|
Na. 062 Jumatano Agosti 23 - 29, 2000 |
|
|
|
|
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekiri kwamba Profesa Ibrahim Haruna Lipumba ni kiongozi makini kwa kuwa siku zote huzungumza mambo ya msingi yanayolenga kuboresha maisha ya wananchi. Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa Kamati ya kampeni ya CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao Kanali Abdulrahmani Kinana mbele ya halaiki ya waandishi wa habari katika ukumbi wa habari MAELEZO jijini. Kanali Kinana alitoa maelezo hayo kufuatia swali aliloulizwa na mmoja wa waandishi kwamba kwanini CCM imekuwa ikitumia muda wake mwingi kujibu shutuma za Profesa Lipumba juu ya hali mbaya ya kiuchumi nchini na sio hoja za mpinzani mwingine yeyote. Swali hilo liliulizwa baada ya Kanali Kinana, Waziri wa Ulinzi wa zamani katika serikali ya Awamu ya Pili kutoa takwimu kuonesha serikali ya CCM ilivyo na itakavyoboresha sekta ya elimu na afya. "Tutaendelea (CCM) kumjibu Profesa Lipumba na CUF kwa kadri itakavyowezekana kwa kuwa anatoa hoja za msingi. "Na kamwe hatuwezi kufanya kazi ya kumjibu kiongozi yeyote tu wakati anazungumza mambo ambayo hayana maslahi kwa wananchi na taifa", alisema Kanali Kinana. Profesa Lipumba mgombea wa urais kwa tiketi ya CUF-CHADEMA katika hotuba zake amekuwa akiishutumu serikali ya CCM kwa kutokuwa na huruma na wananchi wake kwa kuwa katika kipindi cha miaka 40 imeshindwa kuondoa umaskini, ujinga na maradhi. Lipumba amekuwa akitoa mifano kwamba wakati viongozi wa serikali ya CCM wanapeleka watoto wao kusoma Ulaya na Marekani, na wengi wao kwenda kutibiwa nje ya nchi na familia zao,sehemu kubwa ya wananchi wamekuwa wakikosa matibabu na watoto wao kusoma katika mazingira magumu au kukosa elimu kabisa. Pia Profesa Lipumba amekuwa akitoa shutumu nzito dhidi ya serikali ya CCM kuhusu matumizi mabaya ya fedha za wananchi ambazo hazijajibiwa. Miongoni mwa shutuma hizo ni pamoja na matumizi ya mabilioni ya shilingi kukarabati ikulu,ukarabati ambao alidai kuwa hauishi.Akihutubia mkutano wa kampeni Jumapili iliyopita mjini Dodoma, Rais Mkapa alisema endapo atachaguliwa tena kuongoza nchi atahamia Dodoma kwa muda wa miezi sita ili kutoa nafasi kwa Ikulu ya Dar-es-Salaam kufanyiwa ukarabati zaidi. Wakati huo huo katika hali inayodhaniwa kuwa ni mbinu za Chama Cha Mapinduzi kuwarubuni waandishi wa habari nchini juzi chama hicho kiligawa vifaa kadhaa kwa wanahabari hao. Vifaa hivyo ni pamoja na fulana na beji zenye picha ya Rais Mkapa, pamoja na skafu zenye rangi ya njano na kijani na pia ilani ya uchaguzi ya chama hicho. Vifaa hivyo ambavyo vililetwa ukumbini hapo na
Kinana vilisusiwa na baadhi ya waandishi kwa madai kwamba ni sehemu ya
rushwa ya CCM kwa wanahabari ili wakiandike vizuri chama hicho.
Imefanya kazi ya 'kuipendeza' Marekani
KAULI ya mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Benjamin Mkapa, kwamba ziara ya Rais Bill Clinton wa Marekani ni dalili kuwa serikali ya CCM imefanya kazi nzuri, imedaiwa kuwasikitisha wananchi wengi kwa maelezo kuwa 'kumbe Marekani imekuwa ikifurahishwa na kero, taabu na usumbufu wa kijamii na kisiasa mambo ambayo yamekuwa yakiwazonga Watanzania. Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa kampeni za CCM mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, Rais Mkapa alisema, "Mkisikia hata Rais Clinton wa Marekani anakuja Tanzania, mjue tumefanya kazi kweli". Wananchi walioongea na gazeti hili kufuatia kauli hiyo ya mgombea huyo wa CCM wamesema ni jambo la kusikitisha kuona Marekani imekuwa ikifurahia madhila yanayowafika Watanzania yakiwemo mauaji ya raia, matumizi ya nguvu za dola dhidi ya raia, ukosefu wa nafasi za masomo kwa watoto wa wananchi wa kawaida na hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi kiasi cha baadhi yao kujiua. Wananchi hao wameyataja madhila zaidi ambayo wamedai yanawakabili Watanzania chini ya utawala na serikali ya CCM kuwa ni kukithiri kwa rushwa, uuzaji holela wa mashirika ya umma, ukwepaji kodi unaofanywa na wafanyabiashara wakubwa na makampuni binafsi, na ufinyu wa demokrasia. "Katika utawala huu wa (Rais) Mkapa watu wameuawa pale Mwembechai.... Ndugu zetu wamepigwa risasi na kuuawa kwa sababu ya dini yao, na serikali imeridhika asilimia mia moja", alisema Hamid Majaliwa na akaongeza kwa kushangaa, "kumbe mauaji ya Waislamu ndiyo yenye kumpendeza Rais wa Marekani". Akizungunza na mwandishi wa habri hizi katika Viwanja vya Jangwani mara baada ya kumalizika mkutano wa uzinduzi wa kampeni ya CCM, Agosti 19, mwaka huu, Bw. Hamid alisema huko Mwanza Sheikh mmoja, Bw.Ilunga Kapungu, amenusurika kufa baada ya kushambuliwa kwa mapanga hivi karibuni na watu wasiojulikana lakini, amedai mzungumzaji huyo, jeshi la polisi limekataa kufanya uchunguzi wa tukio hilo. "Wakishambuliwa na wakiuawa Waislamu serikali haishituki, utadhani waliouawa ni 'mbwa koko' wanaoleta kero mtaani", alisema Bw. Hamid huku akifuta machozi. Mwananchi mwingine, aliyefahamika kwa jina moja tu la Anestory alisema ameshituka kusikia Marekani inanasibishwa na rekodi ya utawala wa CCM ambapo alidai, huko Bulyankulu Geita, wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu waliuawa kwa kufukiwa, na wananchi wengine kuripotiwa kuuwawa kwenye hifadhi ya wanyama Ngorongoro. Akitoa maoni yake juu ya kauli hiyo ya Rais Mkapa, Bw. David Mussa, mfanyabiashara wa Kariakoo, amesema jeshi la Polisi limekuwa na rekodi "ya kuwanyanyasa raia." "Mara kadhaa Mrema anataka kufanya mkutano yake (lakini)Polisi wanamwekea ngumu, na nimesikia Prof. Lipumba naye alizuiliwa asifanye mkutano huko Kigoma, na jana (Jumamosi) polisi wamewapiga mabomu (ya machozi) watu waliokuwa wakienda kwenye mkutano wa CUF", alisema Bw.David. Akichambua matumizi mabaya ya jeshi la polisi dhidi ya raia katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wa Rais Mkapa, mwananchi mmoja ambaye jina lake halikufahamika alidai uonevu ule ni miongoni mwa mambo yaliyoifurahisha serikali ya Marekani. "Ulipotokea mlipuko katika ubalozi wao (Marekani), polisi walianza kamata kamata ya ajabu sana, Waislamu wengi wenye ndevu walitiwa msukosuko sana.... Kumbe hayo yalimfurahisha Clinton?" alishangaa mwananchi huyo. Aidha, wananchi hao wamedai kuwa kauli hiyo ya Rais Mkapa ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM inaonesha kuwa Marekani inayafutilia masuala ya kisiasa ya Tanzania na inaelekeza ni nchi iendeshwe vipi. "Clinton anafuatilia siasa zetu, ndio maana Balozi wake (hapa nchini) aliingilia siasa za Zanzibar... unakumbuka alipotaja ni mwana-CCM gani anafaa kuitawala Zazibar", alisema Bw. Mhagama ambaye alijigamba ni muuzaji maarufu wa magazeti katikati ya jiji. Mwananchi mwingime, Bw.Hussein Msoma, alidai mbali na hivyo, inawezekana Balozi huyo wa Marekani akafumbia macho mfumo wa serikali unaotoa upendeleo kwa Wakristo. "Mimi nina wasiwasi sana, Balozi wao (Marekani) hapa kwetu ni Padri, na hapa Tanzania kuna mfumo Kristo", alisema Bw. Msoma ambaye alidai hivi sasa unaejiajiri mwenyewe baada ya "kung'olewa" kutoka katika NGO inayohusika na usambazaji wa misaada kwa waliokumbwa na maafa. ".....ikiwa mwakilishi wao ni Padri, kwa vyovyote vile taarifa zake kwa Rais wake (Clinton) hazitaueleza ukweli huu", alidai Bw. Msoma. Balozi wa Marekani nchi ni Mchungaji Charles Stith. Wananchi hao pia wamedai kuwa uhusiano uliopo kati ya nchi mbili hizi ni kama vile Tanzania ni koloni la Marekani. "Kwa nini tuoneshe kusherehekea kusifiwa na wao (Marekani) kama vile wao ni watawala wetu?", alihamaki mwananchi mmoja. Wananchi zaidi waliozungumza na gazeti hili kufuata uzinduzi wa kampeni za CCM wamesema wameshangazwa na majigambo ya Mhe. Mkapa kwamba katika kipindi chake cha miaka mitano amepata mafanikio makubwa ambayo vyama vya upinzani kwa sera zao haviwezi. "Alipochukua madaraka mwaka 1995, aliahidi kutokomeza kero ya rushwa, leo anamaliza miaka yake mitano rushwa imekithiri katika kila ngazi ya chama chake..... rushwa katika udiwani, rushwa katika ubunge", alisema mwananchi mmoja na kuongeza: "lau kama CCM wasingeshituka mapema kuwazuia watu wengine wasijitokeze kuomba kugombea urais wa Jamhuri basi rushwa ingetawala hata katika uteuzi wa mgombea urais. "Serikali hii ya CCM haiko makini kwa rushwa.... Mwana-CCM kashikwa Shinyanga kwa rushwa, badala ya kumkabidhi kwa PCB, wamempeleka Namibia. "hata hao wana-CCM walioenguliwa na wengine kupigwa marufuku wasigombee eti kwa sababu wametajwa kuhusika na rushwa, hao ni wachache tu ambao CCM imewatoa kafara..... CCM imeoza kwa rushwa", alidai mwananchi huyo aliyejitaja kwa jina moja tu la Mmari. Bw. Allan Sichone, mfanyabisha anayesafiri kati ya Mwanza na Dar es Salaam amedai serikali ya Rais Mkapa inaondoka madarakani ikiwa na kashfa kubwa ya kuuza benki ya wananchi ya NBC (1997) "Leo hii Tanzania hakuna benki ya biashara ambayo wafanyabiashara wazalendo tunaweza kukimbilia kupata mkopo na huduma zingine", alisema Bw. Sichone na kuongeza: "walichotakiwa kufanya ni kuwakamata wote walioifilisi NBC, wadeni sugu ambao wote wanafahamika." Wananchi hao pia wamesema ingawa RaisMkapa alipoingia madarakani aliahidi kuimarisha ukusanyaji kodi baada ya kuundwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), zipo taarifa za ukwepaji kodi miongoni mwa wafanya biashara binafsi. Kwa mujibu wa wananchi hao, taarifa hizo zimedai kuwa Shirika la Fedha Duniani limesema atika taarifa yake kuwa baadhi ya makampuni ya mafuta ya petroli yamekwepa kulipa kodiya zaidi ya shilingi bilioni 45. Baada ya kuondolewa kwa ukiritimba uliokuwa limepewa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) wakuagiza mafuta toka nje ya nchi, makampuni kadhaa ya mafuta, ikiwemo TIOT na mengineyo yamefungua shughuli zao hapa nchini. Akizidi kushangaa 'mafanikio' ya CCM katika miaka mitano iliyopita, mwananchi mmoja alihoji: "hakuwahi kutokea katika historia ya nchi yetu Watanzania kufa kwa njaa, lakini katika awamu hii ya tatu, watu zaidi ya 40 wamekufa kwa njaa huko Ulanga." Mwananchi huyo, Bi. Asia Waziri wa Magomeni ambaye alidai kuwa ni mwenyeji wa Singida aliendelea kudai kuwa watoto wengi wamekuwa wakikosa nafasi za kuandikishwa darasa la kwanza. "Siku si nyingi ndugu Mwandishi Tanzania itakuwa nchi ya (watu) wajinga", aliitahadharisha Bi. Asia. "Labda wanachojivunia kuwa ni mafanikio", aliendelea mama huyo, "ni jinsi vigogo wanavyoshindana kuwapeleka watoto wao kusoma Marekani". ".....Na wao wenyewe wakiugua, japo kujipele tu, wanakwenda kutibiwa Uingereza, wakati sisi hapa hata gloves kwa ajili ya mjamzito kujifungua hazipo hospitalini", alilalamika Bw. Asia ambaye alidai aliwahi kufanya kazi ya uuguzi katika miaka ya 1980. Wakiendelea 'kuponda' mafanikio ya CCM wamedai serikali ya CCM imewatia wananchi umaskini mkubwa kiasi cha Watanzania wengi kushindwa kumudu hali ya maisha na kupelekea kuongezeka kwa watoto wa mitaani. "Hali ya majumbani (familia) ni mbaya, siku nzima mlo mmoja tu au siku inapita kapa, watoto wanakimbilia mitaani kuwa 'machokoraa', wazazi wengine wanajitia kitanzi (wanajiua kwa kujinyonga)" alisema mwananchi mmoja. Rais Clinton wa Mzarekani anatarajiwa kuwasili
nchini Agosti 2, mwaka huu.
NA Mwandishi Wetu VITA dhidi ya rushwa ambayo ni moja ya kero zinazoonekana kukithiri hapa nchini haitaleta ushindi wowote iwapo vigogo waliomo serikalini na katika chama tawala ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa hawatashughulikiwa, imeelezwa jijini mwishoni mwa wiki. Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Wananchi (CUF) na Cahama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya vyama hivyo, Prof. Ibrahimu Lipumba amesema vita dhidi ya rushwa inayoongozwa na CCM na serikali yake haielekei kuleta ushindi wowote. Amesema vita dhidi ya rushwa nchini haijaanza, na akaifananisha hali ya rushwa nchini na ugonjwa hatari wa saratani, kwa vile wapo viongozi wa chama tawala, CCM, ambao wamekuwa wakijihusisha katika vitendo hivyo vichafu. Saratani au kansa ni ugonjwa ambao iwapo hautagundulika na kudhibitiwa mapema una kawaida ya kusambaa mwili mzima hatua ambayo ikifikiwa mgonjwa huwa hana tiba tena zaidi ya kusubiri kifo! Prof. Lipumba aliendelea kueleza kuwa iwapo atachaguliwa kuwa rais wa Jamhuri, serikali atakayoiunda itahakikisha inaanza kuwashughulikia wala rushwa vigogo ambazo amewaita 'sangara' badala ya kuhangaika na wala rushwa wadogo wadogo aliowaita 'dagaa' ambao ndio wanaoshughulikiwa na serikali ya CCM iliyopo madarakani. Sangara ni samaki wakubwa sana ikilinganishwa na dagaa. Wakati anaingia madarakani mwaka 1995, Rais Benjamin Mkapa aliahidi kupambana kikamilifu na kero ya rushwa. Hata hivyo, miaka mitano baadaye kero ya rushwa si tu imeongezeka bali pia imekithiri kwa kupenya katika sekta na kwa viongozi wa ngazi mbalimbali serikalini na katika chama tawala, wamedai wananchi hao. Miezi michache iliyopita ilipotolewa taarifa ya rushwa katika nchi za Afrika, Tanzania ilitajwa kuwa ni moja ya nchi tatu zinazoongoza kwa rushwa katika bara hili. Taarifa zingine zilizowahi kuvuma jijini Dar es Salaam zilidai kuwa ujumbe wa Tanzania uliohudhuriwa mkutano wa wawekezaji uliofanyika Afrika ya Kusini mwakahuu ulilalamikiwa kwamba Tanzania ilikuwa 'inanuka rushwa' hali ambayo ilileta usumbugu mkubwa kwa wawekezaji wengi kutoka nje. Ujumbe huo wa Tanzania uliongozwa na Rais Mkapa. Akitaja moja ya mikakati wa kuhakikisha vigogo waliohusika na rushwa wanawajibishwa, mgombea urais huyo kwa tiketi za CUF na CHADEMA alisema akipata urais, Serikali yake itaiangalia upya mikataba yote ambayo serikali ya CCM imeingia na makampuni makubwa ya madini. "Iwapo itabainika kuwa ilihusisha rushwa maofisa waliohusika watafikishwa mahakamani" alisema Profesa Lipumba. Katika zoezi la upigaji wa kura za maoni kupendekeza wana-CCM watakaowania udiwani na ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka, taarifa za kutumika kwa rushwa zilipatikana kutoka karibu kila kata na kila jimbo la ubunge. Taarifa hizo ambazo vikao vya Kamati Kuu ya CCM na baadaye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM vilizifanyia kazi na kuridhika nazo, zilipelekea NEC-CCM kutengua baadhi ya matokeo ya kura za maoni na pia iliwapiga marufuku baadhi ya wanachama wake kugombea tena nafasi hizo. Prof. Lipumba ambaye aliongea katika viwanja vya Kidongo Chekundu jijini, aliwatahadharisha Watanzania kwamba wale wote wanaopata uongozi kwa kutoa rushwa hawawezi kuipiga vita ya kweli rushwa. Mbali na vita dhidi ya rushwa, Prof. Lipumba aliwaambia maelfu ya wananchi waliofurika katika viwanja hivyo, kwamba pia serikali yake itauangalia upya mfumo wa kodi nchini kwa lengo la kuzifuta kodi zenye kuwadhalilisha wananchi. Prof. Lipumba aliitaja kodi ya maendeleo kuwa ni miongoni mwa kodi zenye kuwadhalilisha wananchi na hivyo itafutwa. Katika ziara yake katika mikoa ya Kusini hivi karibuni, Prof. Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF Taifa, alisema ameelezwa na wakazi wa huko kuwa katika baadhi ya maeneo wananchi wanaoshindwa kulipa kodi ya maendeleo huchapwa viboko. Akiendelea kueleza 'uhalali' wa kuifuta kodi hiyo ambayo wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kutoona matunda yake, Prof. Lipumba ambaye kitaaluma ni mchumi alisema mapato yatokanayo na kodi ya maendeleo ni sawa na asilimia nne tu ya mapato yote ya kodi nchini, hivyo kufutwa kwake hakutayumbisha kitu. Alisema kodi ya maendeleo inachangia kiasi cha shilingi bilioni 25. Mgombea Urais huyo wa Jamhuri ya Muungano aliongeza kusema kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na jumla ya shilingi bilioni 45 ambazo zimeripotiwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuwa ni kodi ambayo makampuni ya petroli yalikwepa kulipa. Akizidi kuchambua uonevu unaofanywa na serikali ya CCM dhidi ya wananchi, Prof. Lipumba alisema serikali hiyo imekuwa ikiwadhulumu wakulima wa kahawa nchi kwa kuwalipa bei ndogo zaidi kuliko nchi nyingine yoyote inayozalisha kahawa duniani Aidha, amesema serikali ya CCM imewanyima wakulima hao uhuru wa kuuza kahawa yao sehemu zingine ambazo wangeweza kupata bei nzuri, na hivyo kuongeza kipato kuweza kukabilianana hali ngumu ya maisha inayowakabili mamilioni ya Watanzania. Akiushangaa uonevuhuo wa serikaliya CCMProf.Lipumba alitangazi", wakulima wa kahawa wameikosea nini serikali?" Akizungumzia mwelekeo mbovu wa sera za CCM kiuchumi, Prof. Lipumba alilaumu teankuuzwa kwa iliyokuwa benki kubwa yaBiashara nchini NBC (1997)Ltd. Alisema katika kuhakikisha serikali inakuwa na uwezo wa kuwasaidia vizuri wafanyabiashara wazalendo, nchi yoyote huwa inayo benki ya biashara inayomilikiwa na nchi yenyewe. Akizungumza katika mkutano huohuo, Bw. Seif Shariff Hamad, ambaye anagombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi za vyama vya CUF na CHADEMA, alisema amani na utulivu haviwezi kupatikana mahali popote palipo na dhuluma. Kwa muda mrefu viongozi wa serikali ya CCM wamekuwa wakihubiri kuwa chama chao ndicho pekee kinachoweza kudumisha amani na utulivu. Hata hivyo madai hayo ya CCM yamekuwa yakipingwa na wapinzani kwa maelezo kuwa utulivu ulioopo nchini unatokana hulka ya Watanzania wenyewe na wala sio juhudi ya CCM. |
YALIYOMO
TAHARIRI
Prof. Lipumba ana uwezo wa kuongoza nchi - CCM Kampeni
za uchaguzi 2000, CCM yamalizia muda wake na kusema:
Vita dhidi ya rushwa ianzie kwa vigogo -Lipumba Wakati umefika wanawake kushiriki siasa - Mugissa CUF Kigamboni kuzindua kampeni leo USHAURI NASAHA
MAKALA
MAELEZO BINAFSI
MIPASHO NASAHA
MAKALA
KALAMU YA MWANDISHI
LISHE
|
|
|
|
|