|
Na. 060 Jumatano Agosti 9 - 15, 2000 |
|
|
|
|
|
Baada ya kuitumia kuigaragaza
Simba:
RAOUL Piere Shungu, kocha mkuu wa klabu ya Yanga ya Dares Salaam amesema, siri kubwa ya ushindi wa timu yake dhidi ya Simba ya jijini mwishoni mwa wiki ni kutokana na wachezaji wake kuwa ngangari katika mchezo huo. Amesema, katika mchezo huo, wanandinga wake walicheza kwa kutumia nguvu, akili na maarifa katika kupachika mabao na kulinda lango lao. "Ukweli hayo ndiyo yametusaidia kupata ushindi dhidi ya Simba na kitu kingine ni kucheza kitimu labda na stamina ya hali ya juu waliyokuwa nayo basi", ameongeza. Shungu amekiri kuwa wachezaji wakiwa ngangari kiakili, kiafya na kisaikolojia, wanaweza kushinda mechi yoyote na hivyo akahakikisha kuitumia mpaka atakapochukua ubingwa wa Tanzania bara na Muungano. Katika mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa Taifa Jumamosi iliyopita, Yanga ilishinda kwa mabao mawili dhidi ya sifuri ya Simba. Aidha, Shungu amedai kushawishiwa na wanachama kadhaa wa Yanga wakimtaka ajaze fomu ya kuomba uanachama wa daraja la kwanza katika klabu hiyo. Kwa mujibu wa katiba mpya ya Yanga mwanachama wa daraja la kwanza anatakiwa kulipa ada ya shilingi laki mbili kwa mwaka na hivyo kuingia moja kwa moja katika Baraza Senete. Shungu ambaye ni Raia wa Congo Kinshasa amekubali ombi la kumtaka awe mwanachama wa Yanga na amedai hivi karibuni atawasilisha ombi lake hilo kwa wanachama kupitia viongozi wa klabu. "Kwa kweli sasa nimekubali kuwa mwanachama wa
Yanga kwa vile ninayo mapenzi na Yanga toka nikiwa nyumbani Congo na siku
si nyingi nitawaambia viongozi wangu", amedai.
Manga azikwa Moro Na. Mwandishi wetu
ALIYEKUWA mchezaji maarufu wa timu ya Taifa miaka ya sabini, Kassim Khamis Salum Mlapakoro, maarufu Manga (51) amefariki Jumamosi iliyopita Jijini na kuzikwa Jumapili mkoani Morogoro, ndugu wa marehemu wamelifahamisha Nasaha. Manga alifariki katika Hospitali ya taifa ya Muhimbili ambako alilazwa kwa matatibabu zaidi wiki moja iliyopita akitokea mkoani humo. Kabla ya Kifo chake Marehemu alikuwa akiendesha shughuli binafsi mkoani Mbeya ambako alihamia mara baada ya kurejea nchini kutoka Falme za kiarabu. Manga alianza kujitokeza katika ulimwengu wa kanda kanda miaka ya sitini mwishoni akiwa na timu ya Jogoo (Spurs) iliyokuwa chini ya Ulezi wa Marehemu Mzee Gaugau. Akiwa na wachezaji wenziwe wa wakati huo akina Gonza na Kapteni Jongo waliiwezesha klabu hiyo kuwika sana katika kandanda mkoani humo na Tanzania kwa ujumla. Mwaka 1970 Manga alikuwa mmoja wa Wachezaji walioiwezesha timu ya mkoa huo kunyakuwa kombe la Taifa (Taifa Cup) ambalo lililoshindaniwa na mikoa yote ya Tanzania kwa mtindo wa mtoano. Mikoa ya Morogoro, Tanga, Tabora na Dar ndiyo iliyowika zaidi katika kinyang'anyiro cha kombe hilo lililokuwa na hadhi kubwa kitaifa zama hizo. Baadhi ya wachezaji maarufu aliocheza nao Marehemu Manga akiwa na "Morogoro Combine" mwaka sabini walikuwa ni pamoja na Njenje, Hassan Shilingi, Gonza, Jongo, Shomari na hayati Gibson Sembuli. Akionekana kuimudu vyema nafasi ya ushambuliaji wa kati (9), Manga alichaguliwa timu ya Taifa ambayo ilishiriki mashindano kadhaa ya kimataifa ndani na nje ya nchi. Mwaka 1976 aliondoka nchini kuelekea Abu Dhabi Falme za kiarabu kujaribu soka ya kulipwa . Alirejea nchini mwanzoni mwa miaka ya 90 Manga alizaliwa mtaa wa Nyamwezi (Boma Road) Morogoro mwaka 1949.
KATIBU Mkuu wa Klabu ya Simba ya Dares Salaam, Kassim Dewji amedaiwa kuhusika kwa namna fulani kufanikisha kufungwa kwa timu yake naYanga Jumamosi iliyokwenda. Katika mchezo huo wa ligi kuu Tanzania Bara, nane bora, Simba ilifungwa magoli mawili bila majibu. Dewji amehusishwa na kushindwa kwa timu yake kutokana na kile kinachodaiwa kutofanya mkakati wo wote kama Katibu Mkuu kuhakikisha timu ya Simba inaifunga Yanga. Mwanachama Daniel Kamna amesema kwamba badala ya Dewaji kuiandaa timu yake kwa mchezo huo mgumu dhidi yaYanga, yeye alikuwa mkoani Singida akifanya siasa. Dewji anaelezwa kuweka kambi Singida mjini kwa ajil ya kumkampenia nduguye Mohammed Dewaji apitishwe na CCM kugombea ubunge katika jimbo hilo katika kura za maoni. "Mimi naamini kama Dewji angetumia vema wadhifa wake kuitumikia Simba basi Yanga wasingepata fursa ya kutuadhiri namna hiyo", amedai. Katika mchezo wa Kwanza uliochezwa mwezi ulipita Simba ilishinda kwa magoli mawili kwa moja la Yanga.
Na Hamis Kasabe WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara 'nane bora' inaelekea ukingoni washambuliaji Edibily Lunyamila wa Yanga na Edward Kayoza wa Singida United wanachuana vikali kwa utiaji wa mabao kimiani. Lunyamila ambaye ni mkongwe wa ligi hiyo, amefanikiwa kukwamisha mpira mara sita nyavuni kwa timu pinzani huku Kayoza mchezaji wa zamani wa Simba akipachika idadi hiyo hiyo ya magoli. Washambuliaji hao wanafuatiwa kwa karibu na Steven Mapunda 'Garincha' na Abdallah Sabebe 'Nuno Gomes' ambao ni viungo wa pembeni wa Simba na Coastal Union ya Tanga waliofunga magoli manne kila mmoja. Kutokana na chama cha soka nchini Tanzania (FAT), mchezaji atakayeibuka na magoli mengi kuliko wenziye mwishoni mwa ligi hiyo atazawadiwa kitita cha shilingi milioni moja za Kitanzania. Waliofunga magoli matatu, ni Ali Shah na Iddi Moshi wa Mtibwa naYanga. Wachezaji waliobahatika kupata mabao mawili mpaka leo hii ni Madaraka Selemani, Habib Kondo na Kuresh Ufunguo (Kajumulo) Rajab Shamte (Coastal), Kipanya Malapa (Singida), David Mjanja (Prisons), Vicent Tendwa, Mohammed Hussein (Yanga), Ramadhani Kidilu na Godfrey Kikumbizi na Duwa bin Said wote wa Mtibwa. |
YALIYOMO
KAULI
YA WAISLAMU
Karume adaiwa ‘kutafuta ujiko’ kwa kutofautiana na Mkapa Mkapa akiuka sera yake-Chuo Kikuu Uandikishaji wapiga kura waanza CUF yataja wagombea wake Temeke CCM yamtuhumu Mwenyekiti wake pandikizi Propaganda ya Udini itaisambaratisha nchi - CHADEMA USHAURI NASAHA
MAKALA
MIPASHO NASAHA
MAKALA
KALAMU YA MWANDISHI
Je, unajua haki yako unapokamatwa na polisi? LISHE
|
|
|
|
|