AN-NUUR 
Na.169 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 2 - 8, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
TAHARIRI 

Majeshi ya nje kupelekwa Lesotho: 

Je, ni sera za Nguvumali?
  

HIVI karibuni majeshi ya Afrika Kusini na ya Zimbabwe yaliivamia nchi ya Lesotho ambayo kijiografia imezungukwa na Afrika ya Kusini kwa madai kuwa majeshi hayo yamepelekwa huko kwa kuombwa na nchi za SADCC ili yakamalize mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na vyama vya upinzani kutotambua matokeo ya uchaguzi uliofanyika huko mwaka huu. Kwa maoni yetu tunadhani uamuzi huu wa nchi za SADCC unasikitisha na unastahiki kukemewa kwa sababu unaimarisha mtazamo potofu kuwa "mwenye nguvu ndiye mwenye haki na mnyonge hana haki yoyote". 

Tunafahamu kuwa hali halisi ya siasa za dunia yetu hivi leo, kama ambavyo imekuwa katika vipindi virefu vya historia ya binadamu, inatawaliwa na kanuni ya "Nguvumali" yaani fikra kuwa anachosema, anachotenda au kuamrisha mtu au taifa lenye mabavu ndicho cha kweli na cha sawa! 

Dhulma kwa binadamu na ufisadi katika ardhi vinakuwa ndio haki za binadamu ikiwa mbabe atasema ufisadi huo ni haki, na watu wote watatakiwa wakiri na kutekeleza amri na matamshi ya mbabe hata kama ni yenye kuangamiza. 

Mifano ipo mingi. Hivi leo watu wa dunia nzima wanashinikizwa wakubali kuwa liwati, ushoga, kutoa mimba, kuwafundisha watoto wadogo ngono na kuwapa kondomu, na kumwacha mtoto afanye apendacho bila kumrudi ndio haki za binadamu!. 

Hivi leo nchi zenye nguvu kubwa kijeshi zinazisakama nchi changa zinazotaka kumiliki silaha za nyuklia, ilhali wao wenyewe wanazo! Nchi zenye nguvu kubwa kiuchumi zinatulazimisha kuwa raia wetu hata wakiwa mafakiri vipi serikali isiwape matibabu hata kama wanaumwa vipi, na wafe tu, ilhali wao katika nchi zao raia wote wana haki ya kutibiwa na hata kupewa posho ya kuwakimu! Hayo yote tunayajua, lakini tunaendelea kuamini kuwa ukweli na haki havitegemei ubabe wa mtu au taifa. 

Ukiizingatia migogoro ya kisiasa iliyomo katika nchi wanachama wa SADCC na namna nchi hizo zinavyoishughulikia migogoro hiyo utaona dhahiri kuwa Lesotho imeingiliwa kijeshi kwa sababu tu ni nchi nyonge kijeshi na kiuchumi. 

Angalau Lesotho kuna vyama vya siasa vya upinzani jambo ambalo haliruhusiwi huko Uganda, lakini Uganda hiyo hiyo imeshiriki katika maamuzi ya kupelekwa majeshi Lesotho! Uganda sio tu imejiingiza kijeshi katika nchi ya Kongo, lakini ni katika nchi wanachama wa SADCC zinazomtaka Rais wa Kongo afanye mazungumzo na waasi, ilhali yeye mwenyewe anayo makundi matatu yanayompinga kijeshi na hayupo tayari kufanya nao mazungumzo! 

Utata huo upo katika nchi nyingine ikiwemo nchi yetu ambayo mpaka hivi bado haijaweza kuutatua mgogoro wa uchaguzi wa 1995 kwa upande wa Zanzibar. 

Huko nyuma Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa nchi zilizoishutumu sana Marekani kwa kujiteua yenyewe kuwa ndio polisi wa dunia. Lakini katika ubabe ulioonyeshwa na Marekani hivi majuzi Tanzania haikuipongeza Marekani kwa kuzishambulia kijeshi Sudan na Afghanistan, lakini pia haikuthubutu hata kuilaumu japo kwa mbali! 

Kama SADCC ndiyo iliyoishauri Lesotho ivamiwe kijeshi maana yake nchi yetu pia imeshiriki katika maamuzi ya kuziomba Afrika Kusini na Zimbabwe ziingilie kijeshi Lesotho. 

Kama raia wa nchi hii ya Tanzania tunaishauri nchi yetu itafakari vizuri siasa zake za nje. Na hilo litawezekana tu kwa kuwa na mwelekeo unaoeleweka katika siasa zetu za ndani. Tunaamini kuwa ni makosa makubwa kudhani kuwa mataifa dhaifu kijeshi au kiuchumi hayastahili kutendewa haki kama ambavyo ni makosa kuwanyima haki raia ambao ni wanyonge katika nchi. 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
TAHARIRI 
Majeshi ya nje kupelekwa Lesotho: Je, ni sera za Nguvumali? 

Nyumba ya Wakfu yageuzwa  Baa Dar 
Na Mwandishi Wetu 

‘VAT’ yaingia Bakwata Same 
 Na Mwandishi Wetu 

Mchungaji asema hakuna mihadhara ya kashfa 
 Na Muhibu Saidi 

Maoni yetu: Masheikh tupeni Fatwa 

Safari yangu Ufini 
Ustaadh Ka-Batembo 

Unyanyasaji wa kidini mashuleni, vyuoni ukomeshwe 
Na Abuu Afahah 

Wanaume toeni haki za wanawake 
Na Zabibu Iddi Ng’onda Box 78, Mwadui 

MAONI: Yesu ni yule yule Isa 
Na Saleh Ngoi 

Hatuna uwezo wa kuwapinga manabii 
Na Elia Batendi, S.L.P. 538, DSM 

Ukoloni mwingine unaingizwa nchini? 
Sheikh Thabit H. Mbago,S.L.P. 21486,DSM 

Khatamy ni ‘Gorbacheiv’ mwingine? 
Na Athman Rajab 

Tufuate Uislamu kwa vitendo na siyo kwa maneno 
Mwandishi: Maalim Ali Bassaleh 

AN-NUUR  lina chuki na Wakristo 
Na Charles Kamuhabwa, DSA Mtwara 

Msiiparamie ovyo Biblia 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Yaliyosemwa na viongozi wa dini juu ya idadi ya watu 1989 
Na Rajab Rajab 

Uislamu ulivyoingia Zanzibar -2 

Waislamu Moro watakiwa kutoyumba 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Wanawake Masasi wawataka Masheikh kutangaza sheria za Allah 
Na Muhibu Saidi, Masasi 

Ugaidi na Uislamu siyo kitu kimoja – Sheikh Jongo 
Na Bakari Musa 

Sheikh Abbas awataka wananchi Dodoma waepuke upuuzi 
Na Abu Zubair, Dodoma 

Vijana watakiwa kujiepusha na ‘vijiwe’ 
Na Badru Kimwaga 

Mafundisho ya Quran 
Kutoa katika njia ya Allah: Al-Baqarah aya   261-263 

Barua za wasomaji 

Mashairi 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 
Magonjwa yanayoathiri lishe 
  
 

 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita