|
|
|
AWALI ya yote napenda kuwaweka swa wasomaji wangu wanaoweza kujiuliza swali hili. Kwa nini makala za chakula na lishe siku hizi zina ‘changanya’ siasa na mambo ya chakula na lishe? Jibu la swali hili kwa kifupi ni kuwa: Moja ya sababu za upungufu wa chakula na hatimaye lishe duni katika nchimbalimbali duniani ni siasa (sera) mbaya za nchi zinazohusika. Kwa hoja hii, siasa lazima ichanganywe na maswala ya chakula na lishe kama tunataka kuondoa matatizo ya chakula na lishe katika jamii. Katika kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinachoendelea mjini Dodoma, serikali ya Tanzania imesema kuwa haiwezi kuzuwia tatizo la upungufu wa chakula na hivyo haina mpango wa kuondoa tatizo hilo. Inachofanya ni kugawa chakula pale ambapo kwenye upungufu. Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Bakari Mbonde wakati akijibu maswali ya Wabunge. Kwa mujibu wa elimu ya chakula na lishe, kauli hiyo ya serikali ni sawa na kutaka kuwamaliza Watanzania kwa njaa. Nasema kuwamaliza, kwa sabbu njaa ya sasa tayari imeshasababisha vifo vya wananchi kadhaa, kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari. Madai ya serikali ya kusema wanachofanya ni kugawanya chakula kwa wale walioathiriwa kwa njaa, ni sawa na kusema kuwa tiba ni bora kuliko kinga, jambo ambalo siyo sahihi. Sahihi ni kinga ni bora kuliko tiba. Wananchi wengi wa Tanzania tumekuwa mashahidi mwaka huu ambapo njaa imeenea karibu mikoa yote hata ile mikoa minne bingwa ya kuzalisha mahindi (The Big Four in Maize). Mikoa hiyo ni Rukwa, Ruvuma, Mbeya na Iringa. Hata hivyo, serikali inayodai kuwa wajibu wake ni kutoa chakula kwa walioathiriwa imeshindwa kutoa chakula kwa wananchi wote walioathiriwa. Na kwa wale waliopelekewa chakula. Siyo wote waliopewa chakula hicho bila malipo (fedha au kufanyishwa kazi). Tukizingatia maeneo yaliyoathiriwa kwa njaa tunapata picha kwamba, chanzo kikubwa cha janga hilo siyo uvivu au uzembe wa wananchi. Bali kama tunavyojua ni hali mbaya ya hewa (mfano mafuriko, ukame n.k.). Tatizo la hali mbaya ya hewa linahitaji mipango kabambe na nguvu imara ya serikali na siyo wakulima wetu wa jembe la jadi. Na kwa teknolojia iliyopo hivi sasa ulimwenguni, hali mbaya ya hewa ni jambo ambalo wanadamu wanalimudu kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, mvua zinapokuwa nyingi mwanadamu anatumia teknolojia inayoitwa kuvuna maji (Water harvest technology). Yaani kwa mfano mabwawa makubwa huchimbwa kanda ya mito ili kupunguza janga la mafuriko na pia kuhifadhi maji yasipotee. Pia katika majengo, maji ya mvua hukusanywa (huvunwa) na kuhifadhiwa katika visima (mashimo) vilivyochimbwa kwa kazi hiyo. Wakati wa kiangazi (ukame) wanadamu wanatumia teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji (Irrigation technology) yaani yale maji yaliyovunwa na kuhifadhiwa, wakati wa kiangazi yanatumika kwenye kilimo cha umwagiliaji. Katika nchi kadhaa ulimwenguni, watu wanazalisha na kuweka akiba ya chakula ambacho wanaweza kukitumia kwa miongo kadhaa hata bila ya kuzalisha chakula kipya (kingine). Zaidi ya hayo, kuna baadhi ya nchi ambazo zina ziada ya chakula na hufikia mahali, chakula hicho (zaidi ya kile kilichohifadhiwa) humwagwa baharini! Kwanini? Moja ya sababu ni kuwa, kukisafirisha chakula hicho kwa nchi ambazo zenye upungufu wa chakula, kutailazimu nchi tajiri kugharamia usafirishaji wa chakula hicho! Tukiyatafakari hayo yote, pia tukumbuke kwamba nchi inapokuwa na upungufu wa chakula, wafanyabiashara au nchi wahisani ambao siyo waadilifu wanaweza kuwaletea vyakula vibovu (mfano vyenye sumu, vijidudu) na hatimaye afya za wananchi zinaweza kuathirika. Hata hivyo, pamoja na hatari yote hiyo na kuwepo maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ulimwenguni, serikali yetu inasema haiwezi kuzuia upungufu wa chakula na haina mpango wa kuondoa tatizo hilo! Katika hali kama hiyo, unashindwa kuelewa umakini wa serikali katika janga la njaa. Na unaweza kuchanganyikiwa zaidi unapoipitia misahafu ambayo inatukumbusha namna ya wahenga wetu walivyokuwa na mipango katika kukabiliana na janga la njaa. Kwa mfano katika Qur’an sura ya 12, aya ya 47 mpaka 111, tunakumbushwa mipango ya Nabii Yusufu (a.s.) ambayo siyo tu ilinusuru nchi ya Misri na baa la njaa bali pia nchi kadhaa za Mashariki ya Kati. Tangu Nabii Yusufu (a.s.) aondoke hapa duniani ni maelfu kadhaa ya miaka yameshapita. Lakini serikali yetu ya Tanzania katika neema hizi za sayansi na teknolojia inatuambia haiwezi kuondoa tatizo la upungufu wa chakula. Ama kweli tutakwisha kwa njaa na ujinga. |
YALIYOMO
Tahari
Mwaka mmoja wa mauaji ya Mwembechai:
Waliouawa ni wanne
Waasisi wa TAA waibuka kupigania haki zilizoporwa Kuhujumiwa Waislamu kielimu: Mzazi adai mwanafunzi Adam Rashid kafelishwa Maoni yetu: Tuondoleeni wenye mikono ya damu MARADHI YA KISAIKOLOJIA: MULTIPARAPHILIASIS Askari wa Tume ya Jiji wapora mkaa Kuchangia Radio Kheri Broadcasting Station Yesu Kristo na Yohana Mbatizaji
Wakereketwa CCM wawakosha
wauaji wa Mwembechai
Ufugaji holela wa nguruwe
waikumba Dodoma
Watembelea na kusaidia wagonjwa Arusha Mkuu wa wilaya awatimua Masheikh
ofisini kwake
Sayansi na Teknolojia
Chakula na Lishe
Kumbukumbu ya mauaji Mwembechai
|