AN-NUUR 
Na.171 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 16 - 22, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Mafundisho ya Quran: 
 

Kutoa pasipo masimango 

  
AYA YA 265 - Al-Baqara 

Na mfano wa wale wanaotoa mali zao kwa kutafuta radhi za Allah na kujithibitisha nafsi zao; ni kama mfano wa bustani iliyo mahala pa juu ikiifikia mvua kubwa na ikaleta mazao yake mara mbili na zaidi na kama haifikiwi na mvua kubwa basi mvua ndogo (huitosheleza). Na Allah anayaona mnayoyatenda. 

Kama ilivyo desturi ya mwalimu mzuri - mbali na maelezo ya kinadharia; hutoa mifano kadhaa ili kuona somo lake linafahamika vizuri kwa wanafunzi wake - Allah katika aya hii na ile iliyopita na inayofuatia anasomesha kwa njia ya mifano. Mfano uliopita ulikuwa ni kwa wale ambao sadaka zao haziwanufaishi kwa sababu ya masimbulizi na maudhi. Mfano wa sasa ni wa yule anayetoa sadaka au mali yake kwenye njia ya Allah. Kwa ujumla pasipo na kufuatanisha na masimbulizi wala chochote. 

Kulingana na aya hii mali inayotolewa pasipo na masimango na kwa nia safi inalinganishwa kifaida na bustani ambayo imepata mvua nyingi yenye baraka. Mvua za baraka kikawaida huleta neema kubwa ya mazao ambayo ndilo lengo la ukulima. Bustani yenye rutuba inapopata mvua kubwa na yenye kuendelea si kwa mangamizi basi mavuno yake hufurahiwa na kila mtu. Hata iwapo mvua itakuwa ni ndogo lakini ilivyokuwa bustani tayari ni yenye rutuba bado mavuno ya kawaida yatapatikana. Na hii ni sawa ni ile sadaka au utoaji wenye dosari ndogo ndogo za kibinadamu. 

AYA YA 266 

Je! Mmoja wenu anapenda kuwa na bustani ya mitende na mizabibu ipitayo mito mbele yake, naye humo hupata mazao ya kila namna, na uzee ukamfikia kisha ana watoto walio dhaifu; mara kimbunga chenye moto kikaifikia ikaungua? Hivi ndivyo Allah anavyokubainishieni aya zake ili mpate kufikiri. 

Huu ni mfano mwingine na masuala ya utoaji. Lakini sasa unaelekea kwenye matarajio ya mtu baada ya kazi aifanyayo. Kikawaida mtu anapofanya kazi siku zote hutaraji matunda ya kazi na anapokosa matunda hayo huwa amekula hasara na njia aliyobaki nayo ni kuanza upya iwapo angali ana wasaa na uwezo wa kuanza tena. Pasipokuwepo na uwezo maana yake ni huyu mtu amekuwa muflisi (aliyefilisika) wa moja kwa moja. 

Mtu anapoishi kwa kazi ya kutegemea kilimo tokea ujana wake hadi uzee wake ndiye anayezungumzwa ndani ya mfano huo. Kilimo hicho (cha bustani au shamba la mizabibu na mitende) ndicho pekee ambacho mtu huyu anakitegemea hali ya kuwa nguvu zake za kuweza kufanya kazi zaidi zimekwisha. Akiwa mtu mzima sana Allah anamjaalia kizazi ambacho si muda mrefu yeye mwenyewe anafariki hali ya kuwa hapana mwega mwingine si kwake yeye binafsi wala watoto wake. 

Urithi pekee anaouacha mzee huyu kwa watoto wake ni ile bustani yake ya mizabibu na mitende. Watoto wangali wachanga wa kiakili na (kiwiliwili chao bado hakija komaa) hufanya chochote chenye uwezo wa kuliendesha shamba hilo. Baya zaidi shamba (bustani) hiyo katika hali hiyo nayo inaunguzwa na moto!! Hasara ya hapa iko pande zote mbili kwa watoto na mzee. Watoto hawana msaada wa baba yao ambaye pamoja na uzee wake tayari amefariki. Aidha watoto hao pamoja na udogo wao; shamba nalo ambalo lingekuwa matarajio yao hapo baadae (iwapo wataishi) nalo limepotea. 

Kwa upande wa mzee, laiti angekuwa anategemea shamba lake limsaidie huko aendako basi asingefanikiwa kwani shamba hilo halipo tena. Msaada wa watoto hao haupo kwani ni wadogo hivyo iwapo hakuna chengine cha kumsaidia zaidi ya hivyo basi amekula hasara. Kwa lugha nyingine kutoa kwa nia nzuri na kwa mujibu wa sheria ni matarajio mazuri kama tulivyoona juu. Kwa upande mwingine sadaka isiyozingatia hayo haina tofauti na mtu anayetegemea kitu kibovu kama huyu mzee katika mfano huo. 
 
Juu 
 

YALIYOMO 
 
 

 TAHARIRI 
Serikali iwahurumie wananchi wake 

KUCHOMWA MOTO NYUMBA ZA WANANCHI: Nzasa wamtaka Mkapa awaonyeshe pa kwenda 
Na Mwandishi Wetu, Nzasa 

Mishikaki ya nguruwe Moshi yachomwa mbele ya Msikiti 
Na Mwandishi Wetu 

MAONI YETU: 
Je; ni halali kuchoma Kidungu cha mtu? 

Upimaji huu mpya ni wa nini 
Na Mwandishi Wetu 

TANGAZO LA HIFADHI YA MSITU WA KAZIMZUMBWI 

Ndoa si lengo, ni wasila wa kufikia lengo 
Na Bi. Zuhura Tajiri, Shinyanga 
 
Teknologia:
Jifunze kuunganisha Kompyuta
Na Hassan Omar

Makala:
Nani atakayewahoji Waheshimiwa hawa

Goda Muslim School, Manzese
Na Mwandishi Wetu

Utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa

Historia ya mgogoro wa Nzasa
Na Mwandishi Wetu

DUMT watoa msaada kwa walioathirika Nzasa
Na Mwandishi Wetu

UCHOMAJI NYUMBA NZASA: Wafadhili wana mchango gani?
Na Mwandishi Wetu

Mafundisho ya Quran 
Kutoa pasipo masimango 

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita