AN-NUUR 
Na.171 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 16 - 22, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Ndoa si lengo, ni wasila wa kufikia lengo 

Na Bi. Zuhura Tajiri, Shinyanga 

MAKALA hii Inshaalaah imekusudiwa hasa kwa wale waoaji (wanaume) na waolewaji (wanawake) ambao huitazama ndoa (mume na mke) kuwa ndio lengo lao kuu na hivyo kusahau kutekeleza vizuri majukumu yao waliyowajibishwa na Allah (sw) katika ndoa zao. 

Mjumbe Mtukufu wa Allah (sw), rehma na amani zimwendee anasema: "Mwenye kuoa (au kuolewa) amehifadhi sehemu ya dini yake basi na amche Allah katika sehemu iliyobaki". 

Hadithi hii tukufu inatufahamisha kuwa baada ya ndoa kuna jukumu kubwa la kutekeleza ambalo waliooana wanapaswa walitekeleze. Ndoa ndio mwanzo wa safari ndefu ambayo kufika salama katika safari hiyo kutategemea ni jinsi gani walio katika ndoa wametekeleza vyema wajibu wao. 

Katika safari hii ndefu ya maisha kuna ndani yake haki za mume na haki za mke ambazo zataka kutekelezwa ipasavyo, kuna kupatikana kizazi (watoto) ambao ni amana kutoka kwa Allah (sw) na kizazi hiki chataka ulezi na usimamizi mzuri utakaowawezesha kuja kuwa watumishi kamili wa Allah (sw), kuna maisha ya Kiislamu ambayo ni haki na wajibu wa kila Muislamu wa kweli, kuna kuamiliana kwa wema pamoja na suala la kudumu kuamrisha mema na kukataza maovu. Haya ni majukumu makubwa na mazito sana na ndiyo sehemu ya pili ya hadithi ya Mtume (sw) pale aliposema: "Na amche Allah katika sehemu iliyobakia". 

Bahati mbaya sana Waislamu walio wengi hujiona tumefika au tumemaliza kazi kwa lile tendo la kufunga ndoa. Midhali kila mmoja kampata aliyemkusudia, aliyemkania, "aliye akimuota njozini" kila siku, basi hapo hudhani lengo limefikiwa!  

Ni lazima ifahamike wazi kuwa ndoa ni sababu tu ni kupatia radhi za Allah (sw) ambalo ndilo lengo kuu, kwa kutekeleza vyema wajibu. Ni jukumu la walio katika ndoa ya Kiislamu kuandaa kizazi kitakachokuja kuishi Kiislamu, kuandaa wapiga kura wa Kiislamu watakaokuja ikataa dhulma na shirki na kuiondoa kwa kura zao. 

Kuandaa wanaharakati wa Kiislamu ambao watakuja pigania haqqi ya kusimama dini ya Allah (sw), kuandaa wanawake wema wa Kiislamu ambao watakuja simama imara kuwasuta akina TAMWA, BAWATA na wa mfano wao juu ya harakati zao za ndumilakuwili za "kumkomboa mwanamke", kuandaa mawaziri na wabunge ambao watakuja iambia serikali yao inayotawala kwa dhulma iache kuwadhulumu na kuwabagua raia wake, na hii si kazi ndogo, laitani tuliooana tungelijua hili! 

Uzito wa jukumu hili unaashiria kuwa ushirikiano wa hali ya juu unatakiwa baina ya mke na mume au baina ya wake na mume. Mafanikio ya familia ya Kiislamu hayahesabiwi kwa kukua au kupanuka kwa biashara waifanyayo, wala kwa magari watumiayo, wala kwa mapato wahesabuyo, wala kwa gharama ya mavazi wavaayo, wala kwa nyumba ya kifahari waishiyo, wala kwa chakula na kinywaji watumiavyo, bali kwa msimamo wao wa ki-Tawhiid na maisha yao ya kunyenyekea kwa Allah (sw), Muumba wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo. 

Ukiyaangalia maisha ya Waislamu yalivyo utasikitika mno kuwa hutopata mfano mzuri wa mafanikio katika ndoa zao. Ukipenda unaweza kuanzia juu yaani kwa viongozi wetu (Masheikh na Masheikh wadogo), Maimamu wa Misikiti, waalimu wa vyuo au madrasa, maamiri na kisha ushuke chini kwa "maamuma". 

Ingawa si wote lakini sehemu kubwa ya hao wamekuwa mfano mbaya sana wa maisha ya Kiislamu katika familia zao na hivyo kuwafanya hata wale Waislamu wa kawaida kutoona umuhimu wa ujenzi wa maisha ya Kiislamu katika familia zao. Na tatizo hili huja pale ambapo lengo la kuoa linapokuwa ni yule unayemuoa au anayekuoa na hapa huangaliwa sababu kama vile mali ya mume, uzuri wa sura ya mke na mara zote uchaguzi wa aina hii huzingatia zaidi zile starehe za kimwili (kula na kunywa vizuri pamoja na ngono) anazotaka mume au mke akidhiwe na si kwa lengo jingine. 

Ndio maana basi utakuta ndoa za aina hii huingia katika matatizo mengi sana ya kifamilia kama vile kuachana baada ya kufisilika, mume kuoa mke mwingine baada ya yule wa mwanzo (kuchuja" na kumtelekeza, mke kuwa na "mafiga" mengine wawili baada ya kuoa "figa moja" halifanyi kazi vyema, wake wenza kuwekeana uadui na kuendeana kwa waganga ili ikiwezekana mmoja ampishe mwenzie na atakayebakia aendelee "kufaidi" peke yake. 

Pamoja na vitimbi mbalimbali ambavyo wake wenza hufanyiana majumbani vyenye kuonyesha mfano mbaya sana wa maisha ya Waislamu. Haya yote yanatokea hivi kwa sababu hakuna lengo la Mungu katika ndoa hizi. 

Nadhani ni wajibu wetu mkubwa kusahihisha makosa haya. Walio katika ndoa wajielewe kuwa Allah (sw) amewaneemesha sana kwa kuwajaalia kuwa katika ndoa kwani ni wangapi kama wao na kuliko wao bado "wanasota juani" na ilhali kaka zao wenye wajibu wa kuwasitiri wanawatizama tu. 

Kuonyesha shukrani zetu kwa Allah (sw) ni kule kutekeleza wajibu wetu tuliofaradhishwa na Allah (sw) ametuunganisha pamoja katika udugu huo. Kwa vile kila jambo lataka maandalizi, basi ni wajibu wetu kuandaa leo mazingira ya kuja kusimama Uislamu kwa kuziandaa vyema familia zetu, na hili jukumu la wazazi wote pamoja na katika familia, ni jukumu la kudumu, ni jukumu ambalo kwa kulitekeleza vyema tutakuwa tumetekeleza kwa vitendo maneno ya Mtume (saw) " Na amche Allah (sw) katika sehemu iliyobakia". 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
TAHARIRI 
Serikali iwahurumie wananchi wake 

KUCHOMWA MOTO NYUMBA ZA WANANCHI: Nzasa wamtaka Mkapa awaonyeshe pa kwenda 
Na Mwandishi Wetu, Nzasa 

Mishikaki ya nguruwe Moshi yachomwa mbele ya Msikiti 
Na Mwandishi Wetu 

MAONI YETU: 
Je; ni halali kuchoma Kidungu cha mtu? 

Upimaji huu mpya ni wa nini 
Na Mwandishi Wetu 

TANGAZO LA HIFADHI YA MSITU WA KAZIMZUMBWI 

Ndoa si lengo, ni wasila wa kufikia lengo 
Na Bi. Zuhura Tajiri, Shinyanga 
 
Teknologia:
Jifunze kuunganisha Kompyuta
Na Hassan Omar

Makala:
Nani atakayewahoji Waheshimiwa hawa

Goda Muslim School, Manzese
Na Mwandishi Wetu

Utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa

Historia ya mgogoro wa Nzasa
Na Mwandishi Wetu

DUMT watoa msaada kwa walioathirika Nzasa
Na Mwandishi Wetu

UCHOMAJI NYUMBA NZASA: Wafadhili wana mchango gani?
Na Mwandishi Wetu

Mafundisho ya Quran 
Kutoa pasipo masimango 

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita