AN-NUUR 
Na.171 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 16 - 22, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Historia ya mgogoro wa Nzasa 

  
Na Mwandishi Wetu 

TOKA Msitu wa Kazimzumbwi ufanywe Hifadhi ya Taifa hapakuwahi kutokea mgogoro baina ya Idara ya Misitu na wananchi wa Nzasa wanaoishi kusini mwa msitu huo. 

Wakati wa operesheni Vijiji ya Ujamaa wananchi wengi walilazimika kuyaacha mashamba yao na kuhamia vijijini. Baadae walirejea kwenye makazi yao ya awali kwenye mashamba yao. 

Mgogoro ulianza mwaka 1992 walipojiwa na aliyekuwa Afisa Misitu Mkoa wa Pwani, Bw. Beda Kessy na kuambiwa kwamba wanalima katika Msitu wa Taifa. 

Kwa mujibu wa barua ya wananchi wa Nzasa ya Septemba 5, 1994 kwa Waziri wa Mambo ya Ndani Bw. Kessy alifika kitongojini Nzasa Septemba 13, 1993 akiwa na barua toka kwa Mkuu wa Wilaya inayomruhusu kuweka mipaka ya misitu, kazi ambayo aliifanya. 

Kuanzia hapo ndipo likaanza shinikizo la kuwataka wahame na wananchi hao wakawa wanapinga wakidai kwamba hawapo katika Hifadhi ya Taifa. 

Kumbukumbu za kikao cha Februari 19, 1993 kati ya Bw. Kessy na Wana-Nzasa zinaeleza kwamba Bw. Kessy alikuwa amekwenda na ramani ya mwaka 1971 iliyochorwa kwa mkono ambayo hata hivyo ilionyesha kwamba Nzasa ipo Mkoa wa Dar es Salaam na wala si sehemu ya Mkoa wa Pwani wala sehemu ya Msitu wa Kazimzumbwe. 

Kumbukumbu hizo ambazo zimewekwa sahihi za Mwenyekiti na Katibu wake wa kikao zimeeleza kwamba Bw. Kessy alikiri kwamba Nzasa si sehemu ya msitu, na akaahidi kuandika barua Polisi kufuta kesi aliyokuwa amemfungulia Bw. Mohamed Mtimkavu. 

Kupitia barua Kumb. Na. MD/F.40/1/28 ya April 21, 1994 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Dar es Salaam iliiandikia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini kuhusu suala hilo. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilipendekeza kwamba ili ufumbuzi sahihi upatikane; ni lazima izingatiwe kwamba. Mipaka mipya inayowatia watu wa Nzasa ndani ya Hifadhi ya Msitu iliwekwa na Bw. Kessy mwaka 1993 akiwa Afisa Maliasili Mkoa wa Pwani wakati wananchi hao wapo hapo toka miaka ya 1950. Pili, wananchi hao wana mazao yao ya kudumu, nyumba za kuishi na miradi mbalimbali. 

Tatu kama ni kuhamishwa itabidi wananchi hao walipwe fidia ya mazao na mali zao. Na pia watafutiwe ardhi nyingine ya kuhamia. 

Suala hilo lilifikishwa kwa Mhe. Eduward Lowassa akiwa Waziri wa Ardhi, Mei 18, 1994. Mhe. Lowassa alirudisha suala hili kwa Mhe. Ditopile Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akitoa hoja kwamba suala la misitu lipo nje ya Mamlaka ya Wizara yake na wakati huo kesi ilishafunguliwa mahakamani 

Bw. Mohamed Mtimkavu alishitakiwa na kupigwa faini ya sh.30,000/- na mahakama ya Kisarawe kwa madai kwamba analima katika eneo la msitu. Aidha Bw. Mtimkavu aliamriwa ahame eneo hilo. 

Mtimkavu alilipa faini lakini akakata rufaa Mahakama Kuu Dar es Salaam.Katika kesi hiyo No. 149 ya 1994 Jaji W.J. Maina katika hukumu yake alitengua hukumu ya awali kwa kuzingatia hoja mbili. Kwanza sheria ya misitu Cap. 389 Kf. 6(1) inaagiza kwamba kabla ya eneo lolote kufanywa sehemu ya Msitu; ni lazima Waziri atoe tangazo kwa siku 90 likielezea mipaka ya eneo hilo na tangazo lichapishwe katika Gazeti la Serikali.Katika shauri hili hapakuwa na ushahidi wowote wa kuonyesha kwamba hatua hizo zilifuatwa. 

Pili, kifungu No. 6(1) (c) cha sheria hiyo hiyo ya Misitu kinaagiza kwamba waathirika walipwe fidia, jambo ambalo halikufanyika. Aliyesimama kwa upande wa Misitu wakati huo alikuwa Bw. Charles Secha. 

Pamoja na hayo mgogoro uliendelea kwa wananchi kughasiwa mara kwa mara. Oktoba 17, 1996 Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Capt. T.J. Kasapira akimwandikia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Brg. Gen. H. Ngwilizi alimtahadharisha kwamba mgogoro wa Nzasa unatishia kulipua janga kubwa kwa wakazi wa eneo hilo na kwamba wananchi walishaanza kupoteza imani kwa Chama Tawala na Serikali yake. Capt. Kasapira aliomba chama kifahamishwe nini kiini cha tatizo na ni hatua zipi zinachukuliwa na Serikali. 

Wakati huo wananchi hao walifikisha malalamiko yao kwa Jaji Mkuu; Kitengo cha Sheria na Haki za Binadamu pamoja na Kitengo cha Msaada wa Sheria Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 

Wakati wananchi hao wanahangaika kupata msaada huo wa kisheria ikatoka ilani ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kuwataka wahame. Ilani hiyo ilitolewa Agosti 1, ikitanguliwa na matamko kadhaa ya viongozi wa Serikali akiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dk. Omar Ali Juma. 

Kilichofuatia baada ya hapo ni nyuma zao kuchomwa moto.  
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
TAHARIRI 
Serikali iwahurumie wananchi wake 

KUCHOMWA MOTO NYUMBA ZA WANANCHI: Nzasa wamtaka Mkapa awaonyeshe pa kwenda 
Na Mwandishi Wetu, Nzasa 

Mishikaki ya nguruwe Moshi yachomwa mbele ya Msikiti 
Na Mwandishi Wetu 

MAONI YETU: 
Je; ni halali kuchoma Kidungu cha mtu? 

Upimaji huu mpya ni wa nini 
Na Mwandishi Wetu 

TANGAZO LA HIFADHI YA MSITU WA KAZIMZUMBWI 

Ndoa si lengo, ni wasila wa kufikia lengo 
Na Bi. Zuhura Tajiri, Shinyanga 
 
Teknologia:
Jifunze kuunganisha Kompyuta
Na Hassan Omar

Makala:
Nani atakayewahoji Waheshimiwa hawa

Goda Muslim School, Manzese
Na Mwandishi Wetu

Utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa

Historia ya mgogoro wa Nzasa
Na Mwandishi Wetu

DUMT watoa msaada kwa walioathirika Nzasa
Na Mwandishi Wetu

UCHOMAJI NYUMBA NZASA: Wafadhili wana mchango gani?
Na Mwandishi Wetu

Mafundisho ya Quran 
Kutoa pasipo masimango 

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita