AN-NUUR
Na.167 Jamadul Awal 1419, Septembe 17 - 24, 1998

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita

 

Marekani `ilivyosaidia' Mujahidiin

KWA muongo mzima wa miaka ya 1980s, wakati vita kati ya Urusi na Mujahidiin ikiendelea kuuma, Bwana Casey aliyekuwa Mkugurenzi wa CIA mara kadhaa alifanya ziara katika medani ya vita kutathmini hali ya mapambano na aina ya msaada ambao nchi yake ingeutoa kulingana na maslahi yake ya baadae. Pamoja na ziara za mkuu huyo wa CIA, maafisa wa ngazi za chini wa shirika hilo la kijasusi la Marekani walishirikiana kwa karibu sana na idara ya usalama ya Pakistan ISI, huku wakitoa msaada mkubwa wa silaha kwa shauku ya kuuangamiza Ukomunisti.

"Lazima tulipize vita ya Vietnam kwa washenzi hawa", Bwana Casey amekaririwa kusema hayo wakati wa upelekaji wa silaha Afghanistan.

CIA vile vile ilitoa msaada wa fedha kwa mujahidiin kupitia Pakistan ili kuwawezesha kununua silaha zilizohitajika kutoka China, Misri na Israil. Matazamio ya Mujahiidiin yalikuwa kuukamata mji mkuu wa Afghanistan Kabul. Hivyo mauaji ya ghafla na hujuma mbalimbali zilikuwa nyenzo kuu mbili zilizotumika kufikia lengo hilo kwa haraka. Mwaka 1983, maafisa saba wa Kirusi waliuawa kwa milipuko ya mabomu. Baadae kidogo Jenerali Abdulwaduudi, Kamanda wa Brigedi kuu ya jeshi la Wakomunisti aliuawa ofisini kwake. Hata hivyo operesheni hizi pia ziliwaathiri baadhi ya Waafghan ambao wengi waliuawa kutokana na makombora ya masafa ya mbali yaliyokuwa yakitumwa na Mujahiidiin.

Mashambulizi ya Mujahidiin yaliendelea kuwa makali, Warusi waliingiwa kiwewe, wakaanza kuua ovyo raia wasio na hatia.

Wakitumia helikopta zao za mashambulizi, Warusi walivishambulia vijiji kadhaa na kuua mamia ya watu. Wakati mwingine waliwabeba wafungwa wa vita katika helicopta hizo, kisha kuwadondosha chini kutoka angani!

Mauaji ya aina hii yalifanywa mara kwa mara na majeshi ya Kirusi bila ya upinzani wowote wa kijeshi, hii ilitokana na kwamba Mujahidiin hawakuwa na silaha madhubuti za kukabiliana na helikopta hizo.

"Nusra ilikuja baada ya Mujahidiin kupokea makombora ya kisasa (US Stinger Missile) ya kudungulia helikopta hizo", anaeleza Brigedia Yousaf

Brigedia huyo ambaye ameandika kitabu alichokiita Afghani's the untold story kuelezea vita ya kihistoria baina ya Urusi na Mujahiidin, anaeleza jukumu ililokuwa nalo ISI, kwa kulinganisha na " lile alilolifanya Alexander the Greater karne kadhaa zilizopita". ISI kwa kushirikiana na vikosi vya Mujaheediin ilivuka mto Amu hadi ndani ya Urusi ambako ilifanya mashambulizi ya kushtukiza kuhujumu sehemu kadhaa muhimu".

Brigedia Yousef anaeleza kuwa jaribio la mwanzo kujipenyeza nchini Urusi lilifanywa na Kamanda Wali Beg (53).

Wali ambaye familia yake yote iliuawa na majeshi ya Urusi, akiwa amevaa ngozi ya mbuzi,

alitekeleza dhima hiyo usiku kwa kuogelea kuvuka mto Amu wenye maji yaliyotanda barafu nzito. Akiwa Ng'ambo ya pili ya mto huo, yalikokuwa majeshi ya Urusi mpakani mwa Afghanistani na Urusi, huku akiangaza huko na huko kuhakikisha hakuna doria yoyote ya askari wa Kirusi, Wali alisujudu na kuomba ulinzi wa Allah (sw) kisha alisota kilometa kadhaa kuelekea kijiji cha jirani.

`Wali ni mfano wa Mujahidiin wengi waliojitoa muhanga kutetea Uislamu na Waislamu nchini Afghanistan", ameandika Brigedia Yousaf katika kitabu chake.

Akiwa hapo inaelezwa kuwa alipata mapokezi makubwa, baadhi ya wanakijiji waliomba wapatiwe silaha za kujilinda, wangine walitaka wapatiwe mafunzo ya kijeshi ili wajiunge moja kwa moja katika uwanja wa mapambano na wapo waliotaka wapatiwe silaha ili washiriki katika "operesheni hujuma" ndani ya Urusi.

Nchini Urusi hali ilichafuka zaidi, Waislamu waliamka baada ya Mujahidiin kusambaza tafsiri ya Qur'an na vitabu mbalimbali vya Kiislamu. Waislamu wa majimbo ya Urusi walianza hujuma za milipuko ya mabomu dhidi ya visima vya mafuta, madaraja, viwanda na vituo vya mafuta sambamba na kushambulia kambi za jeshi.

Hali hii iliwachanganya zaidi Wakomunisti ambao malipizo yao yalikuwa kuvipiga mabomu vijiji kadhaa vya Afghanistan na kuua mamia ya wakazi wake.

Kupitia Balozi wake nchini Pakistan, Urusi ilielezea wasiwasi iliokuwa nao juu ya mashambulizi ya Mujahidiin kwamba yalikuwa yakipata usaidizi wa moja kwa moja kutokea Pakistan. Balozi alitishia kuwa nchi yake ingeishambulia Pakistani wakati wowote ule. "Huenda Urusi ikafanya shambulio kali dhidi ya Pakistan", Brigedia Yousef. amemnukuu Balozi huyo alipokuwa akizungumza na aliyekuwa Waziri wa mambo ya ndani wa Pakistan bwana Sahibzada Yaqoob.

Mashambulizi makali ya Mujahidiin dhidi ya majeshi ya Kirusi ndani ya Afghanistan na dhidi ya vituo na visima vya mafuta, viwanda na vituo vya kijeshi ndani ya Urusi yaliishinikiza Urusi kusaini mkataba wa amani wa Geneva na siku chache baada ya mkataba huo Urusi ilianza kuyaondosha majeshi yake kutoka ndani Afghanistan. "Huu ulikuwa mwanzo wa kusambaratika Taifa hilo lililokuwa na nguvu za kutisha kijeshi".


Barua ya mtoto wa miaka minne toka Lebanon kwa Bibi Hillary Clinton

Mpendwa mke wa Rais,

NIMELALA hapa hospitali nikiwa na majeraha na huku nikikaribia kifo. Na mimi ni mdogo sana kuweza kufanya uhalifu au ubaya wowote na hivyo sistahili adhabu ambayo nimepewa. Nakuandikia barua hii kwa kuwa wewe ni mama na unaye mtoto.

Labda unaweza kuelewa kidogo kinachompata mama yangu kwa sasa. Amekaa karibu na kitanda changu akilia. Anajaribu kunionyesha tabasamu hali ya kuwa macho yake yamejaa machozi.

Kila nilipoanguka au kuumia, mama yangu angebusu sehemu iliyoumia na maumivu yangeondoka. Lakini sasa licha ya kuwa anajaribu kupunguza maumivu yangu kwa kunibusu na kuonyesha mapenzi, bado nina maumivu makali kupita kiasi na mwili wangu mdogo umeshindwa kustahimili. Kuna mipira ya kila namna inayoingia na kutoka katika mwili wangu. Siku ya tarehe 18 April nilikimbizwa kwa madaktari baada ya mabomu yaliyorushwa na askari wa Israel katika kambi ya walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa huko Qana kusini mwa Lebanon. Mama alidhani tungekuwa salama hapo. Lakini hakuwa sahihi. Hakuna mtu hata mmoja anayeweza kujificha ili kukwepa mabomu!

Baadhi ya wafanyakazi walinifukua na kunitoa nje ya kifusi na kuniweka katika gari la wagonjwa pamoja na wafu na majeruhi wengine. Mama yangu; naye akiwa amejeruhiwa, aliingia na kukaa karibu yangu. Alikaribia kupoteza fahamu aliponiona. Inatisha sana kukabili kifo ukiwa na umri wa miaka minne tu. Na inakuwa vibaya zaidi ukifariki ukiwa katika umri huo.

Niliomba nimuone dada yangu mdogo kabla sijafa, lakini naye aliunguzwa vibaya na bomu lililotupiga kiasi kwamba hawezi hata kutembea. Nami pia siwezi kabisa kutembea. Baba yangu amepoteza fahamu, nimewasikia madaktari wakisema, na nina matumaini angeamka kabla sijachelewa sana kumuona kwa mara ya mwisho.

Amani ni haki ya kimsingi kwa watoto wote. Ninakuuliza wewe Bibi Clinton, kwa nini inakuwa ni muhimu sana kwa watoto wa kiyahudi kuishi kwa amani na maisha yao yanachukuliwa kuwa ni matakatifu hali ya kuwa maisha ya watoto wa kiarabu yanaonekana kutokuwa na umuhimu wowote? Je mimi sionekani kuwa muhimu kama watoto wengine? Ukweli hii siyo haki. Maisha yangu baada ya kifo yatakuwa katika mahali bora kabisa, ambapo bila kujali rangi au utaifa, kutakuwepo heshima na kuthaminiwa.

Tafadhali sana mkewe Rais, usichukizwe na mimi kwa kuwa ninakwenda peponi. Nitawasubiri wazazi wangu wajiunge na mimi na hapo nitawashika mikono yao na kuwakaribisha katika hiyo pepo.

Ombi langu la mwisho ni kwamba mueleze mumeo Rais Clinton kuwapa watoto wengine kama mimi nafasi ya kufurahi duniani na wawe huru kuishi maisha ya kawaida kama watoto wengine dunia nzima. Na isitokee kwamba mabomu kama yale yatupwe kwa watoto wa kiarabu. Muwafanyie wema watoto wa kiarabu kama mnavyowafanyia watoto wa kiyahudi na hapo ndipo labda hiyo amani mnayoisema, ambayo leo hii inaniua mimi na wengine kama mimi, itakapopata maana inayostahili.

Ninamaliza kwa heshima na mapenzi,

Mohammed Ibrahim.

NB: Mohammed Ibrahim alifariki tarehe 20/04/1996 katika hospitali ya Sidon kutokana na majeraha aliyoyapata katika mashambulio ya mabomu yaliyofanywa na majeshi ya Israel ambayo yaliipiga kambi ya Umoja wa Mataifa katika kijiji cha Qana kusini mwa Lebanon. Kifo chake kiliongeza idadi ya waliokufa katika mauaji ya wakimbizi na kufikia watu 102.

Makala hii imetolewa kwa hisani ya Just World Trust na kufasiriwa toka katika Jarida la ISLAMIC HERALD.

Juu 
 

YALIYOMO  
 
TAHARIRI 
Hakuna Muislamu aliyekufa kutokana na vurugu

Mgogoro wa kiwanja Duma: Wakatoliki wasema kuna njama za Waarabu Same Na Mwandishi Wetu

Wanawake wakutana Mwanza na kusema: Kunyanyaswa sasa basi
Na Mwandishi Wetu, Mwanza

Sheikh Omar Bashir ataka Waislamu waimarishe mshikamano
Na Said Sharif

Ustaadhi Abdallah Mfoyi afariki
Na Muhibu Saidi

Baraza Kuu halina Katibu Nguruka - Sheikh Kilima
Na Abu Adli

Viongozi Msikiti wa Ubungo Darajani waitwa polisi
Na Kassim Juma

Marekani `ilivyosaidia' Mujahidiin

Barua ya mtoto wa miaka minne toka Lebanon kwa Bibi Hillary Clinton

Ujumbe wa waandishi kwa Bw. Batendi, Wakristo
Na Muhibu Saidi

Waislamu wanadhalilishwa au wanajidhalilisha

Tusiwe Jogoo wa Esopo na Almasi
Na MAALIM ALI BASSALEH

Sherehe za wiki ya usalama barabarani: Kauli nzito za waheshimiwa zimekalia kuti kavu
Na Said Omar

Mwanasayansi Avicenna: Tabibu bingwa.
Na Dk. A. A. Amur

Ujenzi wa Msikiti wa Ijumaa Mriti waanza
Na Nasib A. Mziray

Kutoweka kwa hazina adimu za kimazingira
Na Yassir Salim

Mfalme Najashi ni mfano bora wa kuigwa kwa watawala
Na Idi Kikong'ona

Waislamu Moro wasaidia wagonjwa
Na Mwandishi Wetu, Morogoro

KUFUATIA KUTISHIA MAGAZETI: Sheikh Ayoub amjibu Askofu Rajab Rajab
Na Mussa Ally

TAMSA Tanga waahidi kuendeleza mema
Na Ibn Mohammed, Tanga

Ufugaji, uuzaji nguruwe wakera wananchi Dar
Na Mwandishi Wetu

Mafundisho ya Quran 
Kuwepo kwa ufufuo

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 
Haja ya maji ya kunywa

 

 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org  

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita