakusikitisha zaidi ni kuona kuwa kuna baadhi ya viongozi wa dini wanaochukua fursa ya kuzitumia propaganda hizi za "Siasa kali" kuishinikiza serikali itetee dini yao badala ya wao viongozi wa dini hiyo kujenga hoja zenye mashiko ili kuitetea imani yao. Ningependa tukumbushane kuwa; nchi hii ni yetu sote! Amani na utulivu havipatikani kwa kuwadhulumu, kuwakandamiza na kuwaua Waislamu halafu kutoa sababu zisizo za msingi! Na wala havitapatikana kuwa kuwapachika Waislamu wanaodai haki zao kuwa "wanasiasa kali", "wanatumiwa" n.k. Haya hayatasaidia kitu! Ifahamike wazi kuwa amani na utulivu havipatikani katika nchi ambayo Katiba inakiukwa. Kama alivyosema Mhe. Kitwana Kondo kuwa Rais asikaangiwe mbuyu. Nami ningependa kumshauri Mhe. Rais kuiga mfano bora wa Mfalme Najashi. Bado kuna umuhimu mkubwa wa kuunda Tume ili ichunguze madai ya Waislamu kwa ajili ya mustakibali mwema wa Taifa letu!
Waislamu Moro wasaidia wagonjwa Na Mwandishi Wetu, Morogoro KATIKA kuhimiza kuyatafsiri Mafundisho ya Mtume (saw), Waislamu wake kwa waume mjini Morogoro walikusanyika katika Hospitali ya Mkoa ili kuitekeleza Sunna ya Bwana Mtume (saw) ya kuwatembelea, kuwasaidia na kuwafariji wagonjwa. Zoezi hili lifanyika hivi karibuni ikiwa ni maendelezo ya maazimio ya tamasha la awali lililoanzishwa na Daruweshi Kazimoto kwa lengo la kuitafsiri Qur'an kwa vitendo. Katika tamasha hilo, Waislamu walianza kutekeleza ratiba yao kwa kuyafanyia usafi mazingira ya Hospitali. Wanaume walijishughulisha katika kufyeka na wanawake walifyagia maeneo mbalimbali ya Hospitalini hapo. Baada ya kumaliza zoezi la kuyafanyia usafi mazingira, Waislamu hao walianza kuchanga pesa ambazo ziliazimiwa kununulia dawa, matunda pamoja na sabuni za kuwasaidia wagonjwa. Aidha, wagonjwa watano wasiokuwa na ndugu wa kuwasaidia walipatiwa dawa zilizonunuliwa kwa pesa za Waislamu hao ili kuwapatia matibabu wagonjwa hao ambao miongoni mwao walikuwemo wafungwa. Pamoja na kuwasaidia dawa wagonjwa, Waislamu hao waliwapatia matunda na sabuni hasa kwa upande wa akinamama na watoto. Waislamu hao ambao walitembelea wagonjwa katika wodi mbalimbali za hospitalini hapa, waliwaombea dua kwa Allah (sw) ili azijalie dawa na matibabu wanayoyapata ziweze kuwa sababu ya kuponywa maradhi yao na hatimaye kupata afya njema. Waislamu walikamilisha tamasha hilo kwa kumsaidia damu mgonjwa mmoja ambaye alikuwa na upungufu wa damu. |
YALIYOMO
TAHARIRI Hakuna Muislamu aliyekufa kutokana na vurugu Mgogoro wa kiwanja Duma: Wakatoliki wasema kuna njama za Waarabu Same Na Mwandishi Wetu Wanawake wakutana Mwanza na kusema: Kunyanyaswa sasa basi Na Mwandishi Wetu, Mwanza Sheikh Omar Bashir ataka Waislamu waimarishe mshikamano Na Said Sharif Ustaadhi Abdallah Mfoyi afariki Na Muhibu Saidi Baraza Kuu halina Katibu Nguruka - Sheikh Kilima Na Abu Adli Viongozi Msikiti wa Ubungo Darajani waitwa polisi Na Kassim Juma Marekani `ilivyosaidia' Mujahidiin Barua ya mtoto wa miaka minne toka Lebanon kwa Bibi Hillary Clinton Ujumbe wa waandishi kwa Bw. Batendi, Wakristo Na Muhibu Saidi Waislamu wanadhalilishwa au wanajidhalilisha Tusiwe Jogoo wa Esopo na Almasi Na MAALIM ALI BASSALEH Sherehe za wiki ya usalama barabarani: Kauli nzito za waheshimiwa zimekalia kuti kavu Na Said Omar Mwanasayansi Avicenna: Tabibu bingwa. Na Dk. A. A. Amur Ujenzi wa Msikiti wa Ijumaa Mriti waanza Na Nasib A. Mziray Kutoweka kwa hazina adimu za kimazingira Na Yassir Salim Mfalme Najashi ni mfano bora wa kuigwa kwa watawala Na Idi Kikong'ona Waislamu Moro wasaidia wagonjwa Na Mwandishi Wetu, Morogoro KUFUATIA KUTISHIA MAGAZETI: Sheikh Ayoub amjibu Askofu Rajab Rajab Na Mussa Ally TAMSA Tanga waahidi kuendeleza mema Na Ibn Mohammed, Tanga Ufugaji, uuzaji nguruwe wakera wananchi Dar Na Mwandishi Wetu Mafundisho ya Quran Kuwepo kwa ufufuo Barua za wasomaji
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org