AN-NUUR 
Na.188 Shawwal 1419, Februari 12 - 18 , 1999 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Mwaka mmoja wa mauaji ya Mwembechai:
  
Waliouawa ni wanne
 
  • ‘Piga shaba, piga yule’: Sauti hii ya nani?
  • Kwa kukaa kimya Rais Mkapa anapanda mbegu gani?
Na Mwandishi Wetu
 

LEO ni mwaka mmoja kamili toka Waislamu kuuliwa pale Mwembechai. Katika kuikumbuka siku hiyo, Waislamu kote nchini wamekuwa wakisoma Khitma majumbani kwao pamoja na Misikitini ili kuwarehemu mashahidi waliodhulumiwa roho zao. 

Pamoja na Khitma, Waislamu wamekuwa wakiangalia kanda za tukio hilo ambazo zimeenea sasa takribani nchi nzima. 

Baada ya kuiona kanda hiyo baadhi ya waumini wamedai kwamba waliouliwa ni wanne na sio wawili kama ilivyotangazwa awali na vyombo vya habari. 

Jijini Dar es Salaam Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu limeandaa Khitma leo baada ya swala ya Alasiri katika Msikiti wa TIC Magomeni, Jijini. 

Khitma nyingine itakuwa Jumamosi Februari 13, Msikiti wa Tungi, Temeke wakati katika Msikiti wa Ijumaa Mtaa wa Arusha Ilala Khitma itakuwa Jumapili Februari 14. 

Katika Msikiti wa Mtambani, kumbukumbu ya mauaji hayo ilianza kwa kikao cha Maimamu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Kikao hicho kilianza kwa kuangalia kanda ya mauaji ndipo Maimamu wakapata fursa ya kujadili kadhia hiyo iliyoitia doa jeusi historia ya nchi yetu. Kikao hicho kilifanyika jana Februari 11. 

Leo itakuwa ni kikao cha akina mama ambapo pamoja na mambo mengine watapokea taarifa ya kamati ya akinamama baada ya kutazama kanda. 

Kilele cha kumbukumbu hiyo itakuwa kesho ambapo kutakuwa na mkutano wa Waislamu wote. Pamoja na kutazama kanda itakuwepo khitma pamoja na kutafakari kwa pamoja mauaji hayo na nini kifanyike. 

Utafiti uliofanywa na gazeti hili kwa miji ya Arusha, Tanga, Moshi na Dar es Salaam umeonyesha kwamba kanda za mauaji ya Mwembechai zipo takribani katika kila nyumba ya watu wenye video. 

Watu kadhaa ambao wameshautizama mkanda huo wamesema kwamba ukweli mwingi ulikuwa haujasemwa juu ya kadhia ya Mwembechai. 

Baadhi yao wamesema kwamba si kweli kwamba waliouliwa katika tukio lile ni watu wawili tu. 

Mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Hassan Mushi wa Msikiti wa Riadha mjini Moshi alidai kwamba yeye kwa uchache alihesabu watu wanne waliouliwa pale pale. 

Alisema mtu wa kwanza aliyemuona ni kijana aliyekuwa amevaa raba nyeupe zikiwa na mistari mweusi. Alisema kijana huyo ameonekana katika kanda akiwa amelalia ‘bwawa’ la damu sehemu za kichwani kuonyesha kwamba alipigwa risasi ya kichwani. 

Mtu wa pili amesema ni kijana mweusi aliyekuwa amevaa shati mikono mirefu, rangi ya bluu. Katika kanda hiyo amesema mzee Mushi, kijana huyo anaonekana akiwa amelala chali kisha anapumua kwa nguvu, kutoa sauti ya kukoroma na kukata roho. 

Mwingine aliyenaswa na mpiga picha anasema ni kijana mweusi mwenye jiwe mkononi aliyekuwa amevaa shati la mikono mifupi. "Kijana huyo anaonekana kinywa wazi akiwa ameshakufa", amesema mzee Mushi. 

Mtu wa nne kwa mujibu wa maelezo ya mzee Mushi ni kijana aliyekuwa amevaa fulana (T.Shirt) na suruali nyeusi. Kijana huyo anaonekana akiwa kalalia dimbwi la damu kwa sehemu ya mgongoni. 

Amesema mzee Mushi, askari wawili wasio na sare wanaoonekana wakimpiga kwa gongo kijana huyo miguuni na baada ya kuona kafa wakawa wanamburura kama mzoga hadi kwenye Land Rover ya Polisi. 

Alisema askari hao wawili wanaoonekana wakimburura kijana huyo mmoja kavaa fulana ya bluu yenye ukosi mweupe wakati wa pili anaonekana kuvaa shati na suruali zote rangi ya udongo. 

Naye Bw. Farijala Lesika wa Arusha Msikiti wa Bondeni anasema kinachotisha katika kanda hiyo si kushuhudia tu maiti za wadhulumiwa, lakini ile hamasa na bashasha waliyokuwa nayo polisi wakipiga risasi. 

Amesema sauti inasikika ikitoa amri "piga shaba", "piga shaba", huku anaonekana askari aliyekuwa na juhudi sana kulenga shabaha huku akikenua meno. 

Bw. Lesika anasema kabla hajaiona kanda hiyo alidhani kulikuwa na mapambano hasa kati ya polisi na Waislamu na walipozidiwa nguvu ndipo wakaamua kutumia silaha za moto. Lakini anasema kitu kama hicho hakikuonekana kwenye kanda. 

Askari walikuwa mbali na Waislamu wanaonekana wakiwa wamejikusanya mbali huku vijana wakirusha mawe. 

Anasema hata polisi wenyewe wanasikika katika kanda mmoja wao akisema, " watoto wenyewe hata kunyonya hawajaacha". Ikiwa ni msemo wa kumaanisha kwamba walikuwa watoto wadogo au watu wasio na uwezo wowote wa kupambana na polisi. "Vipi basi watoto wadogo wawazidi nguvu polisi wenye marungu, mabuti, mabomu ya machozi, ngao n.k. hata ilazimike kutumia silaha za moto kuwaua", alihoji Bw. Farijala Lesika. 

Bw. Abdurahim Lubuva wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa Arusha, yeye ana maoni kwamba yaelekea askari walishapewa agizo kwamba kwa vyovyote itakavyokuwa lazima waue. 

Anasema, maoni yake yanatokana na ukweli kwamba waliokuwa wamejazana walikuwa ni watoto ambao kuonyesha utoto wao kila risasi ikifyatuliwa hushangilia bila kujali hatari inayowakabili. 

Aidha, alisema hakuna mahali panapoonyesha polisi wakiwa wamezingirwa na kushambuliwa. Bali vijana walikuwa mbali wakirusha mawe ambayo yalikuwa hata hayawafikii polisi. Na hata zilipopigwa risasi za moto inaonekana polisi akiwalenga watu walio mbali zaidi ya mita mia. 

Aidha, anasema ushahidi mwingine ni kuwa hawaajarifiwa mpaka leo kama yupo polisi aliyetiwa ngeu akapelekwa Muhimbili mahututi. 

Mama mmoja wa Tanga aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwanakombo alisema kwamba kilichomtisha ni ile hali ya unyama ambayo anadai aliifananisha na mauaji ya Soweto. 

Hata hivyo, akasema Soweto walionekana askari weupe wakiwafyatulia risasi watu weusi. Lakini katika tukio la Mwembechai wanaonekana Watanzania weusi wakiwamininia risasi Watanzania wenzao weusi. 

Kwa ujumla, waliohojiwa na gazeti hili baada ya kuitazama kanda wameonyesha masikitiko yao na kubaki wakihoji chuki na dhulma hii asili yake nini na mbegu gani inapandwa kwa serikali kukaa kimya na kuchelea kuchukua hatua. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
  

Tahari 
Tusirudishane nyuma 

Mwaka mmoja wa mauaji ya Mwembechai: Waliouawa ni wanne
Na Mwandishi wetu

Waasisi wa TAA waibuka kupigania haki zilizoporwa

Kuhujumiwa Waislamu kielimu: Mzazi adai mwanafunzi Adam Rashid kafelishwa

Maoni yetu: Tuondoleeni wenye mikono ya damu

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: MULTIPARAPHILIASIS

Askari wa Tume ya Jiji wapora mkaa

Kuchangia Radio Kheri Broadcasting Station

Yesu Kristo na Yohana Mbatizaji
Na BERNARD B. MWENDA

Wakereketwa CCM wawakosha wauaji wa Mwembechai
Na Idd Kikong’ona, Morogoro

Ufugaji holela wa nguruwe waikumba Dodoma
Na Abu Zubeir, Dodoma

Watembelea na kusaidia wagonjwa Arusha

Mkuu wa wilaya awatimua Masheikh ofisini kwake
Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Kutoka magazeti ya zamani

Sayansi na Teknolojia 
[Windows: Mambo Mazuri ya Kuyajua] 

Masomo ya Kiislam 

Barua za Wasomaji 

Mashairi

Chakula na Lishe 
[Kauli hii ya serikali itatumaliza Watanzania kwa njaa] 

Kumbukumbu ya mauaji Mwembechai 
[Maazimio ya Maimamu Dar]
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita