|
Na. 062 Jumatano Agosti 23 - 29, 2000 |
|
|
|
|
|
Mungu na mataifa ya dunia Na Mwinjilisti Kamara Kusupa MWANZO wa mada hii dini na siasa haviwezi kutenganishwa niligusia juu ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu kiujumla kwamba ni sawa na ujenzi ulioenda katika awamu tatu, awamu ya kwanza ilikuwa ni Mungu akishughulika na"individuals"yaani mtu mmoja mmoja,ndiyo maana tunaweza kukuta maneno ya Mungu yasemayo "Mimi ni Mungu wa Baba zako, Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka,na Mungu wa Yakobo." Zamani hizo Mungu alikuwa ni Mungu wa mtu mmoja mmoja,lakini baadaye Mungu akajidhihirisha kama Mungu anayehusika na taifa moja tu la Israeli na mwisho wa yote , Mungu amejihusisha na mataifa yote. Kwa ajili hiyo hakuna taifa lolote kati ya mataifa ya sasa ya dunia hii liwezalo kusema mimi kama taifa, huyu Mungu hanihusu kabisa kwa kuwa ninayo katiba na sheria zinazotawala nchi pamoja na viongozi wanaoongoza serikali. Taifa lolote lenye lugha inayofanana na hiyo basi hilo ni taifa lililoasi na dhambi ya taifa hilo yaani dhambi yake ya "uasi"italeta laana kwa wote waishio ndani ya taifa hilo pasipo kujali kwamba kuna baadhi ya wananchi wanaojiona watakatifu na wenye haki mbele za Mungu wa dini zao.Kama kuna watu wa jinsi hiyo wajue wazi kwamba wanaishi kwa haki ya kujihesabia wao wenyewe lakini si haki ya Mungu, maana kama wangekuwa wenye haki, basi wangehakikisha taifa lao linaenenda katika hofu ya Mungu kwa kukemea maovu ya Watawala na Wananchi katika ujumla wao, na pia kukemea maovu yatendwayo na taasisi. Najua wazi kwamba wapo viongozi wa dini wenye ujasiri na bidii ya kuwasakama walevi, wanzinzi, na vibaka tu walioko kwenye tabaka la "Walalahoi" lakini hawana ujasiri kabisa wa kugusa madhambi ya tabaka la watawala, wakihofia kwamba wasije kuonekana wanapinga watawala ama wanazungumzia siasa kwenye mimbari za dini. Matokeo yake ni kwamba tabaka la watawala linahesabiwa haki na viongozi wa dini (siyo na Mungu) na maovu yote yatendwayo kwenye eneo la siasa inabidi wayafumbie macho, na wajifanye hamnazo. Inabidi wafumbie macho umaskini wa taifa,umaskini wa walio wengi yaani "mass poverty" wafumbie macho kuanguka kwa huduma za jamii kwa kuwa wakiyagusa hayo moja kwa moja watakuwa wanagusa sera zilizoshindwa, ambazo zimetungwa na kutolewa na watawala siyo watawaliwa. Ikumbukwe kwamba siku zote yule anayetawaliwa hana nafasi ya kutunga sera bali anashiriki kwenye sera kwa njia ya kupiga kura ya kuzikubali ama kuzikataa. Huo uchaguzi wa sera huwa tu ni kwa nchi zile ambazo zimekomaa kwa maana zote za ukomavu bali katika nchi zingine ambazo zoezi la uchaguzi wengine wanalitumia kama daraja tu la kuvuka na kuyafikia madaraka, kwa kweli watu hawachagui sera wala hawapigi kura, badala yake wanapigishwa kura, alimradi tu kuwezesha nchi kupata viongozi. Vinginevyo kama kweli watu wangekuwa wanachagua sera, basi katika Tanzania watu wasingepigia kura sera zilizoshindwa, sera ambazo zimewafanya watoto kukosa madawati mashuleni na kukaa chini kama wafungwa au kukalia matofali na mawe hadi kupinda migongo wakati wa kuandika, sera zilizofanya wagonjwa wakose madawa mahospitalini, sera zilizosababisha wakulima wakose masoko ya mazao yao, na walalahoi kuishi kwa mlo mmoja kwa siku, tena mlo usio na virutubisho bali kujaza tumbo ili tu kutibu njaa kwa muda mfupi. Nitazungumzia kwa undani juu ya sera zilizoshindwa katika matoleo yajayo, kwa leo wacha niendelee na mada ya Mungu na Mataifa. Nia ni kujaribu kuonyesha kwamba wale wanaodai kwamba tusichanganye dini na siasa eti kwa kuwa YESU alisema "vya Mungu mpeni Mungu na vya Kaisari mpeni Kaisari, wanayatumia maandiko vibaya ili kuhalalisha tu madhambi ya watawala yatendwayo katika eneo la siasa kwa sababu rais wa sasa, na wa nchi yoyote ile ya dunia ya leo hafanani kabisa na Kaisari. Nasema tena Kaisari hafanani na sultani, wala mfalme, wala Waziri Mkuu ama kiongozi yeyote wa taifa la leo. Inapasa tupate picha Kaisari ni nani katika mpango wa Mungu katika kuuleta na kuueneza utawala wake hapa duniani. Baada ya Adamu kuasi, ambaye ndiye baba wa wanadamu wote, kuna mengi yalitokea, ikiwa ni pamoja na kufukuzwa Paradiso, na uzao wake wengine kuchomwa moto, wengine kuangamizwa kwa gharika, na mwisho Mungu kuichafua lugha ya wanadamu, na kuusambaratisha umoja wao, na ujamaa wao ambao ulikuwa unajengwa katika msingi mkuu wa kumwasi Mungu. Maandiko yanasema "Mungu akasema tazama watu hawa ni taifa moja na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya na tushuke huko tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao." Baada ya lugha kuchafuka watu wakatawanyika usoni pa nchi, na mahala pale pakaitwa "Babeli" maana yake machafuko, ama kwa lugha ya leo "confusion" yaani kuchanganyikiwa. Taifa lolote likikaliwa au (kupagawa) na roho ya Babeli lazima lisambaratike tu, na hiyo roho ya Babeli ndiyo inayosumbua nchi za Burundi, Rwanda na Somali. Nchi ya Somalia wote wanazungumza lugha moja ya Kisomali, na dini yao ni moja Islamu, lakini bado vyote hivyo lugha moja na dini moja havitoshi kuwafanya waishi kama ndugu moja ndani ya nchi moja badala yake hawaelewani wala hawasikilizani hiyo ni Babeli. Warundi na Wanyarwanda nao vivyo hivyo ni watu wanaozungumza lugha moja ya Kirundi na Kinyarwanda zaidi ya yote, wote ni Wakristo lakini hata hivyo Ukristo wao hauwaongozi kwenye umoja na maelewano badala yake wameweka pembeni Unyarwanda, Urundi na Ukristo na kuanza mapambano baina ya wenyewe kwa wenyewe, mapambano yasiyokuwa na mshindi hata wangeachiwa kuishi kwa miaka 200 ijayo. Hiyo ni Babeli yao. Baada ya utawanyiko ili Mungu aweze kushughulika na mataifa yote, na kuueneza ufalme wake katika Ulimwengu wote ilibidi kwanza dunia nzima itawaliwe na mtawala mmoja, kisha kuweko na lugha moja inayoeleweka (inayozungumzwa) Ulimwengu mzima ili pasiwepo na kipingamizi cha lugha wakati Mungu anawatuma watumishi wake kunena habari njema za ufalme wake. Hapa ndipo tunapouona umuhimu wa wafalme kama akina Nebukadneza wa Babeli, Dario Mmedi wa Uajemi, Iskanda Mkuu wa Uyunani ama "Alexandar the great" na Kaisari wa Rumi. Aliyefungua dimba katika kuukamilisha huu mpango wa Mungu alikuwa ni mfalme Nebukadneza wa Babeli. Nabii Yeremia alitabiri kwamba Bwana Mungu asema hivi "Mimi nimeiumba dunia hii wanadamu na wanyama walio juu ya uso wa nchi kwa uweza wangu mkuu, na kwa mkono wangu ulioonyooka, nami nawapa watu kama inipendezavyo. Na sasa nimetia nchi hizi zote katika mkono wa Nebukadneza, mfalme wa Babeli mtumishi wangu, na wanyama wa mwituni pia nimempa wamtumikie. Na mataifa yote watamtumikia yeye na mwanawe, na mwana wa mwanawe, hata utakapowadia wakati wa nchi yake mwenyewe ndipo mataifa mengine na wafalme wakuu watamtumikisha yeye. Na itakuwa taifa lile na mfalme yule asiyetaka kumtumikia Nebukadneza huyo mfalme wa Babeli, na kutia shingo zao katika nira ya mfalme wa Babeli, mimi nitaliadhibu taifa lile kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, asema Bwana hata nitakapo kuwa nimewaangamiza kabisa kwa mkono wake." Ulikuwa ni mpango wa Mungu kwamba duni yote itawaliwe na mtawala mmoja Nebukadneza hata kama mataifa mengine hayakuwa radhi kutawaliwa. Hii maana yake ni kwamba dola zingine za dunia ya wakati huo ilibi zife, Muuaji wa dola hizo akiwa ni Mungu mwenyewe kwa ajili ya kuukamilisha mpango wake kwa mataifa yote ya dunia. Baadhi ya viongozi wa dini ya Kiyahudi na wasomi wa torati walimshangaa Yeremia anapotamka Neno Nebukadneza mtumishi wangu kwani kwa wakati huo mfalme Nebukadneza alikuwa hamjui Mungu wa Israeli bali alikuwa na Miungu yake ya dini za Kibabeli. Sasa inakuwaje Mungu amwite Nebukadneza mtumishi wangu? Ni kwanini Mungu hakumwita mfalme wa Israeli mtumishi wangu wakati Israeli ndiyo iliyokuwa na agano na Mungu? Jibu lake ni kwamba chini ya mpango huu wa Mungu kujihusisha na mataifa yote, taifa la Israeli halikuwa chombo sahihi cha kutekeleza matakwa ya Mungu kwani Israeli yenyewe kwa wakati huo ili kuwa ni dola nyonge na isiyoweza kutawala dunia nzima. Kwa hiyo wale watu wa enzi zetu wanaodhani wanaweza kuwa watumishi wa Mungu kwa sababu tu ya maandiko au imani katika "doctrine" zao wanajidanganya. Mungu hawezi kufugwa kama ng'ombe kwenye zizi la dini zao badala yake Mungu anaweza kujipatia watumishi nje ya fahamu za wanadamu, nje ya mazoea yao, nje ya taratibu zao, na nje ya madhehebu yao alimradi tu watu hao wanao uwezo wa kuyatimiza mapenzi yake. Hatimaye Unabii wa Yeremia ulitimia, na Nebukadneza akawa mtawala wa dunia yote ya wakati huo, hata hivyo kwa kuwa Nebukadneza alikuwa hamjui Mungu, Mungu alimshikisha adabu kwa vipigo na magumu yasiyo mithilika, ikiwa ni pamoja na kuadhibiwa kwa kupoteza fahamu za kibinaadamu na kwenda kuishi porini akila nyasi pamoja na wanyama wa mwituni, hadi alipotubu na kusema "sasa najua ya kwamba wewe uliye juu ndiye unayetawala". Siku moja akaota ndoto ambayo waganga na wachawi, na wanajimu na wenye hekima wa Babeli hawakuweza kumtafsiria hadi alipopatikana Nabii Danieli ambaye alimweleza wazi kwamba ndoto yake ni ufunuo wa Mungu wa mbinguni, na kwa hiyo wanadamu hawawezi kumfasiria, na ndoto yenyewe ilikuwa hii Nebukadneza aliona sanamu kubwa inayotoa mwangaza, kichwa chake ni cha dhahabu tupu, kifua chake ni cha shaba, na miguu yake ni ya chuma na vidole vyake ni mchanganyiko nusu chuma, na nusu udongo, kisha jiwe lisilo chongwa kwa mkono wa binadamu liliporomoko toka mlimani likaiangukia sanamu na kuiponda ponda kisibakie hata kipande,baadaye jiwe lile lilikuwa na kuenea hadi kuijaza dunia yote. Na tafsiri yake ndiyo hii, kuna falme nne zitakuja kutawala dunia, kile kichwa cha dhahabu ni ufalme wa kwanza ambao ni ufalme wake yeye Nebukadneza. Na ufalme wa pili ambao ulikuja baada yake, ulikuwa ni wa Umedi na Uajemi, baada ya hapo ukaja ufalme wenye nguvu wa Alexanda Mkuu wa Uyunani ambaye alifananishwa na shaba, baadaye ukaja ufalme wa Mrumi chini ya Kaisari, ambao ulifananishwa na chuma. Tawala zote hizi zilikuwa zimeidhinishwa na Mungu kwa ajili ya kukamilisha mpango wake. Tawala hizi zilikuwa na sera ambazo zilitimizza mapenzi ya Mungu ingawaje wao watawalahawakuwa wanajua.Kwa mfano Iskandamkuu alitawalaakiwa na umri wa miaka 20 tu na tamaa yake ilikuwa dunia moja ,lugha moja ,na utamaduni mmoja wa kabila lake la Kigiriki. Iskanda alipigana na kuteka dola zingine za dunia na hatimaye ndoto yake ikatimia akashinda wafalme wote wa wakati wake na siku alipokosa ufalme wa kupigana nao, alilia kwa uchungu. Kwa miaka mingi dunia ikatawaliwa na Wayunani ambao walofanikiwa kueneza lugha yao na utamaduni wao kiasi kwamba Kiyunani ikawa lugha ya dunia na pia lugha ya kimataifa. Baada ya utawala wa Wayunani ukaja utawala wa Warumi ambao kwenye maono ya Nabii Danieli ulifananishwa na chuma. Utawala huu nao, ulikuwa na sera yake iliyojulikana kama Pax Romana yaani amani ya Kirumi. Kutokana na nguvu za kijeshi na za kiuchumi Rumi ilifanikiwa kuleta amani dunia yote ya wakati huo, pia Warumi walikazania ama walihusudu sana maendeleo waliweka mkazo kwenye ujenzi wa barabara ili kurahisisha mawasiliano kati ya Makoloni yake yote na mji mkuu wa Rumi, na pia ujenzi wa majumba ya fahari. Sasa mambo hayo yakitazamwa kwa jicho la mwili, inaonekana kama historia tu ya ufalme huu ukipita na mwingine kuingia. Lakini yakitizamwa kwa jicho la rohoni inaonekana wazi kwamba falme zote nne zilifanya kazi ya kuandaa mazingira ya utawala wa Masihia ufalme wa Mungu ambao katika maono ya Nabii Danieli ulifananishwa na jiwe kutoka mlimani lisilofanywa kwa mkono wa binaadamu. Kwa ajili hiyo YESU kama mtumishi wa Mungu aliyeyajua vyema mapenzi ya Mungu kutawaliwa na makafiri yasiyokuwa na agano na Mungu, sawa kabisa na kasumba ile ile iliyomkataa Nebukadneza kwamba ni mtumishi wa Mungu. Mrumi alikuwa anatoza kodi makoloni yake yote kwa ajili ya kuleta maendeleo, kwa hiyo basi wale walioleta hoja ya kwamba je, ni halali kumpa kodi Kaisari, walikuwa wanaohiji haujulikani vichwani mwao. Yesu asingeweza kushawishi watu waache (wagome) kumlipa Kaisari kodi wakati anajua wazi kwamba sera ya Kaisari ya Pax Romana pamoja na sera yao ya maendeleo ni vitu vinavyokubalika katika mpango wa Mungu. Ndiyo maana akasema vya Mungu mpeni Mungu, na vya Kaisari mpeni Kaisari. Wakati habari njema za uflame wa Mungu zinaenezwa Ulimwenguni kote, watumishi wa Mungu walitumia njia za mawasiliano zilizotengenezwa kwa kodi ya Kaisari. Wakati wahubiri wanasambaa mataifa yote walifanya kazi yao kwa amani. Kwa sababu ya hiyo sera ya amani ya Kirumi. Hakuna awezaye kuhubiri neno la Mungu katikati ya vita, ingekuwa hivyo mbona wahubiri hawapeleki Injili ya ndugu kumpenda ndugu huko Rwanda ili Watusi wakawapenda wahutu na Wahutu wakawapenda Watusi? Kwa habari ya lugha bado Wahubiri wa habari njema waliitumia lugha ya Kiyunani kama kifaa muhimu kwa mawasiliano, sera ya Iskanda ilinufaisha dunia. Sasa hao wanaopiga debe kwa ajili ya chama tawala waeleze ni sera gani zilizokubaliwa na Mungu hadi watawala wetu wafananishwa na KAISARI? Kaisari hakutawala kwa sera zilizoshindwa. |
YALIYOMO
TAHARIRI
Prof. Lipumba ana uwezo wa kuongoza nchi - CCM Kampeni
za uchaguzi 2000, CCM yamalizia muda wake na kusema:
Vita dhidi ya rushwa ianzie kwa vigogo -Lipumba Wakati umefika wanawake kushiriki siasa - Mugissa CUF Kigamboni kuzindua kampeni leo USHAURI NASAHA
MAKALA
MAELEZO BINAFSI
MIPASHO NASAHA
MAKALA
KALAMU YA MWANDISHI
LISHE
|
|
|
|
|