|
|
|
• Avunjika mguu na kulazwa Muhimbili • Ahusishwa na Mwembechai
Na Mwandishi Wetu Sheikh maarufu nchini, Omari Bashir alikamatwa na polisi Jumapili iliyopita akihusishwa na kadhia ya Mwembechai iliyotokea Februari 12 na 13 mwaka huu. Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo, Sheikh Omari Bashir alikamatwa katika eneo la Manzese, majira ya saa sita mchana wa siku hiyo. Imeelezwa kuwa askari wawili waliovaa kiraia walimvamia ghafla na kumueleza kuwa yuko chini ya ulinzi na walimshurutisha aongozane nao hadi kituo cha polisi Magomeni. Kufuatia shurutisho hilo la askari, imedaiwa kuwa ilitokea purukushani iliyosababisha Sheikh kuvunjika paja la mguu wake wa kulia. Taarifa zinafahamisha kuwa mara baada ya Sheikh Omar kufikwa na madhara hayo, askari hao ambao inadhaniwa walikuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu siku hiyo, walimzoa na kumpeleka kituo cha polisi Mgomeni. Akizungumza na gazeti hili katika hospitali ya Muhimbili Jumatatu wiki hii, Sheikh Omar alisema kabla ya kupelekwa hospitalini hapo aliwekwa kwa muda kituo cha Magomeni ambako alielezwa kuwa alikuwa akituhumiwa pamoja na kuhusika na vurugu za Mwembechai, kutaka kuvamia na kupindua uongozi wa Bakwata makao makuu. Alisema alitajiwa majina kadhaa ya wanaotuhumiwa kuhusika na "njama" za kuipindua Bakwata. Aliwataja baadhi yao ni pamoja na Sheikh Kilemile, Juma Mbukuzi na Hanzuruni Mungula. Aidha alihojiwa mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na vurugu zilizotokea Msikiti wa Mwembechai mapema mwaka huu. Gazeti hili liliwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam,Bwana Alfred Gewe siku ya Jumatatu jioni ambaye alithibitisha kukamatwa kwa Sheikh huyo kwa tuhuma ya kuhusika na vurugu za Mwembechai. Wakati huo huo, Sheikh Omr Bashir alisomewa shitaka lake akiwa kitandani hospitali ya Muhimbili siku ya Jumanne wiki hii. Kwa mujibu wa yeye mwenyewe Sheikh Omar, Hakimu na Mwendesha mashitaka walifika hospitalini hapo siku hiyo na kumsomea shitaka ambalo ameeleza kwa mujibu wa charge sheet, anatuhumiwa kuhusika na vurugu zilizotokea Mwembechai Februari 12 na 13 na kuchochea uhasama wa kidini nchini. Hata hivyo, Sheikh Omar alisema kuwa siku moja kabla ya kusomewa shitaka hilo askari wawili waliokuwa wakimlinda hospitalini hapo walimfahamisha kuwa walipigiwa simu kutoka ngazi za juu iliyowataka kuondoka hapo na kwamba walitakiwa wamfahamishe (Sheikh Omr) kuwa hana hatia. AN-NUUR ilipomhoji Kamanda wa polisi kwa njia ya simu kuhusiana
na "utata" huu siku ya Jumatano wiki hii, alisema hivi sasa mtuhumiwa yuko
chini ya magereza hivyo hangeweza kusema lolote.
Mpango wa ‘Kupindua’ uongozi wa Bakwata: • Sheikh Kilemile, Omar Bashir, Mungula, Khalifa Khamis, Mbukuzi wahusishwa
Na Mwandishi Wetu Polisi jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita iliwahoji masheikh kadhaa kuhusiana na tuhuma ya jaribio la kupindua uongozi wa Bakwata chini ya Mufti, Annuur imefahamishwa. Taarifa kutoka kwa waliohojiwa, zinaeleza kwamba maaskari waliovalia kiraia waliwafuata watu hao majumbani na kuwataka waripoti polisi kituo kikuu kwa ajili ya mahojiano. Akielezea mkasa huu, aliyekuwa Katibu wa Bakwata Sheikh Hanzuruni Mungula alisema, yeye alifuatwa nyumbani siku ya Ijumaa majira ya asubuhi na askari aliyejitambulisha kwa jina la Mollel. Bw. Mungula alisema kwamba askari huyo ambaye alidai kutokea Polisi kituo kikuu (Central Police) alimuomba afike ofisi ya upelelezi kwa ajili hiyo. "Alikuja kwa adabu zote na kutaka niongozane nae hadi central police ambako nilifikishwa hadi kwa Afisa Upelelezi Mkoa (RCO)", alieleza Sheikh Mungula wakati akiongea na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu Jumatatu wiki hii. Akiwa ofisini hapo Sheikh Mungula alieleza RCO alimfahamisha tuhuma juu ya kilichosemekana kuwa mpango wa kuipindua Bakwata na amlitaka aeleze anachofahamu kuhusiana na hilo. "Nilijibu ndio kwanza taarifa hizi nazisikia hapa", ameeleza Bwana Mungula. Aidha alisema alionyeshwa orodha ya watu wengine waliotuhumiwa kuhusika na mpango huo. Alitaja baadhi ya majina yaliomo kwenye orodha hiyo kuwa ni pamoja na yeye mwenyewe (Hanzuruni Mungula), Khalifa Khamis, na Mahawia Karenga, wengine ni Sheikh Kilemile, Kiumbe, Hamim Boza na Omari Bashir. Naye Sheikh Mbukuzi akielezea alivyotakiwa kufika polisi katikati ya wiki iliyopita, alisema yeye kama ilivyokuwa Sheikh Mungula alielezwa juu ya "mpango" huo hata hivyo alijibu ndio kwanza kuusikia pale. Aidha alimwambia afisa wa upelelezi kuwa yeye ni mtu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu hivyo alishangazwa kuhusishwa na maswala ya jumuiya nyingine. "Nilionyeshwa orodha ya majina ya wanaohusishwa na mpango huo; wamo kina Sheikh Kilemile, Omari Bashir, Khalifa Khamis, Hamim Boza, Mahawia Karenga, Hanzuruni Mungula, Abdul Rahman Kileo na Kassim Msangi", Sheikh Mbukuzi alilifahamisha AN-NUUR kwa njia ya simu. Gazeti hili liliongea na kamanda wa polisi mkoa Dar es Salaam, Bw. Alfred Gewe siku ya Jumanne wiki hii ambaye alieleza kifupi kuwa hakuwa na habari zozote juu ya suala hilo. Baadhi ya watu waliohojiwa na gazeti hili kuhusiana na tuhuma hizo za polisi, walidai hata kama ungalikuwepo mpango huo bado serikali isingekuwa na haki kuwalinda viongozi wasiotakiwa na Waislamu ambao kikatiba ndio wenye baraza lao na kwamba Bakwata ni NGO kama zilivyo nyingine. "Kama kuogopa vurugu, mbona Simba na Yanga na Jumuiya nyingine zisizo za kiserikali hubadilisha viongozi wao na hatujasikia polisi kuulinda upande fulani", alihoji mmoja wa watu hao ambaye alijitambulisha kuwa ni mwalimu katika shule moja ya Sekondari Jijini. Mwananchi mwingine alitilia mashaka usahihi wa taarifa za kuwepo kwa
mpango huo na kudai kwamba huenda zilienezwa mtaani na baadhi ya watendaji
ili kujenga hofu miongoni mwa waumini kwa malengo maalum
• Makamanda watamba na panga zao • Sheikh asema; tukiwa
Ansaar na Muhajiriin hakuna atuwezaye
Na Mwandishi Wetu SIKU muhimu kwa chuo cha Zahrau ijulikanayo kama Zahrau Day imemalizika kwa kutolewa nasaha kwamba Waislamu wote washikamane na kuwa kitu kimoja. Akizungumza katika kilele cha sherehe hizo, Sheikh Mnyamisi aliwataka Waislamu wapendane waache kuhasimiana na kuepuka fitna baina ya makundi ya Waislamu. Sherehe za Zahrau ambazo ziliutikisa mji wa Tanga kwa maandamano (Zafa) yaliyosheheni kaswida za aina yake zilizoanza mapema wiki iliyopita na zilifikia kilele chake saa sita usiku wa Novemba 30, 1998. Kivutio kikubwa katika sherehe hizo kilikuwa makamanda waliobeba panga bandia kama ishara ya kuwa tayari kuuhami Uislamu. Aidha barabara zilipambika kwa bendera za kila rangi na maandishi yenye ujumbe maalum. Naibu Mudiir wa Zahrau Sheikh Mnyamisi alisisitiza katika nasaha zake kwamba lau Waislamu wanasahau tofauti zao na kuwa kama Ansaar na Muhajiriin basi haitopatikana nguvu yoyote ya kuwachezea Waislamu. Ili kukiendeleza na kukiimarisha chuo cha Zahran, ilielezwa kwamba zinahitajika fedha za kumalizia jengo la ghorofa, kupatikana usafiri wa kumsaidia Mudiir kwenda sehemu mbalimbali anakohitajika kikazi na shughuli za Da’awah kwa ujumla. Aidha, inahitajika mishahara ya uhakika kwa waalimu, vitendea kazi darasani na malazi pamoja na chakula kwa wanafunzi. Katika kuendeleza majengo ilielezwa kwamba tokea Zahrau Day ya mwaka jana hadi kufikia kilele cha sherehe za mwaka huu jumla ya shilingi milioni kumi, laki nne, ishirini na tano elfu mia mbili zilikuwa zimechangwa. Mudiir Sheikh Muhammad Suleiman aliwahimiza Waislamu kutoa michango yao zaidi ili malengo yaliyowekwa ya kukamilisha ujenzi yasikwame. Taasisi ya Zahrau ina makao makuu yake mtaa wa Madina na Msambweni mjini Tanga na ina matawi, madrasa na Misikiti katika mikoa kadhaa nchini. Ni miongoni mwa taasisi zinazotoa mchango mkubwa sana kusambaza waalimu na maimamu katika sehemu mbalimbali nchini hasa vijijini.
|
YALIYOMO
'White Paper ni ulaghai wa Serikali ya CCM' Na Mwandishi wetu Sheikh Omar Bashir awekwa rumande
Mpango wa 'Kupindua' uongozi
wa Bakwata: Masheikh Dar waitwa polisi kuhojiwa
Zahrau Day yatikisa Tanga
MAKALA: Hatuna haja ya maelekezo ya
yule aliyetufikisha hapa
Huduma za afya Kondoa haziridhishi
Tunahitaji 'UN' ya Waislamu!
Hoja binafsi: Wawekezaji watuondokesha makwetu Jamii inapokuwa soko huria...
Someni kwa ajili ya Allah - Sheikh
Baruti
Madrasa Al-Ii'Tiswamu
Al-Umaahaati Fiisabiililillah - Moro
Madrasat Hidayat Mbagala
Hali ya Uislamu Moro
Vijijini yazidi kuwa mbaya
Sheikh Masoud Mwinyi awaonya
Waislamu kuacha migogoro Babati
Tusikaribishe mfungo wa Ramadhani
kwa Vunja Jungu
'Acheni zinaa muepukane
na ukimwi'
Wavunja jungu watahadharishwa
Hoja/Uchambuzi:
Njia ya uzimani ni nyembamba,
waionao ni wachache
Habari:
Kesi ya Waislamu Mwembechai
yaahirishwa kwa mara nyingine
Kongomano la wanawake wa
Kiislamu Bagamoyo
Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|