|
|
| S.L.P. 55105, SIMU 181365,
DSM
TAHARIRI Hakuna Muislamu aliyekufa kutokana na vurugu GAZETI moja la kila siku katika toleo lake la Septemba 17, mwaka huu lilidai kwamba migogoro ya miliki ya Misikiti Februari mwaka huu ilisababisha vurugu kubwa katika Msikiti wa Mwembechai zilizopelekea watu kuuliwa. Vurugu hizo limedai gazeti hilo kwamba zilitokana na kikundi kimoja cha Waislamu kuutwaa Msikiti wa Mwembechai na kuugeuza kuwa kitovu cha mihadhara ya kashfa za kidini. Awali ya yote, tungependa kusema kwamba Waislamu Mwembechai waliuliwa kwa kulengwa shabaha `piga yule', `bado, mwongeze', ` na yule'. Aliyetoa amri hiyo ni Kamanda wa Jeshi la Polisi la Serikali na aliyefyatua risasi halikadhalika. Hawakuwa Waislamu kutoka makundi yanayogombea Msikiti. Pili, hakuna aliyekufa kwa kukanyagwa au kupigwa jiwe wala hakuna Waislamu waliojeruhiana kuonyesha kwamba palikuwa na vurugu baina ya makundi yanayogombea Msikiti. Tatu, kama ni mihadhara imekuwepo katika Msikiti wa Mwembechai kwa siku nyingi kabla ya tukio la Februari, na kama ni mgogoro wa kiuongozi imekuwepo pia kwa siku nyingi, lakini haikuwahi kutokea vurugu japo watu kuparuzana makucha. Kinachoitwa vurugu leo imetokea baada ya shinikizo la Padri Lwambano ambalo lilitekelezwa na serikali kwa kishindo na hamasa kubwa bila kujali Katiba wala sheria za nchi. Kifungu gani cha Katiba na Sheria gani ya nchi inaruhusu Polisi kuwalenga raia risasi kwa nia ya kuua! Sheria gani ya nchi inazuia aliyeua kufikishwa mahakamani! Kifungu gani cha Katiba na Sheria za nchi kinaruhusu polisi kuvamia Misikiti na kuwapiga waumini wakiwa ndani! Sheria gani ya nchi inaruhusu wanawake wavuliwe nguo na kupekuliwa na askari wanaume! Sheria gani ya nchi inaruhusu watoto wadogo chini ya miaka 18 wachanganywe na watu wakubwa katika mahabusu au jela! Nne, hakuna Msikiti pamoja na huo wa Mwembechai iliyofanya mihadhara ya kashfa. Katika watu zaidi ya mia tatu waliokamatwa hakuna aliyesalia na shitaka hilo. Historia ina nafasi yake muhimu katika jamii. Na ni muhimu historia hiyo ilindwe, isipotoshwe. Mzee Chata Abdallah Kidagaa kaingizwa jela mzima katoka mahututi na sasa katutoka; bado hata Waislamu hawajaanua tanga. Wala hawajui hatma ya wengine ambao nao hali zao si nzuri toka watoke jela. Mzee Chata hakuwekwa jela kwa vile Msikitini kwake kulikuwa na mgogoro wa umiliki wa Msikiti wala hakuwekwa ndani na kupata mateso yaliyokuja kuupokonya uhai wake kwa vile alikashifu dini nyingine. Ndio maana baada ya kuteswa kwa miezi mitano aliachiwa akiambiwa hana kosa! Mtoto Chuki Athumani bado yupo hospitali mwezi wa saba sasa akiwa kapooza baada ya kupigwa risasi iliyoathiri mishipa ya fahamu katika uti wa mgongo. Migogoro katika Misikiti, Makanisa, Jumuiya za kidini, vyama vya siasa na hata ndani ya Serikali na vile vile kati ya nchi na nchi itaendelea kuwepo. Ndio maana akina Kakobe, Father Nkwera, Mtikila n.k. walijitenga kutoka Makanisa yao ya awali wakifuata nyayo za akina Luther. Huo ndio ubinadamu wenyewe; kuwa na uoni tofauti na udhaifu unaobeba dosari nyingi. Pamoja na tofauti kubwa za kiimani Waislamu na Wakristo wamebaki kuwa watu wanaoishi pamoja na kuvumiliana pamoja na juhudi kubwa ya makusudi iliyofanywa na baadhi ya viongozi wenye chuki zao binafsi kujenga chuki kwamba eti Waislamu wanawa kashfu Wakristo na Ukristo. Ni jambo la kusitikisha kwamba vyombo vya habari vimetumika sana kuijenga na kuisambaza sumu hiyo mbaya. Lakini Wakristo wa kawaida wenye busara zao walipuuza. Wameendelea kuishi pamoja kwa amani na utulivu wakivulimiliana na kuheshimiana, japo Mungu wa mmoja kwa mwingine ni Mtume. Huo ni ukweli ambao ni lazima uingie katika historia ya nchi hii. Lakini ukweli mwingine ni kwamba serikali imekuwa ikiingilia uhuru na haki ya Waislamu ya kuwa Waislamu na kuuhubiri Uislamu. Ukweli huo umedhihirishwa na hatua za serikali kuitikia kauli za baadhi ya viongozi wa Makanisa ambapo iliwakamata akina Mzee Chata na kuwaweka ndani kabla ya tukio la Mwembechai ambapo baadhi ya Waislamu waliuliwa kwa risasi, Msikiti ukavunjwa na akina mama kudhallishwa. Damu ya Muislamu yaonekana haina thamani yatosha kufukiwa kwa mchanga. Hivyo yadaiwa hakuna haja ya Tume ya Uchunguzi, wala wahusika kufikishwa mahakamani! Tungependa tuseme kwamba Waislamu hawatachoka kutetea haki yao ya kuishi, haki ya uraia na haki ya uananchi kwa kurejea dai lao kwamba walioua wafikishwe mahakamani. Na historia hii hatutakubali ipotoshwe. Hakuna Muislamu aliyekufa kutokana na vurugu. Waislamu wameuliwa kwa kupigwa risasi na polisi. Tena si kwa bahati mbaya wala kwa kujihami. Bali kwa kumlenga shahaba mtu aliyembali. "Piga yule". Tunamshukuru Allah (sw) aliyejaalia janga hili likawafika Waislamu katika zama hizi za maendeleo makubwa ya kamera za video. |
YALIYOMO
TAHARIRI Hakuna Muislamu aliyekufa kutokana na vurugu Mgogoro wa kiwanja Duma: Wakatoliki wasema kuna njama za Waarabu Same Na Mwandishi Wetu Wanawake wakutana Mwanza na kusema: Kunyanyaswa sasa basi Na Mwandishi Wetu, Mwanza Sheikh Omar Bashir ataka Waislamu waimarishe mshikamano Na Said Sharif Ustaadhi Abdallah Mfoyi afariki Na Muhibu Saidi Baraza Kuu halina Katibu Nguruka - Sheikh Kilima Na Abu Adli Viongozi Msikiti wa Ubungo Darajani waitwa polisi Na Kassim Juma Marekani `ilivyosaidia' Mujahidiin Barua ya mtoto wa miaka minne toka Lebanon kwa Bibi Hillary Clinton Ujumbe wa waandishi kwa Bw. Batendi, Wakristo Na Muhibu Saidi Waislamu wanadhalilishwa au wanajidhalilisha Tusiwe Jogoo wa Esopo na Almasi Na MAALIM ALI BASSALEH Sherehe za wiki ya usalama barabarani: Kauli nzito za waheshimiwa zimekalia kuti kavu Na Said Omar Mwanasayansi Avicenna: Tabibu bingwa. Na Dk. A. A. Amur Ujenzi wa Msikiti wa Ijumaa Mriti waanza Na Nasib A. Mziray Kutoweka kwa hazina adimu za kimazingira Na Yassir Salim Mfalme Najashi ni mfano bora wa kuigwa kwa watawala Na Idi Kikong'ona Waislamu Moro wasaidia wagonjwa Na Mwandishi Wetu, Morogoro KUFUATIA KUTISHIA MAGAZETI: Sheikh Ayoub amjibu Askofu Rajab Rajab Na Mussa Ally TAMSA Tanga waahidi kuendeleza mema Na Ibn Mohammed, Tanga Ufugaji, uuzaji nguruwe wakera wananchi Dar Na Mwandishi Wetu Mafundisho ya Quran Kuwepo kwa ufufuo Barua za wasomaji
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org