AN-NUUR 
Na.188 Shawwal 1419, Februari 12 - 18 , 1999 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Barua
  
Waziri Mkuu Sumaye tukaongelee wapi?

Ndugu Mhariri 

Namshukuru Allah (s.w.) kwa kuniwezesha kushika hii kalamu na kuandika kwa upeo. Pia namtakia Rehema na Amani Mtume wetu (s.a.w.). 

Hawa wanasiasa ambao ndio viongozi wetu wamekuwa ni "wafalme wa propaganda" yaani wanabadilika kulingana na matakwa ya nafsi zao na wala si maslahi ya wananchi. 

Masuala ya jamii ya Tanzania lazima yaongelewe popote pale; tena zaidi basi wale wawakilishi wao lazima wayajadili kama sio wao basi nani atafanya hilo? 

Waislamu wakiongea Misikitini mnasema eti tusichanganye dini na siasa. Halafu Waziri Mkuu anamlaumu Mheshimiwa Kitwana Kondo kwa kusema masuala hayo Bungeni, eti adai huo udini. 

Sasa tuongelee wapi Waziri Mkuu? Msikitini Mwembechai wahuni, Bungeni udini, viwanja vya wazi kashfa, sasa tueleze tufanyie wapi maana unakataza sehemu hizo, lakini hatujaambiwa tukasemee wapi. 

Haya muwatendeayo Waislamu yataipeleka nchi pabaya. Mifano ya wanaodhulumiwa mnaiona, japo wengi wa madhalimu hujidai kuvaa miwani ya mbao. Rwanda, Burundi, Zaire ya zamani na mifano kama hiyo inatokana na kundi moja kunyanyaswa, hivyo tusilete ukereketwa wa dini zenu viongozi kukandamiza za wengine, hii ni hatari. 

Makamu wa Rais alisema hapo nyuma aliwataka Waislamu wakae na waeleze matatizo yao kwa serikali. Je sisi Waislamu tukaongee chini ya miti? Hapa hapana hoja isipokuwa udini wao wanaoutenda wanatugeuzia sisi. "Jihadi iliyo bora kabisa ni kusema ukweli mbele ya kiongozi jeuri". 

Mama Hijira, 
P.O.Box 3540, 
Mwanga, 
Kilimanjaro. 



Mauaji ya Mwembechai hayafai kukemewa? 

Ndugu Mhariri 

NAOMBA nafasi japo kidogo katika gazeti lako la ANNUUR ambalo limechukua nafasi ya ukweli na uwazi katika habari zote ili niweze kutoa machache kuhusu nasaha zilizotolewa na Mheshimiwa Dk. Omar Ali Juma siku ya Idd el Fitr. 

Pamoja na maoni mengi aliyoyasema, jambo ambalo mimi nimelizingatia ni lile la mauaji ya watu wazima hususan wanaodhaniwa washirikina (wachawi) ambao hukatwa mapanga n.k. na watoto wadogo ambao wanapozaliwa hutupwa kwenye vyoo au huuliwa kwa namna yoyote ile na utoaji mimba. 

Mheshmiwa katika nasaha zake alisema ni mauaji ya kinyama na akawakumbusha Masheikh na Maimamu wakemee kwa nguvu mauaji hayo tena hata mimi namuunga mkono. Lakini nilipomsikiliza mpaka mwisho sikusikia aongelee mauaji ya Mwembechai hapo ndipo niliposhangaa ndio maana imebidi niulize yale ya Mwembechai si mauaji ya kinyama? 

Na kama si ya kinyama ni mauaji ya namna gani ya piga yule, muongeze yule au hayo Maimamu hawaruhusiwi kukemea? Hili jambo mimi limenitatanisha kwa maana hii nawaomba viongozi wanapoamua kusema jambo waliseme kwa ukweli na uwazi kama ilivyo sera yetu ya chama tawala ili wapiga kura tusiwe na maswali ya kujiuliza na hatimaye kuandika magazetini. 

Hamisi Mwiru, 
Box 945, 
Singida. 


Rais anatukebehi Waislamu

Ndugu Mhariri 

NAPENDA kuchukua nafasi hii katika gazeti lako la ANNUUR ili niweze kutoa maoni yangu machache kuhusiana na risala ya Waislamu ambayo amepewa Rais na majibu aliyoyatoa mara baada ya kupokea risala hiyo katika Baraza la Idd lililofanyika hivi karibuni. 

Wengine wanadai hotuba ya Rais ni kebehi kubwa sana kwa waumini wa Kiislamu katika nchi hii. Hoja zao ni kama ifuatavyo: Ni nani au ni kiongozi gani wa serikali hii asiyojua kilio cha Waislam? 

Kwa tatizo kama la Mwembechai, nani hajui kama polisi wameua watu kwa shinikizo la viongozi fulani iwe wa dini pamoja na wa serikali? 

Mheshimiwa Rais anasema "atazungumza na Mawaziri wake". Hivi ni Waziri gani hajui suala la mauaji yaliyotokea Msikiti wa Mwembechai? Hata kwenye Bunge limeongelewa sana na mwisho wamediriki kumwambia Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kigamboni Kitwana Kondo ambaye peke yake alijitoa mhanga na aliwasilisha hoja hiyo Bungeni kama ni mtu anayetafuta umaarufu tu. 

Mimi nasema Rais anasikitisha sana kwa maneno yake, wananchi karibu nchi nzima wamedai japo iundwe Tume kuchunguza kwa kina juu ya swala la Mwembechai lakini Mheshimiwa Spika wa Bunge la nchi hii akadai serikali haina pesa za kuunda Tume ya kuchunguza mauaji yaliyotokea Msikitini na kudai kuunda tume ni gharama kubwa sana, hiyo ina maana sawa na kusema bora Waislamu waliuliwe bila ya sababu za msingi kuliko kutumia pesa za serikali kuchunguza matukio yanayoyapata na hatma yake haki itendeke na sheria ichukue mkondo wake. 

Zuberi Mohamed, 
Box 61428, 
Dar es Salaam. 


Kijiji cha Mazizi chavunja Ijumaa

Ndugu Mhariri 

WAISLAMU katika kijiji cha Mazizi wilayani Bagamoyo waliamua kuvunja ibada ya siku ya Ijumaa, kwa kuwa hakuna Imamu. 

Mimi mwenyewe nilizipeleka habari hizi kwa mara yakwanza mwaka jana mwezi wa sita habari hii iliwafikia Waislamu wote ambao wako tayari kujitolea na sasa najitokeza tena kuandika na kuwaleteeni ili unitangazie katika chombo chetu cha Kiislamu cha habari, huenda wakatokea waumini wenye elimu ya kutosha na kwenda kufundisha dini katika kijiji cha Mazizi. 

Juma Mohamed, 
Chuo cha Ualimu, 
P.O. Box 98, 
Ilonga, Kilosa. 


Mh. Kitwana Kondo usikatishwe tamaa
 

Ndugu Mhariri 

NAOMBA nafasi kwenye gazeti lako la ANNUUR ili nitoe pongezi zangu kwa Mheshimiwa Kitwana Kondo Mbunge wa Kigamboni kwa kuishauri serikali ili kuweza kufanya utaratibu utakaotuwezesha sisi Waislamu kupumzika kufanya kazi kuanzia saa 6 mchana kila Ijumaa. 

Kwa mimi binafsi naungana na Mheshimiwa Kitwana Kondo kwa ushauri wake kwa serikali. Serikali inapaswa kuzingatia jambo hili kama ilipozingatia kwa Wasabato walipoomba siku ya Jumamosi kuwa siku ya mapumziko tena siku nzima, sasa sijui kwa zama hizi za ukweli na uwazi kama kutakuwa na uzito kwa serikali kukubali siku ya Ijumaa kuwa siku ya mapumziko tena kwa nusu siku sio siku nzima. 

Aidha, kwa kumalizia pongezi zangu kwa Mheshmiwa Kitwana Kondo namuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe taqwa ili aweze kuendelea na tabia yake ya kusema kweli na kuzidi kuishauri serikali katika mambo mbalimbali. 

Asikatishwe kabisa tamaa na watu wachache wasiokuwa na hoja hai kama Mheshimiwa Kiteto, Benedict Losurutia Mbunge wa CCM ambaye alichangia baada ya Mheshimiwa Kitwana Kondo akisema kuwa baadhi ya wananchi si waumini wa madhehebu yoyote ya dini na hawataki mifarakano, hivyo akaishauri serikali masuala ya dini yasifikishwe bungeni. Vile vile waandishi wa magazeti wenye kushambulia watu badala ya kujenga hoja kama akina Mayage. 

Khamisi Yusufu Matata, 
Manzese, 
Dar es Salaam. 


NSSF nataka pesa zangu

Ndugu Mhariri 

MWANZONI mwa mwaka huu niliamua kusitisha uajiri wangu katika sehemu niliyoitumikia kwa zaidi ya miaka 10. Sababu kubwa ilionifanya nifikie uamuzi huo ni hali yangu ya kipato kuwa kidogo. 

Nilitaraji makato ya asilimia 10 ya mshahara wangu kwa kipindi hicho yangenikwamua angalau kidogo. Lakini nilipoulizia kwa karani wa maulizo nilihisi mwili ukinyong’onyea, eti hadi nifikie uzee. 

Najiuliza kwani hili ni shirika la hifadhi ya jamii au shirika la akiba ya uzeeni? Ikiwa ni hifadhi ya jamii basi mimi nastahiki kuhifadhiwa ili nisikate tamaa na kuharibikiwa kiafya. 

Isingekuwa ni sheria ya serikali, kimshahara changu hicho kidogo ningependa daima nikipate chote mwenyewe. La kushangaza pia sijawahi katika kumbukumbu zangu kusikia shirika hili likitetea viwango vizuri vya mishahara tangu lilipokuwa likiitwa NPF, zaidi ya kukazania kukatwa na kupelekwa fedha za wafanyakazi tu. 

Hivyo, ili nisione shirika lenu ni mbinu ya kiwizi wa kimachomacho kwa kutumia sheria za Bunge, nataka fedha zangu haraka. 

Masoud Mohamed Said, 
S.L.P. 6082, 
Tanga. 


Wanafunzi Waislamu mnakimbia Jihad!

Ndugu Mhariri 

NAOMBA nafasi ili nitoe machache kuhusiana na mitihani ya kidato cha nne. 

Ni kitendo cha kusikitisha kuona baadhi ya wanafunzi (Waislamu) kukimbia katika mitihani ya Maarifa ya Kiislamu (Islamic Knowledge Paper I - II). Kitendo hiki (kukimbia katika mtihani) kwa mujibu wa sheria (hukumu) za Uislamu ni sawa sawa na kukimbia katika Jihad. Kwani katika mgawanyiko wa jihad; elimu ni mojawapo ya vifungu vya jihadi. 

Mwenyezi Mungu (s.w.) anatuambia: "Wanakuomba ruhusa wale wasioamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, nyoyo zao zinashaka, kwa hiyo wanasitasita kwa ajili ya shaka zao. Na kama wangalitaka kutoka (kwenda kutafuta elimu) bila shaka wangaliandalia maaandalio yake (lakini hawakuandaa lolote, ni alama kuwa hawakuwa na nia ya kwenda ..)". 9:45-46. 

Kwa mtazamo mwepesi tu utaona kwamba wanafunzi wote waliokimbia mitihani hiyo (elimu ya Kiislamu) katika miaka minne walioitumia shuleni vipindi vya maarifa ya Uislamu walikuwa hawavipi uzito unaostahiki kama katika vipindi vya hisabati, kemia au fizikia. 

Na wakiulizwa vipi wanapuuzia elimu ya Uislamu wanajenga hoja kwamba si katika chaguo lao. Hawaelewi kuwa somo la maarifa ya Uislamu linamuongezea mwanafunzi alama nzuri za kufaulu iwapo tu watalipa uzito unaostahiki kama masomo mengine ya darasani. 

Kama wanafunzi wanakimbia mtihani unaohusu masuala ya dini yao, kuna uwezekano pia baadhi yao walifungua katika mchana wa mwezi wa Ramadhani (hawakufunga) wakati wa mitihani ya mwanzo ambayo ilikuwa ndani ya mwezi wa Ramadhani. 

Mwenyezi Mungu atujaalie kila la kheri, atuzidishie elimu na atufungulie milango ya fahamu. 

B.R. Ally, 
P.O. Box 6898, 
Dar es Salaam. 

Juu 
 

YALIYOMO 
  

Tahari 
Tusirudishane nyuma 

Mwaka mmoja wa mauaji ya Mwembechai: Waliouawa ni wanne
Na Mwandishi wetu

Waasisi wa TAA waibuka kupigania haki zilizoporwa

Kuhujumiwa Waislamu kielimu: Mzazi adai mwanafunzi Adam Rashid kafelishwa

Maoni yetu: Tuondoleeni wenye mikono ya damu

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: MULTIPARAPHILIASIS

Askari wa Tume ya Jiji wapora mkaa

Kuchangia Radio Kheri Broadcasting Station

Yesu Kristo na Yohana Mbatizaji
Na BERNARD B. MWENDA

Wakereketwa CCM wawakosha wauaji wa Mwembechai
Na Idd Kikong’ona, Morogoro

Ufugaji holela wa nguruwe waikumba Dodoma
Na Abu Zubeir, Dodoma

Watembelea na kusaidia wagonjwa Arusha

Mkuu wa wilaya awatimua Masheikh ofisini kwake
Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Kutoka magazeti ya zamani

Sayansi na Teknolojia 
[Windows: Mambo Mazuri ya Kuyajua] 

Masomo ya Kiislam 

Barua za Wasomaji 

Mashairi

Chakula na Lishe 
[Kauli hii ya serikali itatumaliza Watanzania kwa njaa] 

Kumbukumbu ya mauaji Mwembechai 
[Maazimio ya Maimamu Dar]
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita