|
|
| Ustaadhi
Abdallah Mfoyi afariki
`Inna Lillahi Wainnaa Ilayhi Raajiun' Na Muhibu Saidi USTAADH Abdallah Salum Mfoyi (50) amefariki dunia Alhamisi ya Septemba 10, 1998 majira ya saa sita usiku katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, Jijini baada ya kuugua kwa muda mfupi. Kwa mujibu wa ndugu za marehemu na Amiri Mkuu wa Jamaat Answar Sunna nchini (JASUTA), Sheikh Salum Rajab Sima, maradhi yaliyosababisha kifo cha marehemu ni kushuka kwa mapigo ya moyo kwa kiwango cha chini. Imearifiwa kuwa siku moja kabla ya kifo chake, marehemu baada ya kujihisi vibaya, alikwenda katika Hospitali ya Temeke kupima malaria lakini akajibiwa kwamba hakuwa na maradhi hayo. Taarifa hiyo imeongeza kuwa pamoja na majibu hayo, marehemu alizidi kulalamika kuwa bado anahisi hali kuwa mbaya ambapo jamaa zake wa karibu walilazimika muda huo kumpeleka katika Hospitali ya Muhimbili ili akafanyiwe uchunguzi zaidi. Hata hivyo, taarifa hiyo imesema baada ya kufika Muhimbili wakati akitaniana na mmoja wa marafiki zake ambaye ni mfanyakazi wa Hospitali hiyo, marehemu alimwarifu rafiki yake huyo kwamba "anakufa" na ghafla akakata roho! Marehemu Ustaadh Mfoyi atakumbukwa sana na ndugu, jamaa na marafiki hasa wa mikoa ya Kilimanjaro, Tabora, Singida, Dar es Salaam, Shinyanga na kwingineko kwa juhudi zake adhimu za kupigania na kutetea kwa ujasiri mkubwa kitabu cha Allah (sw) na Sunna sahihi za Mtume (saw) kuwa mwongozo wa maisha ya kila siku ya mwanadamu. Mapema akitoa nasaha zake baada ya mazishi katika makaburi ya Tambaza yaliyo maeneo ya Upanga Jijini, Amir Mkuu Taifa wa JASUTA, Sheikh Salum Rajab Sima alimwelezea marehemu kuwa ni mtu aliyekuwa jasiri katika kupigania haki za Waislamu nchini, kupambana na ukandamizaji na kuhakikisha Waislamu wanaishi chini ya mwongozo wa Qur'an na Sunna za Mtume (saw). Sheikh Salum alisema moja ya tija zilizopatikana kutokana na juhudi za marehemu ni kuwafanya Waislamu wa Kinyerezi kuwa watu wanaomfuata kivitendo Qur'an na Sunna. Ustaadh Abdallah S. Mfoyi alizaliwa mnamo mwaka wa 1948 katika kijiji cha Kibosho Umbwe Sinde, kilichopo wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro. Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi ya Matunya iliyopo wilaya ya Moshi Vijijini mnamo mwaka wa 1955 hadi 1961. Alijiunga na elimu ya Kiislamu katika madrasa ya Mango iliyopo katika Msikiti wa Mango, Moshi Vijijini, chini ya mmoja wa Masheikh zake, Sheikh Abdallah Boshe. Pia alijiendeleza na elimu hiyo katika madrasa moja huko mkoani Iringa mnamo mwaka wa 1965. Baadae kuanzia mwaka wa 1978 hadi anafariki dunia, marehemu alikuwa akijishughulisha na biashara katika mikoa ya Shinyanga, Tabora (Nzega), Singida, Dar es Salaam na kwingineko. Ameacha watoto watano, watatu wakiwa ni wanaume ambao ni pamoja na Abdul'Azizi, Abdallah na Salum. Na waili ni wanawake ambao ni Mariamu na Rehema. Marehemu alizikwa Jumamosi ya Septemba 12, 1998 kwenye makaburi ya Tambaza Jijini Dar es Salaam. Allah (sw) amghufurie makosa yake na amweke mahali pema peponi. Amin.
Baraza Kuu halina Katibu Nguruka - Sheikh Kilima Na Abu Adli BARAZA Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, limekanusha kuwa na Katibu katika tarafa ya Nguruka mkoani Kigoma. Akizungumza na gazeti hili kufuatia taarifa kwamba Katibu wa Baraza Kuu tarafani humo amezuia kongamano la wanawake, Katibu Mkuu wa baraza hilo nchini Sheikh Abas Kilima amesema, Baraza lake halina Katibu katika tarafa hiyo na kwamba masuala yote yanayolihusu Baraza hilo yako Kigoma Mjini. Aidha, Sheikh Abas ameahidi kufuatilia taarifa hizo ili kupata uhakika wa kile kilichotokea Nguruka na wahusika wake. "Baraza haliko tayari kupakwa matope, tutawasiliana na watendaji wa Kigoma ili walifuatilie suala hili", alisema Sheikh Abas Kilima wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi katikati ya wiki. Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Bwana Shaaban wa kijiji cha Nguruka, alidaiwa kutaka kuzuia kongamano la wanawake wa Kiislamu ambalo lilipangwa kufanyika eneo hilo. Imedaiwa mtu huyo alitishia kuwapiga kina mama hao kwa madai kwamba wanashirikiana na wabaya wao (Bakwata). Imeripotiwa kutoka Nguruka kuwa mbali ya vurugu za mtu huyo, kongamano la wanawake ambalo lilihudhuriwa na vikundi kadhaa vya Twarika lilifanyika na kumalizika kwa amani
Viongozi Msikiti wa Ubungo Darajani waitwa polisi Na Kassim Juma VIONGOZI wa Msikiti wa Ubungo Darajani Jijini mwishoni mwa wiki iliyopita waliitwa polisi kituo cha Urafiki kuhusiana na mihadhara inayoendelea katika Msikiti huo. Kwa mujibu wa barua ya Mkuu wa Kituo yenye kumb. Na. MAG/A.4/9/A/Vol.1/106 ya Septemba 10, 1998 iliyosainiwa na Mkuu wa Polisi Kituo cha Magomeni, viongozi hao walitakiwa kufika polisi siku ya Ijumaa ya Septemba 11, 1998 saa tatu asubuhi. "Kutokana na taarifa ambazo tunazipata mara kwa mara za kuendesha mihadhara ya kidini katika Msikiti wenu wa River Side. mnahitajika kufika ofisini kwa OCD bila kukosa", ilidai sehemu ya barua hiyo ambayo gazeti hili limefanikiwa kupata nakala yake. Viongozi hao wamesema walipofika kituoni hapo, miongoni mwa maswali waliyohojiwa ni kwanini mhadhara unasema Yesu sio Mungu. Wakijibu swali hilo, viongozi hao walimwambia OCD kuwa si mihadhara peke yake inayosema Yesu si Mungu, "hata sisi tunasema hivyo kwani Qur'an ndiyo iliyotuamrishasha hivyo". Hatua ya vyombo vya dola kuingilia masuala ya dini ilizua vurugu mwezi Februari mwaka huu ambapo watu kadhaa waliuawa na polisi, wengine kujeruhiwa na kuwekwa mahabusu kwa miezi kadhaa . Wakati huo huo, Katibu wa Msikiti wa Ubungo Darajani amewataka Maimamu na viongozi wengine wa Misikiti nchini waendelee kufanya mihadhara ya kidini na wasiogope polisi na kurudi nyuma. "Kama serikali iliwakamata Waislamu na kuwafungulia mashitaka ya kukashifu dini nyingine na kisha kuwafutia mashitaka na kuwaambia hawana kesi ya kujibu, vipi leo Maimamu waambiwe wanakaribisha mihadhara ya kashfa", alihoji Katibu huyo wakati akitoa wito huo kwa Maimamu. |
YALIYOMO
TAHARIRI Hakuna Muislamu aliyekufa kutokana na vurugu Mgogoro wa kiwanja Duma: Wakatoliki wasema kuna njama za Waarabu Same Na Mwandishi Wetu Wanawake wakutana Mwanza na kusema: Kunyanyaswa sasa basi Na Mwandishi Wetu, Mwanza Sheikh Omar Bashir ataka Waislamu waimarishe mshikamano Na Said Sharif Ustaadhi Abdallah Mfoyi afariki Na Muhibu Saidi Baraza Kuu halina Katibu Nguruka - Sheikh Kilima Na Abu Adli Viongozi Msikiti wa Ubungo Darajani waitwa polisi Na Kassim Juma Marekani `ilivyosaidia' Mujahidiin Barua ya mtoto wa miaka minne toka Lebanon kwa Bibi Hillary Clinton Ujumbe wa waandishi kwa Bw. Batendi, Wakristo Na Muhibu Saidi Waislamu wanadhalilishwa au wanajidhalilisha Tusiwe Jogoo wa Esopo na Almasi Na MAALIM ALI BASSALEH Sherehe za wiki ya usalama barabarani: Kauli nzito za waheshimiwa zimekalia kuti kavu Na Said Omar Mwanasayansi Avicenna: Tabibu bingwa. Na Dk. A. A. Amur Ujenzi wa Msikiti wa Ijumaa Mriti waanza Na Nasib A. Mziray Kutoweka kwa hazina adimu za kimazingira Na Yassir Salim Mfalme Najashi ni mfano bora wa kuigwa kwa watawala Na Idi Kikong'ona Waislamu Moro wasaidia wagonjwa Na Mwandishi Wetu, Morogoro KUFUATIA KUTISHIA MAGAZETI: Sheikh Ayoub amjibu Askofu Rajab Rajab Na Mussa Ally TAMSA Tanga waahidi kuendeleza mema Na Ibn Mohammed, Tanga Ufugaji, uuzaji nguruwe wakera wananchi Dar Na Mwandishi Wetu Mafundisho ya Quran Kuwepo kwa ufufuo Barua za wasomaji
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org