|
|
Sheikh Bafadhil
aitaka Bakwata iwe mtetezi wa Waislamu
SHEIKH Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mjumbe wa Kamati ya Maulamaa Taifa, Sheikh Omar Bafadhil ameitaka Bakwata kuwa mtetezi wa Waislamu badala ya kuwa mbali nao. Aidha, Sheikh huyo aliitaka Bakwata kufungua ukurasa mpya wa mahusiano baina yake na Waislamu inaodai kuwaongoza kwa kutetea haki mbalimbali kwa mujibu wa katiba ya nchi. Sheikh Omar aliyasema hayo katika sherehe za Maulid zilizofanyika kitaifa wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani usiku wa Jumatatu Julai 6, 1998. Huku akisindikizwa kwa takbira toka kwa Waislamu waliofika katika Maulid hayo, Sheikh Bafadhil alisema kwamba hivi sasa Waislamu nchini Tanzania ni kama watoto yatima, hawana mtetezi na Bakwata ambayo ingepaswa kuwa na jukumu hilo imekuwa mbali nao. "Wakati umefika Bakwata kufungua ukurasa mpya ili iwe mtetezi wa haki za Waislamu kwa mujibu wa Katiba ya nchi", alisema Sheikh Umar huku akisisitiza kwamba kuyasema hayo si kuleta fitina katika jamii. Akizungumzia mmomonyoko wa maadili nchini, Sheikh Bafadhil alisema kwamba, jamii ya Watanzania imekumbwa na wimbi la maovu ambapo ulevi na zinaa vimeshika kasi. Aliwataka wazazi kusimamia kikamilifu suala la malezi ya vijana ambao alisema wao ni uti wa mgongo wa Taifa. Huku akirejea makaripio ya Mtume Muhammad (s.a.w) kuhusu pombe, aliitaka serikali iache kutengeneza na kugiza pombe kwani kwa kufanya hivyo inajenga taifa la walevi ambalo halitakuwa na hadhi. "Hao wanaotuletea makontena ya ulevi waelezeni watuletee chakula", alisisitiza Sheikh Bafadhil. Aidha, aliwashutumu wale wanaoshajiisha matumizi ya kondomu kwamba wanachochea uzinifu katika jamii ya Watanzania hivyo kuipeleka katika maangamizi ya ukimwi. "Mtu asiwadanganye eti muwape watoto kondomu ili wajikigne na ukimwi, huko ni kuwachochea wafanye ufuska", alisema kwa ukali huku akiwatakawazazi wasimamie malezi pamoja na kuwataka wanawake wavae mavazi ya stara. Katika hotuba yake hiyo iliyoonekana kuvuta masikio ya wengi, Sheikh Omar aligusia pia shutuma zilizotolewa na kiongozi mmoja hivi karibuni dhidi ya Rais Mstaafu, Mzee Ali Hassani Mwinyi. Sheikh Omar alisema kwamba, aliyoyasema Mzee Mwinyi kuhusu vyombo vya Waislamu na umuhimu wa umoja miongoni mwao hayana budi kufanyiwa kazi na wahusika badala ya kushutumiwa. "Lazima tuwaheshimu viongozi wetu wastaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Mzee Jumbe, alisema Sheikh Omar huku akikazia aliyoyasema katika hotuba yake ambayo ilisikika nchi nzima kupitia RTD kuwa fursa hiyo aliyoipata ni kama amenawa mikono, akimaanisha amefikisha ujumbe. Akimalizia hotuba yake aliwataka Watanzania kudumisha amani nchini na kujiepusha na matendo yote yanayoweza kuvuruga amani hiyo. "Siku zote tumekuwa tukipokea wakimbizi wa nchi jirani, tusije nasi tukawa wakimbizi, fumbo mfumbie mjinga, mwerevu atambue". Sherehe hizo za Maulid zilihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Dk. Omar
Juma na viongozi wengine wa serikali.
|
Maoni yetu: Prof. Juma Kapuya, vipi Muislamu usijue agenda za Waislamu? Hatimaye Mzee Katambo, Chata waachiwa
Sheikh Bafadhil aitaka Bakwata iwe
mtetezi wa Waislamu
Makala: Uinjilisti wa Mbuni haufai
Mussa Katambo: Mzee aliyewekwa rumande kwa kuandaa mihadhara Makala: Elimu ya ngono yapenyezwa
tena Zanzibar
Arusha wasema: Hongera Mhe. KK kwa
kuwa mfano mwema
Wanawake Songea kuandaa maonesho
Kesi ya mgogoro wa Ardhi
AN-NUUR marufuku
gerezani?
Waislamu Karagwe wadai kusalishwa
na imamu asiyejua kutawadha
Ofisi mpya za Rabita
|