|
|
|
| Akina Mrema wapo wengi serikalini | Misikiti isigeuzwe taasisiza Serikali | Kapuya usisahau cheo ni dhamana | Mimi sio miongoni mwa waliompongeza Kingunge | Serikali imetufedhehesha | TAMWA acheni ubabaishaji | Waislamu tumuogope Mwenyezi Mungu | Akina Mrema wapo wengi serikaliniNdugu MahririNACHUKUA nafasi hii kuwapongeza Wabunge waliotoa hoja zao kuhusu kauli au tuhuma nzito alizotoa Mhe. Mrema. Kweli Mhe:A.L.Mrema ametoa tuhuma nyingi tu bila kuwa na ushahidi au uhakika. Hata alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani alifanya hivyo, bila ya kuwa na ushahidi, aliweza kuyatolea maamuzi masuala mbali mbali mazito yanayoiathri jamii. Lakini tusiangalie ya Mrema peke yake, kwani akina Mrema wapo wengi. Mawaziri wa serikali ya Tanzania ambao ni wa Chama Tawala wameungana sana na Mhe. Mrema. Rejea ya Mwembechai, waliofanya fujo hadi kupelekea mauaji ni Askari Polisi ambao wametumwa na Serikali, bila kuangalia athari ambazo wananchi wake wangepata. Mawaziri na Viongozi wa ngazi za juu walihusika na vurugu hizo kupelekea mauaji. Cha kusikitisha ni kama alivyo Mrema, Mawaziri na viongozi bila kuona haya au vibaya walitamka kwamba waliouawa na kukamatwa walikuwa wahuni, vibaka, wamachinga, wavuta bangi, wanaopenda madaraka n.k. Kisha wakawa na kauli kama Mrema yakuwa nchi za Kiarabu zimewapa pesa, nchi za Kiarabu zimechochea vurugu hizo. Mara wafanya biashara wametoa pesa ili kuchochea vurugu hizo na kauli zingine mbalimbali ambazo hazina ushahidi. Ili mradi wameropoka tu au kujitafutia umaarufu bila kuhofia kuwa kauli hizo zitaleta athari katika jamii. Katika kuangalia Sakata la Mrema siyo pekee bali hata Mawaziri waliopo wakapimwe na siyo Mrema pekee. Mbona Wabunge mmeona upande wa Mrema pekee bila kuyapitia matukio ambayo yamesababishwa na Wabunge ambao ni Mawaziri pamoja viongozi wengi. Wale walioua wamechukuliwa hatua gani? Maana walikuwa waongo, wazushi pia wachochezi kama mlivyomwita Mrema. Akina Mrema wapowengi Serikalini. Dr. Bilal Nicholas,
Misikiti isigeuzwe taasisiza Serikali Ndugu Mhariri, Nachukua nafasi hii kutoa lawama zangu juu ya mwenendo wa Serikali wa kudhamiria kufanya misikiti ya Kiislamu kama taasisi zake. Kabla ya yote inatubidi tuielewe misikiti nini. Kwa tafsiri ya karibu, misikiti ni sehemu teule na ni mahala patakatifu ambao Waislamu hufanyia ibada zao. Miongoni mwa ibada ni pamoja na sala, maombi, maadhimisho, mafundisho, mihadhara, makongamano, semina na makutano kadha kwa ajili ya kufuata maamrisho ya Allah. Misikiti hujengwa kwa kujitolea Waislamu kwa hali na mali na wakati mwingine kwa nadra hutokea tajiri au taasisi ya Kiislamu ukajengwa msikiti. Lakini kadiri itakavyokuwa lengo na madhumuni makubwa ni ujenzi wa nyumba ya Mwenyezi Mungu. Hivyo hivyo nakwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah. Baada ya ujenzi kukamilika, waswaliji katika msikiti huo huchagua viongozi watakaoendesha shughuli za ibada. Hata hivyo viongozi wanaochaguliwa wataendelea kuongoza kwa ridhaa ya waumini. Waislamu wanayo mamlaka ya kubadilisha uongozi muda wowote bila ya kuhojiwa au kuingiliwa na chombo chochote nje ya msikiti husika. Huu ndio utaratibu unaokubalika kulingana na sheria zinazotawala kwenye misikiti yetu. Lakini taratibu zetu zimekuwa zikikiukwa na kuingiliwa na serikali bila ya kuwa na madaraka ya kisheria au kikatiba. Tunaiomba serikali yetu ituache huru na misikiti yetu. F. Kahamba,
Kapuya usisahau cheo ni dhamana Ndugu Mhariri NIPE fursa nimjibu Profesa Kapuya juu ya hotuba aliyoitoa katika ukumbi wa Chuo cha Sanaa mjini Bagamoyo. Awali ya yote, anaposema Waislamu yeye anajiweka wapi? Upande wa serikali ambao hauna dini? Au yeye amejiondoa? Pili hotuba yake yote ilikuwa imejaa jazba kinyume kabisa na hadhi ya Uprofesa. Nataka nimfahamishe Profesa Kapuya angekuwa makini na anayoyasema, angefuata Qur’an inavyosema: Mungu anasema: "Enyi watu imekujieni dalili kutoka kwa Mola wenu na tumekuteremshieni nuru iliyo wazi Qur’’an (4:174). Mungu anasema tena: "Sema enyi watu haki imekwisha kukujieni kutoka kwa Mola wenu, basi anayeongoka anaongoka kwa (faida ya) nafsi yake na anayepotea anapotea kwa (khasara ya) nafsi yake (10:108.) Mungu anasema tena: "Enyi watu wa kitabu amekwisha kufikieni Mtume wetu anayekudhihirishieni mengi mliyokuwa mkiyaficha katika kitabu na husamehe mengi, bila shaka imekwisha kufikieni nuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kitabu kinachobainisha (kila jambo) (5:5). Huo hapo ndio mwelekeo wa Waislamu kutoka kwa Mola wao na wote tunaufuata. Tatizo la Waislamu sio mwelekeo, maana tayari tunao mwelekeo. Ila tatizo ni viongozi wa Kiislamu walioko madarakani serikalini kutoujua huo mwelekeo na wamekuwa wakijisahau wanapokaribishwa katika majukwaa katika hafla za Waislamu kuhubiri siasa za kitwaghuti ili ifanane na Uislamu. Profesa kututaka tupapalikie karne ya 21 ni sawa na kutuhimiza tuunge bogi tusilo lijuwa lielekeapo. Waislamu tuna ajenda yetu inayolenga hadi siku ya mwisho sio ubabaishaji unaokomea hapa hapa ulimwenguni. Tatizo la Waislamu linajulikana, maana marehemu Profesa Kighoma Malima aliyaweka wazi matatizo mengi ambayo ni kero kubwa kwa Waislamu, vipi Profesa Kapuya unaturudisha nyuma. Kuna matatizo kama kubanwa katika elimu, kutotambuliwa haki yao ya kuwa Waislamu na hivyo kuwapa fursa ya kufanya ibada yao kwa kadri ya maagizo ya Mola wao, mathalan kuacha kufuga nguruwe kwenye mashule yenye mchanganyiko wa dini mbalimbali. Sisi Waislamu tumechoshwa na matusi yenu viongozi Waislamu mlioko madarakani mnapoalikwa kwenye hafla za Waislamu hamji na tufanye nini ila mnakuja kwa nini mnafanya hivi. Je, kama sio Waislamu kusema dhulma iliyotendeka katika uchaguzi wa Parole nani angejua na baada ya kusema, je, Rais si aliivunja, je, umesahau Profesa Malima alipobadilisha utaratibu wa kutumia namba badala ya majina nafikiri matokeo yake unayajua hapo wizarani. Au wewe ni katika waliokuwa wakimpiga vita Malima? Kuhusu suala la kupigana, Profesa umechemsha, sikiliza Mungu anavyosema: Na ikiwa makundi mawili katika Waislamu yanapopigana, basi fanyeni (suluhu baina yao na likiwa moja la hayo linadhulumu mwenzie basi lipigeni lile linaloonea mpaka lirudie katika amri ya Mungu, na kama likirudi basi yapatanisheni baina yao kwa uadilifu na hukumuni kwa haki. (49:9). Je, anayepigana kwa kuwa kadhulumiwa na yule anayefungua maonyesho ya kutafuta mrembo Miss TZ wanawake wakiwa uchi yupi mwenye mwelekeo? Anayeanzisha sera ya watoto kupewa kondomu mashuleni na mitaala ya ngono kufundishwa mashuleni na yule anayesema msikurubie zinaa kwa kuwa ni uchafu, nani mwenye mwelekeo? Je, wewe umebadilisha vipi utaratibu wa Waislamu kulalamika kwa vitendo au na wewe unalalamika ukiwa wewe ni Profesa Muislamu na tatizo unalijua umelisaidia vipi kuliondoa ukiwa wewe ni mdhamini wa baadhi ya shule hizi. Vinginevyo inaonyesha umepikwa ulivyopikwa kuuzamisha Uislamu. Namalizia kwa kukumbusha kuwa cheo ni dhamana, iwapo unataka utukufu basi utukufu wote upo kwa Allah (s.w). Abuu Hafsa,
Mimi sio miongoni mwa waliompongeza Kingunge Ndugu Mhariri NAOMBA nafasi katika gazeti lako la AN-NUUR ili nitoe dukuduku lango. Waislamu wenzangu katika toleo la gazeti la gazeti hili toleo la 1419, Juni 26 – Julai 3, 1998 kuna kichwa cha habari kinachosomeka "Waislamu wampongeza Kingunge", chini ya kichwa hicho kuna maneno yanayosomeka "Mamia wamtembelea Chuki Muhimbili". Dukuduku langu: Kama wapo Waislamu wanaounga mkono matamshi hayo, kweli nimeamini sisi Waislamu tumerogwa na tumelala usingizi mzito tena usingizi wenyewe ni ule wa sindano inayojulikana kwa jina la "nusu kaputi". Waislamu mimi najisikia uchungu mkubwa sana ninapo kisoma kichwa hicho cha habari kwa sababu huyo Kingunge amekaa kimya kuhusu tukio la kuvamiwa Waislamu wa Mwembechai na kuuliwa kwa makusudi kwa kupigwa risasi na polisi. Nina hakika Kingunge kutokana na cheo chake na mahala anapofanyia kazi, anayo habari ya tukio la Mwembechai kwa urefu na mapana kabla na baada ya tukio. Na tangu Waislamu wa Mwembechai wauliwe zaidi ya miezi 5 imepita, hata siku moja sijapata kumsikia Kingunge katika vyombo vya habari na wala kuona katika magazeti ya kwamba Kingunge amelaani kitendo kilichofanywa na polisi cha kuwavamia Waislamu wa Mwembechai na kuwaua. Na wala kuwapa pole wale waliojeruhiwa na kuishauri serikali iwafunge pingu na kuwaruhusu waganga kuwatibu akina Chuki na wenzake matibabu yanayostahiki. Na wala kuishauri serikali iwape angalau dhamana tu watuhumiwa. Kutokana na hayo niliyoyaeleza hapo juu ndio yanayo nifanya nisiwe miongoni mwa wale wanaompongeza Kingunge na kama yupo Muislamu ambaye amepata kusikia au kumuona Kingunge akiyafanya hayo niliyoyaeleza hapo juu naomba anifahamishe wengine tupate faida. Kuhusu mamia kumtembelea Chuki Muhimbili, napata faraja kwa hilo. Kwa mtazamo wangu, sababu kubwa ya kuachiwa huku Chuki na kupelekwa kutibiwa jengo la MOI ni kwamba lengo la maadui wa Uislamu na Waislamu limetimia kwa hiyo wameona hakuna sababu ya kuendelea kumfunga pingu, na wala kumnyima matibabu stahiki. Mwisho natowa wito kwa Waislamu wote ulimwenguni adui ni adui, awe anakuja kwa vitisho au kwa upole, kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani au ofisi ya Rais, wote hao baba mmoja na mama mmoja, tujihadhari nao. Na Waislamu acheni kulala, amkeni kumekucha. Sheikh M. Awadh,
Ndugu Mhariri NASHUKURU sana kusoma toleo lako la AN-NUUR Aprili 24 –30, 1998 ambalo nimelipata kwa rafiki yangu aliyekuwa huko likizo na akashuhudia mauaji Mwembechai ya Waislamu wasio kuwa na hatia yoyote. Hatia yao ni kwamba ni Waislamu, basi Mola auweke moyo wao pema – Amiin. Suala la Mwembechai ni aibu tupu kwa serikali na viongozi wake huku wakidai kwamba Tanzania ni nchi safi na ina heshimu haki za kibinadamu na kuabudu kama vile ilivyo katika vipengele vya Human Rights – United Nations. Mimi kama Mwanafunzi Mtanzania hapa Ulaya nalaani kitendo hicho kwa nguvu zote, sababu ni kitendo cha aibu, unafiki. Nikiwa kama Mwenyekiti wa Waislamu na Katibu wa Baraza la Wanafunzi wa kigeni hapa chuoni, nalaani hicho kitendo, sababu kimeniweka katika hali ya aibu hapa chuoni na nchi yangu. Hadi nasikia aibu kujiita Mtanzania baada ya kitendo hicho. Mwenyekiti wa Wanafunzi wa Kiislamu
Ndugu Mhariri NAOMBA nafasi japo pembeni mwa gazeti lako ili niweze kutoa dukuduku langu juu ya Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA). Toka kiundwe chama hiki sasa ni muda mrefu kipo hapa nchini, na miongoni mwa shughuli zake ni pamoja na kutoa nasaha, kuelimisha, kulinda na kutetea haki za kina mama na watoto, na tumeshuhudia hivi karibuni namna kilivyoshikilia bango hukumu iliyotolewa na mahakama ya mwanzo ya Kariakoo iliyomhusu msichana mmoja (changudoa) jijini baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuiba simu ya mkononi ya mteja wake. Vile vile macho na masikio yetu yameshuhudia jinsi chama hicho cha TAMWA kilipogeuka kuwa bubu pale wanawake wenzao wa Mwembechai walipovamiwa sehemu yao jinsi ya kufanyia ibada na kupigwa mabomu, virungu na hata kupekuliwa sehemu zao za siri na askari wa kiume ambapo ni kinyume na sheria na katiba ya nchi achilia mbali kuwa ni ukiukaji wa haki za binadamu. Bado "watetezi wa wanawake" nyinyi mkanyamazia tu mateso yote haya. Machi 29, 1998, serikali kupitia kamanda wa polisi wa mkoa ikazuia mkutano wa ndani wa wanawake wenzenu kwa madai kuwa utavunja amani, hata hapo pia pamoja na shahada na diploma zenu zote mkajifanya hamkuona! Leo ndio mnajidai kuandaa warsha ya kuwaelimisha wanawake nini cha kufanya pale wanapokorofishana na wanaume zao ili tuwaone wa maana. Kwa mtaji huo mmechemsha. Na ajabu iliyokuwa kubwa kuliko zote katika chama hicho ni kuwa washiriki wengi ni Waislamu. Je, nyinyi hamna au mnadhani kwa kufanya hivyo mtapendeza sana. Sivyo hivyo mabibi nyinyi. Maisha ya dunia ni starehe ndogo idanganyayo. Rejeeni uchungu na Uislamu? Rahma J. Kamenya,
Waislamu tumuogobe Mwenyezi Mungu Ndugu Mhariri, NAOMBA unipe nafasi kidogo katika gazeti lako ili niweze kuwafikishia ujumbe huu Waislamu popote pale walipo hasa Tanzania. Kila Muislamu anayempenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake Muhammad (s.a.w.) anaelewa fika tatizo tulilo nalo la kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu. Tatizo lenyewe ni kuhusu kesi za Wahadhiri walioshitakiwa kwa kusema; Yesu si Mungu, Mungu hakuzaa wala hakuzaliwa, Yesu alikuwa ni Muislamu, Yesu hakufa msalabani. Mpaka sasa hivi zinatakiwa fedha taslimu Tshs.7,000,000 kwa ajili ya Wakili anayeshughulikia kesi hiyo. Hapa ndipo Waislamu tunaonyesha dhahiri kwamba hatumpendi Mwenyezi Mungu pamoja na dini yake. Watanzania Waislamu tuko 60% ya Watanzania wote ambapo ni sawa na milioni 18, labda wenye uwezo ni milioni 10 kila Muislamu akichanga Tshs. 100/- tunao uwezo wa kupata Tshs. 100,000,000 yaani Waislamu tunashindwa kuweka mikakati thabiti tukapata hizo fedha? Waislamu tumuogope Mwenyezi Mungu na siku nzito ya hukumu, tutamwambia nini Mwenyezi Mungu atakapo tuuliza jinsi tulivyoipigania dini yake. Na Menyezi Mungu anatuambia kwamba piganieni dini kwa mali na nafsi. Ndugu Waislamu tufanye utaratibu wa haraka sana ili tupate hizo fedha kwa muda wa miezi miwili tu inatosha ili tuinusuru dini ya Allah. Inshallah Mwenyezi Mungu atupe moyo thabiti wa kupenda dini yake. Najum. B. Abdilnoor,
|
TAHARIRI Maoni yetu: Wananchi kataeni kupotoshwa SUALA LA MWEMBECHAI: Wabunge
wataka kujua nani aliamrisha kuua
Katiba ya nchi yapuuzwa: Waislamu wapigwa marufuku kuhubiri Mtihani darasa la saba 1998: Manispaa
Moro yaagiza ipewe majina ya wanafunzi Wakatoliki
“Wushu”ya Waislamu wa China
na jinsi ilivyowasaidia kupambana na dhulma dhidi yao
Yesu wa kwenye Mathayo siyo Yesu wa
kwenye Luka
Ni nani hawa Waislamu wa Siasa Kali
?
Waislamu tuondokane na unyonge
Waislamu wana mwelekeo wao
Ni mwaka gani Yesu alianza kuitwa
Mungu
Wanawake wameamua kuwa wazi
kweli kweli
Kimya kingi kina mshindo mkuu:
Vipi Mhe. Rais wale walioua?
Mtazamo wa madhalimu wa Tanzania
kwa Waislamu
Waislamu mkoa wa Morogoro
wampinga Yahya
Polisi wachafua mazingira
ya msikiti wa Mwembechai
Wanawake wa Kiislamu Ubungo
darajani wamuunga mkono Sheikh Bafadhil
Mafundisho ya Qur'an: Kanuni za kumkumbuka Allah na kutumia katika njia yake Chakula na lishe: Lishe ya
mtoto aliyekuwa mgonjwa
|