AN-NUUR
Na.158 Rabi' Awal 1419, Julai 17 - 23, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Maoni yetu

Wananchi kataeni kupotoshwa 

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Ali Ameir katika hotuba yake Bungeni amesema kwamba vurugu za Mwembechai zilisababishwa na vikundi vya dini ambavyo vingine vimesajiliwa na vingine havina uhalali wowote kisheria ila vipo tu na vinatumiwa kuendeleza ghasia na maovu. Aidha akasema vikundi hivyo vinahubiri kashfa na chuki baina ya dini na dini. 

Kutokea hapo Mhe. Waziri akasema kwamba wapo viongozi wamejitumbukiza katika kuvitetea vikundi kama hivyo na kuanzisha malumbano dhidi ya serikali. Na akadai kwamba viongozi wa aina hii hawalitakii mema taifa letu huku akiwashawishi wananchi wote wawakatae viongozi hao na wakatae kupotoshwa na viongozi aliodai "wachache wenye uchu wa umaarufu na madaraka." 

Kwanza tungependa Mhe. Ali Ameir atueleze zile Balozi za nje zilizohusika awali ni zipi na amezichukulia hatua gani. Pamoja na Balozi hizo, wananchi wangependa kujua vyama gani vya siasa vilihusika kwa ushahidi na vimechukuliwa hatua gani. 

Pili, Mhe. Waziri angetueleza ni vyama gani hivyo vya kidini vinavyotumia kivuli cha dini kuendeleza ghasia na maovu. Kisha aueleze umma wa Watanzania ni lini na wapi vyama hivyo vilileta ghasia vikaua au kuharibu mali za raia au serikali kabla ya polisi kuvamia msikiti wa Mwembechai na kuua au pale walipowavamia kule Mwananyamala Februari 12, ni ghasia na maovu gani yaliyokuwa yanafanyika pale msikitini. 

Mhe.Waziri amesema vikundi hivyo vimehubiri chuki na kashfa dhidi ya dini nyingine.Chuki gani na kashfa gani. Dini gani zimeparurana kuonyesha kwamba zinachukiana. Dini gani iliyoshitaki mahakamani kwamba inakashifiwa na ikaiainisha hiyo kashfa yenyewe. Kama ipo kashfa sheria inasema wauliwe au wafikishwe mahakamani. Hatuna kumbukizi ya kiongozi yeyote wa dini yoyote kufungua kesi ya kashfa dhidi ya dini nyingine. Labda Mhe. Waziri atueleze dini hiyo inayokashifiwa dini gani, je; ni dini ya serikali ndio maana inakuja juu na kuua bila hata kwenda mahakamani? 

Kiongozi yeyote mwenye busara na mwenye kujali maslahi ya nchi ya muda mrefu hawezi kuifumbia macho dhulma. Hawezi kuridhika kuona jamii moja katika nchi inaonewa, kudhalilishwa na kunyimwa haki zao. Ataikemea dhulma ili kuepusha yale ya Rwanda, Burundi, Ireland, Lebanon n.k. 

Hawa ndio wenye kuitakia mema nchi. Hawa ndio wazalendo wenye kujali amani na usalama wa nchi wa kudumu. Hawa ndio wenye kujali maslahi ya wananchi wanyonge wote. Hawa wapo pamoja na wananchi.Na wananchi hawatokubali kupotoshwa na wachache wanaotumiwa kutetea maslahi binafsi ya wachache na ya muda mfupi pamoja na ‘better chance’ za dini zao. 

Waislamu na watu kote duniani wameweka historia ya kusimama pamoja na wale wanaopambana na dhulma. Hapa Tanzania haitokuwa kinyume. Wananchi hawatosimama na wale waliowatesa wazee wa mika 83 mpaka wamechanganyikiwa wala hawatosimama pamoja na wale walioua. 

Juu 
 

YALIYOMO
 
TAHARIRI  

Maoni yetu: Wananchi kataeni kupotoshwa 

SUALA LA MWEMBECHAI: Wabunge wataka kujua nani aliamrisha kuua 
Na Mwandishi wetu  

Katiba ya nchi yapuuzwa: Waislamu wapigwa marufuku kuhubiri  

Mtihani darasa la saba 1998: Manispaa Moro yaagiza ipewe majina ya wanafunzi Wakatoliki 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

 “Wushu”ya Waislamu wa China na jinsi ilivyowasaidia kupambana na dhulma dhidi yao 
Na MUSSA ALLY  

Yesu wa kwenye Mathayo siyo Yesu wa kwenye Luka 
Na. Masoud Mohammed 

Ni nani hawa Waislamu wa Siasa Kali ? 
Na USTADH  A.S. FUNDI  

Waislamu tuondokane na unyonge 
Na Abubakar Marwilo 

Maisha ya ndoa kwa Mwislamu 

Waislamu wana mwelekeo wao 
Na Sheikh Pandukizi Dilunga 

Ni mwaka gani Yesu alianza kuitwa Mungu 
Na MCHUNGAJI A.T. MANONI  

Wanawake wameamua kuwa wazi kweli kweli 
Na Bi. Fatma Musa 

Kimya kingi kina mshindo mkuu: Vipi Mhe. Rais wale walioua? 
Na Mussa Ally 

Mtazamo wa madhalimu wa Tanzania kwa Waislamu 
Na Rajab Isa 

Aliyoyasema KK bungeni 

Waislamu mkoa wa Morogoro wampinga Yahya 
Na. Abu Adli  

Polisi wachafua mazingira ya msikiti wa Mwembechai 
Na Badru Kimwaga 

Wanawake wa Kiislamu Ubungo darajani wamuunga mkono Sheikh Bafadhil 
Na Kassim Juma 

Barua za wasomaji  

Mashairi  

Mafundisho ya Qur'an: Kanuni za kumkumbuka Allah na kutumia katika njia yake 

Masomo  

Chakula na lishe: Lishe ya mtoto aliyekuwa mgonjwa 
Na Mujahiid Mwinyimvua 
 

 

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita