AN-NUUR
Na.158 Rabi' Awal 1419, Julai 17 - 23, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Waislamu tuondokane na unyonge

Na Abubakar Marwilo 

WAISLAMU ni lazima tuache kujigawa katika makundi na kufanya uhasama na uadui miongoni mwetu. Tufahamu fika kuwa Uislamu unatukataza kuwa na tabia hii au mwenendo huu katika maisha yetu. Huu ni wakati wa muafaka wa kujenga misingi ya umma mmoja inapatikana katika kitabu chetu Qur-an takatifu na Sunnah za Mtume wetu Muhammad (s.a.w.), ukhalifa na historia yetu.  

HIZI ni zana na endapo tukizitumia kama inavyopaswa tutajenga jamii yenye nguvu katika nchi yetu ya Tanzania na kwa ujumla dunia nzima. Pia tutakuwa kazi bure sana na Mwenyezi Mungu na msaada wetu kutoka kwake utakuwa ni wa mara moja. 

Baada ya sisi Waislamu kuwa mbali na mafundisho ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, madhara yanayotufika dunia nzima, ni Waislamu kudharaulika, kuishi maisha ya taabu, kuuawa kama wanyama, na wakati mwingine unaweza kusema hata hao wanyama ni afadhali. 

Mifano ya hivi karibuni ipo. Waislamu wa Palestina wananyang’anywa ardhi, wanauawa kila siku ati tu Myahudi na wasaidizi wake wapate manufaa. Bosnia, katika nchi za Balkani, Waislamu walianzishiwa vita na watu wa kabila la Waserb; na katika vita hivi Waislamu takriban laki nne waliuawa kikatili na mali zao zote ziliharibiwa, ikiwemo misikiti na maktaba zilizohifadhi kumbukumbu za kale za historia ya Kiislamu. Baada ya Bosnia, sasa Kosovo. Kasovo ni mkoa wa Serbia ambao wakazi wake walio wengi ni Waislam, karibu 97% ni Waislamu na 30% ni watu wasiokuwa Waislamu. Wanafanyiwa mateso makubwa kwa mateso waliofanyiwa Waislamu wa Bosnia. 

Lebanon au kwa kifupi mshariki ya kati hali ni ile ile. Swali: Hivi kuona jambo gani lililopo katika nchi hizi mpaka maisha ya binaadamu yanaharibiwa namna hiyo? Jibu la swali hili ni kwamba katika nchi hizi kuna makundi mawili; kundi la kwanza ni lile kundi linalopigania haki, na kundi la pili ni lile linalopigania batili. 

Vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na Marekani Kaskazini havina utamaduni wa kuwafahamisha walimwengu ukweli wa mambo, hususan masuala ya Waislamu yanapojitokeza. Wanafanya hivi siyo kwa bahati mbaya, bali kwa makusudi ya kulinda wale wanaowataka katika madaraka/serikali na kwa ajili ya maslahi yao. 

Hivi sasa Waislamu hatuwezi kukabiliana na hili kwani mpaka sasa hatuna vyombo vya habari vilivyo madhubuti wala hatuna fikra ya karibu kuanzisha vyombo hivyo. Hata hivyo tusikate tamaa. 

Tunahitajika kuyaweka wazi kwanza malengo yetu kufuatana na historia yetu ya Kiislamu na tukizingatia haswa mazingara yetu yanayotuzunguka. Ni lazima tuandae mipango kabambe ya kitaalamu inayokwenda sambasamba na malengo yetu na tuwe tayari kuitekeleza kwa moyo mmoja. Kuwa na mpango wa kuanzisha na kuunda mfuko wa fedha kwa ajili ya mahitaji yetu mbalimbali nchi nzima ni jambo la lazima na lisiloweza kuepukika. 

Hili linahitaji kamati ya wataalamu kulifanyia uchunguzi wa kina ili kuweza kuona kama linawezekana ua haliwezekani. Mwenyezi Mungu anatufundisha nini kuhusu maendeleo yetu? Mwenyezi Mungu anatufundisha kuwa tushughulike na dunia kama vile tutaishi milele, tuwe na hisa katika dunia hii, na tukumbuke akhera kama kwamba tutakufa kesho. Anaendelea katika kitabu chake kitukufu, Qur-an, kutuambia tusali na tutoe zakah, tukisha kumaliza kusali, tutawnyike katika ardhi aliyotuumbia tutafute neema zake. Hatuwezi kufanya maendeleo yeyote kwa kuswali tu; kama tunavyofanya hivi sasa. Tumekuwa na umasikini wa kupundikia kwa sababu hatujawa tayari kutafuta neema za Mungu. Ni sahihi kusema kuwa Uislamu ni uongozi, tena wa kimataifa. Unahitaji viongozi wenye sifa zifuatazo:- 

Wacha Mungu na wakweli. 

Wenye kuwa na mtazamo wa Quran, Sunnah na ukhalifa. 

Wenye kutenda mema,wenye kuwa na imani ya kuwepo Mwenyezi Mungu na Mtume wake. 

Wenye subira na wenye kuhusiana haki na wawe tayari kupinga dhulma kwa siri na kwa dhahiri. 

Viongozi wetu watakapojipamba na kuweka katika vitendo sifa hizo katika maisha haya ya kila siku, basi kutakuwepo uhakika wa kugeuza hali hii mbaya tuliyonayo na kufanikisha malengo yetu kwa asilimia tisini na nane. Na wafuasi nao watoe mchango wao wa mali na hali kwa Uislamu na waachane na yale mawazo ya kale kuwa Waislamu ni wanyonge. 

Kukaa bure pasipo kufanya jitihada yeyote na kisha kumtegemea Mwenyezi Mungu kuleta mabadiliko ni kujidanganya sisi wenyewe na kujiuwa kabisa. Hatuna budi kuamka nakisha kufanya mapinduzi katika nafsi zetu na tabia zetu. 

Mapinduzi ya kweli ni kutekeleza kwa ukamilifu jukumu letu tulilopewa na Mola wetu la kukataza mabaya na kuamrisha mema katika jamii. Katika jamii zetu nyingi, hivi sasa mabaya yanageuzwa kuwa mazuri, na mazuri yanageuzwa kuwa mabaya. Hali hii inatuweka mbali na Mwenyezi Mungu na kutuweka karibu mno na moto wa Jahanamu. Waislamu hatukuumbiwa moto; Waislamu tumeumbiwa pepo. Lakini hilo linategemea sana katika kutekeleza jukumu letu la kukataza mabaya na kuamrisha mema. 

  
Juu 
 

YALIYOMO
 
TAHARIRI  

Maoni yetu: Wananchi kataeni kupotoshwa 

SUALA LA MWEMBECHAI: Wabunge wataka kujua nani aliamrisha kuua 
Na Mwandishi wetu  

Katiba ya nchi yapuuzwa: Waislamu wapigwa marufuku kuhubiri  

Mtihani darasa la saba 1998: Manispaa Moro yaagiza ipewe majina ya wanafunzi Wakatoliki 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

 “Wushu”ya Waislamu wa China na jinsi ilivyowasaidia kupambana na dhulma dhidi yao 
Na MUSSA ALLY  

Yesu wa kwenye Mathayo siyo Yesu wa kwenye Luka 
Na. Masoud Mohammed 

Ni nani hawa Waislamu wa Siasa Kali ? 
Na USTADH  A.S. FUNDI  

Waislamu tuondokane na unyonge 
Na Abubakar Marwilo 

Maisha ya ndoa kwa Mwislamu 

Waislamu wana mwelekeo wao 
Na Sheikh Pandukizi Dilunga 

Ni mwaka gani Yesu alianza kuitwa Mungu 
Na MCHUNGAJI A.T. MANONI  

Wanawake wameamua kuwa wazi kweli kweli 
Na Bi. Fatma Musa 

Kimya kingi kina mshindo mkuu: Vipi Mhe. Rais wale walioua? 
Na Mussa Ally 

Mtazamo wa madhalimu wa Tanzania kwa Waislamu 
Na Rajab Isa 

Aliyoyasema KK bungeni 

Waislamu mkoa wa Morogoro wampinga Yahya 
Na. Abu Adli  

Polisi wachafua mazingira ya msikiti wa Mwembechai 
Na Badru Kimwaga 

Wanawake wa Kiislamu Ubungo darajani wamuunga mkono Sheikh Bafadhil 
Na Kassim Juma 

Barua za wasomaji  

Mashairi  

Mafundisho ya Qur'an: Kanuni za kumkumbuka Allah na kutumia katika njia yake 

Masomo  

Chakula na lishe: Lishe ya mtoto aliyekuwa mgonjwa 
Na Mujahiid Mwinyimvua 
  

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita