AN-NUUR 
Na.188 Shawwal 1419, Februari 12 - 18 , 1999 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Wakereketwa CCM wawakosha wauaji wa Mwembechai 
 
  • Wadai kuonyesha mkanda wa mauaji ya Mwembechai ni kuleta fitna 
Na Idd Kikong’ona, Morogoro
 

WAKATI madai ya Waislamu dhidi ya hujuma na dhuluma wanazotendewa na serikali ya chama tawala cha CCM kwa miaka mingi kinyume na katiba ya nchi bado yapo kwenye meza ya Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi wa haki, wakereketwa wa CCM mjini Morogoro wameonekana wakitonesha vidonda vya Waislamu kwa kuwakosha wale waliohusika kumwaga kutonesha damu za Waislamu bila ya haki pale Mwembechai. 

Wakereketwa hao wa CCM walionekana wakiwagawia waumini waliokuwa wakikusanyika kwa ajili ya sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Boma Road makaratasi yanayowashutumu Waislamu wanaoonyesha kanda za mauaji ya kinyama yaliyofanywa na askari wa serikali. 

Mwandishi wa habari hizi alibahatika kupaka nakala moja ya makaratasi hayo kutoka kwa anayedaiwa kuwa mkereketwa wa CCM Bw. Yusufu Ngadu mkazi wa maeneo ya Soko Kuu ambaye ndiye kinara wa usambazaji vitini hivyo kama alivyokuwa akifanya Msikitini hapo kwa kuwagawia waumini mmoja baada ya mwingine. 

Katika makaratasi hayo yaliyotawanywa chini ya mwavuli wa kumtetea na kumuunga mkono Sheikh Bafadhil, wakereketwa waliojibatiza nembo ya "wapenda amani" wamedai kuwa baadhi za taasisi zinazojenga Misikiti ili kuitumia kama majukwaa ya kisiasa ya mwaka 2000 na kuongeza kuwa inawagombanisha Waislamu wakichukie chama tawala na serikali iliyopo madarakani. 

"Na kibaya zaidi walitaka kutumia Misikiti hiyo wanayoijenga ili iwe jukwaa la siasa la 2000 na kuwagombanisha Waislamu wachukie chama tawala na serikali yake iliyo madarakani", zinaeleza karatasi hizo. 

Kuhusu kuonyeshwa kwa kanda za mauaji ya Mwembechai kwa lengo kuwaonyesha Waislamu unyama uliofanywa Februari 13, 1998 wakereketwa hao wanadhihirisha hisia zao kwenye makaratasi yao kama ifuatavyo: 

"... na kutaka kuonyesha video ya vurugu za Mwembechai ili iwe kichocheo cha fitina na mgawanyiko wa Waislamu hapa nchini. Na hawa maadui wasifanye Waislamu kafara ya kwenda Ikulu". 

Waumini mkoani hapa wakitoa maoni yao kuhusiana na makaratasi ya wakereketwa wa CCM, baadhi yao wamedai kwamba hawa ni vipaza sauti wanaozifanyia ukasuku mbinu za maadui wa Uislamu za kuwapaka matope Waislamu waonekane kinyaa kwenye jamii ili dhuluma iendelee bila ya pingamizi na kusema kuwa hizi ndizo kauli zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya viongozi wa serikali na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini. 

"Watu hao wamejiandaa kufanya machafuko nchini. Tunaomba serikali na chama chake na wapenda amani kuikomesha kwa pamoja na hasa ukizingatia uchaguzi 2000 umekaribia na hatufahamu hawa watu wamejiandaa kwa lipi", walimwonyesha kipengele hiki mwandishi wa habari hizi. 

Naye Bwana Mohammed wa Mtoni mjini hapa amesema kwa Waislamu si wenye kuzugwa kirahisi hivi sasa. 

Akizungumzia dhana ya kutozungumza siasa Misikitini Bwana Mohammed amesema kuwa Uislamu ni utaratibu kamili wa maisha usiotenganisha dini na siasa na kwamba dhana ya utenganisho haina ushahidi wa Qur’an wala Hadith dhaifu. 

"Qur’an tunaiona ikiwakemea watawala wenye sera na siasa za kuwadhulumu na kuwakandamiza wanaoongozwa kwa misingi ya kujenga matabaka, na Firauni ni mfano wa karibu". 

Bwana Mohamed aliongeza kwa kusema kuwa Mtume (s.a.w.) aliitumia Msikiti kama kituo cha siasa za Kiislamu aliwapokea na kuzungumza na mabalozi waliokufa katika dola ya Kiislamu kutoka sehemu mbalimbali na barua zilizotumwa kwa wafalme mbalimbali ziliandikwa Misikitini na kuwatuma wajumbe maalum wa kuzipeleka hizo. 


Ufugaji holela wa nguruwe waikumba Dodoma
  
Na Abu Zubeir, Dodoma
 

WAUMINI wa Kiislamu katika Kijiji cha Veyula (Masjid Jihad) nje kidogo ya Manispaa ya mji wa Dodoma wameitaka serikali ya kijiji kuchukua hatua za haraka za kumzuia mama mmoja ambaye ni mfugaji wa nguruwe adhibiti mifugo yake na aiweke mbali na eneo la Msikiti na kwa Waislamu wa eneo hilo. 

Kaimu Katibu wa Masjid Jihad Ustadh Amri Juma alitoa taarifa hiyo baada ya sala ya Ijumaa hivi karibuni. Katibu huyo ambaye alimtaja mfugaji kuwa anafahamika kwa jina la mama God, alitakiwa na uongozi wa Msikiti huo ahamishe mifugo yake, hali ambayo haikumfanya akubali wito huo. 

Ustadh Juma na Mwenyekikti wa Msikiti huo Bw. Khamis Nangumbe waliazimia kuchukua jukumu la kumtumia barua yenye Kumb. Na. BWV/MJ/99/01 ya Januari 14, 1999 kwa niaba ya Baraza la Msikiti wa Veyula. 

Barua hiyo ambayo ilisomwa Msikitini hapo ilionyesha na kutegemea nakala zake kusambazwa kwa katibu mtendaji Veyula, kituo kidogo cha polisi Ujenzi, Bakwata Wilaya na kwa mhusika mwenyewe. 

Aidha, barua hiyo ilisisitiza juu ya kulinda haki za jamii ambazo zimewekwa na serikali za mitaa hususan juu ya udhibiti wa mifugo ya nguruwe kuwa mbali na maeneo ya kuabudu hasa Misikiti na maeneo ambayo wanaishi Waislamu. 

Hata hivyo, inasemekana mfugaji huyo anakusudia kuhamisha mifugo yake kabla ya hatua wanazotarajia kuzichukua Waislamu dhidi yake. Kauli hiyo ilisikika ikitoka kwa Katibu Mtendaji wa kijiji cha Veyula alipokuwa akiongea na Ustadh Adam ambaye ni mjumbe na muasisi wa Masjid Jihad akiwa na mwandishi wa habari hizi. 

Mwandishi wa habari hizi amegundua katika maeneo mengi ya mji wa Dodoma umekumbwa na ufugaji holela wa nguruwe, maeneo kama Makole, Makole N.H.C., Nkuhungu na Mnadani ambapo uuzaji na uchomaji wa nyama ya nguruwe unafanyika kwa hatua zisizozidi sabini kufikia machinjio ya ng’ombe na sehemu ya uuzaji wa nyama za mbuzi na ng’ombe. 

Wakati huo huo, kikundi cha akina mama wa Kiislamu cha Bi Khadija cha mjini Dodoma kimewaomba Waislamu wa kiume washirikiane kutunisha mfuko ulioanzishwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini. 

Mwenyekiti wa kikundi hicho Bi Mwanahamisi Abdallah alimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa wanaume lazima wawe karibu kuwaunga mkono kwani wao ndiyo wamiliki wakuu wa mali. 

"Michango yetu ni shilingi 500 kila mwezi na tayari wanawake wameanza kutunisha mfuko huo", Bi Mwanahamisi alisema. 


Watembelea na kusaidia wagonjwa Arusha 
 

WAISLAMU mkoani hapa wameazimia kufanyia kazi majukumu yote yaliyoagizwa na Allah (s.w.) na Mtume Muhammad (s.a.w.) kadri watakavyojaaliwa katika maisha yao. 

Wamesema hayo baada ya kumaliza amali ya kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa waliolazwa hospitali mbalimbali ndani ya Manispaa ya mjini hapa, kama ilivyokuwa ada yao, ambapo wamelenga siku maalumu ya Ijumaa kwa ajili hiyo kwani ni muda mrefu amali hiyo iliachwa bila kutekelezwa kama si kusahaulika uongozini mwa walio wengi hapa nchini. 

Akiongoza msafara wa Waislamu toka Masjid Riyaadh Daraja II pamoja na baadhi ya wanafunzi wa Madrasat An-Swar-Sunnah Majengo kiongozi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini amewakumbusha Waislamu kote nchini kuwa mstari wa mbele katika kufanyia kazi maamrisho yote ya Allah (s.w.) yaliyo ndani ya mafundisho sahihi ya Mtume Muhammad (s.a.w). 

Akitoa mfano alisema zama za Mtume Muhammad (s.a.w.) alikuwa akiwaamrisha Masahaba zake na yeye mwenyewe kutembelea nyumba hadi nyumba na kutoa misaada pale ilipohitajika, waumini leo wanafanya amali gani, aliuliza kwa uchungu kiongozi huyo. 

Aliyapa nguvu maneno hayo kiongozi huyo kwa kutoa kisa kimoja mashuhuri ambacho kilitendeka zama za Mtume (s.a.w.) kwamba siku moja akiwa anazungumza na masahaba zake ghafla alitokea Bwana mmoja aliyemtaka msaada wa kwenda kumkombolea bidhaa zake alizonyang’anywa na kafiri mmoja aliyekuwa mkorofi sana zama hizo, bila kusita Mtume (s.a.w.) alikwenda moja kwa moja kwa yule Bwana (Kafiri) na akazikomboa bidhaa za yule Bwana na ikawa ni sababu ya yule Bwana kuingia ndani ya dini ya Allah (s.w) kwa hiyo hapo limepatikana funzo kwamba msaada hupewa mtu yoyote mwenye shida na akawataka Waislamu kutofanya ubaguzi yoyote kwani sisi sote tumetokana na Baba Adam (a.s.) aliyetokana na udongo. 

Wakati huo huo, wauguzi mbalimbali walioongea na Mwandishi wa habari hizi siku hiyo wameonyesha kuridhishwa kwao na kitendo hicho cha Waislamu, pia wamechukua fursa hiyo kumpongeza mfanyabiashara mmoja hapa mjini ambae ni kichocheo katika kufanikisha suala hili na kutoa wito kwa wafanyabiashara, jumuiya na taasisi zote mkoani hapa kuiga mfano wa kujitolea kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wasio na uwezo. 

Nao wagonjwa kwa upande wao wamefurahishwa sana na kitendo cha Waislamu hao kwa kuwajulia hali na kujaribu kuwatatulia baadhi ya matatizo yao na dua walizoombewa ili Allah (s.w.) awajaalie dawa wanazopewa iwe ni sababu ya kupona maradhi yao. 


Mkuu wa wilaya awatimua Masheikh ofisini kwake 
 
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
  

WAISLAMU mjini Morogoro wametoa shukrani zao za dhati kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Hawa Ngulume kwa kuwapa ushahidi mwingine muhimu na wa wazi kwa mlolongo wa dhulma za serikali dhidi yao.  

Wakiongea na ANNUUR hivi karibuni katika Msikiti Mkuu wa Boma, Mafiga na Kiwanja cha Ndege kwa nyakati tofauti kufuatia malalamiko yao juu ya ujenzi wa baa mbele ya Msikiti wa Qiblatain (Mafiga A) kufumbiwa macho na ujumbe wao kutimuliwa serikalini, waumini hao walisema kuwa subira yao itafikia kikomo. 

Walisema kwamba kitendo cha Bi Ngurume kuutumia ujumbe wa Waislamu uliokwenda kufuatilia kadhia hiyo ambao uliongozwa na Sheikh Gugulu si tu kuwadhalilisha Waislamu bali pia kimewapa ushahidi mwingine tosha wa mlolongo wa dhulma dhidi yao zinazofanywa na serikali ya CCM. 

"Kwa kuichagua CCM matokeo yake ndiyo haya ya sisi kuonekana kama wakimbizi ndani ya nchi yetu", amesema Sheikh Abdallah Salum mkazi wa Boma Road mjini hapa. 

Muumini mwingine Bw. Othman Msema Kweli wa Mafiga A alimueleza Mwandishi wa habari hizi kuwa kiongozi yoyote wa serikali yuko kwa ajili ya watu wale na si tu ikiwa kundi fulani la raia lililojipa hadhi ya daraja la kwanza, sasa Bi Ngulume kuutimua ujumbe wao kwa kuwanasibisha na siasa kali kabla ya kusikiliza undani wa madai yao unawaacha na alama nyingi za mshangao. 

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umegundua kuwa kabla ya malalamiko hayo kufika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya huyo, kwanza yalifikishwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa Julai 23, 1998 kwa maandishi na nakala yake iligawanywa kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, RPC, OCD, Madiwani wote wa Manispaa, Katibu Mtendaji kata ya Mafiga, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa (Bw. Muhina ambaye ni mmoja wa wajumbe waliotimuliwa na Bi. Ngulume ofisini kwake kwa tiketi ya siasa kali), mmiliki wa baa na gesti husika (Three Ways Guest and Bar) na kwa Waislamu wote. 

Katika waraka huo, Waislamu wa Qiblatain (Mafiga) walionyesha masikitiko yao kwa Manispaa kutoa leseni ya vileo kwa mmiliki wa nyumba namba 337 Block CC Misufini iliyo umbali usiozidi mita kumi toka Msikiti ulipo. 

"Tunatambua fika kuwa kila raia ana haki ya kufanya atakalo ili mradi havunji sheria za nchi. Nasi tuna malalamiko juu ya hili kwa kuwa tuna ushahidi wa kutosha kwamba sheria na taratibu zinazohusika hazikufuatwa na pengine inawezakana hata njia zilizotumika ni za ulaghai. Aidha tunaamini kwa uadilifu wa ofisi yako na kwa taratibu zingefuatwa kwamba leseni isingetolewa kwa kuzingatia nukta zifuatazo: Maoni ya wakazi (waathiriwa) katika eneo hili, umbali unao kubalika kisheria toka Msikiti au nyumba yoyote ya ibada na hisia za imani za waumini wa Msikiti wa Mafiga", ilisema sehemu ya waraka. 

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Manispaa hakutoa jibu lolote la maandishi kwa Waislamu zaidi ya kuwazungusha na baadhi ya watendaji wake kutoa lugha za kukatisha tamaa kila wanapofuatilia. 

Katika barua yao ya Agosti 11, 1998 yenye Kumb, Na. MM/MG/GF/98/02, waumini hao walimueleza Mkuu wa Wilaya kwamba hoja za malalamiko yao hazitegemei tu msimamo wa imani ya Kiislamu dhidi ya ulevi, bali pia wanao ushahidi juu ya ukiukwaji wa sheria za nchi kuhusiana na uanzishaji wa Bar hiyo ya "The Three Ways". 

Hivyo, Waislamu hao walisema kuwa wameamua kulipeleka suala hilo kwa Mkuu wa Wilaya Bi Ngurume ili lipatiwe ufumbuzi wa kudumu. Nakala ya barua yao walidai imefikishwa kwa Waziri wa Serikali za Mitaa, Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Manispaa, Mwenyekiti Kamati ya Maendeleo Mafiga (Diwani Suleiman Yange ambaye imedaiwa kutamka wazi kuwa taratibu za kutoa leseni ya Baa hiyo zilikiukwa), mmiliki wa Baa husika na kwa Waislamu wote. 

Mkuu wa Wilaya Bi Hawa Ngulume ambaye pia ni Mbunge wa viti maalum wanawake alianza kushughulikia suala hilo na lingine jipya kwa kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa kuchunguza ukweli wa mambo na kuchukua hatua za haraka, hususan katika kiwanja namba 10/C eneo la makazi ya watu huko Boma Road ambapo pamewekwa klabu ijulikanayo kama DAKAU na eneo la Mafiga. 

"...Kazi ya ofisi yako ni kulinda sheria, hivyo si vyema kuacha watu wafanye vile wapendavyo. Nangojea jibu la utekelezaji wako haraka. Izingatiwe kuheshimu maeneo ya Ibada", ilisema sehemu ya barua ya Bi Ngulume ya Agost 19, 1998 yenye Kumb. Na. HD/R.60/13/93 kwa Mkurugenzi huyo na nakala kupelekewa Mkuu wa Mkoa (kwa taarifa) na Sheikh wa Mkoa Morogoro (Omar Bafadhil kumfahamisha kuwa hatua zinachukuliwa). 

Naye Mkurugenzi wa Manispaa akitekeleza agizo la bosi wake, alimwandikia barua mmiliki mmoja tu wa DAKAU (ambaye alilalamikiwa na BAKWATA kuuza vileo kando ya Msikiti wao) Agosti 5, 1998 yenye Kumb. Na. 110/MTC-2/52 ikirejea barua yenye Kumb. Na. L.20/MMC-2/87 ya Aprili 14, 1998 na L.20/MMC-2/92 ya Mei 18, 1998 zote zikimtaka afunge mara moja biashara ya vileo anayoifanya kinyume na sheria. 

"Nimeagizwa tena nikuarifu yafuatayo: Kwamba ufunge biashara ya kuuza vileo hapo mara moja pindi upatapo barua hii, haruhusiwi mtu yeyote kunywa pombe kwenye eneo lako la biashara. Endapo hutatimiza masharti haya, hatua za kisheria zitafuatia pamoja na kunyang’anywa lesini ya biashara inayotumika mahali hapo", imesema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Bw. G.J. Mwaijonga kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa na nakala yake kupelekwa kwa Mkuu wa Mkoa (kwa taarifa), Mkuu wa Wilaya (kwa taarifa) na mkuu wa polisi wilaya kumuomba msaada wake (panapohitajika) juu ya suala hilo. 

Kutokana na suala hilo jinsi lilivyoshughulikiwa kwa kuyafanyia maombi ya BAKWATA na kuyapuuza ya waumini wengine juu ya "The Three Ways Guest House and Bar" waumini wa Mafiga wakateua ujumbe wa watu wanne chini ya Mzee Gugulu, Mzee Kiswanya na Mwenyekiti wa Mtaa Mzee Muhina pamoja na Katibu wa Msikiti huo Ustadh Said kwenda kumuona Mkuu wa Wilaya ili kujua hatima ya suala hilo. 

Katika ofisi za mkuu wa wilaya ambapo mwandishi wa habari hizi pia alikuwapo Bi Ngurume hakutoa kabisa nafasi kwa ujumbe huo kueleza kile kilichowaleta, badala yake aliuvika joho la "siasa kali" na kuwalaumu wazee hao kwa kile alichokiita "kuburuzwa na vijana wa mujahidina" ambao alidai wanajiona kuwa wana haki juu ya kila kitu kuliko wengine, kisha akawatimua kwa kuwaaambia "nina kazi nyingi muhimu za kufanya, sina muda wa kusikiliza mambo yenu... ondokeni ofisi kwangu". 

Mwandishi wa habari hizi alipotaka kujua kwanini aufukuze ujumbe ho bila kusikilizwa vizuri akajibiwa "kijana wewe mkorofi sana, kuanzia sasa sitaki kabisa kukuona ofisi kwangu", alisema Mheshimuwa Mbunge huyo kwa ukali huku akigonga meza kwa ngumi ya mkono wake wa kuume. 

Wakati huo huo, uchunguzi wa ANNUUR mapema wiki hii umegundua kuwa biashara ya vileo ingali ikiendelea kama kawaida katika klabu ya DAKAU kando ya Msikiti wa Boma Road licha ya kupigwa marufuku. 

Juu 
 

YALIYOMO 
  

Tahari 
Tusirudishane nyuma 

Mwaka mmoja wa mauaji ya Mwembechai: Waliouawa ni wanne
Na Mwandishi wetu

Waasisi wa TAA waibuka kupigania haki zilizoporwa

Kuhujumiwa Waislamu kielimu: Mzazi adai mwanafunzi Adam Rashid kafelishwa

Maoni yetu: Tuondoleeni wenye mikono ya damu

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: MULTIPARAPHILIASIS

Askari wa Tume ya Jiji wapora mkaa

Kuchangia Radio Kheri Broadcasting Station

Yesu Kristo na Yohana Mbatizaji
Na BERNARD B. MWENDA

Wakereketwa CCM wawakosha wauaji wa Mwembechai
Na Idd Kikong’ona, Morogoro

Ufugaji holela wa nguruwe waikumba Dodoma
Na Abu Zubeir, Dodoma

Watembelea na kusaidia wagonjwa Arusha

Mkuu wa wilaya awatimua Masheikh ofisini kwake
Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Kutoka magazeti ya zamani

Sayansi na Teknolojia 
[Windows: Mambo Mazuri ya Kuyajua] 

Masomo ya Kiislam 

Barua za Wasomaji 

Mashairi

Chakula na Lishe 
[Kauli hii ya serikali itatumaliza Watanzania kwa njaa] 

Kumbukumbu ya mauaji Mwembechai 
[Maazimio ya Maimamu Dar]
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita