AN-NUUR 
Na.171 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 16 - 22, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu 

  
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa, 
P.O. Box 96, 
Korogwe. 
  

NIMESOMA vitabu vingi vilivyoandikwa na Wanatheologia vikijaribu kuonyesha utabiri (unabii) wa kuibuka "dini" ya Kiislamu ndani ya Biblia. Vyote vimeegemea (vine-base) katika tafsiri potofu ya kitabu cha Wasabato "Ufunuo wa Yohana" kikifasiri Ufunuo 9:1-11. Kitabu hicho kuwa mnyama namba 666 ni Papa kinasema "U=V kwa hiyo ni 5". Japo mimi nimeweza kusoma na kuandika kwa taabu kutokana msaada wa elimu ya ngumbaru (watu wazima) lakini siwezi kukubali uongo huo. 

Elimu ya theologia haina uwezo wa kufasiri unabii. Unabii hufasiriwa kwa uwezo mtakatifu (Roho Mtakatifu). "Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote hata mafumbo ya Mungu. Maana ni nani katika binadamu ajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu (theologia), bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi mwanaadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu. Maana kwake huyo ni upuuzi. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu". (1 Kor 2:10-15). Wanatheologia hawajapata neema hiyo ya Mwenyezi Mungu (sw) ndio maana wanatoa tafsiri zisizoingia katika kichwa kizima. 

Alhamdulil Liaahi Rabbil aalamin. Mimi nimejaaliwa neema hiyo adhimu na nyingine. Hivyo hapa nitafasiri utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu ndani ya Biblia. Inshallah tafsiri hii itatua vizuri kabisa katika kichwa kilicho kizima. Kwa kichwa kilicho kibovu, neno la Mungu linasema: "Hata ukimtwanga mpumbavu kwa mchi kinuni pamoja na ngano, upumbavu wake hautamtoka". (Mithali 27:22). 

Kuibuka kwa Uislamu: 

Kuibuka kwa Uislamu kunafuatia kidokezo cha Yesu (a.s.) kifuatacho: "Kwa sababu hiyo nawaamba ufalme wa Mungu (utukufu) utaondolewa kwenu (Wayahudi)nao watapewa taifa jingine lenye kuzaa matunda yake". (Mathayo 21:43) Yesu (a.s) alizingatia unabii wa Nabii Isaya ufuatao: "Ufunuo juu ya Misri. Tazama BWANA amepanda juu ya wingu jepesi, anafika Misri; na sanamu za Misri zinatikisikika mbele yake, na moyo wa Misri unayeyuka ndani yake ?2 Nami nitaawaamsha Wamisri juu ya Wamisri, nao watapigana, kila mtu na ndugu yake, na kila mtu na jirani yake, mji juu ya mji, na ufalme juu ya ufalme. 3 Na roho ya Misri itamwagika kabisa katikati yake, nami nitayabatilisha mashauri yake, nao watakwenda kwa sanamu zao, na kwa waganga, na kwa wapiga ramli na kwa wachawi. 4 Nami nitawatoa hao Wamisri na kuwatia katika mikono ya Bwana mgumu na Mfalme mkali atawatawala, asema BWANA, BWANA wa Majeshi." (Isaya 19:1-4). 

Tafsiri: 

Aya ya kwanza: Ufunuo juu ya Hijaz (Uarabuni). Malaika Jibril (Gabriel) anakwenda Uarabuni akiwa anapeleka ujumbe mtakatifu wa Mwenyezi Mungu kwenda kwa Muhammad. Ujumbe huo (Uislamu) unazua mtafaruku mkubwa miongoni mwa Waarabu. 

Aya ya pili: Ujumbe huo unasababisha Waarabu wenyewe kwa wenyewe kuanza kupigana. Kisha vita kali ya mji na mji (Madina na miji mingine) na hatimaye vita kati ya Dola na Dola (Dola ya Kiislamu na Dola zingine). 

Aya ya tatu: Mapenzi ya Waarabu ya kuabudu masanamu na ushenzi wao mwingine yanakwisha kabisa. Badala yake Mwenyezi Mungu anawabadilishia utaratibu wao wa maisha (ukafiri) na kawapa utaratibu (dini) mwingine (Uislamu). Hivyo watayaendea masanamu yao na kuyavunja na kuwakomesha Waarabu wote wanaojihusisha na uchawi (uganga, ramli na vituko vingine). 

Aya ya nne: Kisha Mwenyezi Mungu atawaweka Waarabu na Waislamu wote chini ya uongozi wa Mtume Muhammad (saw) aliye mgumu kwa makafiri na mkali kwa wote wanaomwasi Mwenyezi Mungu (sw). 

Utabiri huu (Isaya 19:1-4) unaungana na Unabii mwingine wa Isaya 43:16-21. Kwa ufafanuzi zaidi soma pia Unabii huo. 

Hija mpya na makundi matatu matakatifu 

Watu wengi wanashangaa imekuwaje dini moja ya Mwenyezi Mungu imekuwa na makundi matatu ya Wayahudi (Judaism), Wakristo (Wanazarayo) na Waislamu. Wahubiri wengine kwa ni njema wamejaribu kushutumu kundi lingine kuwa limeibuka bila idhini ya Mwenyezi Mungu (sw). Lakini si hivyo kabisa. Mwenyezi Mungu alisha sema katika Unabii wa Isaya zaidi ya miaka 2730 iliyopita kuwa litatokea hili linalotushangaza. Tatizo ni kushindwa kufasiri Unabii kutokana na kutokuwa na Roho Mtakatifu. 

Hapa nitanukuu kisha nitafasiri Unabii unaouhusu hija mpya na mgawanyiko wa makundi ya dini ya Mwenyezi Mungu. Unabii huu uko katika sura ile ile ya 19 inayotabiri kuibuka kwa Uislamu. Lakini kabla ya kuona utabiri huo, kwanza tuzingatie maneno ya Yesu (a.s) yafuatayo: "Yesu akamwambia, mama unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu (Genzini), wala kule Yerusalem". (Yohana 4:21). Maneno hayo ya Yesu (as) yanajieleza yenyewe. Sasa tuone watu watahiji wapi. 

"Katika siku hiyo itakuwako madhabahu katika nchi ya Misri kwa BWANA, na nguzo mpakani mwake kwa BWANA. 20 Nayo itakuwa ishara na ushuhuda kwa BWANA wa Majeshi katika nchi ya Misri. Kwa maana watamlilia BWANA kwa sababu ya watu wawaoneao, naye atawapelekea mwokozi mwenye kuwatetea, naye atawaokoa. 21 Na BWANA atajulikana na Misri na Wamisri watamjua BWANA katika siku hiyo. BWANA dhahiri, na kuzitekeleza. 22 Naye BWANA atapiga Misri, akipiga na kuponya; nao wakirudi kwa BWANA atakubali maombi yao na kuwaponya. 23 Katika siku hiyo itakuwako njia kuu itokayo Misri na kufika hata Asharu; Mwashuri atafika Misri na Mmissri atafika Ashuru, na Wamisri wataabudu pamoja na Waashuri. 24 Katika siku hiyo Israel atakuwa wa tatu pamoja na Misri na Ashuru, watakuwa baraka kati ya dunia; 25 Kwa kuwa BWANA wa Majeshi amewabariki; akisema, wabarikiwe watu wangu Misri; na wewe Ashuru, kazi ya mikono yangu; na wewe Israel, urithi wangu". (Isaya 19:19-25). 

Tafsiri: 

Aya ya 19: Wakati Uislamu utakapokamilika, kutakuwa na sehemu ya kuchinja wanyama (madhabahu) katika nchi ya Hijaz mahali paitwapo Minna. Aidha itakuwepo "nguzo" yaani Al-Kaaba karibu na Minna. Nguzo hiyo (Al-Kaaba) itakuwa alama na ushuhuda kwa Mwenyezi Mungu katika nchi ya Hijaz (Saudi Arabia). Na kwa kuwa Waarabu baada ya kunyanyaswa na kudharauliwa kwa muda mrefu watapelekewa Mtume (mwokozi) ataayewaokoa na manyanyasao na madhambi yao. 

Aya ya 21: Waarabu watamjua Mwenyezi Mungu ipasavyo na watatoa mihanga (kafara) na sadaka kwa mujibu wa diin ya Mwenyezi Mungu. Aidha, wataweka nadhiri halali na kuzitekeleza kwa mujibu wa dini ya Kiislamu. 

Aya ya 22: Kwa kuwa Waislamu watakuwa umma bora (tazama Qur. 3:10) kama walivyokuwa Wayahudi zamani (tazama Kumb. 26:16-19 na Qur. 2:122), Mwenyezi Mungu atawaadhibu kwa kutumia makafiri endapo watamwasi Mwenyezi Mungu kwa kuwaogopa makafiri na kukataa kuutangaza Uislamu na maasi mengine makubwa yanayoathiri diin ya Kiislamu. Endapo Waislamu watatubu na kuacha woga na kuanza kuutangaza Uislamu kwa nguvu zao zote, Mwenyezi Mungu awasamehe na kuwaondolea bughudha na mateso ya makafiri. 

Aya ya 23: Wakati wa "Agano Jipya" ukifika kutakuwa na kiunganisho kikuu (njia kuu) kati ya Waislamu (Wamisri) na Wakristo (Waashuri) yaani dini ya Kiislamu. Mkristo atasilimu na kwenda Uarabuni kuhiji au vinginevyo, na Waislamu wataingia na kutawala nchi zilizokuwa za Kikristo. Kisha Waislamu wataabudu pamoja na Wakristo waliosilimu. 

Aya ya 24-25: Baada ya kuibuka kwa Uislamu, Wayahudi (Judaism) waliokuwepo kabla ya kuja Mtume Yesu (as) watakuwa wa tatu kwa utukufu pamoja na Waislamu na Wakristo waliokuwepo kabla hajaja Mtume Muhammad (saw). Mwenyezi Mungu atayabariki makundi haya matatu akisema, wabarikiwe watu wake kama ifuatavyo: "Wa kwanza kwa ubora ni Waislamu (Wamisri), Wa pili ni Wakristo (Waashuri) nawa tatu ni Wayahudi. Hapa tuzingatie kuwa Wayahudi na Wakristo waliobarikiwa ni hao niliowataja. Wayahudi waliomkataa Yesu (as) na Muhammad (saw) wamelaaniwa kwa kuukataa "uzima wa milele". (Yohana 3:16-18), na kwa kumkufuru (kumkataa Roho Mtakatifu (Mathayo 12:31-32). Aidha Wakristo waliomkataa Mtume Muhammad (saw) nao wamefanya kosa (dhambi) kubwa sana isiyosameheka ya kumkataa Roho Mtakatifu (Mathayo 12:31-32). 

Unabii huu (Isaya 19:19-25) unaungana na Isaya 66:17-23. Kwa ufafanuzi zaidi soma Unabii huo. 

Sababu za kutumika mafumbo katika Unabii 

Katika Unabii nilioufasiri na Unabii mwingine katika Biblia yametumika mafumbo (mithali). Hikma ya Mwenyezi Mungu ya kufanya hivyo inafafanuliwa na Mtume Yesu (as) kama ifuatavyo: "Wakaja wanafunzi, wakamwambia, kwanini wasema nao kwa mifano (mafumbo) akajibu kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. Na neno la Nabii Isaya litatimia kwao, likisema, kusikia mtasikia, wala hamtaelewa, kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watuhawa imekuwa mizito. Na kwa masikio yao hawasikii vyema. Na macho yao yamefumba; wasije wakaona kwa macho yao, wakasikia kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, wakaongoka nikawaponya". (Mathayo 13:10-15) 

Hitimisho 

Makala hii inahusiana na Unabii wa Yeremia uhusuo Agano Jipya (Yeremia 31:31-32). Hivyo ili kukamilisha makala hii, rejea makala yangu "Injili sio Agano Jipya" katika AN-NUUR Na 145 Uk. 10 la Aprili 17-23, 1998. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
TAHARIRI 
Serikali iwahurumie wananchi wake 

KUCHOMWA MOTO NYUMBA ZA WANANCHI: Nzasa wamtaka Mkapa awaonyeshe pa kwenda 
Na Mwandishi Wetu, Nzasa 

Mishikaki ya nguruwe Moshi yachomwa mbele ya Msikiti 
Na Mwandishi Wetu 

MAONI YETU: 
Je; ni halali kuchoma Kidungu cha mtu? 

Upimaji huu mpya ni wa nini 
Na Mwandishi Wetu 

TANGAZO LA HIFADHI YA MSITU WA KAZIMZUMBWI 

Ndoa si lengo, ni wasila wa kufikia lengo 
Na Bi. Zuhura Tajiri, Shinyanga 
 
Teknologia:
Jifunze kuunganisha Kompyuta
Na Hassan Omar

Makala:
Nani atakayewahoji Waheshimiwa hawa

Goda Muslim School, Manzese
Na Mwandishi Wetu

Utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa

Historia ya mgogoro wa Nzasa
Na Mwandishi Wetu

DUMT watoa msaada kwa walioathirika Nzasa
Na Mwandishi Wetu

UCHOMAJI NYUMBA NZASA: Wafadhili wana mchango gani?
Na Mwandishi Wetu

Mafundisho ya Quran 
Kutoa pasipo masimango 

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe  

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita