AN-NUUR 
Na.169 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 2 - 8, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Ukoloni mwingine unaingizwa nchini? 

Sheikh Thabit H. Mbago,S.L.P. 21486,DSM 

Taasubi (kasumba) iliyojengwa na Kanisa Katoliki, kupandikizwa kwa watu na baadhi ya vyombo vya habari, viongozi wa serikali kuistawisha kisha kulitia shemere jeshi la polisi kuwa Waislamu wa nchi hii hawana haki ya kuarifu na kufafanua dhana na wasifu wa Yesu, ni ya hatari inayoweza kuisukasuka nchi. 

Ni vema ieleweke kuwa dhana ya Mungu Muumba (sw) katika Uislamu ni tofauti na jinsi ilivyo katika dini nyingine zote duniani. 

Kwenye Uislamu kabla ya kuabudu ni lazima kumfahamu unayemuabudu ndio maana kuna somo la Tawhiid linafundisha kumfahamu Mwenyezi Mungu (sw) na kutomshirikisha na vyote alivyoviumba kwa jinsi yoyote ile. 

"Sio ustaarabu kuwalazimisha watu kuimba na kukubali kuwa "Yesu ni Mungu" au "Ni Mwana wa Mungu". 

Maneno haya yananenwa sana kwenye vyombo vya habari hata baadhi ya viongozi fulani wenye majina ya Kiislamu waliwahi kushiriki katika kuimba "Yesu ni Mungu Mkuu". 

Kitendo hiki hakiashirii kwamba Uislamu unakubaliana na hayo, hao wamefanya kwa kutoielewa dini yao husika, inasikitisha sana wakoloni wa Kijerumani na Waingereza wana mtazamo wao kwa kumnasibisha Mungu na alivyoumba. 

Uislamu uliingia hapa nchini 800 AD. Wazungu hawa walipokuja hapa kutafuta makoloni walitukuta tukiwa na amani na utulivu pamoja na kuwa Uislamu ulikuwa umetangulia kuingia miaka 1000 kabla yao, hizi sera za kubatiza zilianza kutekelezwa hapa nchini miaka 100 iliyopita. 

Jambo la kushangaza ni kwamba huko kwao hao Wazungu ambao walikuja kutubatiza wanavumiliana na pengine hawajali kabisa wanaposikia Waislamu wakitaarifu dhana ya Mungu mmoja na hatujapata kusikia askari wamepiga Waislamu au kuwakamata kwa mahubiri yao ya Tawhid, lakini huku ambako Ukristo uliletwa tena kwa lengo la kutengeneza makoloni linakuwa ni kosa na watu kuwekwa kizuizini zaidi ya nusu mwaka kwa kuhubiri kwamba Yesu sio Mungu. 

Vipi tudai tumejitawala na tuna uhuru wa kuabudu mazingira ya uzumbukuku kiasi hiki?. Ni kwa nini viongozi wa serikali pamoja na jeshi lote la polisi wasitetee kwa nguvu zao zote imani zilizokuwepo kabla ya kuja hawa Wazungu wanatuyumbisha kwa vijisenti vyao? 

Vita dhidi ya ukoloni maana yake nini? Huu si ukoloni mwingine unaoanzishwa nchini kupitia Kanisa? Ikiwa Maaskofu walikiri kuwa hakuna kashfa yoyote Waislamu wanaposema Yesu si Mungu, je, ni vipi viongozi wa serikali na jeshi la polisi kung’ang’ania kashfa? 

Sasa katika mafunzo ya upolisi kuna somo la Ukristo? Ama huwa msiba mkubwa, watu wanaotegemewa kutetea imani za dini zote wanapoegemea upande mmoja. 



  
Khatamy ni ‘Gorbacheiv’ mwingine?
Huenda Iran ikawa ‘USSR’

Na Athman Rajab 

CNN inamuita Rais wa sasa wa Iran "The People’s President", mataifa ya Magharibi yanamsifu kwa kuwa na "msimamo wa wastani". Walimkubali tangu kwenye kampeni za uchaguzi uliomuweka madarakani. Mohammed Khatamy alitumia sana hoja za kuwapa nafasi za uongozi wa juu wanawake na kulegeza masharti ya vazi la hijab. Aliahidi pia kuboresha uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mataifa ya Magharibi. Kwa ujanja wake wa kuzungumza na ufundi wa kutangaza ahadi nzuri, alijizolea kura nyingi za kinamama na Wairan wa kawaida. 

Baada ya kuunda serikali yake, Rais wa Iran alikuwa na shauku kubwa sana ya kurejesha mahusiano mazuri baina ya Iran na mataifa ya Magharibi hususan Marekani na Uingereza. 

Uhusiano wa Iran na Marekani uliharibika tangu mwaka 1979 wakati Iran ilipofanya mapinduzi ya Kiislamu yaliyoung’oa utawala wa Kisekula wa Shah. Hali ya uhusiano ilikuwa mbaya zaidi pale Marekani ilipofanya jaribio la kijeshi lililoshindwa la kuwakomboa mateka wa Kimarekani waliokuwa wakishikiliwa na Iran. 

Sababu hasa ya uhasama ni kwamba Marekani na washirika wake hawataki kuona dola ya Kiislamu ikisimama popote pale duniani. 

Uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uingereza uliingia dosari zaidi mwaka 1988 wakati mwandishi wa vitabu Bwana Salman Rushdie alipoandika kitabu chenye kuukashifu Uislamu (The Satanic Verses). Iran ilitoa fatwa ya kuuawa kwa mwandishi huyo popote pale atakapopatikana. Serikali ya Uingereza ikapinga adhabu hiyo na ikaahidi kumlinda Rashdie kwa gharama yoyote ile. 

Mataifa ya Magharibi yote yakaiunga mkono Uingereza katika mgogoro huo, na yakautumia vyema kuchora picha mbaya ya Iraan na Uislamu kwa ujumla. Iran nayo ikajiongezea umaarufu kwa ulimwengu wa Kiislamu kama nchi isiyotetereka katika kutoa hukumu za Kiislamu. 

Kwa ujumla, uhusiano wa Iran na mataifa ya Magharibi unaharibika pale tu viongozi wa Iran watakaposimama kidete kuutetea, kuulinda na kuuhami Uislamu. Marekani na wenzake hawataki Uislamu utawale Waislamu. Hawapendi kabisa kuona wananchi wa Iran wakiutumia uhuru wao waliopewa na Mwenyezi Mungu wa kujichagulia mfumo wa serikali wanaoutaka. 

Lakini pamoja na uadui wote huo dhidi ya Uislamu, inasikitisha kuona kuwa watawala wa Iran wameshawekwa sawa na maadui wa Uislamu. Iran ina sababu gani ya ‘kujigonga’ kwa mataifa ya Magharibi? Ni dola ya Kiislamu kweli au wanatumia Uislamu kama ngao dhidi ya maadui zao wa kisiasa? 

Iran imelegeza msimamo wake mkali dhidi ya maadui wa Uislamu wakati maadui hawa wanazidi kujiimarisha kupambana na Uislamu! Nini matokeo ya hilo? Ni kusambaratika kwa dola ya Kiislamu ya Iran na kusimikwa kwa utawala wa kisekula kama ilivyokuwa wakati wa Shah. 

Huu uhusiano mpya na Magharibi unaotaka kuletwa na viongozi wa Iran utaleta mambo! Hauna mwisho mwema kwa taifa la Iran na Uislamu kwa ujumla. 

Mataifa ya Magharibi hayako tayari kushirikiana na dola za Kiislamu kwa lengo la kuboresha hali ya Waislamu kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kadhalika. Watakuwa marafiki wazuri pale tu dola za Kiislamu zitakapobadilisha msimamo wake wa kiitikadi na kisiasa ili ulingane na viwango vilivyowekwa na mataifa ya Magharibi. Hali hii italiweka taifa la Kiislamu katika barabara nyororo ya kuelekea kwenye usekula. 

Mkakati huu wa mataifa ya Magharibi dhidi ya dola ya Kiislamu ndiyo sababu ya Iran kumuondolea adhabu ya kifo mwandishi wa "The Satanic Verses" Bwana Salman Rushdie. 

Iran imefanya hivyo kama hatua moja muhimu ya kurejesha uhusiano mzuri na Uingereza na Magharibi kwa ujumla. Kana kwamba haitoshi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Bwana Robin Cook alinukuliwa na televisheni ya "SKY NEWS" hivi karibuni akisema kwamba "kuondoa adhabu ya kifo pekee haisaidii sana kwa sababu kuna washabiki wa kidini wanaoweza kumuua Rushdie. Ni vyema serikali ya Iran ikashirikiana na Uingereza na nchi nyinginezo kuwadhibiti watu hawa". 

Yaani Bwana Robin Cook anaiomba Iran ishirikiane na Uingereza na serikali zote zinazopinga Uislamu kuwadhibiti Waislamu wanaotaka kutekeleza fatwa ya kuuawa Rushdie. 

Rushdie amekuwa mtu muhimu wa kulindwa na Iran kwa haja ya kurejesha uhusiano na Uingereza tu! Lakini Waislamu wa dunia nzima wakumbuke kuwa Rushdie amewakosea Waislamu na siyo Iran. Na fatwa ya kumuua ni ya Kiislamu wala siyo ya Kiiran. 

Kufuatia ziara ya Rais wa Iran nchini Marekani, Bwana Mohammed Khatamy, hotuba yake katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na msimamo wa siasa za wastani za kiongozi huyo kama anavyopambwa na mataifa ya Magharibi imewapa moyo sana Wairan wanaopinga Uislamu walioko nchini Marekani. 

Wairan hawa wachache waliandamana mbele ya jengo la Umoja wa Mataifa mjini New York wakidai serikali ya Kisekula nchini Iran. Na kama ilivyo ada, vyombo vya habari vya Magharibi vikapata fursa nyingine adhimu ya kuupiga vita Uislamu kwa kuwapa waandamanaji hao wachache ‘Positive Publicity’ dunia nzima. 

Hoja iliyojengwa ni kwamba sheria za Kiislamu zinapingana na haki za binadamu na zinamkandamiza mwanamke. Lakini ukweli wenyewe ni kwamba sheria za Kiislamu ndizo zinazolinda haki za binadamu na hazimkandamizi yeyote. Hicho ni kisingizio chao tu cha kukataa Uislamu. 

Wanachosahau Matwaghuti hawa ni kwamba sheria zote duniani zina msingi na tabia inayofanana ingawa sheria zenyewe hutofautiana kiutendaji. Sheria yoyote ili iwe sheria lazima iwe ‘Binding and Enforced’ yaani ibane wanaoifuata na ilazimishwe kuwepo. Kama kuna watu wachache hawaitaki haina maana kwamba sheria hiyo haifai. Huenda wao ndio hawafai kuishi katika jamii husika. Lakini sheria lazima ifanye kazi ya sheria. 

Ningependa kuwarudisha wasomaji katika maudhui hasa ya makala hii kwa kuwakumbusha historia fupi ya kuporomoka kwa dola kubwa la Kisovieti lililopata kutokea duniani, USSR walipobadili msimamo wao mkali wa Kikomunisti nakuleta siasa za wastani dhidi ya maadui zao (Marekani), kiongozi wa USSR wakati ule, Bwana Mikhail Gorbachiev alipendwa sana na Marekani na Magharibi kwa ujumla kama ilivyo sasa kwa Mohammed Khatamy wa Iran, kwa sababu ya msimamo wake ‘poa’ dhidi ya maadui zake (Magharibi). 

Hoja ya kuleta uhusiano na Marekani aliyoitumia Gorbachiev ilikuwa kuinua uchumi wa Urusi uliodidimia kutokana na Urusi kuendekeza mashindano ya kutengeneza silaha za maangamizo. Alisema hali ya uhasama na vita baridi iliyokuwepo kati ya USSR na Marekani lazima iondoke ili kujenga Urusi mpya yenye matumaini. Kwa maana hiyo Gorbachiev alifungua ukurasa mpya wa mahusiano baina ya Urusi na Marekani (mahasimu wakubwa kiitikadi). 

Kwa mara ya kwanza katika historia ya mataifa hayo viongozi wao (Gorbachiev na Reagan) walitembeleana kwa mialiko ya kiserikali. 

Gorbachiev alianzisha mageuzi yake ya kiuchumi aliyoyaita ‘Perestroika’ na ‘Glarnost’ na Marekani ilitoa msaada mkubwa sana kusaidia mageuzi hayo kwa sharti kwamba viwanda vyote vinavyotengeneza silaha vibadilishwe na vianze uzalishaji bidhaa za kawaida (Consumer’s goods). 

Hakuna aliyejua kuwa sera za ‘Perestroika’ zililenga kung’oa kabisa mizizi ya Kikomunisti nchini Urusi. 

Vingunge wa Kikomunisti walipogutuka, tayari maji yalishakuwa mengi, wakachukua uamuzi wa haraka wa kumng’oa Gorbachiev madarakani na kumpeleka sehemu isiyojulikana. Marekani ikatishia kuondoa misaada yake yote na kuvunja uhusiano na Urusi iwapo Gorbachiev hatorejeshwa madarakani. Na wafuasi wa Gorbachiev wakaanza kuleta taabu. 

Wakuu wa Urusi waliofanya mapinduzi wakaona ni busara kumrejesha Gorbachiev madarakani ili kuepusha machafuko makubwa zaidi ya kisiasa nchini humo. 

Mara tu baada ya kurejeshwa madarakani, Gorbachiev alivunja shirika la kijasusi la KGB ambalo liliundwa kwa gharama kubwa kwa lengo la kulinda na kutetea itikadi ya Kikomunisti duniani. 

Na hapa ndipo mambo yalipoanza. Baadhi ya majimbo (nchi) yaliyounda Shirikisho la USSR yalikuwa hayana imani na Gorbachiev na yakatangaza kujitenga kutoka USSR. ‘Perestroika’ na ‘Glarnot’ ikazaa mtafaruku mkubwa wa kisiasa ambao ulipelekea dola nzima ya USSR kusambaratika kama biskuti. 

Na Gorbachiev akaingia katika mabuku ya historia kama kiongozi wa Urusi aliyefanikisha zoezi zima la kuusambaratisha Ukomunisti duniani. 

Historia ya kusambaratika kwa USSR ni somo zuri sana kwa mataifa ya Uislamu yanayolegeza msimamo wake dhidi ya Marekani na ulimwengu mzima wa Magharibi. Inatia shaka sana kuona hatua inazopitia Iran kuhusu uhusiano na Magharibi ndizo hizo hizo ilizopitia Urusi iliyosambaratika. 

Imefikia mahala Iran inapeleka mgogoro wake na Waislamu wenzake kwa maadui wa Uislamu! Inawaita wapiganaji wa Twalaban Waislamu wenye msimamo mkali kama wanavyoitwa na makafiri. Na imeunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa la kupambana na unaoitwa ugaidi wa kimataifa. 

Iran inajipendekeza kwa makafiri wakati makafiri msimamo wao ni madhubuti kuhusu Uislamu. Je, dola ya Kiislamu ya Iran itadumu kwa mtindo huu wa uhusiano na Magharibi? Hakuna jibu bora la swali hili zaidi ya aya ya Mwenyezi Mungu: "Hawatakuwa radhi Mayahudi na Wakristo mpaka ufuate mila yao". 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
TAHARIRI 
Majeshi ya nje kupelekwa Lesotho: Je, ni sera za Nguvumali? 

Nyumba ya Wakfu yageuzwa  Baa Dar 
Na Mwandishi Wetu 

‘VAT’ yaingia Bakwata Same 
 Na Mwandishi Wetu 

Mchungaji asema hakuna mihadhara ya kashfa 
 Na Muhibu Saidi 

Maoni yetu: Masheikh tupeni Fatwa 

Safari yangu Ufini 
Ustaadh Ka-Batembo 

Unyanyasaji wa kidini mashuleni, vyuoni ukomeshwe 
Na Abuu Afahah 

Wanaume toeni haki za wanawake 
Na Zabibu Iddi Ng’onda Box 78, Mwadui 

MAONI: Yesu ni yule yule Isa 
Na Saleh Ngoi 

Hatuna uwezo wa kuwapinga manabii 
Na Elia Batendi, S.L.P. 538, DSM 

Ukoloni mwingine unaingizwa nchini? 
Sheikh Thabit H. Mbago,S.L.P. 21486,DSM 

Khatamy ni ‘Gorbacheiv’ mwingine? 
Na Athman Rajab 

Tufuate Uislamu kwa vitendo na siyo kwa maneno 
Mwandishi: Maalim Ali Bassaleh 

AN-NUUR  lina chuki na Wakristo 
Na Charles Kamuhabwa, DSA Mtwara 

Msiiparamie ovyo Biblia 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Yaliyosemwa na viongozi wa dini juu ya idadi ya watu 1989 
Na Rajab Rajab 

Uislamu ulivyoingia Zanzibar -2 

Waislamu Moro watakiwa kutoyumba 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Wanawake Masasi wawataka Masheikh kutangaza sheria za Allah 
Na Muhibu Saidi, Masasi 

Ugaidi na Uislamu siyo kitu kimoja – Sheikh Jongo 
Na Bakari Musa 

Sheikh Abbas awataka wananchi Dodoma waepuke upuuzi 
Na Abu Zubair, Dodoma 

Vijana watakiwa kujiepusha na ‘vijiwe’ 
Na Badru Kimwaga 

Mafundisho ya Quran 
Kutoa katika njia ya Allah: Al-Baqarah aya   261-263 

Barua za wasomaji 

Mashairi 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 
Magonjwa yanayoathiri lishe 
  
 

 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita