|
|
|
Na Muhibu Said MKURUGENZI wa shirika la kiislamu la kutoa misaada la Islamic African Relief Agency (I.A.R.A.) nchini, Sheikh Idrisa Omari Baruti, amewakumbusha Waislamu wajibu wao wa kuitafuta elimu oyote popote bila kubagua. Aidha Sheikh Baruti amewatahadharisha Waislamu kwamba daima watakuwa ni wenye kupata hasara kwa ibada zao kwa kuambulia patupu iwapo wataendelea kuzifanya ibada hizo bila Ikhlas (kwa ajili ya Allah S.W.T.). Sheikh Baruti aliyasema hayo Jumapili ya Novemba 29, mwaka huu, akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya kuhitimisha mwaka wa tano wa kozi ya kuandaa vijana wa madrasa ya IEC Centre, kuingia katika shule za Sekondari (Orientation Kozi). Mahfali hiyo iliyofanyika katika msikiti wa Shadhily, Jijini Dar es Salaam, iliandaliwa na taasisi maarufu ya Kiislamu ya Jijini ya Islmic Education Centre (IEC Centre) ambayo ndiyo inayoendesha kozi hiyo. Sheikh Baruti alisema jambo la kutafuta elimukwa muislamu limekuwa ni wajibu kwake na kamwe halina mipaka kwani ujumbe wa kwanza alioshushiwa Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) ulikuwa ni "kusoma". Akifafanua nukta hiyo, Sheikh Baruti alisema ili kuleta ufanisi mzuri katika shughuli zetu za halali za kila siku, Allah (s.w.t.) bado anazo sababu za msingi za kuifanya elimu kuwa ni "amri" kwetu hasa kwa vile imekwishatukirimu vipawa mbali mbali. "Kwa hiyo ndugu zangu, tujifunze kwa ajili ya Allah, kwa ajili ya kumtumikia yeye. Na kama hatukumnuia Allah katika ibada zetu, basi tujue kuwa hatupati kitu. Vile vile tusome kwa ajili ya kujenga akhera", alisema Sheikh Baruti. Pamoja na maonyesho mbali mbali, ikiwemo Tamthilia iliyobeba ujumbe wa kumcha Allah (s.w.t.) popote ulipo iliyoigizwa na vijana wa madrasa hiyo, pia pamoja na risala ya wanafunzi hao iliyosomwa na mabinti wa madrasa hiyo, kilele cha mahfali hiyo kilihitimishwa kwa baadhi ya washiriki, akiwemo mgeni ramsi wa mahfali hiyo, Sheikh Idrisa O. Baruti, gazeti la AN-NUUR na vijana wanaharakati wa Kiislamu wa Jijini Dar es Salaam kutunukiwa na taasisi hiyo shahada za uhusiano mwema kati yao na taasisi hiyo. Shahada nyingine zinazothibitisha tabia njema ikiwa ni pamoja na kutimiza mavazi ya heshima na stara ya Kiislamu ndani na nje ya madrasa, zilitolewa kwa baadhi ya wanafunzi wa madrasa hiyo. Aidha zawadi nyingine mbalimbali zilitolewa kwa baadhi ya wanafunzi wa madrasa hiyo wenye sifa za usomaji mzuri wa Qur-an Tukufu, Hadithi sahihi za Mtume (S.A.W.) na wenye mwenendo mzuri na tabia njema madrasani hapo. Zawadi hizo pia zilitolewa kwa wanafunzi wenye ushirikiano mwema na waliofanya vizuri katika masomo. Taasisi ya IEC Centre yenye makao yake makuu, Mtaa wa Udoe No. 24, Kariakoo, Dar es Salaam, kupitia madrasa yake hiyo yenye mfumo wa kisasa, pamoja na mambo mengine ina programu ya kuendesha kozi mbali mbali, ikiwemo Kiingereza, elimu ya Kiislamu na kadhalika, kwa ajili ya kuwaandaa vijana kuingia katika shule za Sekondari, na kwa watu wazima na wengine wasiojua kusoma kabisa. Mafanikio ya madrasa hiyo tangu kuasisiwa kwake ni kuwa kwa asilimia
zaidi ya tisini 90% imekuwa ikiwawezesha wanafunzi wake kufaulu vizuri
katika shule za Sekondari wanazoingia baada ya kupikwa vizuri na kozi yake.
• Ni ushirikiano wa kina mama wa Kiislamu • Ilitokana na changamoto
ya BALUKTA
Na Rajab Rajab, Morogoro MADRASA hii ya ushirikiano wa kina mama wa Kiislamu ipo katika Msikiti maarufu mjini hapa wa Uwanja wa Ndege, ambapo ilianzishwa kutokana na changamoto ya iliyokuwa BALUKTA upande wa kina mama chini ya Mwenyekiti wake Mama Mwanaidi Bashiri na Katibu wake Mariam Amir Mponda. Historia ya madrasa hiyo inaanzia mwaka 1988 ambapo ilianza kwa kuwa na wanafunzi kina mama thelathini (30) hadi sasa hivi ina jumla ya wanafunzi 40 na inasimamiwa na walimu watatu ambao ni Mariam Mponda , Mwanaidi Nasibu Jaka na Aisha Juma. Aidha, madrasa hiyo katika jitihada zake za kuwapatia elimu kina mama wa Kiislamu wa Morogoro, imeanza kufungua matawi mengine katika Msikiti wa Mafiga (B) ambapo kuna jumla ya wanafunzi 30, madrasa nyingine imefunguliwa Vibandani pamoja na Msikiti wa Nurain uliopo eneo la MUDECO. Katika kuhakikisha kuwa wanajiendeleza kiujuzi na kiuchumi, madrasa hiyo ya Al-Iitiswamu wana mpango wa kuanzisha darasa la ushonaji nguo kwa kutumia mashine za cherehani, lakini hata hivyo mpango huo bado unalega lega kutokana na upungufu wa fedha na vifaa mbalimbali. Vile vile madrasa hiyo inajishughulisha kwa undani zaidi na utoaji wa Da’awah kwa kutoa mihadhara kwa kina mama ndani na nje ya mji huu hususani vijijini ambapo wanawake wengi wamekuwa nyuma kuhusu elimu ya dini yao na kukosekana madrasa na walimu wa kuwafikishia ujumbe na kuwasomesha. Madrasa hiyo ambayo inapokea wasichana wenye umri wa kuanzia miaka 15, inafundisha masomo mbalimbali kama vile Fiqh, Qur’an, Maarifa ya Uislamu, Hadith pamoja na Lugha. Akitaja matatizo yanayoikabili madrasa hiyo, Mwalimu Mariam Amir Mponda ameyataja kuwa ni pamoja na upungufu wa vitabu, na wanaume wengi kuwawekea vikwazo wake zao hali ambayo inafanya mahudhurio ya baadhi ya wanafunzi kuwa ya kutoridhisha na kulazimika walimu kurudia rudia masomo yaliyokwisha fundisha. Pia Bi. Mariam amewataja watu waliochangia kwa kiasi kikubwa katika kuanzisha na kuendeleza madrasa hiyo ambao amemtaja mama Mwanaidi Muhenga, Sheikh Ayubu Muinge pamoja na Ustadh Suleiman Saddy. "Ninatoa wito kwa kina mama wa Kiislamu kuwa suala la kupigania Uislamu
siyo la kina baba peke yao, bali kina mama nao wana wajibu mkubwa katika
kupigania dini yao kwa hali na mali pamoja na kuipa elimu kipaumbele",
alimalizia Bi. Mariam Mponda.
Na Mussa Salum Miongoni mwa madrasa zilizopata kuwa na kipaji cha kutoa watoto wenye uwezo wa kukariri aya na sura mbalimbali kutoka kwenye kitabu kitukufu chaQur’an na vitabu vingine vya hadithi ni madrasat Hidayat ya Mbagala Kibonde maji Jijini. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mbagala hivi karibuni, mwalimu mkuu msaidizi wa Madrasat hiyo Omari Sultan Mtuliya alisema kuwa Madrasat Hidayat ilianzishwa miaka 13 iliyopita ikiwa na wanafunzi 170 lakini idadi hiyo imekuwa ikishuka kila mwaka kutokana na matatizo kadhaa wa kadhaa ambayo yamekuwa yakiikabili Madrasat hiyo. Aliyataja matazo hayo kuwa ni upungufu wa vitabu vya kufundishia kama vile juzuu, misahafu, ubovu wa madrasa ambayo inavuja wakati wa masika na hivyo kuhathiri usomesaji wa watoto katika shule hiyo. Matatizo mengine darasa kutokuwa na milango wala madirisha hali ambayo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa fedha za kufanyia ukarabati. Mwalimu Mtuliya alisema kuwa matatizo ya fedha ambayo yanaikabili madrasat yake yamesababisha mwaka huu kutofanya maulidi ya kupima vipaji vya wanafunzi wa madrasat yake hali iliyomfanya aombe kwa wafadhili mbalimbali ili waisaidie madrasat hiyo kuendesha maulidi hiyo ambayo ilikuwa inafanyika kila mwaka. Mwalimu huyo alisema kuwa kwa sasa shule yake ina wanafunzi 120 ambapo idadi ya wavulana na wasichana ni sawa na hupokea wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali za mikoa ya Pwani na Dar es Salaam hasa katika wilaya za Mkuranga, Kisarawe, Rufiji na Temeke. Alizitaja mbinu mbalimbali anazotumia kufundishia Mwalimu Omari alisema kuwa anatumia kuwaandikia ubaoni halafu humsimamisha mwanafunzi mmoja mmoja kusoma mara baada ya kumaliza kukariri yale aliyosoma hapo awali. Alisema mbinu hii humfanya mwanafunzi kuyaweka yale aliyofundishwa kichwani
mwake kwa muda mrefu hali iliyokifanya chuo chake kupata sifa kemkem kutoka
kwa wazazi wa wanafunzi wake, shule hiyo hufundishwa na walimu watatu Omari
Sultan Mtuliya, Omari Kassimu Mbembeni na Hassan Lyoto.
|
YALIYOMO
'White Paper ni ulaghai wa Serikali ya CCM' Na Mwandishi wetu Sheikh Omar Bashir awekwa rumande
Mpango wa 'Kupindua' uongozi
wa Bakwata: Masheikh Dar waitwa polisi kuhojiwa
Zahrau Day yatikisa Tanga
MAKALA: Hatuna haja ya maelekezo ya
yule aliyetufikisha hapa
Huduma za afya Kondoa haziridhishi
Tunahitaji 'UN' ya Waislamu!
Hoja binafsi: Wawekezaji watuondokesha makwetu Jamii inapokuwa soko huria...
Someni kwa ajili ya Allah - Sheikh
Baruti
Madrasa Al-Ii'Tiswamu
Al-Umaahaati Fiisabiililillah - Moro
Madrasat Hidayat Mbagala
Hali ya Uislamu Moro
Vijijini yazidi kuwa mbaya
Sheikh Masoud Mwinyi awaonya
Waislamu kuacha migogoro Babati
Tusikaribishe mfungo wa Ramadhani
kwa Vunja Jungu
'Acheni zinaa muepukane
na ukimwi'
Wavunja jungu watahadharishwa
Hoja/Uchambuzi:
Njia ya uzimani ni nyembamba,
waionao ni wachache
Habari:
Kesi ya Waislamu Mwembechai
yaahirishwa kwa mara nyingine
Kongomano la wanawake wa
Kiislamu Bagamoyo
Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|