|
MASHAIRI
Madiwani wa Temeke (Na.1)
Haya haya amkeni, wasomaji wa NASAHA,
Wasomaji namba wani, kila wiki mwalitwaa,
Masikio yategeni, jipya mpate sikia,
Nkawa Mtarajiwa, diwani Mbagala Kuu.
Rajabu S. Nkawa, Mwenyeji wa Morogoro,
Alokaa sawasawa, timamu hana kasoro,
Kwa HAKI kateuliwa, tena pasi migogoro,
Nkawa mtarajiwa, diwani Mbagala Kuu.
Kifaa Mbagala Kuu, wote wanamtambua,
Kijana aso makuu, uongozi aujua,
JUSHAKA na KIJUKUU, debe watampigia,
Nkawa mtarajiwa, diwani Mbagala Kuu.
Kijana hana maringo, ni moja ya sifa zake,
Na pia ana malengo, kuboresha kata yake,
Zaidi ana usongo, kije shinda chama chake,
Nkawa mtarajiwa, diwani Mbagala Kuu.
Rajabu ‘ametanua’, kwenye kura za maoni,
Wenzake ‘amewaua’ tawini hadi jimboni,
Maarufu amekua, hana tena mpinzani,
Hoya MBAGALA Kuu, Nkawa anabembea.
Haji Maulidi Haji, ni turufu ya Temeke,
Kijana mwenye kipaji, na pia Mwenye ‘Makeke’,
Sheria si mvunjaji, hiyo siyo sifa yake,
Hoya Temeke hoya, Wakati umewadia.
Na pia yupo Kinjenge, wa Kata ya Miburani,
Kata ataka ijenge, akipewa udiwani,
Ataondoa unyonge, uloshamiri katani,
Chonde chonde Miburani, Kinjenge msimtupe.
Juma M. Mtimbuko, na huyu yupo Mbagala,
Kifaa chenye kicheko, na mtu aso papala,
Uzembe kwake ni mwiko, wajua kila maala,
Haya shime wa Mbagala, kifaa mmekiona!!
Chivi chivi chivi chivi, chivi ticha wa Charambe,
Chivi yeye ni ‘Mgavi’, wa ung’eng’e kama tembe,
Ticha hapendi ugomvi,chuki hana japo chembe,
Hoya hoya wa Charambe,turufu yenu ni Chivi.
Kisura bint Salehe, ni ‘Chombo’ cha Kigamboni,
Ni dada alo biyee, apendeza udiwani,
Si mpenda starehe, bali mpenda jirani,
Kigamboni msilale, dada yetu ndio huyoo!
Hapa ndipo nakomea, kalamu naweka chini,
Lakini sijaishia, wengi kuwatajieni,
Baadae taendelea, majinaye kuwapeni,
Haya Temeke haya, 2000 Ngangari.
MTAGALUKA RASHID - MTAALUMA,
Maarifa Media Trust,
Dar es Salaam.
Nganenga (Ushauri)
Naingia ushairi, nipokee Mhariri,
Nipate kumshauri, Nganenga mwana Bakari,
Ametuomba Ngangari, toka kwetu ushauri,
Usipumzike Nganenga, safari mwendo mdundo.
Kaza buti we...Nganenga, safari mwendo mdundo,
Usije tupiga chenga, Ngangari ikawa uvundo,
Kishairi sema longa, “Machavi” wapige nyundo,
Usipumzike Nganenga, Ngangari mwendo mdundo.
Nganenga ujiandae, kuufanya mtihani,
Na pia usizubae, kuifanya kampeni,
Hatupendi upotee, kukukosa NASAHANI,
Usipumzike Nganenga, kuwa “mgumu” kwa yote.
Hatutaja kukusema, kwa kufeli mtihani,
Bali twafahamu vyema, dhuluma toka zamani,
Alitujuza Malima, data toka Wizarani.
Usipumzike Nganenga, Ngangari mwendo mdundo,
Misemo haitazuka, nahau kutofutuka,
Hatutopanda mzuka, na maneno kuyapika,
Si bora kupumzika, endelea kutupika,
Usipumzike Nganenga, Ngangari ni kote kote.
Munu nazifunga beti, kwaheri washairi,
Fani hii sinacheti, natumia ujasiri,
Nganenga acha kuketi, endeleza ushairi,
Usipumzike Nganenga, Ngangari ni kote kote.
Salum Mwago (Munu),
S.L.P. 45511, Temeke, Dar es Salaam.
Ngangari muwe makini
Ngangari nawakumbusha, ngangari muwe makini,
Kwa mbinu za kuzidisha, muwabane namba wani,
Wameapa kuzidisha, kumi mpaka tisini,
Katika kuandikisha, ngangari muwe makini.
Mbinu hii inatisha, ndugu zangu si utani,
Yakuzidisha zidisha, laki hadi milioni,
Hawa tusipo watisha, Lipu watamweka chini,
Katika kuandikisha, ngangari muwe makini.
Mwenzenu wanihofisha, mbinu hii hatari sana,
Mapema nawajulisha, tusije kutafutana,
Kwani watapozidisha, Lipu watamwacha sana,
Katika kuandikisha, ngangari muwe makini.
Tuwahini vituoni, alfajiri mapema,
Tuwape yetu maoni, tuwaonyeni mapema,
Tuwabane vituoni, kuzidisha pate koma,
Katika kuandikisha, ngangari muwe makini.
Majina tudadisini, yakizidi tukiona,
Ngangari tuonyesheni, haki tusipo iona,
Kibano tuwapigeni, hadi haki kuiona,
Katika kuandikisha, ngangari muwe makini.
Tukizubaa lakini, ushindi kwetu kizani,
Benjamini atawini, ngangari hilo amini,
Yapasa tuwabaneni, hadi dakika tisini,
Katika kuandikisha,ngangari muwe makini.
Jino kwa jino lazima, tuwapasheni jamani,
Haki sawa ni lazima, kwa haki andikisheni,
Mkizidisha twasema, moto tutawachomeni,
Katika kuandikisha, ngangari muwe makini.
Ngangari kote nchini, Bara hadi Visiwani,
Ngangari muwe makini, mijini na vijijini,
Tuwabane vituoni, wandikishao jamani,
Katika kuandikisha, ngangari muwe makini.
Nazo shahada jamani, idadie tuijue,
Waziuzao jamani, mashitaka tufungue,
Wafike mahakamani, kifungo wakichukue,
Katika kuandikisha, ngangari muwe makini.
Salamu zangu nyingine, ngangari nawasalimu,
Ni hamasa si nyingine, jama kwa kila sehemu,
Kwa miguu watuone, kwa Lipumba wasalimu,
Twendeni Mbeya, Iringa,na Moro kuhamasisha.
Tubebeni picha kubwa, ya Profesa Lipumba,
Kwenye magari makubwa, na nyimbo pia kuimba,
Kwa yote miji mikubwa, “wimbo” Lipumba Lipumba,
Twendeni Mwanza,Kagera, na Mara kuhamasisha.
Tuyapambeni magari, kwa picha za Profesa,
Wote tuimbe ngangari, tumnadi Profesa,
Baba aso na kiburi, “UCHUMINI” anatesa,
Twendeni kila mahali, ngangari kuhamasisha.
Beti ni kumi na tatu, na waaga wana kwetu,
Kidumu tuseme katu, tumweke mchumi wetu,,
Zirudishwe haki zetu, heshima na nema yetu,
Twendeni kule Ruvuma, na Rukwa kuhamasisha.
HAKI BIN USAWA
S.L.P. 0000000,
Hewani,
“Mapumzikoni Mbinguni”.
Hiki ndicho
Nnaandika zitoke, humo mwenu gazetini,
Kapuni msiziweke, mtanitia huzuni,
Tungo hizi zisomeke, mijini na vijijini,
Zipate zieleweke, kwa watao zithamini.
Haki sawa akisema, Lipumba akitwambia,
Sisi tusikae nyuma, upesi kukimbilia,
Mungu akipe neema, ushindi kujipatia,
Tukipende chama chetu, CUF ndio chama chema.
Chama chakuleta haki, ni kizuri nawambia,
Tena hakina mikiki, wanyonge kuwaonea,
Hakina mtafaruki, haki chawa chotetea,
Tukipende bila shaka, CUF chapenda amani.
Uchumi kitainua, elimu taiboresha,
Hapa petu Tanzania, ujinga tauondosha,
Maradhi yatakimbia, na dhuluma itakwisha,
Tukipende kwa hakika, CUF ndio chama bora.
Lipumba anatwambia, sera zake za usawa,
Hamadi ashikilia, watu wote wawe sawa,
Kura zetu nawambia, lazima tuwape hawa,
Tukipende chama chetu, CUF hakina hiyana.
Sisi twakuomba wewe, Rahmani ya rahimu,
Mola uso mfanowe, sisi kwako ni karimu,
Twakuomba ukingowe, kijifanyacho chadumu,
Twakuomba kiondowe, katika hii awamu.
Tungo saba zinatosha, kalamu naweka chini,
Nisije nikawachosha, mukajangia mitini,
Tuweze kukiboresha, chama hiki cha amani,
Tukipende chama chetu, CUF hakiwezekani.
Ummul Jamillah,
Mapumzikoni Dodoma.
Madaraka yana mwisho
Kwa jina lake manane, Mola mwenye upendo,
Asokua na khiyana, sifa zake ni mrundo,
Mwana Adam ni dhaifu, usijifanye komando,
Madaraka yana mwisho, usiwe mwenye kiburi.
Salmin ulitamba, kwamba wewe ni kombando,
Sasa muda umekwisha, umebaki ni kondoo,
Umekuwa kama kuku, aloshikwa na mdondo,
Madaraka yana mwisho, usiwe mwenye kiburi.
Zanzibar kama yako, ulishika kwa kishindo,
Wenzio unawatesa, gerezani kwa marundo,
Watu tulikirahika, kwa maneno ya uvundo,
Madaraka yana mwisho, usiwe mwenye kiburi.
Pemba walikukataa, mavi ukanya mrundo,
Maji ukayachafua, watu wakenda kando,
Ukajifanya kifaru, hakuna tena upendo,
Madaraka yana mwisho, usiwe mwenye kiburi.
Ukajifanya kafiri, Mungu kumuweka kando,
Sasa leo kiko wapi, umechezeshwa msondo,
Na bado kesho Akhera, utakipata kipondo,
Madaraka yana mwisho, usiwe mwenye kiburi.
Madhila uliyofanya, wewe ukaona bado,
Muda wataka ongeza, utufanyie kishindo,
CCM namba moja, wakakupiga kwa nyundo,
Madaraka yana mwisho, usiwe mwenye kiburi.
Ndugu zako wawatesa, kuwapiga kwa upondo,
Sheria ukaipinda, kama nguo ya upindo,
Wenzio wakakupamba, kwamba wewe ni komando,
Madaraka yana mwisho, usiwe mwenye kiburi.
Sasa ujirekebishe unavyokwenda si mwendo,
Mimi ninae kuonya, ninaitwa Mwela Bondo,
Sikama nakusimanga, ninaondoa mfundo,
Madaraka yana mwisho, usiwe mwenye kiburi.
Mwela Bondo (Kipupwe),
Makumbusho,
Dar es Salaam.
|
YALIYOMO
KAULI
YA WAISLAMU
BAKWATA na Kanisa
Karume
adaiwa ‘kutafuta ujiko’ kwa kutofautiana na Mkapa
Mkapa
akiuka sera yake-Chuo Kikuu
Uandikishaji
wapiga kura waanza
NLD,
NRA, PONA vyamruka Mrema
CUF
yataja wagombea wake Temeke
CCM
yamtuhumu Mwenyekiti wake pandikizi
Propaganda
ya Udini itaisambaratisha nchi - CHADEMA
USHAURI NASAHA
Kumsaidia
mtoto aweze kujitegemea
MAKALA
Lengo
la propaganda
MIPASHO NASAHA
NJOZI!
NJOZI!
MAKALA
Tujihadhari
na risasi za sukari
KALAMU YA MWANDISHI
Popo
Bawa la kisiasa
Je,
unajua haki yako unapokamatwa na polisi?
Habari
za Kimataifa
LISHE
Ulaji
wa matunda
MASHAIRI
MICHEZO
Baada ya kuitumia kuigaragaza
Simba: Shungu akiri ‘ngangari' ni kiboko
Manga azikwa Moro
•••Dewji ahusishwa na kifo cha
mnyama Simba
Lunyamila, Kayoza waongoza kwa
mabao
|