|
|
| BARUA:
Tuwe na elimu ya
maisha ya ndoa kabla ndoa
Ndugu Mhariri KWA hakika elimu imepewa umuhimu wa kwanza kuliko kitu chochote kile, ndio maana jambo la kwanza kufaradhishwa Mtume wetu Muhammad (saw) na Waislamu wote ni kusoma. Turejee Qur’an sura ya 96 aya 1-5, kwani bila ya elimu hatuwezi kufanya chochote kile kwa sababu tutafanya hali ya kuwa hatujui tunafanya nini. Kufuatia kipindi cha Sema Kweli (DTV) CHA Alhamisi ya Oktoba 8, 1998 kilizungumzia mas-ala ya ndoa na kuvunjika kwa ndoa. Mama mmoja miongoni mwa akina mama wa Kiislamu alizungumzia baadhi ya mambo ambayo yalikuwa ni shutuma dhidi ya mafungishao ndoa wa Kiislamu (Masheikh) kwamba hawamfundishi muolewaji namna ya kuishi na mumewe katika ndoa kama wafundishavyo kwenye unyago. Na kuwaita kuwa ni Masheikh ubwabwa na hawaelimishi mabinti waolewao. Ninafikiri kwamba kazi ya yule Sheikh kwa kipindi hicho si kufundisha namna ya kuishi na mume, bali kazi yake ni kufungisha ndoa kwani hata ukifundishwa kwa wakati ule si rahisi kuyaelewa majukumu yako yote kwa mumeo. Cha kukumbushana ni kwamba tunatakiwa tukasome kabla, kwani kuna madrasa nyingi zifundishazo na Al-Hamdulillah vitabu mbalimbali vinatolewa vihusuvyo maisha ya ndoa ya Kiislamu tena kwa Kiswahili na kuhusu mas-ala ya unyago katika Uislamu hakuna kabisa mambo hayo. Enyi kina mama na mabinti wa Kiislamu kwa nini tusisome mapema na tusubiri kufundishwa siku ya ndoa ? Hebu tuipe elimu daraja lake la kwanza na ndiyo tutafanikiwa katika mambo yetu bila shaka. Na tutakaposimama kutoa fatwa mbalimbali tujitahidi kutoa yale ambayo tuna ushahidi nayo na kujiepusha na kuudhalilsha Uislamu mbele ya Makafir tusije tukaangamia.
Katiba isiwe ‘Kakakuona’ Ndugu Mhariri MIONGONI mwa mambo adimu kuonekana kwa wananchi wa kawaida mfano wa mnyama aitwaye kakakuona ni katiba ya nchi. Na hii inatufanya tuwe hoi tunapotakiwa sasa tutoe maoni na mapendekezo yetu kwa katiba ambayo hatujaiona, hatujaisoma na hatuielewi. Kutokana na haya, mjadala huu wa marekebisho ya katiba utafanya uwe wa bendera kufuata upepo. Na hatari kubwa kuliko zote ni hapo walio wengi wanapoonekana wamepitisha ama kupendekeza jambo likafanywe sheria huku hawalielewi vizuri. Madhara yanarudi kwao wakati jambo hilo tayari limefanywa sheria na linaanza kufanya kazi. Linaanza kuwauma na kuwaumiza na ndiyo chanzo cha matata. Ombi langu kwamba, elimu ya kuifahamu katiba iongezwe ili watu walio wengi watoe maoni na mapendekezo yao kwa jambo wanalolifahamu kwa kinagaubaga. Tena katiba ya nchi isiwe siri ama kitu cha wachache. Mwinjilisti E.B. Dettu,
Dini ni nyingi, lakini ya haki ni Uislamu Ndugu Mhariri HAPA duniani, zipo dini nyingi. Na jinsi dunia inavyokwenda mbele, dini nazo zitaongezeka. Hivi sasa binaadamu alie na akili timamu ni lazima ajiulize swali hili ambalo lina maana na manufaa makubwa katika maisha yake ya kila siku na maisha yake baada ya kifo chake. Je, dini ya haki hapa duniani na huko akhera ni ipi? Uislamu ndio dini ya haki hapa duniani na huko akhera, na kwa ujumla mbele ya Mewnyezi Mungu. Dini nyingine kwa mfano Ukristo, ubepari, Ukomunisti, Ujamaa, Upagani na sasa demokrasia si dini za haki hapa duniani na huko akhera. Maadui wa dini, kwa njia mbalimbali wameeneza fikra potofu kwa jamii mbalimbali kuhusu dini. Watu walio wengi wana fikra za kudumu kuwa dini na mambo ya Misikitini na Makanisani tu na nje ya nyumbaa hizo mbili hakuna dini. Na pia dini ni jambo la binafsi la mtu. Watu wa namna hii wako mbali na ukweli aliyoudhihirisha Mwenyezi Mungu. Dini ya Mwenyezi Mungu inadhihirisha ukweli wa maumbile ya dunia hii tunayoiona na hiyo tusiyoiona. Dini ni nyingi hapa duniani, lakini misingi yake na mafundisho yake hayajafafanua ukweli wa maumbile tunayoyaona. Hii inatupelekea kumuunga mkono Muumba kuwa dini ya kweli ni Uislamu. Kwa kuthibitisha kauli hii rejea kusoma surat Al-Imran aya ya 19. Hakuna mtu anaweza kuvunja hoja yangu hii. Uislamu ni sawa na maumbile tuanyoyaona. Mwenyezi Mungu amekwsha tufahamisha na kutangaza nafasi yetu katika dunia. Binaadamu ndio mwakilishi wa Mwenyezi Mungu hapa duniani. Tangazo hili halipatikani katika dini alizoasisi mwanadamu. Mwakilishi hawezi kufanya anavyotaka na kuacha amri ya Muumba wake. Anatakiwa kila siku kuwa mtufu na mnyenyekevu kwake. Leo binadamu amepoteza uhalali wake wa kushika nafasi hiyo. Yuko hasarani duniani na akhera kwa sababu hana imani sahihi, hatendi mema kwa binaadamu wenzake na hawala hapingi dhulma wanayofanyiwa binaadamu. Ili kuepuka hasara hii Mwenyezi Mungu anatuamrisha kusoma. Matokeo haya yamo katika surat ya 96, ambayo ni sura ya kwanza kufunuliwa kwa Mtume wetu (saw). Aya tano za sura hii zinazungumza hivi: Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba mwanaadamu kwa pande la damu. Soma, na Mola wako ni mkarimu sana. Ambaye amemfundisha (binadamu ilimu zote hizi) kwa wasita wa kalamu. Amemfundisha mwanaadamu mambo aliyokuwa hayajui. Pia kuhusu elimu, Mtume (saw) alisema: Kutafuta elimu ni faradhi kwa kila Muslamu mume na mke.Tafuteni elimu japo Uchina. Mwenye kupita njia kutafuta ilimu Mwenyezi Mungu humsahalishia njia ya peponi. Kwa ujumla, Uislamu unatufundisha kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kujua, mwenye elimu zote, tunazozijua na tusizozijua. Historia inashuhudia jinsi Waislamu wa hapo awali walivyopata mafanikio mbalimbali katika nyanja ya elimu kutokana na kuyafanyia kazi maelekezo haya. Waislamu wataalamu wa awali hawakufanya wala kueneza uharibifu katika ardi inayokaliwa na bianadamu. Hwakuunda silaha kali kali kuangamiza binaadamu na mazingira yao. Hali hii ni tofauti sanana hali tuliyonayo wakati wetu huu. Wataalamu wa sasa, usiku na mchana wanatengeneza silaha kumuharibu binaadamu na mazingira yake. Ebu rejea Japan ilivyoangamizwa katika vita vikuu vya dunia vya pili. Ebu rejea Vitnam. Ebu rejea Bosnia, Kossovo na kadhalika. Mizani ya Mwenyezi Mungu haiyakubali matokeo haya mabaya ya dunia hii. Sababu Mwenyezi Mungu anapenda ssana uadilifu na yeye mwenyewe ana sifa hiyo, Aliye mwandifu agenda yake ni kusimamisha mema na kukataza mabaya. Mtume Muhammad (saw) ni mwalimu wetu mkuu ya agenda hii ya mema na mabaya. Tunapoona baya katika jamii zetu na duni yetu tunalazimika kuchukua hatua zifuatazo: Kuzuia kwa mkono wetu, tutumie nguvu za dola au nguvu ulizonazo katika madaraka yako ya kibinafsi kuhakikisha kuwa mabaya hayastawi au yanakufa. Kusema dhidi yake. Unao uchaguzi wa kusema au kuandika dhidi ya baya au mabaya yanayojitokeza. Kuchukia mabaya: Lakini hii ni imani dhaifu. Hii ni hatua ya mwisho baada ya hizo za awali kushindikana. Dini ya Kiislamu ndiyo dini ya maumbile ya mwanaadamu; na din inayokwenda na wakati. Binaadamu yuko hasarani kama akiiacha dini hii. Na anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi hatakubalika kwake. Naye akhera atakuwa katika hasara (kubwa kabisa). (Al-Imran 3:85). Abubakar Suleyman Marwilo,
Mkoa wa Shinyanga upatiwe shule ya sekondari ya Kiislamu Ndugu Mhariri NAOMBA nisema machache kuhusiana na maswala ya kielimu katika mkoa wa Shinyanga. Mkoa wa Shinyanga ni moja kati ya mikoa yenye wanafunzi wengi wa Kiislamu. Wanafunzi hao wa Kiislamu ambao wapo katika shule zilizopo Shinyanga mjini na kati ya hao baadhi yao wapo katika shule za serikali na wengine wapo katika shule za Private. Kwa hiyo, tatizo kubwa linalowakumba wanafunzi hao ni kukosa kufundishwa somo la elimu ya Kiislamu ipasavyo (Islamic knowledge). Shinyanga mjini kuna shule nne (4) za sekondari nazo ni Uhuru, Buluba, Shycom na Buhungija. Shycom ina wanafunzi wa kidato cha tano na sita, wanafunzi hawa hawana tatizo kubwa la somo hili kwa sababu wanafundishwa na Ustaadh Muhammed Issa. Kuna wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule za Uhuru, Buluba na Buhangija, mwalimu aliyejitolea kufundisha somo hili ni mmoja, Ustaadh Jihad, lakini kufuatana na muda hautoshelezi kwa sababu ni kipindi kimoja kwa wiki ambacho kina dakika 80. Kulingana na hali hiyo baadhi ya wanafunzi ambao wenye moyo wa kufanya mtihani wa dini wanakatishwa tamaa ukizingatia pia na vitabu vya kusoma kwa ajili ya kujiandaa pia inakuwa ni tatizo. Kwa hiyo, sisi wanafunzi wa Kiislamu tunaomba Waislamu mkoani Shinyanga tuangalie umuhimu wa elimu kwa ujumla hasa hii Islamic knowledge wajitahidi kuangalia upatikanaji wa shule hata ya sekondari ya Kiislamu katika mkoa wa Shinyanga hii itasaidia kuinua kiwango cha elimu kwa vijana wa Kiislamu. Mwanafunzi, TAMSA –Shinyanga,
Ndugu Mhariri TUNAOMBA kujitokeza katika gazeti lako tukufu la AN-NUUR tutoe dukuduku letu tunalotendewa katika kampuni hii ya ulinzi ya Ultimate Security Ltd, ya Jijini haswa katika malipo ya mishahara, huduma, nauli na kodi ya nyumba. Kwanza kabisa tunapenda kuelezea hali yenyewe ya mshahara tunayolipwa kiasi cha shilingi 17,500 ambao mshahara huu uliongezwa tkea mwaka 1995 hadi leo tunalipwa mshahara huo huo. Kila tukiilalamikia kampuni hii tunaambiwa bado serikali haijatulea barua ya nyongeza ya mshahara. Sisi kama wafanyakazi wa kampuni hii, tunafahamu kuwa serikali imeongeza mshahara kutoka shilingi 17,000 hadi shilingi 30,000 na leo hii serikali imepandisha mshahara kutoka 30,000 hadi 35,000 kwa mwezi. Lakini sisi kama wafanyakazi wa kampuni hii ya ulinzi bado tunalipwa mshahara ule wa shilingi 17,500 ambao ulikuwa mshahara wa mwaka 1995. Pili: Nauli, kodi ya nyumba na chakula tunalipwa shilingi 6,500 kwa mwezi, yaani kwa kugawa kiasi hicho ni kama ifuatavyo; chakula shilingi 2,250, nauli 2.250, kodi ya nyumba 2,000 zote hizo wanafungasha katika malipo ya mwezi kwa mahesabu ya jumla ni shilingi 6,500. Halafu bado malipo mengine ambayo bado hatutendewi haki sawa, kama Vice huduma na usafiri. Hasa kama wale watokao mikoani ukilinganisha na hali yetu tuliyokuwa nayo sisi wafanyakazi wa kampuni hii, na mshahara huu tunateseka na familia zetu. Ama kampuni imejitungia tu malipo ya kodi, nauli na chakula? Au wao wanachofahamu kuwa malipo ya Over time, Bonus na nauli pamoja na hivyo vipengele vingine. Basi tueleweshwe tujue. Kadhalika, tunaomba serikali pia imulike kampuni ya ulinzi inavyotufanya sisi kama farasi wanaoendeshwa bila kujali kuwa sisi ni binaadamu kama wao viongozi wa kampuni hii. Ukizingatia ugumu wa kazi yenyewe na pia tunaomba kiongozi wetu wa kampuni hii ya ulinzi asiyejali maslahi yetu ajiuzulu kwa manufaa ya kampuni. Pia tukiangalia huduma ya hospitali nazo ni dhaifu. Daktari aliyekuwepo hakuna anachokifanya, anakuja anavyotaka yeye. Hata kama kuna mgonjwa mahututi mpaka akaitwe, je, ama mgonjwa atakuwa amezidiwa si atakufa? Kwa ujumla kampuni hii ya ulinzi inatuendesha wanavyotaka, yaani hawajali wafanyakazi wao wala nini. Hayo na mengine mengi. Wakereketwa,
Popatlal hijab ziko wapi na Waislamu wako wapi? Ndugu Mhariri NAPENDA kujitokeza kwa mara kwanza katika gazeti lako tukufu la AN-NUUR. Naomba unipe nafasi katika gazeti lako nitoe dukuduku langu kwa wanafunzi wa Popatlal. Hijab ni miongoni mwa sheria muhimu kabisa katika dini yetu ya Kiislamu na ni vazi linalompa heshima na utu wake. Pia linampa hadhi anayostahiki mwanamke. Kwa muda mrefu sana mkereketwa sana na vitendo vyao vya kunipa sifa mbaya, ambavyo ya kudharaulika kwa shule hii. Na wanafunzi wengi vitendo vyao ya kuvaa hijab na kuziweka mabegani na wengine kuzitia katika mifuko na mambo mengi yaliyo nje na maadili ya Uislamu. Nia yenu ni nini enyi wanafunzi wa Popatlal ? Je, ni kufedhehesha Uislamu au nini? Kwani hamna maana yoyote ya kuvaa hizo hijab kama manavyozivaa. Na matokeo yake mnawaharibia hata wanafunzi ambao hujihifadhi vizuri kwa ajili ya Allah (sw). Jambo jingine la kuwasisitiza ni kwamba wale Waislamu ambao hawavai hijab isipokuwa kipindi cha dini tu ndio wanavaa. Ni bora kama hawavai siku zote na hivyo siku moja ya kipindi cha dini pia usivae. Kwani haujui kama mnaudhalilisha Uislamu? Kipindi cha dini ambayo ni mara moja kwa wiki. Unapowaambia jamani Waislamu wenzangu twendeni kwenye dini wanaanza majibu ambayo hayaridhishi. Na wengine huenda katika dini ambazo si zao. Na mimi nitachoka kuwahimiza kuvaa hijab na kwenda katika dini. Kwani ni aibu Waislamu wengi katika shule hii. La kushangaza ukienda kwenye dini unawakuta Waislamu ni wachache sana. Na jambo la mwisho ni kwamba tusiache kuvaa hijab na kuingia katika dini yetu ya Kiislamu. Isipokuwa naomba Waislamu wenzangu tusiache kuhimizana juu ya mambo hayo. Mwanafunzi,
Nguruwe katika basi la Metro Ndugu Mhariri GAZETI la AN-NUUR Septemba 11, 1998 nilisoma barua kuhusu nguruwe aliyebebwa katika basi la METRO lisafirilo kati ya Dar es Salaam na Marui (Kisarawe). Napenda kuthibitisha barua hiyo. Ni kweli nguruwe huyo aliuziwa dereva wa basi hilo Eveline na muuzaji anajulikana. Ila Bw. Hamisi Mdugi hahusiki kama alivyotajwa. Naomba Waislamu wasimuelewe vibaya. Selemani Abdallah Kirumbi,
|
YALIYOMO
TAHARIRI
KUCHOMWA MOTO NYUMBA ZA WANANCHI:
Nzasa wamtaka Mkapa awaonyeshe pa kwenda
Mishikaki ya nguruwe Moshi yachomwa
mbele ya Msikiti
MAONI YETU:
Upimaji huu mpya ni wa nini
TANGAZO LA HIFADHI YA MSITU WA KAZIMZUMBWI Ndoa si lengo, ni wasila wa kufikia
lengo
Makala:
Goda Muslim School, Manzese
Utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu
Historia ya mgogoro wa Nzasa
DUMT watoa msaada kwa walioathirika
Nzasa
UCHOMAJI NYUMBA NZASA: Wafadhili
wana mchango gani?
Mafundisho ya Quran
|