AN-NUUR 
Na.169 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 2 - 8, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Nyumba ya Wakfu yageuzwa Baa Dar
Ilikuwa ya Hajat Aziza Omar

Na Mwandishi Wetu 

NYUMBA iliyokuwa imewekwa Wakfu na marehemu Hajat Aziza Omar inadaiwa kuchukuliwa na Bw. Daniel Zakaria ambaye naye amemuuzia Bw. Pius Kipengele. Nyumba hiyo No. 58 iliyopo Mtaa wa Somali sasa imewekwa baa. 

Nyumba nyingine No. 59 iliyopo Mtaa wa Mchikichi nayo inadaiwa kuchukuliwa na huyo huyo Bw. Daniel na kisha kumuuzia Bw. Steven Mwamkoa. 

Kwa mujibu wa maelezo ya wadhamini wa Masjid Mwinyi, nyumba hizo mbili zilikuwa za Hajat Aziza Omar na alizitoa Wakfu kwa Msikiti kwa hati ya kiapo MCA 284 2/84 ya Oktoba 11, 1990 katika mahakama ya Mwanzo Kariakoo. 

Katika hati hiyo ya kiapo Hajat Aziza Omar wakati huo akiishi katika nyumba No. 58 Mtaa wa Somali aliithibitishia mahakama kwamba hana udugu wa damu wa kumrithi na hivyo akasema: "Natoa wosia kwamba nikifa nyumba hizo ziwe Wakfu kwa ajili ya Masjid Mwinyi uliopo Na. 66 Moshi St. Ilala Dar es Salaam". 

Msikiti huo Masjid Mwinyi aliujenga yeye Hajat Aziza kwa kuvunja nyumba yake iliyokuwa Ilala ili kiwanja hicho ujengwe Msikiti. 

Aidha, fedha zilizojengea Msikiti huo alizitoa yeye baada ya kuuza nyumba yake nyingine iliyokuwa Mtaa wa Agrey. 

Hajat Aziza bint Omar alifariki Mei 5, 1991 ambapo wasimamizi wa Wosia wake walikwenda mahakamani kutoa tangazo la Usimamizi wa Mirathi, tangazo hili lilitoka katika gazeti la UHURU la Ijumaa Septemba 13, 1991, likieleza kwamba Shauri litasikilizwa Desemba 10, 1991 na kwamba Wosia wa marehemu upo mahakamani, hivyo waweza kukaguliwa na yeyote. 

Baada ya kutokutokea yeyote kupinga Wosia huo, Januari 23, 1992 Mahakama ya Mwanzo Kariakoo ilitoa haki ya kusimamia mirathi hiyo kwa waombaji. 

Hata hivyo katika rejea ya shauri la madai No. 3 la 1993 Hakimu Natalia Kimaro alitoa haki ya kusimamia nyumba hizo kwa Bw. Daniel Zakaria. 

Hoja iliyozingatiwa na mahakama hiyo ni kwamba Bw. Daniel aliomba usimamizi wa Mirathi ya Hajat mahakama ya Kisutu Septemba 6, 1991. Kwamba tangazo la Mirathi hiyo lilitolewa katika gazeti la Serikali (Government Gazette) No. 469 la Septemba 20, 1991 na Bw. Daniel kupewa kibali Desemba 22, 1991 na mahakama ya Kisutu. 

Toka hukumu hiyo itolewe Waislamu wa Masjid Mwinyi wamekuwa wakikata rufaa mahakamani, lakini mpaka hukumu ya mwisho ilipotolewa na Jaji J.M. Mackanja Mei 12, 1998 bado mahakama inamtambua Bw. Daniel kama msimamizi wa nyumba hizo. 

Hukumu hiyo ya Mei 12, mwaka huu ilitolewa bila ya mawakili wa pande zote mbili kuwepo mahakamani. 

Kwa mujibu wa vielelezo ambavyo AN-NUUR inavyo, hakuna mahali ambapo uhalali wa kiapo cha Wakfu umehojiwa. Aidha, Masjid Mwinyi bado wanalipia kodi ya majengo kwa nyumba hizo. 

Mei 1, 1996 Halmashauri ya Jiji iliwaandikia Masjid Mwinyi kutaka walipe kodi ya nyumba No. 59 ambayo ilikuwa shilingi 5700, kodi hiyo ililipwa Julai 30, 1996 na wakapewa stakabadhi Na. 0570256. 

Aidha, Aprili 29, 1997 Tume ya Jiji iliwaandikia Masjid Mwinyi walipe kodi ya shilingi 10,000 ya nyumba hiyo ambapo walilipa Juni 23, 1997 na kupewa stakabadhi Na. A00117860. 

Wadhamini wa Masjid Mwinyi waliwahi kulalamika serikalini (ofisi ya Rais) wakionyesha jinsi wasivyoridhika na mwenendo wa shauri hili katika mahakama. 

Katika malalamiko yao ya maandishi kwa Rais, walidai kwamba Bw. Daniel alifanya hadaa. Badala ya kupinga Mirathi waliyofungua mahakama ya Kariakoo yeye alifungua nyingine katika mahakama ya Kisutu. Lakini zaidi ya hivyo, akaitangaza mirathi hiyo katika gazeti la Serikali ambalo hakuna mwananchi wa kawaida anayelisoma. 

Aidha, wamelalamika kwamba ni vipi Bw. Zakaria anapewa haki ya kurithi nyumba za Wakfu wa Muislamu wakati sheria ya Mirathi ipo wazi kwamba Muislamu kwa namna yoyote hawezi kurithiwa na Mkristo. Na zaidi hawana udugu kabisa, si wa damu wala wa kuoleana. 

Aidha, wamelalamika kwamba baada ya hukumu ya Hakimu Natalia Kimaro walikata rufaa Mahakama Kuu chini ya Jaji Mapigano na ikashauriwa shauri lirudishwe mahakama ya Kisutu ili Hakimu aliyeamua shauri hilo bila kusikiliza upande wa pili apate nafasi ya kuwasikiliza Waislamu. 

Hata hivyo wamedai kwamba mahakama hiyo haikuisikiliza kesi hiyo na wakashangaa kuletewa hukumu kutoka Mahakama Kuu kwa Jaji huyo huyo D.P. Mapigano (Februari 25, 1994) ikitupilia mbali ombi lao la rufaa kinyume na agizo la awali kwamba isikilizwe.Kutokana na hukumu hiyo, Bw. Daniel Zakaria ashaivunja nyumba ya Mchikichi sasa ni kiwanja kinasubiri kujengw Juhudi za gazeti hili kumpata Bw. Daniel kuzungumzia suala hili hadi tunakwenda mitamboni hazikuweza kufanikiwa. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 

TAHARIRI 
Majeshi ya nje kupelekwa Lesotho: Je, ni sera za Nguvumali? 

Nyumba ya Wakfu yageuzwa  Baa Dar 
Na Mwandishi Wetu 

‘VAT’ yaingia Bakwata Same 
 Na Mwandishi Wetu 

Mchungaji asema hakuna mihadhara ya kashfa 
 Na Muhibu Saidi 

Maoni yetu: Masheikh tupeni Fatwa 

Safari yangu Ufini 
Ustaadh Ka-Batembo 

Unyanyasaji wa kidini mashuleni, vyuoni ukomeshwe 
Na Abuu Afahah 

Wanaume toeni haki za wanawake 
Na Zabibu Iddi Ng’onda Box 78, Mwadui 

MAONI: Yesu ni yule yule Isa 
Na Saleh Ngoi 

Hatuna uwezo wa kuwapinga manabii 
Na Elia Batendi, S.L.P. 538, DSM 

Ukoloni mwingine unaingizwa nchini? 
Sheikh Thabit H. Mbago,S.L.P. 21486,DSM 

Khatamy ni ‘Gorbacheiv’ mwingine? 
Na Athman Rajab 

Tufuate Uislamu kwa vitendo na siyo kwa maneno 
Mwandishi: Maalim Ali Bassaleh 

AN-NUUR  lina chuki na Wakristo 
Na Charles Kamuhabwa, DSA Mtwara 

Msiiparamie ovyo Biblia 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Yaliyosemwa na viongozi wa dini juu ya idadi ya watu 1989 
Na Rajab Rajab 

Uislamu ulivyoingia Zanzibar -2 

Waislamu Moro watakiwa kutoyumba 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Wanawake Masasi wawataka Masheikh kutangaza sheria za Allah 
Na Muhibu Saidi, Masasi 

Ugaidi na Uislamu siyo kitu kimoja – Sheikh Jongo 
Na Bakari Musa 

Sheikh Abbas awataka wananchi Dodoma waepuke upuuzi 
Na Abu Zubair, Dodoma 

Vijana watakiwa kujiepusha na ‘vijiwe’ 
Na Badru Kimwaga 

Mafundisho ya Quran 
Kutoa katika njia ya Allah: Al-Baqarah aya   261-263 

Barua za wasomaji 

Mashairi 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 
Magonjwa yanayoathiri lishe 
  

 

 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita