AN-NUUR 
Na.181 Ramadhan 1419, Desemba 25 - 31, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Hoi hoi zatawala ziara ya Mwinyi Mwanza
 
  • Wasafiri watelekeza mizigo kumshangilia
  • Wamkumbushia enzi za ‘Colgate’ kuwa anasa
ZIARA ya Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi mkoani Mwanza hivi karibuni imeacha gumzo na historia ya aina yake kutokana na jinsi alivyopokelewa na wananchi. 

Japo ziara hiyo ilikuwa ni ya kidini, watu wa dini zote walijitokeza kumshangilia kila alipopita. 

Hoi hoi zilianzia uwanja wa ndege wa mjini Mwanza ambapo wasafiri walijisahau na kuungana na wasindikizaji na kuanza kumshangilia Rais huyo mstaafu kwa nguvu. 

Wasafiri hao ambao walikuwa wakisubiri ndege ya ATC kuelekea Dar es Salaam bila kujali kupoteza au kuibiwa mizigo yao walijikuta wakijumuika na wafanyakazi wa Uwanja huo katika fujo la shangilio la aina yake lililomkaribisha Alhaj Mwinyi mara baada ya kushuka kwenye ndege iliyomleta kutoka Dar es Salaam. 

Katika kila njia alikopita watu walijitokeza kwa wingi kumshangilia huku wengine wakitoa sauti ya juu kukariri hali ilivyokuwa nyuma wakati anachukua uongozi na neema aliyowaachia wakati anaondoka. 

Akiwa Nyakato, umati mkubwa wa aina yake ulijitokeza bila kuhamasishwa na kuanza kupaza sauti kumshukuru kwa yote mema aliyowatendea wananchi. 

Ratiba ya Alhaj Ali Hassan Mwinyi mjini Mwanza ilianza kwa kuhudhuria mashindano ya kusoma Qur’an katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa ambayo yalianza saa 4:20 asubuhi hadi saa 8:50. Katika mashindano hayo mtoto Hudhaifa bin Saleh Hazaa mwenye umri wa miaka tisa alishinda. Mtoto Hudhaifa anasoma katika kituo cha kuhifadhia Qur’an cha Ibn - Masoud kilichopo Bwiru, amehifadhi juzuu ishirini. 

Vyuo vingine vilivyoshiriki ni Nyakato Islamiya, Taqwa Madrasa, Thaqaafa Muslim School, Khalqa-Nyakato, Habibu Swaleh - Nyakato, Madrasa Fallah - Kirumba na Madrasa Khayria - Nyakato.  

Madrasa zilipangwa katika makundi kufuatana na washindani walivyohifadhi. Kundi A - Juzuu moja, kundi B juzuu mbili, kundi C juzuu tatu, kundi D juzuu nne. Kundi E juzuu tano, kundi F juzuu sita, kundi G juzuu nane. 

Mshindi wa jumla katika madrasa walikuwa Madrasa ya Habib Swaleh chini ya Ustadh Kibira, walipewa kikombe moja kwa moja kutokana na kushinda mfululizo mara tatu. 

Mgeni rasmi Rais Mstaafu Alhaj Mwinyi alitumia nafasi hiyo kwa kupongeza ushirikiano aliouona tangu afike Mwanza na alihimiza ushirikiano miongoni mwa Waislamu ili kujiletea maendeleo. 

Alisisitiza kuepukana na dharau miongoni mwa Waislamu, taasisi na vikundi mbalimbali vya harakati za Kiislamu, alisema kila taasisi iendeshe shughuli zake kama ilivyoamua bila ya kuingiliwa madamu lengo ni kuupeleka Uislamu mbele. 

Alisema ni ruhusa kila madhehebu kuendesha ibada kwa mujibu wa mapokezi yao maadam hawavunji nguzo za sala. 

Siku hiyo baada ya mashindano hayo alihudhuria chakula cha mchana nyumbani kwa Mwenyekiti wa madhehebu ya Ibaadh Sheikh Nassoro Ally Farai. Siku iliyofuatia aliweka mawe ya msingi katika chuo cha Habib Swaleh kilichopo Nyakato, Nyegezi na Mkoani wakati mchana wake alihudhuria karamu ya chakula nyumbani kwa Bw. Mustapha Hassan Manengero nyuma ya mtaa wa Uhuru. 

Siku hiyo hiyo jioni alitembelea kituo cha yatima Ilemela; kuweka jiwe la msingi la madrasa Taqwa na kuhudhuria chakula cha usiku kilichoandaliwa maalum shuleni hapo kwa ajili ya kutunisha mfuko wa ujenzi wa shule nyingine ya Kiislamu chini ya shule hiyo hiyo ya Taqwa sekondari Mwanza. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Hakuna Idd kwa wanafunzi Waislamu mwaka huu 

Baada ya wanafunzi Wakristo kusherehekea Krismasi: Wanafunzi Waislamu kuikosa  Id el Fitr 

Hoi hoi zatawala ziara ya Mwinyi Mwanza 

Waislamu Tunduma waswali ndani ya kilabu cha ulanzi  

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: FROTTEURISM 

Barabara za Tabora zimepitwa na wakati 

Jicho la Uzalendo: Nihiari yetu kuendelea kujidanganya! 
Na Sompo wa Kahambwe 

Kuanza na kwisha mwezi wa Ramadhani 

Taarifa ya Kamati  juu ya yaliyotokea Mwembechai 

Hotuba ya Mwenyekiti wa Wanawake wa Kiislamu katika Kongamano lililofanyika Masjid Nnuur Sinza  19/12/1998 

Maazimio ya kongamano la wanawake wa Kiislamu 

Waislamu kijijini Kidunda Moro wahitaji mwalimu 

Waislamu Mtwara wadai jengo la Wakfu kwa CCM 

Wakati Makanisa yakimeremeta: Msikiti wageuka gofu Sanya Juu 

Sheikh Khalifa Suleiman afariki dunia 

Sheikh wa wilaya ya Lushoto afariki 

Ijue Madrasat Riyaadhwa ya mjini Dodoma 

Somo la Zaka 

Maiti ya Muislamu yasusiwa 

Mwinyi apongeza juhudi za kulea yatima Mwanza 

Tuhuma za kupindua uongozi wa Bakwata: Sheikh Hamim Boza akanusha kuhusika 

Kuongezeka kwa ajali za barabarani 

Njia ya uzimani ni nyembamba,  waionao ni wachache - 4 
Na Yasin Valerian Massawe 

Matajiri wahimizwa kutoa zaka 

Saggaf awataka watoto wahifadhi Qur'an 

Waislamu watakiwa kujitolea kupigania dini yao 

Kesi  nyingine Mwembechai yaahirishwa  

Sayansi na Teknolojia  
[Kuirekebisha Modem Yako]  

Masomo ya Dini ya Kiislamu  

Barua za Wasomaji  

Mashairi  

Chakula na lishe  
[Saumu na lishe ya mama mjamzito] 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita