AN-NUUR 
Na.171 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 16 - 22, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
DUMT watoa msaada kwa walioathirika Nzasa 

Na Mwandishi Wetu 

JUMUIYA ya Waalimu na Wafanyakazi Waislamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUMT) wametoa msaada wa vyakula kwa wananchi waliochomewa nyumba zao na Serikali katika kijiji cha Nzasa Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam. 

Misaada iliyotolewa na Jumuiya hiyo mapema wiki hii ni pamoja na viroba sita (kilo 300) vya mchele, maharage kilo 70 na unga kwa sembe viroba vitatu (kilo 210). 

Mbali ya misaada ya Jumuiya hiyo, wananchi kadhaa Jijini wamewasilisha kijijini Nzasa michango ya mitumba ya nguo mbali mbali kwa waathirika. 

Kwa muda wa wiki mbili sasa Serikali imekuwa ikiendelea na operesheni ya uchomaji wa nyumba za wananchi wa Nzasa ikidai kwamba wananchi hao wamevamia msitu wa Kazimzumbwi ambao ni Hifadhi ya Taifa. 

Habari zaidi zimeeleza kwamba maombi ya kupata misaada zaidi yamewasilishwa na waathirika katika Kanisa la Chanika na Askofu muhusika ameahidi msaada. 


Uchomaji nyumba Nzasa: 
  

Wafadhili wana mchango gani? 
  
Na Mwandishi Wetu 

WANANCHI wa Nzasa wanaeleza kwamba wamekuwa wakiishi katika eneo hilo kabla hata Misitu ya Kazimzumbwe kutangazwa kwamba ni hifadhi ya Taifa. 

Bibi Halima Mwinyimvua anayekisiwa kuwa na miaka 90 huku akionyesha eneo la makaburi anasema baba yake mzazi Marehemu Mwinyimvua Ngunduli kaishi na kuzikwa hapo hapo Nzasa.  

Toka Mkoloni mpaka operesheni Vijiji vya Ujamaa hawakuwahi kuambiwa kwamba wanaishi ndani ya msitu.  

Anasema Serikali ya Mkoloni na ile ya Mwalimu Nyerere isingewaacha waendelee kukaa kama kweli walikuwa wamevamia msitu. Ni kwa ajili hiyo kwamba hiyo ndiyo asili yao na hawana pengine pakwenda; Bibi Halima Mwinyimvua anasema japo kachomewa nyumba na kupigwa marufuku kukanyaga shambani kwake, lakini anasema atakaa hapo hapo ama Mhe. Rais Mkapa aje amuonyeshe pa kwenda au afe. 

Nyaraka ambazo AN-NUUR imefanikiwa kuzikusanya pamoja na maongezi iliyofanya na wanakijiji, zinaonyesha kwamba mgogoro huu ulianza mapema mwanzoni mwa miaka hii ya tasini. 

Wananchi wa Nzasa wanadai kwamba aliyekuwa mstari wa mbele katika kutaka kuwahamisha ni Afisa Misitu Wilaya ya Kisarawe aliyejulikana kwa jina la Beda Kessy. Wananchi hao wameendelea kudai kwamba ni katika kipindi hicho Wazungu wawili mke na mume waliwajia na kutaka eneo la kupanda miti. Wazungu hao waliwatambua kwamba ni kutoka Sweden. Aidha walimtambua mmoja kwa jina la Anna. 

Akiongea na mwandishi wa habari hizi Jumanne Oktoba 13, Bw. Mohamed Mtimkavu alisema kwamba yeye binafsi aliendewa na huyo Mzungu Anna, akiwa na mzungu mwingine ambaye hakukumbuka jina lake na kuwaeleza kwamba wanataka eneo la kupanda miti.  

Bw. Mtimkavu anasema kwamba aliwaambia kama wanataka kupanda miti waende msituni Kazimzumbwe ilipo Hifadhi ya Taifa. Hata hivyo anadai kwamba Wazungu hao walisisitiza kwamba wanataka eneo hilo waanze upandaji wao mpya. Bw. huyo amedai Wazungu hao walitaka waelewane na wachuke mashamba ya watu wengine lakini wamwachie la kwake. Mtimkavu anadai kwamba aliwaambia kwamba hilo halitowezekana ila wakitaka waiombe Serikali iwapimie eneo lingine nje ya makazi na mashamba ya wananchi. 

Bw. Mohamed Mtimkavu anadai kwamba Wazungu hao walimwambia kwamba atakufa masikini na wakaondoka na gari yao wakamwacha porini walikokuwa wanafanyia mazungumzo. 

Aidha, aliendelea kumweleza Mwandishi wa Habari hizi kwamba kwa muda mrefu mzungu huyo alikuwa ameondoka lakini sasa hivi amerudi na anakaa nyumbani kwa Afisa Misitu, Bw. Secha. Alidai kwamba toka arudi Mzungu huyo walinzi wa misitu wamekuwa wakiwanyanyasa na kuwaambia kwamba malalamiko yao hayatasaidia kitu kwani hawana pesa kama Anna. 

Ili kuzithibisha habari hizi Mwandishi siku hiyo hiyo alienda Kisarawe kwa lengo la kumwona Bw. Secha hata hivyo akaambiwa yupo Nzasa kwenye operesheni. mwandishi aliporudi Nzasa kutaka kuonana na Bw. Secha, askari walinzi wa msitu wakamzuia kuonana naye kwa madai kwamba yupo porini kwenye operesheni ya upimaji na shida yoyote imsubiri ofisini. 

Jumatano Oktoba 14; Mwandishi wa Habari hizi aliwasiliana na Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Saidi Iddi kuhusiana na suala hili la wafadhili. Lakini Profesa Idd alisisitiza kwamba yeye asingeweza kuzungumza lolote kwani Msemaji ni Waziri au Mkuu wa Mkoa wa Pwani.  

Hata hivyo, baadhi ya watumishi wa Idara ya Misitu walisema kwamba wafadhili kama hao wanaosaidia miradi ya Misitu wapo na wala sio jambo geni kwa Nzasa.  

Siku hiyo hiyo AN-NUUR iliwasiliana tena na ofisi ya Maliasili Kisarawe kutaka kujua habari za Anna, Mswideni ambayeamekuwa akitajwa sana huko Nzasa na kila aliyechomewa nyumba yake. 

Nyumbani kwa Bw. Secha AN-NUUR ilifahamishwa kwamba Anna pamoja na mzungu mwingine wanaishi hapo ila waliondoka jana yake kwenda mjini (Jumanne) na hawakuweza kurudi. 

Katika Ofisi ya Maliasili, AN-NUUR ilifahamishwa kwamba Anna na mwenzake mmoja wamekwenda Morogoro kufuata mbegu za miti na haikujulikana kwamba wangerudi lini.  

Katika mazungumzo baadhi ya wafanyakazi wa ofisi hiyo; AN-NUUR ilifahamishwa kwamba wazungu hao hufadhili miradi ya misitu ya Pugu, Kazimzumbwe na Vikindu.  

Aidha AN-NUUR ilifahamishwa kwamba Wazungu hao hulipa mishahara ya walinzi wa misitu na kugharamia utunzaji wa mipaka ya misitu ikiwa ni pamoja na kuifyeka mara kwa mara. 

Baadhi ya taarifa kutoka Ofisi ya Maliasili Kisarawe zimeeleza kwamba Wazungu hao wanafanya kazi chini ya Shirika liitwalo "Swedish Society for Nature Conservation (SSNC) ambalo ni mfadhili wa chama cha Hifadhi ya Maliasili na Mazingira Tanzania (WCST). 

  
Juu 
 

YALIYOMO 
 
 

TAHARIRI 
Serikali iwahurumie wananchi wake 

KUCHOMWA MOTO NYUMBA ZA WANANCHI: Nzasa wamtaka Mkapa awaonyeshe pa kwenda 
Na Mwandishi Wetu, Nzasa 

Mishikaki ya nguruwe Moshi yachomwa mbele ya Msikiti 
Na Mwandishi Wetu 

MAONI YETU: 
Je; ni halali kuchoma Kidungu cha mtu? 

Upimaji huu mpya ni wa nini 
Na Mwandishi Wetu 

TANGAZO LA HIFADHI YA MSITU WA KAZIMZUMBWI 

Ndoa si lengo, ni wasila wa kufikia lengo 
Na Bi. Zuhura Tajiri, Shinyanga 
 
Teknologia:
Jifunze kuunganisha Kompyuta
Na Hassan Omar

Makala:
Nani atakayewahoji Waheshimiwa hawa

Goda Muslim School, Manzese
Na Mwandishi Wetu

Utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa

Historia ya mgogoro wa Nzasa
Na Mwandishi Wetu

DUMT watoa msaada kwa walioathirika Nzasa
Na Mwandishi Wetu

UCHOMAJI NYUMBA NZASA: Wafadhili wana mchango gani?
Na Mwandishi Wetu

Mafundisho ya Quran 
Kutoa pasipo masimango 

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita