|
|
|
Unaponunua modem mpya na kuiunga na kompyuta yako, utakapoitumia modem hiyo, ama kuiunganisha kompyuta yako na kompyuta nyengine, au unapopeleka fax, itafanyakazi kwa kutumia mfumo (setup) wa ufanyaji kazi uliowekwa kwenye modem hiyo ilipokuwa kiwandani, yaani factory settings. Mara nyingi mfumo huo unakidhi haja na mtumiaji huwa hana haja ya kuubadilisha. Chambilecho Wamarekani, "If it ain’t broke, don’t fix it!’, yaani kama kitu hakijaharibika, hakuna haja ya kukitengeneza. Lakini zinaweza kuwepo sababu kadhaa za kuhitaji kuubadilisha mfumo wa utendaji kazi wa modem yako. Modem takriban zote zinatengenezwa na makampuni ya Marekani na Ulaya. Mfumo wa utendaji kazi wa modem hizo unaowekwa kwenye viwanda vya modem hizo bila shaka utakuwa ni ule ambao utafanyakazi vizuri zaidi katika mazingira ya Marekani na Ulaya kuliko na wateja wengi zaidi wa modem hizo. Mazingira hayo ni pamoja na kuwepo line za simu zilizo safi na zinazotumia mitambo ya kisasa. Kwa bahati mbaya mazingira ya mawasiliano ya simu katika nchi za Afrika Mashariki ni tafauti kabisa na mazingira ya Marekani na Ulaya, na kwa kweli si mazuri. Kwanza, line za simu sio safi. Unapozungumza kwa simu ya mdomo, mara kwa mara unasikia mikwaruzo, au mara nyengine unasikia sauti kama mvua inayonyesha juu ya paa. Sauti hizo na mikwaruzo ni athari ya kitu kinachojuilikana kama "noise" kwenye line za simu. Mara nyengine noise hizo zinakuwa nyingi sana kiasi cha mtumiaji simu kuhitajika kuzungumza kwa sauti kubwa ili anayezungumza naye aweze kumsikia. Unapotumia modem kwenye line chafu za simu, mfumo wa ufanyaji kazi wa modem hiyo hauna budi kuwa na uwezo wa kuikabili hali hiyo. Tafauti nyengine iliyopo ni mfumo wa upigaji simu. Simu za Marekani na Ulaya zinatumia mfumo wa "tone" (yaani tone dialing), wakati baadhi ya line za simu za Afrika Mashariki bado zinahitaji kutumia mfumo wa "pulse" (yaani pulse dialing). Katika mfumo wa "tone", kila nambari (yaani 0 mpaka 9), ukiibonyeza inatoa sauti (yaani "tone") tafauti, kama vile kila kifungo cha kinanda (piano) kinavyotoa mlio tafauti. Sauti hizo zikipokelewa na mtambo wa simu zinazitafsiri kuwa sawa na nambari zilizobonyezwa. Kwa upande mwengine, kwenye mfumo wa "pulse", kila nambari ukiibonyeza inatoa idadi tafauti ya mipigo (yaani "pulse"). Kwa mfano, nambari 5 ukiibonyeza inatoa mipigo mitano: "ta-ta-ta-ta-ta", nambari 3 inatoa mipigo mitatu: "ta-ta-ta", n.k. Mipigo hiyo ikipokelewa na mitambo ya simu inatambulisha nambari hasa zilizobonyezwa. Ukitumia programu ambayo inahitaji kuitumia modem kupiga nambari ya simu fulani, ni lazima amri ya kupiga simu (dialing command) ieleze ni mfumo gani ("pulse" au "tone") iutumie. Kwenye makala hii, pamoja na mambo mengine, tutajifunza suala hilo. Lakini kwanza, kwa ujumla tu tujifunze namna ya kuirekebisha modem kwa kutumia Windows 95. Ukiwa kwenye Windows 95 (au Windows 98) , ukitaka kuirekebisha modem yako bonyeza Start -> Settings -> Control Panel -> Modems. Ichague modem unayotaka kuirekebisha na uchague Properties. Kwenye sehemu ya General ya kidirisha kitakachojitokeza, kama kinavyoonekana kwenye Picha 1, unaweza kubadilisha port iliyoungwa na modem. Unaweza kuchagua yoyote kati ya COM1, COM2, COM3, na COM4 kutegemeana na wapi hasa ulipouunga waya wa modem yako ya nje, au namna ulivyoitayarisha modem yako ya ndani. ![]() Unaweza pia kwenye sehemu hiyo ukabadilisha kiwango cha sauti inayotoka kwenye modem wakati wa kupiga simu na inapounganika na modem nyengine. Ukiwa una tabia ya kuitumia modem yako wakati wa usiku, wakati watu wamelala; au kama uko kwenye ofisi na hupendi kuwabughudhi wafanyakazi wenzako, unaweza kuiweka "Speaker volume" kwenye sehemu ya "Off" ili modem isitoe sauti kabisa. Kwa ujumla unaweza kuchagua ama sauti kubwa, ya kati na kati, ndogo au sauti isitoke kabisa, yaani Off. Unaweza pia kwenye sehemu hiyo ya General, kuchagua kasi ya kutumika kusafirishia data kati ya modem yako na kompyuta yako. Kasi hii inaitwa "DTE (Data Terminal Equipment) speed." Ukisoma kitabu (manual) kilichokuja na modem yako utaona ni kasi gani ya juu unayoweza kuichagua. Vile vile unaweza kubonyeza Start -> Settings -> Control Panel -> Modems -> Properties -> Diagnostics, na ukiichagua modem yako na kubonyeza More Info kama inavyoonekana kwenye Picha 2, utaweza kuona kasi ya juu inayoweza kuhimiliwa na modem yako kwenye mstari wa Highest Speed. ![]() Kasi za data zinazosafirishwa na modem ziko za aina mbili. Kasi ya kusafirisha data kati ya modem na kompyuta inaitwa "DTE speed", wakati kasi ya kusafirisha data kati ya modem na modem nyengine inayounganishwa nayo inaitwa "DCE (Data Communications Equipment) speed." Ukiona modem imeandikwa kuwa ni ya kasi ya 14.4 kbps (yaani 14.4 kilobits per second), basi hiyo mara nyingi inaweza kuhimili DTE speed ya juu ya 57600 bps; modem za kasi ya 28.8 kbps au 33.6 kbps huwa na DTE speed ya juu ya 115200 bps. Kutokana na hali mbali mbali hasa kwenye line chafu za simu, unaweza kulazimika kuchagua DTE speed ndogo japo kuwa modem yako ina uwezo wa kutumia DTE speed kubwa zaidi. Itabidi ujaribishe kasi mbali mbali (kwa kuanza na ya juu zaidi), na utumie ile ambayo itakufaa zaidi – yaani ambayo haitasababisha kukatika kwa mara kwa mara kwa mawasiliano kati ya modem yako na modem nyengine inayoungana nayo. Kikawaida, programu fulani ya mawasiliano, (kwa mfano programu ya kutuma fax, au programu ya kuunganisha kompyuta yako na Intaneti), inapoipa amri modem ya kupiga simu, kwanza modem hucheki kama kwenye line ya simu unasikika mlio maalum unaoitwa dial tone unaothibitisha kuwa line ya simu iko hai. Baadhi ya modem zinaweza kushindwa kuitambua dial tone japokuwa ipo kutokana na namna na namna zilivyotengenezwa. Modem kama haikuusikia mlio wa dial tone kikawaida haitaendelea kupiga simu kama hukuiambia tangu mapema kuwa ipige simu hata kama hakuna dial tone. Kuweza kuiambia modem ipige simu bila ya dial tone, kwenye sehemu ya Connection ya kidirisha cha Properties kinachoonekana kwenye Picha 1, hakikisha kuwa kisanduku cha "Wait for dial tone before dialing" hakina tiki kama inavyoonekana kwenye Picha 3. ![]() Ukibonyeza sehemu ya Advanced, tunapendekeza uweke tiki kwenye sehemu ya "Use error control", kama inavyoonekana kwenye Picha 4. Hii ni muhimu sana kwenye line chafu za simu. Unaweza pia kuchagua "Use cellular protocol" kama modem yako inatumia protokali maalum ya kutumika pamoja na simu za mikononi (cellular). Pia weka tiki kwenye sehemu ya "Use flow control" na pia uchague "Hardware (RTS/CTS)" flow control – kwa modem hicho ni kitu kinachopendekezwa ![]() Sehemu muhimu ya kidirisha cha Advanced Connection Settings kinachoonekana kwenye Picha 4, ni kisanduku kilicho cini ya maneno, "Extra settings". Hapa unaweza kuweka amri kadhaa za kuifanya modem yako ifanyekazi kama unavyotaka. Amri za modem (modem commands) zinaanza na "AT" yenye maana "ATTENTION", kama kuiambia modem ikae tayari kupokea amri. Modem nyingi zinatumia amri zilizoanzishwa na kampuni ya kutengeneza modem inayoitwa Hayes. Lakini ziko modem ambazo sio "Hayes-compatible," yaani hazielewi amri (zote) zinazotumiwa na modem za hayes. Na kuna baadhi ya modem huwa zina amri zake zenyewe za ziada ingawa zinazielewa amri zote za Hayes. Kama unapotumia modem yako kuunganisha na modem nyengine unasikia sauti ya kuonesha kuwa modem hizo mbili zinajaribu kuungana, lakini zinashindwa kumalizia hatua za kuungana, basi inawezekana modem yako haikufanywa isubiri kwa muda wa kutosha na kwa hivyo inakata tamaa mapema sana. Kama tatizo ni hilo utahitaji kuiongozea modem yako muda unaoitwa "Carrier Wait Time." Ukiweka kwenye kisanduku cha Extra settings, amri: ATS7=90, utaifanya modem isubiri majibu (Carrier) kutoka kwenye modem nyengine, na isikate tamaa kwa muda wa sekunde 90 badala ya sekunde 60 au chini ya hapo zinazowekwa kikawaida. Muda mrefu wa kusubiri Carrier unahitajika unapopiga simu za mbali, au kwenye line chafu za simu, au unapotumia modem yako pamoja na simu ya cellular au unapounganisha modem yako na modem ya mbali ambayo yenyewe imeunganishwa na simu ya cellular. Kikawaida, modem mbili zinapotaka kuungana, hufanya mapatano yanayoitwa "handshaking". Wakati wa handashaking, modem hizo mbili, pamoja na mambo mengine, zinakubaliana juu ya protokali ya kutumia ya kusahihisha makosa mbali mbali yatakayotokea wakati wa kupelekeana data – hii huitwa "Error correction protocol" ambayo maarufu ni ITU-TSS V.42 na nyengine ni MNP-4 (Microcom Network Protocol class 4). Protokali ya V.42 inatumia protokali ya msingi inayoitwa LAP-M (Link Access Procedure for Modems), na nyengine ya ziada inayoitwa MNP-4. MNp-4 yenyewe inajumuisha pia protokali MNP-2 na MNP-3, zote za kusahihisha makosa. Kwa namna hiyo, modem inayotumia protokali ya V.42 inaweza kuelewana na modem nyingi. Wakati wa handshaking pia, modem hizo hukubaliana protokali ya kutumia kubana data, yaani "Data compression protocol." Data zikibanwa, zinasafirishika kwa wingi zaidi. Protokali maarufu za kubana data ni pamoja na CCITT V.42bis na MNP-5. Protokali za kubana data ndizo zinazoifanya, kwa mfano, modem ya kasi ya 14,400 bps kuweza kupeleka data kwa kasi ya 57,600 bps, yaani mara nne zaidi. Wakati wa handshaking, modem hizo pia hukubaliana juu ya kasi ya salama, (yaani ambayo haitasababisha matatizo), ya kutumia kusafirishia data kati ya modem hizo mbili. Kwa mfano, zinaweza kukubaliana kutumia DCE speed ya 28,800 bps kama modem zote mbili zinaihimili kasi hiyo. Kama modem moja ni ya kasi ya 28,800 bps na nyengine ni ya kasi ya 14,400 bps, kasi ya juu ya kutumika modem hizo zinapoungana itakuwa ni 14,400 bps au chini ya hapo. Wakati mwengine, baada ya modem kuungana, yanaweza kutokea matatizo, kwa mfano yanayosababishwa na "noise" kwenye line ya simu. Ikitokezea hivyo, modem zinaweza kulazimika kupunguza DCE speed ya kutumia ili data zifike bila ya matatizo. Ni kama vile unapopita kwenye utelezi unalazimika kwenda polepole ili usianguke. Kupunguza DCE speed kwa namna hiyo kunaitwa "fallback." Modem zinaweza kulazimika kupunguza DCE speed mpaka kufikia kasi ndogo sana ya 1,200 bps au chini ya hapo. Lakini tatizo ni kwamba modem nyingi za kisasa unapozinunua huwa tayari zimefanya zisiweze kupunguza DCE speed chini ya kasi ya 2,400 bps. Na kutokana na hivyo, inapohitajika DCE speed kushushwa chini ya 2,400 bps kukabiliana na "noise", modem inakata mawasiliano. Kwenye line chafu za simu, na hasa kama moja kati ya modem imeunganishwa na simu ya aina ya cellular, huna budi kuifanya modem yako iweze kutumia DCE speed iliyo chini ya 2,400 bps. Kwenye modem zilizo Hayes-compatible, utahitaji kuweka amri N1 kwenye kisanduku cha Extra settings. Kwenye modem isiyokuwa Hayes-compatible, itabidi uangalie kwenye manual ya modem hiyo uone ni amri gani ya kutumia kuruhusu DCE speed zote zinazowezekana. Kwa mfano, kwa modem za U.S. Robotics, itakupasa kutumia amri &U0&N0. Wakati modem mbili zinapopatana juu ya DCE speed ya kutumiwa, mapatano hayo huanzia kasi ya juu inayoweza kutumiwa na modem iliyoipigia simu modem nyengine. Kwa mfano, kama modem ya kwanza inaweza kusafirisha data kwa DCE speed ya juu kabisa ya 28,800 bps, lakini kutokana na ama hali ya line ya simu au namna inavyofanyakazi modem ya pili, DCE speed ya juu inayoruhusika ni ya 9,600 bps tu, basi katika hali hiyo handshaking huendelea kama ifuatavyo: Modem 1: Je, tunaweza kutumia DCE speed ya 28,800 bps? Modem 2: lo! Hapana! Hiyo ni kubwa sana! Modem 1: Sawa! Je, utaiweza DCE speed ya 26,400 bps? Modem 2: Bwana we! Hiyo bado ni kubwa sana! Modem 1: 24,000 bps? Modem 2: Siiwezi! Modem 1: Sawa! Tujaribu 21,600 bps basi! Modem 2: Bado siiwezi! Modem 1: 19,200 bps? Modem 2: Siiwezi! Modem 1: 16,800 bps? Modem 2: Siiwezi! Modem 1: 14,400 bps? Modem 2: Ninaiweza hiyo lakini line ya simu ni chafu. Punguza! Modem 1: Sawa! Tujaribu 12,000 bps basi! Modem 2: Pia nayo si nzuri! Modem 1: 9,600 bps? Modem 2: Sasa umesema! Tunaweza kutumia DCE speed hiyo. Modem zinapopatana juu ya DCE speed ya kutumiwa na kulazimika kuipunguza, kitendo hicho huitwa "fallback" kama tulivyosema kabla. Wakati wote wa mapatano, wewe mtumiaji kompyuta, utakachokisikia ni ule mlio wa modem tu. Lakini kama ulivyoona hapo juu, mapatano hayo kwa vile yameanzia DCE speed kubwa sana yanachukua muda mrefu, na kama modemimewekewa muda mfupi wa kungojea Carrier, itakata mawasiliano kabla ya kufikiwa makubaliano ya DCE speed ya kutumika. Hapo ndipo ile amri ya S7=90 inaposaidia. Lakini kitakachosaidia zaidi ni kuifanya modem ifanye mapatano kuanzia DCE speed ndogo. Rai hiyo itakusaidia sana, kwa mfano, kama umegundua kuwa unashindwa kuunganisha mawasiliano kati ya modem mbili na mara zote mawasiliano hukatika wakati wa handshaking. Amri ya kuifanya modem ianze mapatano ya DCE speed kuanzia kiwango fulani zitafautiana kati ya modem na modem. Kwenye modem nyingi unaweza kutumia rejesta S37 kuchagua DCE speed ya kuanzia mapatano. Manual za modem zitakueleza namna ya kuchagua nambari ya kuhifadhiwa kwenye rejesta hiyo kwa DCE speed mbali mbali. Kwa mfano, S37=9 kwa modem ambazo ni Hayes-compatible, inafanya mapatano yaanze na DCE speed ya 9,600 bps. Kwenye line za simu chafu, hiyo ni DCE speed nzuri ya kuanzia mapatano. Kwenye modem za U.S. Robotics, DCE speed ya juu ya kutumika inachaguliwa kwa kutumia amri &Nn lakini pia utahitaji kuchagua DCE speed ya chini kabisa. Kwa mfano, kuyafanya mapatano ya DCE speed yawe kati ya 300 bps na 9,600 bps utahitaji kuipa modem amri &N6&U1. Amri hizo, pamoja na tulizozitaja hapo, ukiziweka kwenye kisanduku cha Extra settings utaziandika kwa pamoja: ATS7=90&N6&U1, kwa modem ya U.S. Robotics; na kwa modem ambayo ni Hayes-compatible utaziandika kwa pamoja: ATS7=90N1S37=9 kama zinavyoonekana kwenye Picha 4. Kuna mambo mengi ambayo unaweza kuyafanya kurekebisha utendaji kazi wa modem yako. Tunakushauri uipitie kwa makini manual ya modem yako ili upate kuelewa zaidi namna modem yako inavyofanyakazi.
|
.YALIYOMO
Tahariri Hakuna Idd kwa wanafunzi Waislamu mwaka huu Baada ya wanafunzi Wakristo kusherehekea Krismasi: Wanafunzi Waislamu kuikosa Id el Fitr Hoi hoi zatawala ziara ya Mwinyi Mwanza Waislamu Tunduma waswali ndani ya kilabu cha ulanzi MARADHI YA KISAIKOLOJIA: FROTTEURISM Barabara za Tabora zimepitwa na wakati Jicho la
Uzalendo: Nihiari yetu kuendelea kujidanganya!
Kuanza na kwisha mwezi wa Ramadhani Taarifa ya Kamati juu ya yaliyotokea Mwembechai Maazimio ya kongamano la wanawake wa Kiislamu Waislamu kijijini Kidunda Moro wahitaji mwalimu Waislamu Mtwara wadai jengo la Wakfu kwa CCM Wakati Makanisa yakimeremeta: Msikiti wageuka gofu Sanya Juu Sheikh Khalifa Suleiman afariki dunia Sheikh wa wilaya ya Lushoto afariki Ijue Madrasat Riyaadhwa ya mjini Dodoma Mwinyi apongeza juhudi za kulea yatima Mwanza Tuhuma za kupindua uongozi wa Bakwata: Sheikh Hamim Boza akanusha kuhusika Kuongezeka kwa ajali za barabarani Njia ya
uzimani ni nyembamba, waionao ni wachache - 4
Saggaf awataka watoto wahifadhi Qur'an Waislamu watakiwa kujitolea kupigania dini yao Kesi nyingine Mwembechai yaahirishwa Sayansi
na Teknolojia
Chakula
na lishe
|