AN-NUUR 
Na.169 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 2 - 8, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
AN-NUUR lina chuki na Wakristo

Na Charles Kamuhabwa, DSA Mtwara

MIMI ni msomaji mzuri wa gazeti la AN-NUUR, jambo nililogundua katika siku zote hizi za kulisoma gazeti hili ni kuwa Mhariri wa gazeti hili pamoja na wachangiaji wengi wa makala mbalimbali katika gazeti hili wana chuki zisizo za msingi na Ukristo pamoja na Wakristo wenyewe kwa ujumla.

Sioni ni kwa sababu gani gazeti hili kuchukua nafasi kubwa na muda mwingi kuukosoa, kuulaumu, kulaani na hata kuukashifu Ukristo. Kinyume kabisa na mafundisho ya Qur’an inayosema katika moja ya aya zake kwamba "Hakuna watu walio karibu yenu zaidi ila ni wale wasemao sisi ni watu wa Kitabu".

Badala yake gazeti la AN-NUUR kwa sababu mnazozijua wenyewe mmekuwa mnauandama Ukristo na Wakristo kama vile Qur’an imewaambia "hakuna watu walio adui zetu ila ni wale waliosema sisi ni watu wa kitabu".

Kila kitu kinachohusiana na Ukristo iwe ni utawala au mtawala, taasisi, elimu na hata kitabu chetu kitakatifu Biblia hupigwa vita na kutuliwa kila aina ya lawama.

Kwa mfano, pamoja na huduma nzuri za hospitali zitolewazo na taasisi nyingi za Kikristo katika mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) kuna wakati mchangiaji mmoja wa makala zako alipoitaka serikali kuwatoza kodi Wamisionari wanaoagiza dawa kwa ajili ya hospitali za Ndanda, Nyangao na nyinginezo nyingi.

Hivi mtu huyo anafahamu kuwa hospitali hizi ndio tegemeo kubwa la wananchi wa sehemu hizi? Ambao karibu 80% ni Waislamu? Je, ni taasisi gani ya Kiislamu ambayo imechukua angalau hatua ya kuwajengea hata ki-dispensary watu hawa au chuki tu dhidi ya Ukristo inaweza kumpasua mama mjamzito anayehitaji huduma hii? Au angalau kumpasua mzee mshipa?

Mfano mwingine ni utawala wa kikoloni (Wajerumani na Waingereza) hulaumiwa kuwa kwa kuwa walikuwa Wakristo ndio chanzo cha Waislamu wa nchi hii kuwa nyuma kimaendeleo katika nyanja za elimu, uchumi na afya, lakini cha ajabu gazeti hili halijawahi kutuambia kuwa Waarabu (Waislamu) ambao ndio wa kwanza kufika na kutawala mwambao huu wa Pwani ya Afrika Mashariki kabla ya hao Wajerumani na Waingereza wameacha wamewafanyia nini Waislamu wa sehemu hizi katika nyanja zilizotangulia hapo juu yaani elimu, uchumi na afya?

Mbali ya kuwapeleka mamilioni utumwani ambao hadi hivi leo hatujui vizazi vyao vimepotelea wapi.

Pili, si siri kuwa ni Waarabu hao hao ambao waliwazuia wananchi wa maeneo haya (Waislamu) kupeleka watoto wao shule kwa visingizio vya "watakula nyama za nguruwe" au kufundishwa Injili.

Matokeo yake Waislamu wengi wa maeneo ya Mwambao wa Afrika Mashariki hawakuwapeleka watoto wao shule hata kama shule zenyewe zilikuwa za serikali. Wengine walifikia hata hatua ya kufikishwa mahakamani na wakoloni hao hao.

Sasa wa kulaumiwa hapo kuwa alirudisha nyuma maendeleo kielimu ya watoto hao ni nani, Waingereza na Wajerumani au Waarabu? Matunda ya hatua hiyo ndio huko kubaki nyuma kielimu kwa watu wa sehemu hizi.

Sasa basi nakuomba Mhariri wa AN-NUUR na watu wengine wanaokuunga mkoni mnieleze kupitia gazeti hili maendeleo yoyote ambayo watu wa Afrika Mashariki tunaweza kujivunia kuwa tumepata kutoka kwa utawala wa miaka mingi wa Waarabu katika Pwani ya sehemu hii (tangu enzi za Seyyid Said) mbali ya magofu ya masoko ya watumwa na kuandika kombe (mijarabati).

Hatuoni angalau hata Msikiti ambao mtu anaweza kusema ulijengwa na Waarabu, achilia mbali shule, daraja au barabara. Pili Waislamu wenzenu wa Zanzibar ambao wao ndio waliotawaliwa zaidi na Waarabu na hawakuonja utawala wa Wajerumani na hata huo wa Waingereza ulikuwa kupitia kwa Sultani wa Kiarabu wana maendeleo gani kielimu, afya na uchumi zaidi yenu nyinyi mliotawaliwa na wakoloni hao (Wajerumani na Waingereza)?

Kuhusu madai kuwa Waislamu wa Tanzania wana haki ya kulipwa fidia na Wajerumani na Waingereza vipi kuhusu Waarabu mimi nadhani wao ndio wanaopaswa kulipa fidia kubwa zaidi. Thamani ya mwanadamu ni shilingi ngapi? Ndugu zetu waliobebwa na kupelekwa utumwani wakapotelea huko watalipwa na nini?

Kama tendo la kukusanya kodi, mazao na maliasili yetu kulikofanywa na Wajerumani na Waingereza kunatakiwa kufidiwa vipi maisha ya mababu na bibi zetu? Vipi pembe za ndovu? Na utajiri mwingine walio ubeba Waarabu? Nadhani AN-NUUR mtanipa jibu zuri kuhusu maswali haya.

Nchi nyingi za Ulaya hasa zile za Nordic hivi sasa zinaongoza katika kutoa misaada bila ubaguzi wa kidini kwa nchi yetu lakini sikia msaada ukitoka Uarabuni unakuwa na vikwazo lazima upelekwe kwa Waislamu au taasisi ya Kiislamu. Je, hizi nchi za Nordic (Wakristo) nao walituchukulia nini? Au wamewahi kuitawala nchi hii?

Waislamu wengi wanaochangia makala katika gazeti la AN-NUUR hupenda kuwasadikisha Waislamu pamoja na wasomaji wote kuwa Biblia si kitabu cha Mwenyezi Mungu, imebadilishwa badilishwa, imepunguzwa na kuongezwa mambo mengi ambayo wala hawatoi ushahidi kuwa mambo hayo ni yepi.

Lakini hawasemi lolote kuhusu hadithi za Kiislamu zilizotolewa na kuandikwa na Waislamu wenyewe (sio Wakristo) kwamba hata Qur’an yenyewe imepunguzwa punguzwa. (Tazama sahihi Bukhari mlango wa Ash-Shahada Takunu Indal Hakim Fii Wilayatihi Qaadhaa katika Al-Alkaani) utaona hadithi isemayo kwamba Umar bin Khatab (Khalifa) amesema: "Lau kama si kuogopa watu kusema Umar amezidisha (kitu) katika kitabu cha Mwenyezi Mungu ningeliandika aya ya Rajm kwa mikono yangu mwenyewe". Je, hii si kuonyesha kuwa Qur’an pia imepunguzwa baadhi ya aya zake maana aya hiyo ya Rajm hivi sasa haimo kwenye Qur’an tuliyo nayo.

Soma pia sahihi Bukhari mlango Wamaa Khalkadh Wal Unthaa katika Kitabut Tafsir utaona kuwa hapo mwanzoni Qur’an sura 92:3 ikisomwa tofauti na leo. Aya Alqama anasema walikuwa wakiisoma hivi "Wadh Dhakari Wal Unthaa" anaendelea kusema, "ninashuhudia kwamba nimesikia Mtume (saw) akisoma hivi: "Ila hawa (baadhi ya masahaba) wanataka nisome: "Wamaa Khalaqadh dhakara wal unthaa". Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu sitawafuata".

Pia kuna hadithi nyinginezo nyingi zisemazo kuwa Qur’an tuliyo nayo hivi sasa ni hadithi tu (1/3) ya ile ya asili Hii inaonyesha kuwa masahaba wa Mtume Muhammad (saw) (hasa makhalifa) waliondoa au kuongeza waliyoyataka katika Qur’an maana Qur’an hapo mwanzo hakuandikwa (enzi za Mtume) ilikuwa ikihifadhiwa moyoni sasa kumbukumbu za binadamu kama tunavyozijua mwambie leo "pi" leo kesho atasema "pa".

Ushahidi mwingine ni kutoka kwa Ibn Umar mwenyewe angalia Al Itqan (juzuu ya pili Uk. 32) utaona imeandikwa kuwa imepokewa kwa Nafi kwamba Ibn Umar amesema "Huenda mmoja wenu akasema kwamba ameichukua Qur’an yote (ukweli ni kwamba ) Qur’an nyingi imetoweka lakini aseme nimeichukua sehemu iliyodhihiri (niliyoipata)".

Sasa mheshimiwa Mhariri wa AN-NUUR hayo mbona huwa hamtuambii au Waislamu wote wanayajua kuna baadhi ya Waislamu hapa Mtwara hata hao Makhalifa wenyewe hawawajui ila Paulo. Oh wanamjua sana mpaka historia yake.

Kuna mambo mengi yanayofanywa na Waislamu wengi siku hizi lakini hayakuwepo enzi za Mtume (saw) wala hayamo kwenye Qur’an kama Maulidi ya Uzawa wa Mtume, Kudhikiri, kuswali Taraweih jamaa na mengine mengi yameanzishwa au kubuniwa na masahab haswa (makhalifa).

Hayo AN-NUUR hamyasemi wala hamyaelezei ingawaje mara kwa mara yanaleta migongano miongoni mwa Waislamu wa madhehebu mbalimbali.

Siwezi kuitetea Biblia kuwa imepunguzwa au kuongezwa ongezwa lakini na jua moja tu ndio kitabu sahihi kuliko vyote duniani. Hata Waislamu mna haki ya kuiona hivyo Qur’an yenu sasa hizi kelele zote za "Biblia imepunguzwa" za nini? Maana kinachotakiwa ni kufuata amri za Mwenyezi Mungu na mapenzi yake.

Sasa basi ni vyema AN-NUUR na wote wanaoona kuwa Uislamu ndio bora kuliko dini nyingine zote ndio ufuatao sheria za Mungu, Kitabu chenu hakikubadilishwa na Nabii wenu ndiye Mkuu kuliko wote mtujulishe ni nini kilichopelekea Waislamu kuuana wenyewe kwa wenyewe mara tu baada ya kifo cha Mtume? Ni kwanini Mzee wa miaka zaidi ya 80 Seyyid Uthman (Khalifa) aliuawa kikatili Msikitini akiwa kwenye sala? (Taz. Maisha ya Seyyid Uthman).

Uislamu ni nini? Maana ubora wa dini huonekana kwenye waumini wa dini yenyewe. Sasa mbona hatuoni tofauti katika maisha ya Waislamu na watu wengine wasio Waislamu kama Wakristo (ambao dini yao si bora kama yenu). Sasa huo Uislamu upo hapa duniani au mbinguni? Kama vile Wakristo kuua Waislamu walevi, wazinzi, wadhulumaji, wafitini, waongo na zaidi ya yote washirikina wakubwa.

Ukitaka kuroga timu ya mpira ishinde nenda kwa Sheikh akusomee kitabu, ukitaka kumtia mtu uwendawazimu nenda kwa mwalimu wa Kiislamu (akuandikie kombe), ukitaka hata kuua nenda kwa mtaalamu wa Kiislamu akuandikie au amsomee huyo mbaya wako Albadiri.

Tazama sehemu zote zenye wakazi wengi ni Waislamu sehemu za Pwani, Bagamoyo, Tanga, Zanzibar, Mtwara (mikindani) na Mombasa mtajie mtu miji hiyo halafu muulize sifa yake kubwa nini. Miji hiyo kama sio ushirikina. Sasa ubora wa Qur’an na Uislamu wake dhidi ya diin nyinginezo uko wapi?

Badala ya kuuandama Ukristo na habari za Mwana wa Mungu, kula nguruwe, kusali na viatu, bassi kwanza warekebisheni hao wenzenu niliowataja hapo juu.

AN-NUUR, wahadhir wa Kiislamu wote na mtu mwingine yeyote yule ajue aya hii: "Watendao maovu wote, wawe ni Waislamu, Wakristo na wengineo wote sehemu yao ni jehanamu ya moto".

Bwana Yesu anasema "Si wote wasemao Bwana Bwana wataingia ufalme wa Mungu. Wale watendao maovu nitawakataa na kusema siwajui nyinyi mtokako nendeni zenu motoni". 

Na Mtume Muhammad (saw) anasema "kundi la sahaba wangu litanijia siku ya kiama lakini watafukuzwa kwenye hodhi; hapo nitasema Ewe Mola wangu (hao) ni sahaba wangu. Naye atasema hajui walizua nini baada yako. Wao walirejea nyuma kwa visigino vyao". Hadithi nyingine inasema ingawa Mtume (saw) aliwatambua kwa alama za swala kwenye vipaji vya nyuso zao, lakini anaongezea kuwa "Basi sikuwaona yoyote miongoni mwao aliyesalimika isipokuwa (wachache) mfano wa ngamia wasio na mchunga."

Sasa ndugu yangu hapa Bwana Yesu na Muhammad (saw) wanatuonyesha kuwa siku hiyo si dini yako wala Nabii wako watakaokuokoa na moto kama ulikuwa mtenda maovu. Ila kila mtu atatoa habari zake mwenyewe! Kama Mtume hataweza hata kuwatetea sahahaba zake je wewe mwenzangu? Si hivyo tu Mtume Muhammad (saw) kasema kumwambia mwanawe (Fatma) kwamba atende mema. Yeye hana msaada wowote kwake mbele ya Mungu.

Tunaishika Biblia yetu ishikeni Qur’an yenu tukutane mbele ya Kiti cha Hukumu!



Msiiparamie ovyo Biblia

Na Sheikh Bernard P. Nyangasa

NIMEKUWA nikisoma makala mbalimbali za kidini (Ukristo) katika magazeti mbalimbali zikijaribu kuthibitisha au kukanusha madai mbalimbali. Nimegundua kuwa waandishi wengi hawana elimu ya theologia hasa masomo ya Bible Knowledge na Church History. Waandishi hawa wanaandika vitu visivyo na kichwa wala miguu. Wanaandika kile wanachosikia Makanisani na kwenye mikutano ya dini bila kujua kuwa wanachosikia hakimo katika vitabu vitakatifu wala vitabu vya theologia.

Vitu vingine hata havihitaji elimu kuvigundua kuwa ni upuuzi. Maneno kama "Isa sio Yesu" ni upuuzi! Nikimwambia mtu huyo kuwa Yesu sio Yehoshua atakubali? Kwani Yehoshua (maana yake Bwana aokoa) ndio jina asili la Yesu la Kiebrania alilotumia.

Hapa nitatoa mfano mmoja tu wa Bwana Eliya Batendi. Nimechagua barua yake: "Ujumbe kwa waandishi" (AN-NUUR No. 164) kwa kuwa ina ‘wimbo wa taifa’ ambao unaimbwa katika Makanisa yote duniani na unaaminika ndio ‘wimbo sahihi wa taifa’.

Bwana Batendi anasema: " watu hawa hawawezi kunukuu Isaya 9:6 Tumepewa mtoto mwanamume (Yesu) ataitwa Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu".

Kwanza naomba ili tuendelee na kipengele hiki, tujifanye hatujasoma Topic ya nyakati (tense) katika somo la sarufi (Grammer.) Kwani tukijifnya tumesoma somo hilo tutakwamia hapa hapa. 

Tuangalie watalaamu wa Biblia (Wanatheologia) wanasemaje "9:1. Inaonekana kuwa ni utangulizi wa uaguzi ulio katika aya zifuatazo. Uaguzi ulitabiriwa wakati Wagalatiya walipohamishwa na Tiglath – Pileseri wa tatu Mfalme wa Ashura mwaka 732 K.K. Uaguzi huo unatangaza "siku ya Bwana" (AMO 5:18). Siku ya Bwana itawakomboa waliohamishwa na kuwaletea ufalme wa amani atakaoshika mtoto wa ukoo wa kifalme. Mtoto huyo haikosi ni Immanuel anayetajwa katika 7:14. Kufika kwa Kristo Galilaya watatimiza uaguzi huo (Mt. 4:13016) " Tazama Biblia Takatifu Tabora Uk. 658. Hapo tunaelekezwa kuwa Isaya 9:1-7 inahusiana na Isaya 7:14 isemayo "Kwa hiyo BWANA mwenyewe atawapa ishara. Tazama bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume naye atamwita jina lake Immanueli". 

Hapa ‘wimbo wa taifa’ tunaousikia kila siku ni kuwa Immanuel ni Yesu na bikira ni mama Maria. Sasa tuzame ndani sana katika vyuo vya theologia ili kujua kweli huo ni ‘wimbo sahihi wa taifa?’

Hapa nanukuu kitabu kimojawapo ambacho ni mwongozo kwa walimu wa theologia (Teacher’s guides to religions education series) uliokubaliwa na Wanatheologia wote (Agreed Sylabases).

Kitabu hiki kinaitwa "The Rise the Prophets" Senior lessons – Volume Six cha Norman J. Bull, M.A – Champlain and lecturer in Divinity Saint Luke’s College. Mfululizo wa miongozo hii imetayarishwa na The Religious Education Press Ltd.

Wallington Survey (1961) katika ukurasa wa 156 kikizungumzia "Imanuel" kinasema "(b) Immanu-el. It was Isaiah’s Unwavering Conviction that Yahweh was with His people – Immanu-el (God with us) – If they would but put their whole trust in Him. The Prophet offered a sign of this to the weak and wavering Ahaz (see above). A ‘Young woman’ – not ‘ a virgin’ – was with child, and would bear a son to be called Immanu-el. Before he was old enough to know good from evil, Israel and Syria will have been destroyed. This ‘sign’ is given in a concrete historical situation (7:14, 8:8,10 cf. Rom 8.31); it is not visionary future possibility. The ‘young woman’ may well have been Isaiah’s own wife (ef. 8:3) or even the wife Ahaz. From the point of view of Isaiah, there is no Prophecy here of a virgin birth".

Hicho ndicho wanachofundishwa Makadinali, Maaskofu, Mapadre n.k. kuwa huyo mwanamke hakuwa bikira (not a virgin) na tayari alikuwa na mtoto (was with child) na wala sio Maria bali mke wa Nabii Isaya au mfalme Ahazi. Na wanasisitiziwa kuwa hakuna utabiri wa uzazi wa mwanamke bikira hapo " there is no Prophecy here of a virgin birth".

Hii ingawa inashangaza sana, lakini ndio ukweli wenyewe. Kwani neno asili la Kiebrania lililotumika hapo ni "Almah" yaani mwanamke bikira au mwanamke aliyeolewa karibuni hata kama alikuwa mjane mwenye watoto sita. Hivyo kwa kuzingatia na mapokeo mengine ya Kiebrania na Kiaramu (hayamo katika Biblia) tafsiri sahihi hapo ni hiyo ya pili, ingawa ‘wimbo wa taifa’ ni tafsiri ya kwanza. Sasa tuondoke huko kwenye vyuo vya watu tunamrudia Bwana Batendi.

Bwana Batendi anasema: "Wakati Yesu anaagiza lianzishwe Kanisa Mathayo 16:18 alikuwa na maana waswali humo Waislamu? Inaonekana huyu Bwana (pamoja na wengine) anadhani Kanisa alilozungumzia Yesu ni jengo. 

Tuwaachie wataalamu wetu watusaidie. "16:18 Neno Kanisa lilivyoeleweka katika nchi za Mashariki ni mkutano. Katika Agano la Kale mara nyingi Kanisa ni jumuiya ya wateule, hasa taifa takatifu jangwani (Mdo. 7:38) Yesu atumia neno hili Kanisa katika maana ya jumuiya ya Kimasiya atakayofanya nayo Agano Jipya kwa kumwaga damu yake (26:28, Efe. 5:25).

Pengine Kanisa kadiri ya Yesu ni kama Ufalme wa Mbinguni (9:19, 4:17). Ni jumuiya ya "Nyakati za Mwisho" itakayoanza hapa duniani ikiendeshwa na Katiba na Mkuu wake (Mdo. 5:11)" Tazama Biblia Takatifu Tabora Uk. 894.

Bwana Batendi anaendelea kusema: "Wakati Yesu anawatuma wanafunzi wake waende duniani kote, wawafanye watu kuwa wanafunzi wa Yesu, wawabatize kwa jina la Baba la Mwana na Roho Mtakatifu (Mathayo 28:19) alikuwa na maana Waislamu wabatizwe? Huyu Bwana kama ilivyo kwa Wakristo wengine (wasio wanatheologia) anadhani "ubatizo" ni kumwagiwa maji kichwani au kutoswa majini. Maana ya ubatizo ni hii ifuatayo:

"6:4 Watu wa zamani hubatizwa kwa kutoswa majini, na maana ya neno la ubatizo kwa Wayunani ni kutosa majini ubatizo kadiri ya Biblia una habari zaidi ya huko kufa na kufufuka katika Kristo pengine una maana ya kumtakasa mtu (Efe. 5:26, Ebr. 10:22).

Pengine ni kuzaliwa kupya (Yn 3:5, Tit 3:5), pengine ni kuangazwa kupya (Ebr 6:4, 10:32), kadiri ya 1 Pet. 3:21 Safina ya Nuhu ni mfano wa ubatizo".Biblia Takatifu Tabora Uk. 1032.

Wanatheologia wanatufahamisha zaidi kuwa hata Wapagani nao walikuwa wanabatiza. "3:6 Ibada ya kutosa mwili ni mfano wa utakaso au wa kujitengeneza upya. Ibada kama hiyo ilijulikana na kutendeka katika dini za kale za Kipagani na dini ya Kiyahudi pia (kama ubatizo wa waongofu. Mdo. 2:10, Waesseni)" BTT Uk. 879 Yesu mwenyewe japo alishabatizwa (Mt. 3:16) bado alikabiliwa na "ubatizo" mwingine aliouhofia sana. "Nimekuja kutupa moto duniani, na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi? Lakini nina ubatizo unipasao kubatizwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe (Luka 12:49 – 50).

Bwana Batendi na Wakristo wanadhani maneno ya Yesu katika Mathayo 28:19 ni mepesi sana. Ukweli ni magumu sana kwani yamejumuisha neno gumu sana la Roho Mtakatifu.

Rejea makala yangu ambayo bado kumaliziwa "Tafsiri sahihi ya Roho Mtakatifu" (katika ANNUUR Na. (60).

Nikisema nitafsiri maneno hayo kiutaratibu ili kujua Yesu alimaanisha nini, nitajaza si chini ya kurasa nne za gazeti. Hebu fikiria, neno moja tu la Roho Mtakatifu kwa ufupi imeshindikana kumalizika katika kurasa moja, sasa tukichanganya na maneno ubatizo, jina, baba na mwana itakuwaje?

Kwa ufupi sana Yesu aliposema kubatiza katika Mathayo 28:19 alimaanisha kuwatoa wapagani katika hali ya kutomjua Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na kuwafanya (kuwabatiza) wawajue Mwenyezi Mungu, Mtume Yesu (as) na Mtume atakayekuja baada ya Yesu (Roho Mtakatifu).

Kitendo cha kutosa majini ni uthibitisho (shahada) kuwa mtu ameshamwamini Mwenyezi Mungu na Mtume anayehusika (aliyepo). Hivi sasa ubatizo (shahada) kwa kutosa majini umeshafutwa kama alivyotabiri Mtume Yohana (as) ingawa alidhani Yesu ndiye Mtume ambaye hatatumia ubatizo huo. "Akahubiri akisema, yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake. Mimi niliwabatiza kwa maji, bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu", yaani watafanywa wamwamini Mwenyezi Mungu na Mtume anayehusika kwa mafundisho matakatifu (Tazama ANNUUR Na. 60 Uk. 14 tafsiri Na (V) ya Roho Mtakatifu).

Sisi Waislamu tunabatizwa na kubatiza kwa Roho Mtakatifu kama alivyotabiri Mtume Yesu (as) "Yesu akamwambia, mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu (Gerizim) wala kule Yerusalem. Ninyi mnaabudu msichokijua, sisi (Mitume) tunaabudu tukijuacho, kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. Lakini saa inakuja nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo Yeye imewapasa kumwabudu katika Roho na Kweli" (Yohana 4:21-24.

Bwana Batendi anaendelea: "Au wakati Yesu alipotabiri kuwa wafuasi wake watafukuzwa kwenye Misikiti (masinagogi) Yoh. 16:1-2, je, utabiri huo ulitimia vipi? Ni kina nani waliobaki Misikitini? 

Maneno haya yananitia mashaka juu ya elimu yake ya darasani. Hivi hajui waliosema "sinagogi ni Msikiti wa Wayahudi" (Biblia Uk. 1229) ni wafasiri wa Kiswahili wa Biblia wakizingatia kuwa Msikiti ni jengo (sehemu) la ibada. Hivyo Kanisa nalo ni Msikiti wa Wakristo.

Hata baa ni "Msikiti" au "Kanisa" la walevi na Casino au danguro ni hivyo hivyo wakimwabudu Mungu wao Shetani. Tazama 2 Wakorintho 4:4 na Ufunuo 3:9.

Mimi siwezi kulumbana na watu aina ya akina Batendi kwani siwezi kuelewana nao. Ndio maana nawataka Wanatheologia wapinge makala zangu kama wana ubavu. (Taz. ANNUUR Na. 145 Uk. 10) akina Batendi siwezi kuwa reffer kwenye vitabu vinavyotumika katika vyuo vya theologia kwani hawavijui. Sasa tutaelewana vipi! 

Hata makala hii lengo lake sio kumjibu Bwana Batendi, bali nimetoa mfano tu wa upuuzi unaofanyika. Imekuwa bahati mbaya sana kura imemwangukia Bwana Batendi. Ningeweza kumtolea mfano hata Mwinjilisti Kusupa. Tena huyu Mwinjilisti amenichoma sana kwa mahubiri yake aliyoyaingiza katika makala yake iliyo katika ANNUUR Na. 162 Uk. 11.

Maneno yaliyo mwanzoni kabisa kifungu (b) yameniuma sana. Imekuwa kama ameniambia mimi peke yangu. Hata hivyo imenibidi nijikaze sana nisimjibu kwa sababu kwanza hatanielewa kwa kuwa ndo akina Batendi wenyewe, pili atanichelewesha kwenda kupalilia mihogo yangu.

Hivyo kwa kuchelea kukumbwa na njaa, imenibidi niendelee kumvumilia. Bwana Kusupa anapenyeza mahubiri yake katika gazeti la Kiislamu (ANNUUR) kwa kutumia filosofia ya hali ya juu sana ambayo kwa mtu mwenye elimu ndogo hawezi kugundua lengo lake.

Mwisho nawashauri Wanatheologia waache kudanganya watu. Wachukue mfano mzuri wa Mchungaji A.T. Manoni. Tazama AN-NUUR Na. 144 Uk. 11 na Na. 158 Uk. 11 makala hizo ni sahihi kabisa. Kwa msimamo huo kama hajawa Muislamu, huo ni mwanzo nzuri wa kuwa Muislamu.

Hata mimi nilianza hivyo hivyo kuyakubali mafundisho ya Kiislamu, kisha baada ya miaka mitatu nilisilimu rasmi mwaka 1989 nikiwa na umri wa miaka 27.

Aidha nawashauri Wakristo wengine wasikubali kuburuzwa. Wazingatie maneno haya Matakatifu "Mjinga huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo" (Mithali 14:15).
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 

 

 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita