NASAHA
Na. 062 Jumatano  Agosti 23 - 29, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
KALAMU YA MWANDISHI

Mkijirekebisha mtakaribishwa

Na Maalim Bassaleh 

BIBLIA inasema, "Mjinga huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo." (Mithali 14:15).

Na Waarabu wa Yemen,ambao hapa Tanzania wanaitwa Washihiri, wana msemmo wao unaokaribiana sana kwa maana na methali hiyo. Wao wanamsema,"Ikiwa msemaji ana wazimu, msikilizaji huwa ana akili!" 

Kwa mwenye kuzingatia hataacha kugundua kuwa misemo yote hiyo miwili ina maana moja tu.. Yote inasema kuwa mtu asiamini kila analolisikia. Ni lazima kwanza ayafanyie utafiti yale yanayosemwa ajue ni ya kweli au ni ya uongo; kisha ndiyo aamue kuyakubali au kuyakataa.Asipofanya hivyo atakuwa hana tofauti na mjinga au punguani! 

Siku moja nilikuwa nimesimama sehemu fulani nikizungumza na mwenzangu mmoja. Akapita kijana mmoja wa Kihindi. Nilikuwa nikimfahamu siku nyingi. Aikuwa ni kijana mwenye kuipenda sana dini; lakini alikuwa ana tatizo la akili. 

Alipotuona, alitutolea salamu, kisha akamgeukia yule mwenzangu akamwuliza, "Habari za siku nyingi Sheikh? Mko wapi siku hizi, mbona huonekani?" Yule mwenzangu AKAMJIBU. "Habari nzuri; kwani huna habari? Siku hizi nimehamia mbinguni, sishuki isipokuwa siku za Alhamisi tu!" Kusikia hivyo yule kijana wa Kihindi ambaye ni mgonjwa wa akili aliangua kicheko, akacheka kwa sauti kubwa sana, kisha akauliza kwa kustaajabu, "Hizi ni habari kubwa! Hivyo siku hizi binadamu wanaishi mbinguni? Si ajabu hiyo?" 

Naam, kweli hiyo ni ajabu! Hakuna binadamu anayeweza kuishi huko. Juu ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, bado mwanadamu hajaweza kuifanya mbingu kuwa maskini yake.Ndiyo maana,hata yule mgonjwa wa akili aliona vigumu kuamini yale maneno ya mwenzangu, alipomwambia kuwa yeye siku hizi amehamia mbinguni. 

Lakini jambo la ajabu ni kuwa vipi chizi aweze kuchuja habari, akaelewa zipi za kweli, azikubali,na zipi za uongo, azikatae; wakati sisi wenye akili timamu, iwe rahisi, kwetu kukubali mambo tunayoyasikia hata bila ya kuyachunguza kwanza? 

Ninauliza hivyo kwa sababu hivi sasa, humu nchini, magazeti mengi yamejenga tabia ya kuandika habari bila ya kuzifanyia utafiti. Haiingii akilini kuwa magazeti hayo,yanafanya hivyo, kwa bahati mbaya. Lazima yawe yana lengo maalumu. 

Ili kuthibitisha maneno yangu haya, Gazeti moja, la kila wiki, katika toleo lake la wiki iliyopita, limekosoa baadhi ya magazeti kwa kuandika habari za matukio bila ya kuzihakikisha. Gazeti hilo limeyalaumu magazeti hayo kwa kuvurunda katika kuripoti zoezi la kura za maoni, la kugombania ubunge,kwa tiketi ya CCM. Limeandika kuwa kulikuwa na upotoshaji wa habari wa makusudi katika zoezi hilo zima. 

Kwa mujibu wa gazeti hilo, jinsi baadhi ya waandishi wa habari walivyokuwa wakiripoti juu ya kinyang'anyiro hicho cha kugombea nafasi za udiwani na ubunge, kupitia chama hicho,walikuwa wakionesha waziwazi kuwa walikuwa na wagombea wao maalumu waliokuwa wakiwashabikia. 

Jambo hilo ni la kweli.Halikuwa na kificho. Kila aliyekuwa akisoma magazeti alikuwa akiona jinsi waandishi walivyokuwa wakiwapigia debe baadhi ya wagombea; na kuwaponda wengine, japokuwa wagombea hao wote walikuwa kutoka chama kimoja! 

Lakini jambo linalosikitisha zaidi ni kuwa magazeti mengi yanaonekana yameamua kuvikandia vyama vya upinzani. Na wamekifanya chama cha wananchi CUF,kuwa ndiyo bunga yao! 

Magazeti mengi, ama yatanyamazia kabisa kuandika habari njema za CUF; au kama yakiamua kuandika juu ya chama hicho basi yatakipakazia au yatakitaja chama hicho kwa ubaya tu! Magazeti hayo yanaiona CUF haina heri yo yote. Kwao CUF ni chama cha wakorofi! Ni chama cha wahatarisha amani! Na eti ni chama chenye udini! 

Kwa mfano magazeti mawili,ya Kiswahili, yanayoto kakila siku,katika matoleo yake ya Jumapili, Agosti 20, 2000,yameandika maelezo ya kukilaumu chama hicho cha CUF,bila ya sababu yo yote ya msingi. 

Gazeti moja kati ya hayo mawili, katika safu yake ya maoni ya Mhariri, limeandika, "Kampeni zimeanza,CUF wachunge sera ya jino kwa jino." Mhariri wa gazeti hilo amedai kuwa watu wengi hawaielewi sera hiyo; ingawa amekiri kuwa viongozi wa chama hicho wamejitahidi sana kuieleza. Mhariri huyo ametahadharisha kuwa kama viongozi wa CUF hawataiacha sera hiyo,au hawataieleza ikaeleweka sawasawa,basi kama litatokea jambo lo lote baya,kutokana na utekelezaji wa sera,hiyo, CUF itabidi ibebe lawama! 

Kwa kuyasoma maelezo hayo kijuu juu tu,mtu anaweza kudhani kuwa mhariri wa gazeti hilo amekusudia kukisihi chama cha CUF kijiepushe na vitendo vya vurugu; lakini kwa mwenye kuzingatia barabara maelezo hayo hataacha kugundua unafiki uliomo ndani yake. 

Maoni hayo hayana maana yo yote, isipokuwa kukipakazia tu chama cha CUF kuwa ni chama kinachodhamiria kuleta fujo, kwa kuvunja sheria kwa makusudi, kwa hivyo Watanzania wawe na tahadhari nacho! 

Laiti kama kweli Mhariri huyo alikuwa ana nia ya kutaka kuonya vyama vya siasa visifanye vurugu katika uchaguzi mkuu ujao, basi angelikionya na chama tawala, cha CCM,ambacho nacho kimetangaza bayana kuwa kina sera ya shavu kwa shavu, mtu kwa mtu na kofi moja kwa makofi matatu! 

Isitoshe kama kweli Mhariri huyo alitaka kutoa nasaha basi anagelikinasihi na kikundi cha uhamasishaji cha CCM, TOT,kwa kusamba zakanda za nyimbo zinazowaponda wapinzani, na kuwahamasisha wana-CCM kuwachanachana na kuwatupa wapinzani hao. 

Viongozi wa CUF wamekwisha eleza,mara nyingi, kuwa sera ya chama chao ni UTAJIRISHO na HAKI SAWA KWA WOTE. Ama JINO KWA JINO na NGANGARI si sera, bali ni UJUMBE maalumu wa kuingilia katika uchaguzi mkuu ujao; ujumbe ambao utawahakikishia kuwa hawadhulumiwi wala hawaibiwi kura zao! 

Na lile gazeti la pili katika safu yake iitwayo, Asemavyo Mhariri limesema, "CUF ubabe kwa waandishi hausaidii." Mhariri wa gazeti hilo naye amekilaumu chama cha CUF kwa kuwadhibiti waandishi wa habari wanaokwenda kuripoti matukio katika hadhara za chama hicho. Amedai kuna waandishi wa habari waliopigwa na wafuasi wa chama hicho, kinachovuma kwa jina la NGANGARI . 

Mhariri wa gazeti hilo amemalizia maelezo yake kwa kusema kuwa kama chama cha CUF kinajihisi kuwa si chama cha kuwasaidia wananchi, basi kieleze wazi, kwani Watanzania wanataka kufahamu nini kinafanywa na kila chama ili wawe na fursa nzuri ya kuchagua siku itakapofika. Mhariri huyo akasisitiza ubabe hautasaidia kamwe historia inavyoonesha. 

Lakini Mhariri wa gazeti hilo amesahau kuwa ni gazeti lake hilo hilo, ndilo lililoandika taarifa za kupotosha kuvuruga mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa chama hicho, uliofanyika Kidongo Chekundu, Dares Salaam, Jumamosi, Agosti 19, 2000. 

Gazeti hilo,toleo lake la siku ya uzinduzi, lilieleza kuwa mkutano wa CUF ulifutwa na Tume ya uchaguzi na badala yake ungelifanyika siku ya Jumatatu Agosti 21, 2000, eti kwa kuwa siku ile ya Jumamosi, chama cha CCM,kilikuwa kinazindua kampeni zake katika viwanja vya Jangwani, kwa hivyo haiwezekani siku moja katika eneo moja ikafanyika mikutano miwili! 

Mbali ya gazeti hilo, gazeti jingine,linalotoka kila siku mchana, katika toleo lake la siku hiyo, lilitoa taarifa eti CUF ingalifanya mkutano wake Temeke Mwisho, badala ya Kidogo Chekundu. 

Na kwa kweli kama siku hiyo CUF isingekuwa ngangari uzinduzi huo usingelifanyika! Kama kuna watu waliokuwa hawaelewi ule ujumbe wa CUF NGANGARI SIKU HIYO WALITAMBUA! Wana-CUF walisema potelea mbali, liwalo na liwe,lakini mkutano wataufanya tu; na kweli waliufanya! Ama kweli CUF ni ngangari! 

Siku ya uzinduzi vyombo vingi vya habari vilionesha upendeleo wa dhahiri kwa chama cha CCM na kukikandia chama cha CUF. Kuna baadhi ya vituo vya televisheni vilionesha "Laivu" mkutano wa CCM; lakini hakuna hata kituo kimoja kilichofanya hivyo kwa chama cha CUF! Kwa nini? Au vituo hivyo, kwa siku hiyo, vilikodiwa na chama tawala? Na kama vilikodiwa ilibidi watueleweshe wananchi ili tusivituhumu vituo hivyo bure. 

Aidha, kuna kituo kimoja cha televisheni kilipokuwa kikionesha watu waliohudhuria mkutano wa CCM, Jangwani, kilielekeza kamera yake mbele ya msongomano wa watu ili ioneshe kuwa watu wengi sana walihudhuria mkutano huo; lakini walioonesha wale waliohudhuria mkutano wa CUF, Kidongo Chekundu, kilielekeza kamera yake, penye watu wachache, waliokuwa wakiingia katika mkutano huo. Walikuwa wakirejea rejea kuonyesha eneo hilo lililokuwa na watu wachache, kwa kulirudia mara kwa mara! Kwa nini walifanya hivyo? 

Isitoshe magazeti yote yaliyoripoti juu ya uzinduzi wa kampeni hizo katika kurasa zake za mbele yaliweka picha za watu waliohudhuria mkutano wa Jangwani; lakini hakuna hata gazeti moja la Kiswahili, kwa siku hiyo lililoonesha picha ya mkutano wa Kidongo Chekundu!Kwa nini iwe hivyo? 

Waandishi wa habari wa magazeti hayo walifika katika mkutano huo, na walipiga, picha. Lakini hawakuzitoa picha hizo katika magazeti yao! Au tuseme kwa vile CUF ni chama cha wakorofi basi picha za chama hicho huungua? Sasa wana-CUF wanapovinjari na kuwadhibiti waandishi wa habari wa namna hiyo magazeti yanakilaumu chama cha CUF, badala ya kuwauliza wale waandishi wa habari kulikoni? 

Sisemi kuwa hao wanaowafanyia hivyo waandishi wa habari wanafanya sawa, la hasha! Lakini ni waandishi hao wenyewe ndio wanaosababisha hali hiyo ya kutoelewana baina yao na wafuasi wa chama hicho cha CUF. Bila ya shaka yo yote, wakijirekebisha, watajikuta wakialikwa na kukaribishwa kuhudhuria hadhara za chama hicho. 

Niliwakuta watu wamekaa barazani wakijadili swali hilo la magazeti, mara kwa mara,kukilaumu chama cha CUF tu, mmoja katika watu hao akasema, "Hamwaoni watoto? Hupopoa mti wenye matunda tu!" Pale pale nikakumbuka maneno ya kigogo mmoja mkongwe wa CCM aliyesema kuwa yeye katika vyama vyote vya upinzani anakiogopea chama cha CUF tu! 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Kama hamtaki demokrasia, mnataka nini basi?

Prof. Lipumba ana uwezo wa kuongoza nchi - CCM

Kampeni za uchaguzi 2000, CCM yamalizia muda wake na kusema:
Imefanya kazi ya ‘kuipendeza’ Marekani

Vita dhidi ya rushwa ianzie kwa vigogo -Lipumba

Wakati umefika wanawake kushiriki siasa - Mugissa

TLP yadaiwa kuukejeri Uislamu

CUF Kigamboni kuzindua kampeni leo

USHAURI NASAHA
Nimechoka kuwa mtangazaji wa redio

MAKALA
Mungu na mataifa ya dunia

MAELEZO BINAFSI
Mjue mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Prof. Lipumba

MIPASHO NASAHA
Krosi matiplikesheni!

MAKALA
Wananchi kajiandikisheni kupiga kura ili kuleta mabadiliko ya serikali kwa njia ya amani

KALAMU YA MWANDISHI
Mkijirekebisha mtakaribishwa

Habari za Kimataifa

LISHE
Unakula au unaliwa?

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga, Mtibwa nani bingwa leo?
  • Ugomvi mkubwa baina ya Simba na Yanga waibuka 
  • Arsenal yaitandika Liverpool
  • Ngorongoro Heroes yaenda Msumbiji

  •  


    Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita