|
|
Wasiwasi huo umetokana na ukweli kwamba kwa mujibu wa kanuni za Baraza hilo ratiba ya mitihani ikishapangwa haiwezi kubadilishwa kwa sababu yoyote ile. Baadhi ya wananchi mbalimbali walioongea na gazeti hili wameelezea masikitiko yao kuhusu uamuzi wa Baraza kupanga mitihani hiyo ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na katika sikukuu za Idd el Fitri. Wamesema kuwa ratiba hiyo inathibitisha kutokutambuliwa kwa imani ya Kiislamu katika upangaji na uendeshaji wa masuala mbalimbali ya kinchi. Bwana Maulid Hassan wa Manzese akizungumzia suala hili alisema upangaji huo wa ratiba umezingatia Krismasi na Boxing Day yake, umezingatia Mwaka Mpya na pia umezingatia sikukuu ya Mapinduzi lakini haukuweza kukumbuka mfungo wa Ramadhan na sikukuu ya Eid. Naye Bwana Masoud wa Ilala Boma yeye alitilia mashaka ratiba hiyo kuwa huenda imepangwa hivyo ili kuwakomoa Waislamu kwani shughuli nyingi zote za kitaifa zimezingatiwa. "Ratiba imeanza siku ya Jumatano badala ya Jumatatu ili wanafunzi wasifanye mitihani wakati wa sikukuu ya Mapinduzi ya Zanzibar", alisema kwa hisia Bwana huyo. Wengi wametuhumu ratiba ya mtihani kuwa ni ya "kibaguzi" isiyozingatia walipa kodi Waislamu wa nchi hii. Mitihani ya kidato cha nne iliyofutwa Novemba 1998 sasa itafanyika kuanzia Janauri 13 hadi Janauri 27 mwakani kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na baraza la mitihani hivi karibuni. Jumatatu imetangazwa kuwa ni siku ya mapumziko ili kufidia siku ya Boxing Day iliyoangukia Jumamosi. Kutangazwa kwa siku ya hiyo ya Jumatatu kuwa ni ya mapumziko kumekuja wakati vyombo vya habari huko nyuma viliwahi kuripoti kuwa utaratibu wa kufidia sikukuu zinazoangukia Jumamosi na Jumapili ulifutwa na Bunge. Wakati huo huo, imefahamika kwamba linaandaliwa Tamasha kubwa la Jiji kuanzia Januari 16 ambalo litadumu kwa wiki moja. Tamasha hilo ambalo litafanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja limekuwa likilalamikiwa na baadhi ya wakereketwa wa CCM kwa kutozingatia hisia za waliofunga. Japo ratiba maalum ya Tamasha hilo haijajulikana lakini wengi wanaojua kuwepo kwa tamasha hilo wamesema kwamba ngoma na unywaji ni vitu ambavyo havitakosekana. Kupangwa kwa Tamasha hilo ndani ya Ramadhani bila ya kujali kwamba miongoni mwa washiriki watakuwa ni Waislamu ambao watakuwa wamefunga kumeelezwa kwamba kumetokana na Tume ya Jiji kujaa Wakurugenzi wa dini moja. Hali hiyo imeelezwa kwamba inawafanya wasiwe makini wala kuzingatia uwepo wa Waislamu na hisia zao kutokana na imani yao. Gazeti hili liliwasiliana na Katibu wa Tume ya Jiji ambaye alithibitisha
kuwepo kwa tamasha hilo.
|
YALIYOMO
Tahariri Hakuna Idd kwa wanafunzi Waislamu mwaka huu Baada ya wanafunzi Wakristo kusherehekea Krismasi: Wanafunzi Waislamu kuikosa Id el Fitr Hoi hoi zatawala ziara ya Mwinyi Mwanza Waislamu Tunduma waswali ndani ya kilabu cha ulanzi MARADHI YA KISAIKOLOJIA: FROTTEURISM Barabara za Tabora zimepitwa na wakati Jicho la
Uzalendo: Nihiari yetu kuendelea kujidanganya!
Kuanza na kwisha mwezi wa Ramadhani Taarifa ya Kamati juu ya yaliyotokea Mwembechai Maazimio ya kongamano la wanawake wa Kiislamu Waislamu kijijini Kidunda Moro wahitaji mwalimu Waislamu Mtwara wadai jengo la Wakfu kwa CCM Wakati Makanisa yakimeremeta: Msikiti wageuka gofu Sanya Juu Sheikh Khalifa Suleiman afariki dunia Sheikh wa wilaya ya Lushoto afariki Ijue Madrasat Riyaadhwa ya mjini Dodoma Mwinyi apongeza juhudi za kulea yatima Mwanza Tuhuma za kupindua uongozi wa Bakwata: Sheikh Hamim Boza akanusha kuhusika Kuongezeka kwa ajali za barabarani Njia ya
uzimani ni nyembamba, waionao ni wachache - 4
Saggaf awataka watoto wahifadhi Qur'an Waislamu watakiwa kujitolea kupigania dini yao Kesi nyingine Mwembechai yaahirishwa Sayansi
na Teknolojia
Chakula
na lishe
|