AN-NUUR 
Na.178 Shaaban  1419, Desemba 4 - 10, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
BARUA:
 

Kwa nini Sheikh Bashir akamatwe! 

Ndugu Mhariri 

TAARIFA za kukamatwa Sheikh Omar Bashir zilizagaa Jijini mchana wa Jumapili Novemba 29, mwaka huu. 

Ilielezwa kuwa Sheikh huyo alivamiwa na askari wawili waliovalia kiraia katika eneo la Manzese akiwa katika shughuli zake za kawaida. 

Katika purukushani ile alivunjika paja lake la kulia, askari walimzoa hadi kituo cha polisi Magomeni kabla ya kumpeleka Hospitali ya Muhimbili. 

Kinyume na taarifa zinazotolewa hivi sasa, kabla ya kukamatwa kwake, hapakuwa na fununu yoyote ya polisi kumtafuta kwani tangu hapo hakuwa na hatia, mbali ya matamshi ya jazba yaliyowahi kutolewa na baadhi ya watendaji serikalini. 

Nayaita matamshi ya jazba kwa sababu hapakuwa na hoja yoyote ya msingi katika matamshi yale kuonyesha uhusika wa Imamu huyo na kile kilichoitwa vurugu za Mwembechai. 

Ni kweli Sheikh Bashir alikuwa Imam na Mhadhari Mkuu wa Msikiti wa Mwembechai kabla ya ‘vurugu’, msimamo wake wa kupinga dhulma aliusema wazi kuitahadharisha serikali ichukue hatua kurekebisha upogo. 

Vipi mtu huyo mwenye moyo wa uzalendo kiasi hiki aitwe mchochea vurugu. Au kukemea uovu hakutakiwi nchi hii. Hili viongozi wetu lazima waliweke wazi. 

Kabla ya kukamatwa Sheikh Omar alikuwa akiendelea na shughuli zake kama kawaida, alikuwa akihudhuria swala na kutoa mawaidha katika Misikiti mbalimbali, vipi leo idaiwe alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu. 

Dai hili la kumtafuta muda mrefu linatengeza mwanya wa kuwazuga wananchi ili kuhalalisha dhulma inayokusudiwa. 

Inavyoonekana jitihada kubwa inafanywa kufunika ukweli kuhusiana na kadhia ya Mwembechai. Vinginevyo tuelezwe ni nani hasa anayepaswa kutafutwa ili afikishwe katika vyombo vya sheria; ni Omar Bashir na Ponda walioikumbusha serikali kwa nyakati tofauti irejee katika wajibu wake au Lwambano na wenziwe walioandaa huzuni ya Mwembechai! 

Hebu tufike mahali tuonee aibu vitendo vyetu, nafsi zijishitaki kwa dhamira mbaya. Misimamo ya kulindana na kupendeleana kidini hata katika maovu haitakuwa na mwisho mwema. Hatuna budi kutumia kiadilifu dhamana tulizokabidhiwa. 

Nchi hii ni ya Watanzania wa dini na makabila yote yaliyomo ndani ya mipaka yake. Tusibaguane. 

Viongozi, wanasheria, makamanda na wengine mliokamata dhamana nzito, msiandae mtengano na maafa kwa vizazi vyetu. Tuepushe "Rwanda" nyingine katika sehemu hii ya Afrika. 

Mwananchi Mpenda amani, 
Dar es Salaam. 


Tuandae madaktari wanawake 

Ndugu Mhariri 

NINAOMBA fursa hii katika gazeti letu tukufu ili niweze kuufikisha ujumbe wangu mdogo kwa wahusika In-sha-Allah. 

Kutokana na uhaba wa madaktari na manesi wa kike wenye maadili ya Kiislamu katika nchi yetu, kumekuwa na udhalilishaji mkubwa wa kijinsia kwa mabinti wa Kiislamu. 

Leo hii binti wa Kiislamu endapo hospitali ahitajipo kuchomwa sindano hata kama akimkuta daktari au nesi wa kike atatafutwa mwanamume ili amchome eti kwa sababu tu anajidai Mujahidat. 

Pia ina umiza sana pale binti wa Kiislamu anapohitajika kupiga X-Ray ya kifua ili achunguzwe maradhi yake, anakutana na daktari wa kiume na kuamriwa afunue kifua chake ili aweze kupigwa X-Ray. 

Jamani hebu tufikirie kama ni wewe au mdogo wako wa kike au mkeo utakuwa katika hali gani? Ilhali kifua hicho hata baba yako, mama yako, kaka yako au ndugu yeyote asiyemaharimu wako haruhusiwi kukiona leo vipi akione John ambaye haruhusiwi kuona hata unywele wako mmoja! Inna Lillah Wainna Ilayhi Raajiun. 

Ee! Mwanaume umpelekae mkeo ambae ni mgonjwa hospitali na unaambiwa usubiri nje mkeo anaingia ndani na daktari mwanaume kufanyiwa uchunguzi huwa unajisikiaje? 

Basi ndugu zangu Waislamu kuna umuhimu mkubwa kabisa wa kuwahimiza wasichana wote waliochukua mchepuo wa sayansi kusoma kwa bidii zote na kuwafundisha kama mnaweza na kuipenda kazi ya udaktari pia kuwapa moyo katika masomo ili waje wakomboe wananchi wapenda maadili. 

Na enyi mabinti wenzangu msomao PCB, tusome kwa bidii, tuipe elimu umuhimu wake tuazimie kuwa madaktari na manesi wenye maadili ya Kiislamu ili tujikomboe na kukomboa umma wa Kiislamu katika hii fedheha iliyo kubwa kabisa. 

Rahman bint Salum, 
P.O. Box 72740, 
Dar es Salaam. 


Bakwata acheni kuchanganya haki na batili 

Ndugu Mhariri 

KATIKA gazeti hili toleo Nambari 174 ukurasa wa 13 ulituonyesha picha za mahafali ya shule za sekondari za Jamhuri na Al-Hijra za Mjini Dodoma. 

Sherehe za kuwaaga wanafunzi hao katika shule ya sekondari ya Jamhuri inayomilikiwa na Bakwata zilisindikizwa na kikundi cha taarab pamoja na kikundi cha ngoma cha Nindo Group. Kinachotushangaza sisi Waislamu ni kile kilichofanyika ambacho kilikuwa ni kinyume na taratibu za Kiislamu wakati shule hiyo inamilikiwa na Bakwata. 

Bakwata imeandaa mahafali ikiwepo taarab pamoja na ngoma, hii inatosha kuonyesha ni jinsi gani mnavyokuwa watovu wa nidhamu ya Kiislamu. 

Je, viongozi wa Bakwata mnategemea mlichokizalisha kitakuwa na tabia za aina ipi? Wakati nyinyi wenyewe mnachanganya taratibu za Kiislamu na za kikafiri katika sherehe zenu.  

Hebu tufikiri, hivi kweli viongozi hawana aibu wala woga kwa kuamua ngoma ije kutumbuiza katika sherehe hizo? Je, hamuoni mwanafunzi aliyemaliza katika shule hiyo atakapoulizwa suala la ngoma au taarab si atasema ni halali kutumbuiza katika sherehe za Kiislamu? 

Hebu Muislamu fikiri Baraza la Kiislamu linapoamua kufanya mahafali ya shule zake kwa kuwachezesha wanawake uchi (hawana hijab)?  

Ndugu Waislamu chukueni hatua mtaulizwa na Allah siku ya Malipo. Bakwata mnatuumiza roho sisi Waislamu wa kweli, acheni ukafiri. 

Zawadi Salim, 
Popatlal Sec. School, 
P.O. Box 5007, 
Tanga. 



Marekebisho ya Katiba 

Ndugu Mhariri 

Napendekeza maeneo yafuatayo yafanyiwe maelekezo ya ziada kama jinsi yafuatavyo:- 

1. SURA YA NNE: Sehemu ya pili (wabunge) katika; 

a) Iwapo wabunge ni wawakilishi wa wananchi katika uongozi wa Shirikisho la Tanzania, iwapo Wabunge wanatarajiwa kuchochea maendeleo na kuongoza katika shughuli hizo (za kuleta maendeleo) katika Majimbo yao ya uchaguzi, hawanabudi kuishi na kufanya kazi zao ndani ya Majimbo yao ya uchaguzi. 

b) Uteuzi wa Wabunge kushika nyadhifa nyinginezo (Serikalini na kwinginepo) kunawanyima wapiga kura utumishi wa Wabunge wao na hivyo kukosa maendeleo kwa jumla kwa sababu:- 

1. Wabunge hao (walioteuliwa kushika nyadhifa mbali mbali) hawatoishi ndani ya Majimbo yao ya uchaguzi na kwa ajili hiyo, hawatoshiriki katika shughuli za kuleta maendeleo Majimboni mwao. 

2. Wabunge hao, hawata wawakilisha vilivyo wapiga kura wao kwa kuwa hawatoishi ndani ya shida, maafa na ndani ya matatizo mengineyo yaliyomo na yatakayotokea ndani ya Majimbo yao ya uchaguzi. 

3. Aidha, hawatoweza kutumikia kikamilifu sehemu mbili tofauti kwa pamoja, yaani majukumu ya Wadhifa wa kuteuliwa baada ya kuwa Mbunge kwa upande mmoja na wajukumu ya Ubunge ndani ya Majimbo yao ya uchaguzi kwa upande mwingine. 

c) Idadi ya Majimbo ya Uchaguzi ipunguzwe kufikie idadi ya Wilaya. Wilaya zote nchini pamoja na kuzidiana ukubwa kieneo, zina Mkuu wa Wilaya Mmoja na kazi Wilayani zinafanyika. Kupunguzwa majimbo ya uchaguzi kutawapunguzia uzito wa mizigo wanayobeba wananchi (wapiga kura) ya kuwalipa wabunge mishahara na marupurupu mengine. Aidha tutakuwa tumeshona koti kulingana na kitambaa tulicho nacho. 

2. Sehemu ya Pili - Makamu wa Rais: 

a) Ibara 56 (4): Siyo tuiwe jinsi Ibara hivyo ilivyo (Mwaziri na Naibu Mawaziri si lazima wote watateuliwa kutoka miongoni mwa Wabunge) bali "wawe ni watumishi wa Serikali walioajiriwa katika nyadhifa hizo" Wabunge wabaki kuwa Wabunge tazama maelezo katika Ibara I. yote kwa pamoja. 

b) Mawaziri na Naibu Mawaziri watakao ajiriwa watawajibika kwa Serikali kikamilifu zaidi kuliko wanaoteuliwa kutoka miongoni mwa Wabunge ambao hulindwa na /Chama-Tawala kila wanapo tibua kazi. Linajitokeza sula la "huyu ni mwanachama mwenzetu n.k. mifano halisi na hai imetokea mara nyingi kwa Mawaziri (wa kuteuliwa) wanapoharibu Wizara moja wanahamishiwa Wizara nyingine! Yote hayo ni kwa gharama ya mlala hoi aliyepiga kura na kwamba hiyo ndiyo "haki yake". 

3. Taarifa za Utekelezaji wa Ilani za Uchaguzi 

Kiwepo Kifungu kama siyo Ibara katika Katiba kitakachoibana Serikali itakayokuwepo itoe taarifa ya utekelezaji wa Ilani za Chama Tawala zilizoiweka madarakani. Taarifa hizo zitolewe kila baada ya miaka miwili kuwajulisha (kuwataarifu) wapiga kura nini Serikali yao imefanya, n.k. Tofauti na vikao vya Bajeti. 

Maj. V.M. Kapaya, RTD



Huree! Mohamed Said 

Ndugu Mhariri 

NAOMBA nafasi kidogo katika gazeti lako ili nitoe pongezi za dhati kabisa kwa Bwana Mohamed Said, mwandishi wa kitabu "Abdulwahid Sykes 1924 - 1968". 

Bwana Mohamed Said ameeleza mambo kadhaa ya kihistoria ambayo waandishi waliomtangulia hawakuweza kuyaeleza kwa sababu moja au nyingine. 

Kitabu Abdulwahid kimeonyesha utafiti wa kina alioufanya mwandishi kabla ya kukamata kalamu. 

Mwandishi amethibitisha umahiri pale alipogusia mambo ambayo kwa jicho la kawaida mtu anaweza akasema hapakuwa na ulazima wa kuyaeleza. Ni katika nukta za namna hiyo ameweza kuuangusha uongo mwingi uliotia giza historia ya mapambano ya uhuru wa nchi yetu. 

Historia ya mapambano ya kudai uhuru na baada ya uhuru kama ilivyoandikwa na Bwana Mohamed ina mambo mengi ambayo nadhani wengi hatuyafahamu. 

Haitakuwa busara kwa yeyote yule mwenye kuitakia mema nchi hii kutokisoma kitabu hiki. 

Wale watendaji waropokaji wajifunze kutokana na hazina hii! 

Huree Mohamed Said kwa kazi yako nzuri. 

Rajab Saleh, 
Box 1876, 
Morogoro. 



Ianzishwe elimu ya watu wazima Waislamu 

Ndugu Mhariri 

NAOMBA nafasi kidogo katika gazeti lako tukufu ili niweze kuwafahamisha ndugu zangu Waislamu pamoja na viongozi wa Kiislamu vile ambavyo Uislamu umefikia katika miji yetu na vijiji. 

Ndugu zangu viongozi, wakubwa na wadogo tunaomba msaada wenu wa kujitolea kutufundisha sisi watu wazima. Tunaomba mfungue vituo vya elimu ya watu wazima (Waislamu) nchini kote Tanzania. 

Hata kama vituo hivyo vitakuwa chini ya mibuyu au miembe au milimani au kwenye viwanja vya mpira au pembezoni mwa Misikiti, mkifanya hivyo mtatuokoa maamuma wengi sana. Kuna vijana wengi sana wa Kiislamu ambao walitoroka madrasa, na hivi sasa hawajui chochote katika dini yao. 

Namuomba Allah (s.w.) asaidie kuwekezana kwa zoezi hili hapa Tanzania. 

Abedi Rashid, 
Mbezi Beach, 
Dar es Salaam. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
'White Paper  ni ulaghai wa  Serikali ya CCM' 
Na Mwandishi wetu 

Sheikh Omar Bashir awekwa rumande 
Na Mwandishi Wetu 

Mpango wa 'Kupindua' uongozi wa  Bakwata: Masheikh Dar waitwa polisi kuhojiwa 
Na Mwandishi Wetu 

Zahrau Day yatikisa Tanga 
Na Mwandishi Wetu 

MAKALA: Hatuna haja ya maelekezo ya yule aliyetufikisha hapa  
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC USA 

Huduma za afya Kondoa haziridhishi 
Na Abu Zubeir 

Wasemavyo wanaharakati 

Tunahitaji 'UN' ya Waislamu! 
Na Twahir Rashid 

Hoja binafsi: Wawekezaji watuondokesha makwetu 

Jamii inapokuwa soko huria...  
Na Said Rajab 

Someni kwa ajili ya Allah - Sheikh Baruti  
Na Muhibu Said 

Madrasa Al-Ii'Tiswamu Al-Umaahaati Fiisabiililillah - Moro 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Madrasat Hidayat Mbagala 
Na Mussa Salum  

Hali ya Uislamu Moro Vijijini yazidi kuwa mbaya  
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Sheikh Masoud Mwinyi awaonya Waislamu kuacha migogoro Babati  
Na Abu Zuberi - Babati 

Tusikaribishe mfungo wa Ramadhani kwa Vunja Jungu  
Na Abeid Poyo 

'Acheni zinaa muepukane na ukimwi'  
Na Mussa Salum 

Wavunja jungu watahadharishwa 
Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

Hoja/Uchambuzi: 
Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? 
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu 

Njia ya uzimani ni nyembamba,  waionao ni wachache 
Na Yasin Valerian Massawe 

Habari: 
Semina ya Maimamu Tanga yadai: Maimamu wanapuuzwa  
Na Mwandishi Wetu 

Kesi ya Waislamu Mwembechai yaahirishwa kwa mara nyingine  
Na Muhibu Saidi 

Kongomano la wanawake wa Kiislamu Bagamoyo 
Na Mwandishi Wetu 

Sayansi na Teknolojia 
[Kuongeza RAM kwenye Kompyuta] 
 
Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Madini ya Zinc] 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita