|
|
|
Yaliyosemwa na viongozi wa dini juu ya idadi ya watu 1989 HIVI karibuni nchi yetu itaingia katika zoezi gumu la kujua idadi ya watu wake hapo Agosti 1999. Ifuatayo ni sehemu ya maoni ya viongozi wa madhehebu mbalimbali waliyoyatoa wakati wa semina ya idadi ya watu na maisha ya familia (POFLEP) iliyofanyika Novemba 23, 1989 mkoani Morogoro kama inavyoelezwa na Mwandishi RAJAB RAJAB. SEMINA hiyo ya siku moja ilifunguliwa na aliyekuwa Katibu wa CCM mkoa, Bibi Mtoro Katele na kufungwa na Mkuu wa Mkoa wa kipindi hicho Bw. John Mhavile, ilihudhuriwa na wajumbe 21 kati ya 23 walioalikwa. Semina hiyo ilidhaminiwa na ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais. Madhumuni ya semina hiyo yalikuwa kuwapa fursa viongozi wa dini kuelimishwa juu ya elimu ya idadi ya watu na maendeleo yao. Pia kuwapa fursa viongozi hao kujadili na kutoa mapendekezo na maoni yao kuhusu suala la idadi ya watu nchini pamoja na uzazi wa majira. Na kupanga mkakati kuhusu kuwaelimisha waumini wa madhehebu mbalimbali katika jamii. Watoa mada katika semina hiyo walikuwa ndugu E.K. Mduma wa POFLEP Morogoro ambapo yeye alizungumzia dhana ya idadi ya watu na mwenendo wake. Ndugu G. S. Ngakuya wa Ofisi ya RDD wa Idara ya Mipango Mkoa wa Morogoro alitoa mada ya Hali ya Idadi ya Watu Tanzania na mkoa wa Morogoro. Mada nyingine katika semina hiyo ilitolewa na ndugu D.M. Muna, yeye ni Mhadhiri IDM Mzumbe ambapo alizungumzia uwiano wa idadi ya watu na maendeleo kiuchumi na kijamii. Mada ya mwisho ilitolewa na ndugu H. Dutilo wa Wazazi Mkoa ambaye alizungumzia sera ya malezi ya watoto na vijana. Akichangia mada hizo, Rev. Mwakibala wa Kanisa la SDA alionyesha masikitiko yake kwa kuona binadamu wa sasa wamepoteza kabisa maadili ya Mungu na mkazo umetiliwa katika kuridhisha zaidi mwili. "Malezi ya kiroho yangetangulizwa kwanza majumbani ili kuwafundisha watoto mapenzi na maelekezo ya Mungu", alisema Rev. Mwakibala. Rev. Mwakibala aliendelea kusema kuwa kwa njia hii hata idadi ya watoto kwa familia haiwezi kuachwa ikazidi uwezo wa familia kwa vile wanaounda familia wamepewa elimu ya Kikristo ambayo inaelimisha utaratibu mzuri wa kuzaa watoto. Ameongeza kusema kuwa bila kumcha Mungu binadamu ataendelea kupata maangamizi. Naye Imam wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa Morogoro Mohamed Kairo alisema kuwa watoto wetu wamezaliwa na kulelewa katika hali mbaya na ngumu sana hapa nchini. "Toka mimba hadi kulelewa mtoto mpaka kujitegemea ni matatizo pamoja na juhudi zinazofanywa na jamii zetu. Huduma zetu za afya, elimu na usafiri ni ghali sana na kama mtu hana uwezo maisha yake yatakuwa hatarini", alisema Imam huyo. Aliendelea kusema, ili kujikwamua na hali hiyo binadamu asianze kujilaumu kwa nini amezaa sana bali tujirudi na kuanza kurekebisha tabia zetu. Aidha, Imam Kairo alisisitiza kuwa wanaohusika katika familia wafuatilie kwa dhati malezi ya mimba na mtoto hadi anapojitegemea na hapo madhehebu yanaweza kutegemea kupata waumini bora. Alisema kila familia ikifanya marekebisho hayo basi taifa litakuwa na watu bora baadaye na alitoa mfano kuwa Uislamu unafunza kuwa mtoto azaliwe kati ya muda wa miaka si chini ya miwili ili yeye na mama wawe na afya nzuri. Mhadhiri wa IDM Mzumbe, ndugu D. Muna alisema kuwa kuna kifo cha mama mzazi kila dakika ulimwenguni na kati ya vifo hivyo, theluthi mbili hutokea katika nchi zinazoendelea kama Tanzania. Akitoa rai yake, alisema kuwa wakati umefika kwa UMATI kutoa msimamo mpya kuhusu huduma zake kwa wasioolewa kwani haitegemewi kwa sasa kama wanawake wote wataolewa. Pia alitoa ushauri kwa dhehebu la RC kuelimisha waumini wake kuhusu aina ya FP inayoipendelea. "Si vyema kukataa FP za kisasa wakati hakuna badili yake inayotolewa, nia ni kulinda afya ya mama na mtoto na uzazi wa mpangilio ni muhimu sana", alisema Mhadhiri huyo wa IDM Mzumbe na kuongeza kwamba njia ipi atumie nani ni juu ya kila mtu mwenyewe na hali ya mwili wake. Naye Katibu wa Sekretarieti ya Mkoa ya Itikadi na Elimu ya Siasa na Mafunzo, ndugu S.D. Mgombera alisema uzazi unafuata maandiko, ambapo Biblia inasema kuwa watu wazae lakini wajidhatiti kuishi kwa jasho lao wenyewe. "Hivi yupo mtu yeyote katika jamii yetu ambaye alijiandaa au anajiandaa na mwenzake kuhusu dhamira ya kutaka mtoto, sababu ya kumtaka mtoto, chakula chake na huduma zingine kama zipo au zitapatikana?" alihoji ndugu S.D. Mgombera. Aliendelea kudai kuwa ni wazi hakuna watu wa namna hiyo na kama wapo ni wachache sana. Hivyo ndugu S.D. Mgombera alishauri si vyema kuzaa tu holela bila ya mpangilio na watu waelimishwe kwa kutumia semina mbalimbali. Ndugu P. Petro Mwenyekiti wa UWT (mkoa Morogoro) alilaani vikali tabia ya wasichana na watoto wa shule wanaodanganyika kula vidonge vya majira kwa siri bila ushauri wa kitaalamu. Alipendekeza wasichana wajitunze kwa kufuata mila maadili ya dini. "Maadili ya Mungu yameachwa, mila na desturi zetu nzuri zimeachwa, watoto hawapewi kazi za kuwashughulisha, wanaachwa wakizagaa ovyo hata mpaka usiku", alisema ndugu Petro Mwenyekiti wa UWT (M) wa Morogoro. Aidha, mwenyekiti huyo wa UWT Mkoa alikemea tabia ya wazee wengi siku hizi ya kujivuta vuta na visichana vidogo na kudai tabia hiyo ipigwe vita kwa kuwa inaharibu maadili ya utu katika jamii. Mwenyekiti huyo wa UWT mkoa aliongeza kusema kuwa, siku hizi watoto wa madhehebu yote yameharibika na lazima wote tukae tufikirie namna ya kurudisha jamii katika mkondo sahihi. Akichangia mada hizo, Rev. T. Funemi wa Kanisa la Lutheran Mji Mpya Morogoro alisema maongozi bora ya nyumbani yakiwa ya kiroho na maisha yakiwa ya kumheshimu Mungu basi mwenendo utakuwa wa kumpendezesha Mungu na jamii itakuwa bora. Rev. T. Funemi alitilia mkazo kuwa watoto sharti watunzwe kiroho kwanza halafu kiakili, kimwili na kiuchumi. "Haya yakikamilika tutakuwa na jamii yenye maadili mema na hata wasichana wanaopoteza watoto wao kwa kutoa mimba watapungua", alisema Rev. T. Funemi. Aliongeza kusema kuwa kutaka juhudi za shule zifanywe kwa vijana hasa wa kidato cha pili na nne, kuwa kwa hawa ndio wenye matatizo makubwa sana. Mchangiaji mada mwingine alikuwa Mama H. Mwagalama wa Kanisa la Anglikana Uaskofu wa Jimbo la Morogoro ambapo alipendekeza kila mtu ajiulize kwanini ongezeko la watu limekuwa la haraka haraka sana nchini mwetu. Vile vile Mama H. Mwagalama alishauri kuwa kila mtu ahusike na suala la kutuliza vijana wetu ambao hali zao za maisha zinatia wasiwasi sana. Aliendelea kusema Mama Mwagalama kuwa ni lazima semina za mara kwa mara zifanywe kuhusu somo hili na mila nzuri zirudiwe ili kufunda vijana wanaoingia hatua mpya ya kuunda familia. Wakati huo huo amewataka baba na mama waonyeshe mfano pale nyumbani na watoe malezi bora. Akitoa maoni yake katika semina hiyo, Rev. C. Kadeghe wa Kanisa la Anglikana , alisema jamii ipo katika kipindi cha mpito ambapo maisha hayapo upande wa jadi za zamani wala maisha ya nchi zilizoendelea, jamii yetu ipo hapa katikati. "Kwa ajili hiyo, mila na desturi za zamani hazifundishwi tena kama ilivyokuwa mashuleni pia mafunzo hayapo sana sana", alisema Rev. Kadeghe. Pia alipendekeza juhudi mpya zifanywe tena kwa pamoja, madhehebu, vyama na serikali katika kuendesha semina na maekelezo mapya il kujenga maadili bora na kukemea maovu yaliyopo sasa. Mjumbe mwingine aliyechangia hoja alikuwa ni Mama Mwakibala wa Kanisa la DSA, alianza kwa kusema kuwa wazee wetu walilelewa vizuri sana kwenye maadili mema ya Mungu ila kizazi hiki ni kigumu kwasababu hakina muelekeo, tumemuasi Mungu. Mama Mwakibala aliendelea kusema dini ya SDA inatoa mafunzo na maono kwa mzazi na mtoto wakipata maelekezo mazuri katika maisha yao watasikia na kufuata. Mwingine aliyepata fursa ya kutoa maoni yake alikuwa ni Rev. J. Mhina wa Kanisa la RC ambapo alieleza kuwa Kanisa la RC lina kawaida ya kutoa mafunzo ya uzazi bora wakati wa mafundisho ya ndoa za waumini wao. Akizungumzia wajibu wa madhehebu katika jamii, Rev. Mhina alifafanua kwamba ni wajibu wao kutoa mafunzo ya mwenendo bora wenye maadili ya Mungu. "Isipokuwa upo umuhimu wa kubadilisha namna ya mahubiri ili theolojia iwe ya Kitanzania zaidi na iguse matatizo yaliyopo", alisema Rev. Mhina. Aidha, Rev. Mhina alitoa msisitizo kuwa vijana wetu mashuleni hawapati elimu ya dini ipasavyo kwasababu inakuwa vigumu kwa dhehebu lake kupata watumishi wa kutosha kutoa mafunzo katika muda wote wa siku maalum ya wiki. Rev. Mhina aliendelea kutoa maoni yake kwa kudai watoto wa viongozi wamezidi kwa tabia mbaya ukilinganisha na watoto wa watu wengine na hii ni kwa sababu wazazi wa watoto hawa hawana muda wa kuwalea kwa karibu zaidi kila siku kwa kisingizio cha kazi zao. Mwingine aliyepata fursa ya kuchangia alikuwa Ndugu S.D. Mgombera ambapo alisema kuwa hapo zamani madhehebu ziliwahusisha walimu wa shule kutoa mafunzo ya dini kadri ya madhehebu yao. Alidai kuwa huu ulikuwa mfumo mzuri na yeye aliwahi kushiriki katika mfumo huu. "Suala la kufundisha dini ni suala la msingi na ni la lazima lau kama chama tawala na serikali yake havina dini", alisema ndugu S.D. Mgombera. Pia alisisitiza kwa kuongeza kuwa hivi sasa fedha imegeuza mioyo ya watu wengi na huduma kugeuzwa biashara. Ndugu Mgombera aliendelea kusema kuwa hakuna mtu anayeweka vipingamizi kwa madhehebu kufikia waumini wake kwa neno la Mungu na CCM itafuatilia kwa makini suala hili kupitia Idara yake ya huduma kwa umma. Naye Mratibu wa UMATI mkoa wa Morogoro Ndugu G. Chegema, alisema chimbuko la matatizo ya vijana lililopo sasa ni matatizo ya watu wazima kwa ujumla. Hivyo, alisema ili kurekebisha tabia za vijana lazima kazi ya kwanza iwe kudhibiti tabia ya watu wazima kwanza. "Kwa kadri kijana anavyoendelea na shule, ndivyo anavyozidi kupungukiwa na muda wa kukaa na wazazi wake na mambo mengi huamua mwenyewe na mabadiliko ya mfumo wa sasa katika jamii yetu umeathiri sana tabia za vijana na hata wazazi wao", alisema Ndugu Chegema. Kuhusu juhudi za UMATI, ndugu Chegema alisema kuwa inajitahidi kutoa mafunzo ya malezi bora na uzazi wa mpangilio kwa kutumia njia zote na uchaguzi ni wa watu wanaohusika (wenyewe) wakisadiwa na taaluma ya uganga. Ndugu Chegema alitoa ushauri kuwa lazima kuwepo juhudi za pamoja katika kudhibiti tabia na mwenendo wa watu, tabia ya vijana pamoja na kuanzisha na kueneza elimu ya familia (Family Education). Afisa utumishi wa mkoa wa Morogoro Ndugu S.Y. Kiguo alisema, kipindi cha mpito kinakuwa na matatizo kwa vijana kwa sababu waliokuwa na majukumu ya kutoa elimu ya jadi yaani babu na bibi sasa hawapo au hawapati nafasi ya kukaa na vijana kwa sababu ya mabadiliko ya mfumo wa maisha na mfumo wa elimu tuliyonayo ambayo haina masomo hayo mashuleni. "Inapaswa kazi hiyo sasa ifanywe na mzazi mwenyewe pamoja na walimu shuleni, taasisi za nje mbali na wazazi nazo ziwe na sera ili majukumu yake katika kulea vijana yafafanuliwe na kutambuliwa na maadili ya jamii katika mila zetu yafufuliwe maana yapo na yalikuwa yanafanya kazi nzuri hapo mwanzo", alisema ndugu Kaguo. Naye Katibu wa CCM (M) Morogoro ndugu M. Katele alisema tabia za vijana zilitegemea taratibu za kila kabila na ukoo. "Siku hizi watu wamechanganyika na si rahisi kabila au ukoo mmoja kuishi peke yake na mchanganyiko huu umeleta matatizo kwa sababu hapakuwa na mwongozo au maelekezo ya namna ya kukabili yale ambayo yangetokana na mchanganyiko huo", alisema Katibu huyo wa CCM. Katibu wa CCM ndugu Katele aliendelea kusema kinyume na ilivyokuwa zamani, michezo ya watoto na vijana sasa inakuwa haina udhibiti mzuri na ni kama wanajidhibiti wenyewe jinsi wapendavyo. Pia Katibu huyo aligusia suala la nidhamu kuwa chini (mbovu) kwa watoto wa viongozi na kukiri kuwa ni kweli muda wa viongozi wengi kama si wote wa kukaa na watoto wao na kuwalea vizuri haupo kabisa. Hivi karibuni katika madai ya kukabiliana na kuongezeka kwa wagonjwa wa UKIMWI, watoto wetu wa shule (watoto wadogo) wameanza kupewa mipira ya kiume (kondomu) na kufundishwa matumizi yake kwa madai ya kuwafundisha jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo. Kwa kuwa hali hii imeshaanza kwa kisingizio cha ugonjwa wa UKIMWI, kuna hatari masomo hayo ya ngono kwa watoto wetu yakaongezeka kwa kasi sana kwa madai ya mbinu ya kuongezeka kwa watu (Over Population). Waislamu hawapaswi kufuata vitu vya namna hii kwa kuwa kitabu chao kimeweka wazi juu ya mpango wa uzazi, hivyo shime ndugu zangu Waislamu hatua ya watoto wetu kulazimishwa kufanya uzinzi inabidi mzazi aiangalie kwa macho mapana, maana serikali isije ikaona kuwa inapunguza idadi ya watu kumbe ndio inachochea zinaa! |
YALIYOMO
TAHARIRI Majeshi ya nje kupelekwa Lesotho: Je, ni sera za Nguvumali? Nyumba ya Wakfu yageuzwa Baa
Dar
‘VAT’ yaingia Bakwata Same
Mchungaji asema hakuna mihadhara ya
kashfa
Maoni yetu: Masheikh tupeni Fatwa Safari yangu Ufini
Unyanyasaji wa kidini mashuleni, vyuoni
ukomeshwe
Wanaume toeni haki za wanawake
MAONI: Yesu ni yule yule Isa
Hatuna uwezo wa kuwapinga manabii
Ukoloni mwingine unaingizwa
nchini?
Khatamy ni ‘Gorbacheiv’ mwingine?
Tufuate Uislamu kwa vitendo na siyo
kwa maneno
AN-NUUR lina chuki na
Wakristo
Msiiparamie ovyo Biblia
Yaliyosemwa na viongozi wa dini juu
ya idadi ya watu 1989
Uislamu ulivyoingia Zanzibar -2 Waislamu Moro watakiwa kutoyumba
Wanawake Masasi wawataka Masheikh
kutangaza sheria za Allah
Ugaidi na Uislamu siyo kitu
kimoja – Sheikh Jongo
Sheikh Abbas awataka wananchi
Dodoma waepuke upuuzi
Vijana watakiwa kujiepusha
na ‘vijiwe’
Mafundisho ya Quran
Chakula na Lishe
|