AN-NUUR 
Na.178 Shaaban  1419, Desemba 4 - 10, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
MAKALA:
Hatuna haja ya maelekezo ya yule aliyetufikisha hapa
 

Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC USA 

PLATO alikuwa mwana-falsafa mkubwa sana. Sifa zake zimeenea, zinajulikana na kukubalika katika pembe zote za dunia. Na falsafa aliyoimwaga na kuiacha duniani, ndio inayosomwa katika vyuo vyote vinavyoendesha masomo ya elimu ya fani ya falsafa. 

Yeye hakuenda shule kama tunavyozijua sisi siku hizi au katika mfumo wa shule tulizonazo au tunazozitambua. Wala hakupata shahada wanazopata wenzetu wanaojiita wasomi. 

Kwa maneno mengine, alijipatia elimu yake kwa mfumo waliopatia elimu wengi wa Ma- Sheikh, Ma-Mufti, Ma-Ulamaa, Ma-Ustaadh,Ma, Aalim wetu wa Kiislamu. Kwa mujibu wa mpangilio wa usomi wa wasomi wetu wa siku hizi, hao wote niliowataja hapo juu, hawakusoma, hawana elimu, nao wote wako nyuma. 

Lakini la kushangaza na la ajabu kubwa ni kwamba, hizo shahada, degrees, masters na Ma-PhD, baadhi yake hazipatikani mpaka waipitie elimu ya falsafa iliyoachwa na akina Plato, ambao kwa mpangilio wetu wa kisiku hizi wao hawakuenda shule na katika hali hiyo basi hawana elimu na bado wako nyuma. (Jamani tumesahau kuwa na wazazi wetu nao waliotusomesha kwanza nyumbani na baada ya kwenda kwetu shule na wanatusomesha mpaka leo hii baada ya kupata shahada zetu, nao hawakwenda shule, lakini walikuwa na elimu ya namna yao iliyowawezesha kutupeleka shule tulikosoma? Nao pia tunawavunjia heshima na kuwaita hawakusoma na kuwa bado wako nyuma. Huo ndio usomi wetu tuliofuzu)? 

Siku moja mtu mmoja alikwenda kwa Plato kumuomba ampe maana ya neno "haki". Naye Plato akamwambia huku akitabasamu, kwanza tuhakikishe kuwa kuna haki kabla kuhangaika kutatufa maana ya "haki". Hicho kitu kinachoitwa haki kipo? Plato akamwambia yule mtu kuwa kwa kuwa hakuna haki duniani, hatutaweza kupata maana ya neno "haki". 

Haki inaweza kupatikana pale tu ambapo wahusika wawili wote wawe na nguvu sawa na katika mazingira sawa. Hivyo hakuna haki hapa duniani ila katika ufalme wake Mwenyezi Mungu (s.w.). Hata wahenga (ambao nao hawakusoma) walituambia "mnyonge kupata haki ni mwenye nguvu kupenda". Ukweli wa maneno hayo haujapata kupingika, haupingiki wala hautapingika. 

Katika hali hiyo basi Waislamu kupata haki katika serikali inayoendeshwa na walio wengi wasiokuwa Waislamu ni muhali. Ni lazima na muhimu tuwe na nguvu za uwiano katika vyama vyote vya kisiasa nchini, itatubidi tuyazingatie sana mafunzo ya maadili ya Kiislamu na kuutekeleza Uislamu wenyewe kwa kuwa pamoja kwa mali na hali, ndipo tutakapofanikiwa kuipata haki ya dunia. 

Haki ya mwenye nguvu kupenda. Ikiwezekana ningependa hapa hapa nizungumzie kidogo kuhusu hili neno "elimu". Neno hili nimegundua linapendwa sana kutumiwa na watu wadhulumuji, wajanja wajanja wafifilishi. Mara ya kwanza nililisikia likitumiwa na wakoloni, nilikuwa ndo kwanza nimeanza kazi katika serikali ya mkoloni nchini mwetu, huo ulikuwa wakati wa mwanzo mwanzo wa kupamba moto harakati za ukombozi wa Tanganyika. 

Wakoloni walisema hatuwezi kupewa uhuru wetu wa kujitawala wenyewe, kwa kuwa hatuna elimu ya kutosha, bado hatujasoma na kuwa bado tuko nyuma sana. Ikawa vigumu sana kupata haki hapo, kwa kuwa wananchi na wakoloni hatukuwa na usawa wa aina yoyote ile. 

Sasa kwa bahati mbaya na kwa mshangao mkubwa, nalisikia hili neno "elimu" likitumika, tena safari hii na wananchi wenzetu wasiokuwa Waislamu katika ujanja ujanja ule ule wa kutudhulumu haki zetu sisi wananchi wenzao wa Kiislamu. 

Hivi hili neno "elimu" hasa maana yake nini? Kwa kuwa mimi sio msomi nashindwa kuliezea maana yake kitaalamu. Hivyo nitalitolea mfano ili sote tupate kulielewa neno hili. 

Tujifikirie tumefungwa pangoni, sisi sote nchi nzima. Tumefungiwa mlango wa pango lakini pale mlangoni kwa bahati njema pamebakia kitundu kidogo sana kiasi cha kuweka jicho moja tu, kuchungulia nje. Katika wingi wetu mle pangoni, mmoja wetu kapata bahati ya kuwa katika usawa ule wa kitundu, akaweza kuweka jicho lake yeye tu pa kitunduni, akawa anaweza kuona kule nje yeye peke yake kati yetu. 

Bahati ile imemwangukia tu. Siyo kwa kuwa yeye ni hodari zaidi au ana akili au maarifa zaidi yetu sisi sote, la hasha. Tumpe jina la Julius. Akituambia yaliyomo na yasiokuwemo sisi hatuna budi kuyakubali na kuyasadiki. Akituambia ya kweli yasiyokuwa kweli sisi hatuna budi kuyaamini. Akiyapotosha au kuyanyoosha sisi kwetu ndio hayo hayo hata kama anayafanya kwa kukusudia au kwa kutokujua. Ili muradi tumo pangoni tunasimuliana ya nje kwa kufuatana na maelezo ya Julius mwenzetu. 

Kwangu mimi ule upenyo au kitundu au dirisha ndio "elimu" na Julius ndio msomi, sio kwa uhodari wake ila kwa bahati yake ya kuwa na usawa na kitundu kile na kuweza kuona kule nje. Kwangu huo si usomi unaoweza kutosheleza kukupa nafasi ya kujigamba na kudharau wenzako. Kwanza ile hali ya kufanya hayo tu inatosha kutufahamisha wenzio kuwa bado hujapata elimu ya kutosha. Asinyimwe mtu haki yake kwa umri wake, elimu yake, rangi yake, umbile lake au dini yake au alikotokea. Lile jiwe la mlangoni hivi sasa halipo tena. Sote tumetoka pangoni na nje tunakuona. Hatuna haja ya maelezo au maelekezo ya mtu. 

Tukiangalia tunaona baadhi ya vitu mwenzetu alivyokuwa akitueleza tulipokuwa pangoni siyo sahihi au havikubaliani na wakati tulionao hivi sasa. Tukimkabili kwa hoja au tukimsaili kwa masuala mwenzetu anatujia juu kama moto wa kifuu au pengine anatunyamazia kimya, kama Rais Mkapa alivyokaa kimya kuhusu masuala ya kadhia ya Msikiti wa Mwembechai na mengineyo. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
'White Paper  ni ulaghai wa  Serikali ya CCM' 
Na Mwandishi wetu 

Sheikh Omar Bashir awekwa rumande 
Na Mwandishi Wetu 

Mpango wa 'Kupindua' uongozi wa  Bakwata: Masheikh Dar waitwa polisi kuhojiwa 
Na Mwandishi Wetu 

Zahrau Day yatikisa Tanga 
Na Mwandishi Wetu 

MAKALA: Hatuna haja ya maelekezo ya yule aliyetufikisha hapa  
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC USA 

Huduma za afya Kondoa haziridhishi 
Na Abu Zubeir 

Wasemavyo wanaharakati 

Tunahitaji 'UN' ya Waislamu! 
Na Twahir Rashid 

Hoja binafsi: Wawekezaji watuondokesha makwetu 

Jamii inapokuwa soko huria...  
Na Said Rajab 

Someni kwa ajili ya Allah - Sheikh Baruti  
Na Muhibu Said 

Madrasa Al-Ii'Tiswamu Al-Umaahaati Fiisabiililillah - Moro 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Madrasat Hidayat Mbagala 
Na Mussa Salum  

Hali ya Uislamu Moro Vijijini yazidi kuwa mbaya  
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Sheikh Masoud Mwinyi awaonya Waislamu kuacha migogoro Babati  
Na Abu Zuberi - Babati 

Tusikaribishe mfungo wa Ramadhani kwa Vunja Jungu  
Na Abeid Poyo 

'Acheni zinaa muepukane na ukimwi'  
Na Mussa Salum 

Wavunja jungu watahadharishwa 
Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

Hoja/Uchambuzi: 
Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? 
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu 

Njia ya uzimani ni nyembamba,  waionao ni wachache 
Na Yasin Valerian Massawe 

Habari: 
Semina ya Maimamu Tanga yadai: Maimamu wanapuuzwa  
Na Mwandishi Wetu 

Kesi ya Waislamu Mwembechai yaahirishwa kwa mara nyingine  
Na Muhibu Saidi 

Kongomano la wanawake wa Kiislamu Bagamoyo 
Na Mwandishi Wetu 

Sayansi na Teknolojia 
[Kuongeza RAM kwenye Kompyuta] 
 
Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Madini ya Zinc] 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita