AN-NUUR 
Na.181 Ramadhan 1419, Desemba 25 - 31, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Saumu na lishe ya mama mjamzito 

Na Mujahid Mwinyimvua 

BADO tunaendelea na kutoa taaluma maalumu kwa wasomaji wetu walio Waislamu ambao wanaendelea na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kwa leo tunaeleza ibada ya saumu na lishe ya mama mja mzito. 

Awali ya yote, watu wakumbuke kuwa Uislamu ni mfumo kamili wa maisha. Hivyo basi, ibada zote katika dini hii zinazingatia hali zote za mwanadamu. 

Yaani hali ya kimwili na zile za kiroho. Kwa vile funga ya Ramadhani ni chuo maalumu kinachokusudiwa kuwandoa waumini, hali za waumini hao zimezingatiwa katika sheria ya utekelezaji wa ibada hiyo. 

Kwa mfano, mtu kuwa na afya nzuri na utulivu ni masharti muhimu kwa Muislamu ili aweze kuitekeleza ibada ya saumu. Ni kwa msingi huo, sheria ya dini ya Kiislamu inawataka baadhi ya Waislamu kufunga na pia imewasamehe wengine kufunga pindi wanapokuwa katika hali isiyo kuwa ya afya njema, safari, umri mkubwa, hedhi, nifasi, ujauzito, kunyonyesha n.k. 

Katika makundi hayo, kuna wanaostahili kufunga wakati wakiwa katika hali zao za kawaida na kuna wale waliosamehewa kabisa. 

Makala hii si lengo lake kuyatazama makundi hayo kwa kina, kwa hiyo tunawaomba wasomaji wetu watazame rejea zinazohusika na somo hilo kwa kina. 

Mama mjamzito anaruhusiwa na sheria ya dini ya Kiislamu kuahirisha funga ya Ramadhani. Yaani Ramadhani ikimkuta hali ya kuwa mjamzito na mwenyewe (au daktari) ana wasiwasi na afya yake au ya mtoto wake (kuwa wataathirika) ni ruhusa juu yake kula katika mwezi huo wa Ramadhani na atawajibika kuilipa funga hiyo wakati hali yake imerejea ya kawaida. 

Kama tulivyosema awali, swala hili (la kulipa saumu) lina maelezo marefu, kwa hiyo watu wafanye rejea katika vyanzo vingine (siyo makala hii). 

Kama tunavyojua, mtu akifunga pamoja na mambo mengine anajizuia kula na kunywa, takriban kwa masaa 15 au 16. Kitendo cha mwili wa mama mja mzito kukosa chakula kwa muda huo ni wazi kuwa kinaathiri kwa lishe na afya ya mama na mtoto wake aliyetumboni. 

Kwa hiyo, kina mama wajawazito ni vyema kuipokea ruhusa ya sheria ya dini ya Kiislamu ya kuahirisha funga ya Ramadhani mpaka pale atakapokuwa katika hali ya salama (kawaida). 

Tuliwahi kusema katika makala zilizopita za chakula na lishe kuwa: Wakati wa ujauzito ni muhimu mama ale vyakula vya kutosha, ahudhurie kliniki, apumzike hasa miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito na lazima apate tiba na kinga ya maradhi. 

Pia tulisema kuwa, mama mjamzito anahitaji kula vyakula vya kutosheleza mahitaji yake yeye mwenyewe na mtoto aliye tumboni. Kwa kawaida mama anatakiwa aongezeke kilo kumi na mbili kwa muda wote wa ujauzito wake. 

Vile vile chakula chake kiwe mlo kamili (yaani cha mchanganyiko wa virutubisho vyote muhimu) Mama mjamzito asiyepata muda wa kupumzika na asiye kula vizuri anaweza kutokuongezeka uzito, kuwa na upungufu wa damu, kujifungua mtoto mwenye uzito pungufu (chini ya kilo 2 1/2), mimba inaweza kuharibika, anaweza kujifungua kabla ya wakati n.k. 

Kwa kuzingatia maelezo ya hapo juu ni imani yetu kuwa hikma ya sheria ya dini ya Kiislamu ya kuwaruhusu kina mama wajawazito kuahirisha funga zao iko wazi. 

Na pia watu wasidhani kuwa kujilazimisha kufunga hali ya kuwa wana mimba ni ucha Mungu, Hapana, bali huko ni sawa na kujiua jambo ambalo Mwenyezi Mungu ametukataza: 

"...Wala msijiue, hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kukuhurumieni". (4:29) 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Hakuna Idd kwa wanafunzi Waislamu mwaka huu 

Baada ya wanafunzi Wakristo kusherehekea Krismasi: Wanafunzi Waislamu kuikosa  Id el Fitr 

Hoi hoi zatawala ziara ya Mwinyi Mwanza 

Waislamu Tunduma waswali ndani ya kilabu cha ulanzi  

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: FROTTEURISM 

Barabara za Tabora zimepitwa na wakati 

Jicho la Uzalendo: Nihiari yetu kuendelea kujidanganya! 
Na Sompo wa Kahambwe 

Kuanza na kwisha mwezi wa Ramadhani 

Taarifa ya Kamati  juu ya yaliyotokea Mwembechai 

Hotuba ya Mwenyekiti wa Wanawake wa Kiislamu katika Kongamano lililofanyika Masjid Nnuur Sinza  19/12/1998 

Maazimio ya kongamano la wanawake wa Kiislamu 

Waislamu kijijini Kidunda Moro wahitaji mwalimu 

Waislamu Mtwara wadai jengo la Wakfu kwa CCM 

Wakati Makanisa yakimeremeta: Msikiti wageuka gofu Sanya Juu 

Sheikh Khalifa Suleiman afariki dunia 

Sheikh wa wilaya ya Lushoto afariki 

Ijue Madrasat Riyaadhwa ya mjini Dodoma 

Somo la Zaka 

Maiti ya Muislamu yasusiwa 

Mwinyi apongeza juhudi za kulea yatima Mwanza 

Tuhuma za kupindua uongozi wa Bakwata: Sheikh Hamim Boza akanusha kuhusika 

Kuongezeka kwa ajali za barabarani 

Njia ya uzimani ni nyembamba,  waionao ni wachache - 4 
Na Yasin Valerian Massawe 

Matajiri wahimizwa kutoa zaka 

Saggaf awataka watoto wahifadhi Qur'an 

Waislamu watakiwa kujitolea kupigania dini yao 

Kesi  nyingine Mwembechai yaahirishwa  

Sayansi na Teknolojia  
[Kuirekebisha Modem Yako]  

Masomo ya Dini ya Kiislamu  

Barua za Wasomaji  

Mashairi  

Chakula na lishe  
[Saumu na lishe ya mama mjamzito] 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita